NJIA YA WOKOVU YA SASA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU apewe sifa.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Tunaishi wakati wa Kanisa duniani.
Wakati wa Kanisa ndio pia wakati wa Agano jipya.
Mafundisho makuu ya kuliongoza Kanisa la MUNGU sasa yapo katika agano jipya.
Ni kosa kubwa kuyaacha mafundisho ya agano jipya na kujaribu kufuata mapokeo machache ya agano la kale.
Kumbuka njia ya Wokovu ya agano la kale ilikuja kabla ya njia ya wokovu ya agano jipya.
Njia ya Wokovu ya agano la kale ni torati na njia ya Wokovu ya agano jipya ni YESU KRISTO na Neno lake ambalo Biblia inaliita Neno la KRISTO.

Chanzo cha uzima wa milele ni kutii Neno la KRISTO
Yohana 20:31 ''1 Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba YESU ndiye KRISTO, Mwana wa MUNGU; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.''

Chanzo cha uzima wa milele ni kumpokea YESU kama Mwokozi
Yohana 1:12-13 '' Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''
 
Chanzo cha uzima wa milele ni kulitii kusudi la MUNGU la Wokovu
Yohana 3:17-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

Leo kimakosa kuna makanisa wanaoa wake wengi kwa sababu tu wamemfuata Suleiman aliyeishi wakati wa Torati, kwenye suala ya Suleiman au Daudi kuoa wake wengi hakuna agizo kwa Kanisa kuoa wake wengi.
Kuna makanisa Leo wanamkataa YESU bila kumjua YESU ni nani katika agano la kale.
Yaliyo katika agano la kale ni muhimu sana kwa kanisa ili yatusaidie kujua na kutenda katika mpango wa MUNGU.
Biblia inasema kwamba yaliyoandikwa katika agano la kale yaliwapata wao kwa jinsi ya mwili, yalikuwa kwa ajili ya kutusaidia sisi kujua kazi ya MUNGU na ni jinsi gani tunaweza kumpendeza MUNGU.


1 Wakorintho 10:11 "Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani."


Pia ni muhimu kujua kwamba tunaposema agano la kale hatumaanishi Vitabu vyote 39 vya agano la kale Bali tunakuwa tunamaana ya torati.

Hebu ona mifano hii ya kutofautisha vitu kati agano la kale na jipya.

1. Njia ya Wokovu ya agano la kale inasema "Usizini"
Lakini njia ya Wokovu ya agano jipya haisemi tu usizini Bali inasema usizini na hata usitamani mke/mume wa mwenzako.

Mathayo 5:27-28 " Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;
lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake."


2. Njia ya Wokovu ya agano la kale inakataza baadhi ya vyakula kwamba ni najisi.
Lakini njia ya Wokovu ya agano jipya vyakula hivyo vimetakaswa, sio najisi tena, Bali mawazo machafu ndio najisi na sio vyakula.
Baadhi ya madhebebu hujanganyikiwa katika hili nakuanza kuwahukumu wanaotumia vyakula ambavyo vilikatazwa katika torati.
Hao wanasahau kwamba MUNGU aliyeviumba viumbe vyote na akasema baadhi ya viumbe visiliwe ndio MUNGU huyo huyo aliamua kwa upendo wake kuvitakasa vyakula vyote.

Marko 7:18-19 " Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote."

Tuna mambo mengi sana ya kukifunza katika agano la kale lakini ni vyema tukajifunza Agano la kale kwa jinsi ya KRISTO ndipo tutaweza kuwa kanisa hai la MUNGU.
Fundisho letu kuu ni lile ambalo liko kwa jinsi ya KRISTO lakini hatuwezi kuelewa Biblia kama hatujajifunza agano la Kale.
Kuna watu Biblia zao ni agano jipya tu na Zaburi, hao hawawezi kuelewa vyema kusudi la MUNGU.

Ni vyema sana kulifanyia kazi Neno la KRISTO.
Neno la KRISTO ni la milele na halitapita kamwe.

1 Petro 1:25 "Bali Neno la Bwana(YESU) hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu."

Neno la KRISTO ndilo neno la Wokovu.
Neno la KRISTO ndio injili ya KRISTO iokoayo.
Ndio neno tunalotakiwa kulitii Mimi na wewe tulio kanisa la MUNGU.

Ndugu, usiliongeze Neno la KRISTO wala kulipunguza.

Ufunuo wa Yohana 22:18-19 " Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki."


Kuliongeza Neno la MUNGU au kulipunguza ni kufundisha uongo na kuwapotosha watu.
Ni kuwatoa watu kwa YESU ndio kuliongeza Neno la MUNGU au kulipunguza.

MUNGU akubariki na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments