DHAMBI HAIPAKWI RANGI BALI INAKEMEWA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kutenda dhambi wakati mwingine huzaa mapigo ndio maana Biblia inakataza kufanya maovu.
Zaburi 34:13-14 '' Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
Kama huwa unatenda dhambi ukitarajia tu kutubu naomba utambue kwamba wakati mwingine unaweza ukapata mapigo na kutubu umetubu na umesamehewa.

Mfano mtu anaweza akafanya dhambi ya uzinzi kisha akatubu lakini kama uzinzi ulizaa mimba au magonjwa hatari ya zinaa basi japokuwa amesamehewa lakini ugonjwa huo upo na unaweza kumtesa.
Mwizi anaweza akaiba na akikamatwa anapigwa, hivyo hata akama atatubu baadae lakini madhara ya kipigo yatakuwepo, kama mkono ulivunjika basi utaendelea kuwa umevunjika, kama jicho liliondolewa basi litaendelea kutokuwepo hata kama ametubu.

Dhambi ni mbaya na haifai mtu yeyote anayempenda YESU aifanye.
Mtii MUNGU wako kwa kuiogopa dhambi, kuiacha dhambi, kuikimbia dhambi na kujitenga mbali na dhambi.

Biblia inasema  '' Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.-Warumi 12:21''


Kuna Watu wanafanya juhudi ili wawe maarufu badala ya kufanya juhudi ili wawe watakatifu.
Umaarufu bila YESU ni maangamizo.
Hata wateule wanatakiwa  kuwa makini sana. Watumishi wa YESU hawatakiwi kuwa watu wa udaku au kushika udaku au kupost udaku, hayo hunajisi.

BWANA YESU anashauri kwamba '' Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.-Marko 9:43.  

Dhambi ina madhara mengi mno na haifai.
Kuna watu baada ya kupata magonjwa mabaya jamii yao ilijua hawawezi kuishi miaka 3 mbele, lakini wagonjwa hao walipomtegemea Bwana YESU waliishi miaka 30 huku waliokuwa wamewapangia muda wa kuishi wenzao ndio waliokufa kwanza. MUNGU anaweza kumponya ugonjwa  mteule wake anayeishi maisha matakatifu na pia BWANA anaweza asimuondolee ugonjwa  mteule wake aliyeokoka lakini akampa kuishi miaka mingi ya furaha na amani kuliko hata ambaye hana huo ugonjwa.
  Magonjwa ya zinaa ni mabaya sana na wakati mwingine inaweza kuwa  ni dalili mojawapo ya mtu aliyelipwa duniani sawa sawa na tabia zake chafu za dhambi ya uzinzi, lakini ukiamua kuokoka na kuanza kuishi maisha matakatifu katika KRISTO hakika MUNGU ukimuomba akuponye anakuponya hakika.

Kumbuka Bwana YESU anaponya magonjwa yote.
Mathayo 9:35 '' Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.''
 
Kuna mchungaji mmoja ambaye ni rafiki yangu sana yuko Uganda kabla hajaokoka alikuwa na ukimwi lakini alipookoka na akajitoa kufanya kazi ya injili MUNGU alimponya na sasa anahubiri injili kwa viwango.
Inawezekana unaumwa ugonjwa huo au ugonjwa mwingine mbaya wa aina yeyote na umepoteza tumaini, ndugu nakuomba okoka na anza kumtii MUNGU na Neno lake.
Mtegemee Bwana YESU kwa maombi hakika utashinda.


Warumi 6:23 Biblia inasema '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu.''

 
 Ni vizuri sana tuwajulishe watu kwamba dhambi ni mbaya na ina madhara mengi mno.
Tuwaambie watu madhara ya ngono na sio tuanze kuipaka rangi dhambi inayozalisha magonjwa mabaya ya zinaa. Dhambi ina madhara mengi na madhara mengine hutokea katika maisha haya haya ya duniani na sio kwamba madhara hayo ni adhabu kutoka kwa MUNGU bali madhara ya dhambi yanayosababishwa na dhambi yenyewe. Mtu akiiba kisha watu wakamkamata na kumpiga, hiyo ni sehemu ya madhara ya dhambi hiyo hata kama na wao wanatenda dhambi pia.
  Binti akizini na kupata mimba na akafukuzwa shule hayo ni sehemu ya madhara ya dhambi hiyo maana atakosa elimu kwa muda sahihi. Kama mtu akivuta sigara kisha baadae madhara yakampata, madhara hayo ni malipo ya dhambi. Ndugu mmoja alikuwa na tabia ya kutoa mimba, alipokuja kuolewa akapima na kukutwa hana kizazi tena kwa sababu ya kutoa zile mimba, wakati huu alikuwa analia sana na kujuta, kwanini alikosa mtoto wakati huu? Dhambi imezaa madhara.

Agizo la  MUNGU ni watu wote waache dhambi na mambo mabaya na wamrudie MUNGU kwa toba na utakatifu.
 Isaya 55:6-7 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.   ''

Katika kuwasaidia watu walioko dhambini Usiipake rangi dhambi bali iseme ili na mwingine apone.  Kuna Watu YESU Akiwaita Leo Wanafyonza. Ndugu Yangu Ipo Siku Utalia Na Kusaga Meno, Yaani Utasaga Meno Kwa Kulia Hadi Meno Yataisha Yote Na Bado Hujamaliza Kulia. Kitambo Kidogo Kuna Kuondoka, Usiishi Kama Hutaondoka Bali Ishi Ukijua Kwamba Kuna Kuondoka. 
Je Ukiondoka Utaenda Wapi? Ndiposa Leo Tunakuambia Kwamba YESU KRISTO Anaokoa, Ukimwamini Leo Unaokoka. 
Kataa Dhambi, Ogopa Dhambi, Ikimbie Dhambi Na Usifanye Dhambi. BWANA YESU Anakupenda Sana Na Anataka Uende Uzimani Aliko Yeye.
Huu ni wakati wa Neema ya MUNGU na Neema hiyo inatutaka kuokoka na kuacha maovu yote.
Yohana 3:16-21 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee(YESU), ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.
 Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.'
'


  MUNGU anawataka watumishi wake kuikemea dhambi na kuwaambiwa wanadamu waache dhambi maana dhambi ni mbaya na ina madhara mengi.
MUNGU Baba anasema ''Nimwambiapo mtu mbaya, hakika utakufa; wewe usimpe maonyo wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka mikononi mwako. Lakini ukimwonya mtu mbaya wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake; bali wewe umejiokoa roho yako.-Ezekieli 3:18-19.
 
NDUGU USIACHE KUWAMBIA WATU WAACHE UOVU NA WAMPE YESU MAISHA YAO.


 Je saa ya ibada Kanisani huwa unaitendea haki?
Hakikisha unalitii Neno la MUNGU unalofundisha ibadani maana MUNGU yuko ndani ya Neno lake akitaka kukusaidia.
Hakuna dhambi ambayo haiwezekani kuiacha kama ukiamua.
Ndugu hakikisha tu unalitii Neno la MUNGU.
Fundisho kuu la Kanisa ni watu waokoke na waishi maisha matakatifu.
Inawezekana hakika kuishi maisha matakatifu kama tu ukiamua kulitii Neno la MUNGU.
 Kuna furaha sana siku ya mwisho kwa wale ambao tuliokoka tukiwa hai na tukaliishi neno la MUNGU. Biblia inasema '' Kwa sababu BWANA mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika KRISTO watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki BWANA hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na BWANA milele.- 1 Thesalonike 4:16
 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments