PASAKA NI NINI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kuhusu Pasaka.
Kwa uchunguzi wangu mimi nimegundua Neno Pasaka linapatikana mara 51 katika agano la kale pekee.
 na katika Agano jipya likipatikana mara nyingi pia.

Pasaka ni nini?
Kwa mjibu wa Kamusi ya kiswahili sanifu Pasaka ni sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa YESU KRISTO.
Kibiblia Neno Pasaka lina mapana zaidi.
Pasaka hasa ni Mwanakondoo aliyechinjwa ili kuwa upatanisho.
Bwana YESU ndiye pasaka wa kanisa maana alikufa na kufufuka ili kuwapatanisha wanadamu watii na MUNGU wao.

Neno Pasaka linatokana na Neno Passover la kiingeleza.
Kwa kiebrania Neno hilo ni Pesach na kwa Kiyunani ambayo ndio lugha iliyoandikwa agano jipya Neno hilo ni Pascha, Na Neno hilo la Kigiriki au kiyunani linashabihiana na neno Pasaka katika kiswahili.

Katika Biblia kuna matukio makuu mawili yanayoonesha Pasaka.

1. Waisraeli waliamuriwa na MUNGU kusherekea Pasaka ili kukumbuka jinsi walivyotoka utumwani Misri.
Kutoka 12:21-28 '' Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje PASAKA. Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele. Itakuwa hapo mtakapoifikilia hiyo nchi, BWANA atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu. Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N'nini maana yake utumishi huu kwenu? Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya PASAKA ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia. Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama BWANA alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.''

Walisherekea waliotoka Misri.

 2. Katika Agano jipya yaani wakati wa Kanisa Pasaka wetu ni Bwana YESU.
1 Kor 5:7 '' Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana PASAKA wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, KRISTO;''

Biblia haitoi agizo kwamba Kanisa lisherekee Pasaka lakini hiyo hiyo haiondoi kwamba tunaye Pasaka wetu ambaye alishinda ili atushindie na sisi.
Tukumbuke pia Biblia inasema 
''Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.  Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa BWANA; naye alaye, hula kwa BWANA, kwa maana amshukuru MUNGU; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru MUNGU.-Warumi 14:5-6''

 Ni nani basi anayetakiwa kuiadhimisha Sikukuu ya Pasaka  akikumbuka alivyotoka utumwani kwa shetani?
Ni Mkristo aliyeokolewa na Bwana YESU, maana waliookolewa na Bwana YESU hao ni viumbe wapya waliohama kutoka katika utumwa wa shetani na dhambi na sasa wako kwa Bwana YESU.
2 Kor 5:17 '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''

Hatutakiwi kusherekea tu katika hii siku ya Pasaka bali kukumbuka kwamba tumeokolewa na Bwana YESU hivyo tuongeze sana kuishi maisha matakatifu.

Kuna watu pia huuliza kwamba kwanini YESU alisherekea Pasaka huku na sisi tukisherekea Pasaka huku tukisema kwamba tunakumbuka alivyotuokoa?
Majibu ni kwamba Bwana YESU alisherekea Pasaka ya kiyahudi na hiyo Pasaka ni tofauti ni hii ya sasa.
Bwana YESU alipoamua kuja duniani aliamua kupitia Israeli na alishika sheria za Neno la MUNGU za wakati ule, hivyo alizaliwa chini ya sheria/torati na aliishika torati ila kwa madhumuni.
Wagalatia 4:4 inajulisha kwamba alikuwa chini ya sheria/torati alipokuja duniani, Biblia hapo inasema ''Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, MUNGU alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,''
Bwana YESU alizaliwa chini ya sheria/Torati ili awasaidie walio chini ya sheria na hata sisi ambayo torati haikutuhusu maana ilikuwa special kwa wayahudi.
Jambo la pili kujua kwanini YESU alisherekea Pasaka ni kwamba Torati ni kivuli tu cha mwili ambao ni KRISTO.
Waebrania 10:1 ''Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.''
 Maana yake ni kwamba torati ilikuwa mtangulizi tu na kivuli tu lakini mhusika ni KRISTO hivyo alipokuja KRISTO badiliko jipya lilikuja. Bwana YESU baada ya kuila ile Pasaka ya kiyahudi  ya mwisho, muda mfupi baadae aliutoa uhai wake kisha kuutwaa tena na kuwa sadaka moja idumuyo milele kwa ajili ya ondoleo la dhambi kwa wanaomtii na kulitii Neno lake.
Luka 22:7-16 '' Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja PASAKA. Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie PASAKA tupate kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo. Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa PASAKA. Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila PASAKA hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa MUNGU.''

Kumbe Pasaka ilitimizwa katika Ufalme wa MUNGU.
Luka 22:16 ''kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa MUNGU.''

Kwa Kanisa leo ni heri tumgejiuliza kwa wayahudi maana wao walisherekea Pasaka baada ya kutoka utumwani Misri.
Leo kuna watu hawajaokoka na ni watumwa wa dhambi, lakini wao wanasherekea Pasaka.
Hao hawajui Pasaka ni nini maana hata Waisraeli walisherekea baada ya kutoka utumwani sio wakiwa utumwani.
Pasaka kusherekea haimuhusu mtu aliye utumwani  kwa shetani.
Kama wewe bado ni mtumwa wa dhambi au mtumwa wa shetani hakika pasaka kwako haina thamani  waka maana kwako.
Kama umeokolewa na Bwana YESU aliye Pasaka wetu basi unaweza ukamtukuza MUNGU kwa kukuletea Wokovu.
Kama bado uko dhambini hakika Pasaka kwako haikufai maana wanaotakiwa kusherekea ni watu waliotoka utumwani kwa shetani.
Maombi yangu ni kwamba Damu ya YESU KRISTO ya Pasaka ikukomboe Moto wako, roho yako, nafsi yako na mwili wako.
Nakutakia Pasaka njema na hakikisha utakatifu wa wakati huu wa Pasaka unaendelea miaka yote.
 MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.

0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments