IMANI YA KUOMBA NA IMANI YA KUPOKEA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
MUNGU Ni Mwema Sana Kwa Wanaompenda.
 Je Unampenda MUNGU?
 Kumpenda MUNGU Ni Kulitii Neno Lake.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la zamu ya leo.
Imani ni uhakika wa mambo yajayo yasiyoonekana kwa sasa ila baadae yatakuja.
 Imani ni nguvu muhimu sana katika maisha ya Mkristo Yeyote.
Imani hutengenezwa kwa kulisikia Neno la KRISTO YESU Mwokozi.
Warumi 10:17  ''Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''

Imani ya MKRISTO ni kuokoka na kisha kuanza kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO maana baada ya hapo ni uzima wa milele.
 Yuda 1:3 ''Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.''

 Katika Imani kuu yaani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi kuna imani mbalimbali ndani yake za kutusaidia kushinda, kufanikiwa na kupona.
-Kuna imani katika maombi.
-Kuna imani katika utoaji.
-Kuna imani katika kufanya kazi ya MUNGU n.k
 
Leo nazungumzia hasa Imani katika maombi.

Yakobo1:5-8 ''Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa  MUNGU, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa. ILA AOMBE KWA IMANI, PASIPO SHAKA YEYOTE; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa BWANA. Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.''

 Kwenye maombi Kuna Imani ya kuomba na kuna Imani ya kupokea.
=Imani ya kuomba ni imani ya kuomba kwa imani huku ukiamini kwa imani utapokea ulichoomba.
=Imani ya kupokea ni imani ya kuvumilia baada ya kuomba.
Imani ya kupokea inaendelea mpaka mtu atakapopokea hitaji lake.
Kuna somo moja niliwahi kufundisha hapa linaaitwa ''UNAKIRI NINI BAADA YA KUOMBA'' ni somo ambalo linaonyesha pia kwamba watu wengi huomba kwa imani lakini baada ya kuomba kukiri vitu vinavyofuta maombi yao. Mfano mtu anaumwa na anaomba kwa imani kwamba apone na katika maombi anakiri kwamba sasa anaenda kupona, Lakini baada ya maombi mtu huyo huyo anaanza kusema sijui kama nitapona. Huyo anakuwa na imani ya kuomba ila hana imani ya kupokea.


Isaya 30:15 ''Nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali.''

 Watu wengi wana Imani ya kuomba ila hawana Imani ya kupokea.
Watu wengi ni waombaji wazuri ila majibu ya MUNGU wakati mwingine yanaweza kuja katika njia inayohitaji Imani zaidi.
Mfano kanisa Fulani Uganda walikuwa na uhitaji Wa ujenzi Wa kanisa na kununua vyombo. Walifunga Mara nyingi na waliomba sana. Siku moja mzee mmoja wasiyemjua alikwenda kuomba maji Nyumba ya mchungaji ambayo iko jirani tu na kanisa.
Yule mzee alikuwa mchafu hatari na ilikuwa ni jioni.
Mchungaji ilibidi ashauriane na mama mchungaji juu ya kumsaidia yule mzee maji, chakula na sehemu ya kulala maana mzee yule alikuwa amechoka sana.
Kwa Neema ya MUNGU walimsaidia yule mzee hadi kesho yake. Wakati yule mzee anaondoka alisindikizwa na yule mchungaji mbele kidogo yule mzee akageuka malaika na kumwambia mchungaji kwamba hakika kanisa linastahili kupokea walichoomba. Baada ya hapo malaika akaenda mbinguni huku mchungaji akitazama.
Hata saa moja haikupita akaja mtu akiwaletea vitu vyote walivyohitaji vya ujenzi Wa kanisa na akawapa na Pesa nyingi Kwa ajili ya kazi ya MUNGU.
Japokuwa walikuwa wameomba sana lakini jibu La MUNGU lilikuwa Kwa njia yakupima Imani yao.
Hawa walikuwa na Imani ya kuomba na Imani ya kupokea.
Leo Mtu anaweza kuomba sana juu ya jambo Fulani lakini MUNGU akapitishia jibu lake Kwa Mtu anayedharauliwa na muombaji huyo.
Huyo muombaji ni ngumu kupokea maana hadi amsikilize mwenye jibu aliyepewa na MUNGU.
Imani ya kuomba kila mtu anayo lakini Imani ya kupokea ni wachache walionayo.



Waebrania 11:6 ''Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.''

Pasipo hauwezi kumpendeza MUNGU, Je imani yako inaishia tu kwenye kuomba au hata kwenye kupokea unaimani.

 Nisikilize kwa makini itakusaidia.
Vitu vinavyoihitaji imani ya kupokea vinavyoweza kumfanya mtu asipokee hata kama ameomba kwa imani sana.

1. Kuwadharau watu wa MUNGU.

Unaweza ukaomba kwa imani sana na MUNGU akakujibu. Kumbuka MUNGU hutumia watu hivyo kuna baadhi ya watu MUNGU anaweza akawapa jibu lako lakini kwa kuwadharau hakika hawatakupa na utakuwa umekosa baraka yako.
Mfano ni huu, Mtu mmoja alikuwa ameomba kazi kwa muda mrefu na hakupata kazi. Mtu huyu alikuwa naomba kwa imani sana lakini tatizo lake lilikuwa ni kuwadharau watu asiowajua.
Siku moja mama mmoja aliyeonekana wa kawaida tu alimsaidia katika mazingira ambayo ni neema ya MUNGU tu. Mama yule anafanya kazi katika idara ambayo inahusika na uajiri serikalini, akamwambia yule kijana ''nakuona kama unauhitaji wa kazi'' Kesho njoo kazini kwangu na vyeti vyako nami nitakuunganisha na mtu anayehusika na kuajiri.
Yule kijana alipoenda kwa yule mama alipata kazi siku ile ile maana ana elimu nzuri. Baadae alianza kujilaumu kwanini hakumheshimu yule mama miaka miwili nyuma na angeshapata kazi zamani.
Ndugu imani ya kupokea inakuhitaji sana kuwaheshimu watu wote, Kutokuwaheshimu watu kunaweza kukukosesha baraka zako hata kama umeomba kwa imani, kama baraka hizo MUNGU atazipitisha kwao hakika itakuwa ngumu wewe kuzipata maana una roho ya dharau.
Biblia inakushauri hivi.

Waebrania 13:1-2 ''Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.''

 
2. Kuwa na roho ya kiburi.

Kiburi kina madhara mengi sana na hata katika maombi kiburi kinaweza kuwa kikwazo kikubwa sana pia.
Mtu mmoja alielekezwa kwa ufunuo kwamba aende akamuone mchungaji mmoja wa kawaida sana ili amwombee na atafanikiwa.
Yule ndugu anatoka Kanisa kubwa na kanisa la mjini lenye maelfu ya watu na kuna wachungaji wazuri sana lakini kwa maombi alielekezwa kwenda kwa mchungaji ambaye wala sio maarufu. Alikaa siku kadhaa bila kwenda na hakufanikiwa katika hitaji lake. Aliomba sana na alifunga sana lakini majibu ya mahitaji yake yaliunganisha na Mchungaji wa kawaida kabisa, nadhani MUNGU alikuwa anataka kuiua roho ya kiburi ndani yake.
Alipoamua kwenda kwa Mchungaji yule hakika alistaajabu maana Mchungaji mwenyewe suti ina viraka na mazingira wala sio mazingira mazuri. Yule kijana alijieleza kwa yule Mchungaji na Mchungaji akamwombea na kumwambia asikubali kuwa na roho ya kiburi. Wakati anatoka tu kwa Mchungaji yule alipigiwa simu kutoka Ofisi tatu ili kesho yake akaanze kazi. Yule ndugu alikuwa ameshapeleka maombi ya kazi maeneo mengi na hakufanikiwa na wengine waliishia kumtukana lakini baada ya maombi ya mchungaji yule ilibidi sasa yeye ndio achague sehemu ya kufanya kazi maana sehemu tatu zote walimhitaji  kwa kumbembeleza kabisa kwamba kazi ipo tayari.
Tunajifunza nini?
roho ya kiburi ni machukizo kwa MUNGU na roho hiyo inaweza kukufanya usipokee baraka zako hata kama uliomba sana kwa imani. 
Majibu yako uliyomuomba MUNGU yanaweza kumwekwa kwa watu fulani wa MUNGU, ukiwafanyia kiburi watu hao hakika unaweza kukosa baraka hiyo uliyoomba kwa imani ili uipate, hutakiwi kuchagua watu wa kuwaheshim bali waheshimu wote na usikubali kuwa na kiburi kwa yeyote.
Hebu Jifunze kitu hapa kwamba Ili rafiki za Ayubu wasamehewe na MUNGU sharti waende kwa Ayubu ili awaombee kwa MUNGU.

Ayubu 42:7-8'' Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.''

Unaweza kujiuliza swali kwamba MUNGU kwanini hakuwasamehe tu hawa marafiki watatu wa Ayubu kipindi anasema nao?
MUNGU naamini angeweza kuwasamehe kipindi anaongea nao lakini MUNGU akawaambia kwamba waende na sadaka  nzuri kwa Ayubu na atakapoomba Ayubu ndipo MUNGU atajibu na kuwasamehe. Ni Kanuni ngumu sana kwa mtu mwenye roho ya kiburi.
Watu wale watu wangemdharau Ayubu wasingesamehewa na MUNGU. Hata wewe unaweza kuwadharau watu fulani kumbe MUNGU amepitisha kwao baraka yako ambayo umeomba kwa MUNGU.
 
4. Kujiona unaweza na huhitaji msaada.

Rafiki yangu mmoja ni mtumishi wa MUNGU mwenye upako, yuko Morogoro.
Katika ndoa yake walikaa miaka minne bila kupata mtoto, waliomva sana na waliombewa sana hadi wakachoka na kutulia tu.
Siku moja kanisani kwao alikuja Mchungaji kutoka Malawi, yule Mchungaji alikuwa anapita tu eneo hilo lakini kutokana na muda akamua kuabudu kanisi kwa huyo mtumishi rafiki yangu. 
MUNGU akasema na yule Mtumishi wa Malawi na katikati ya ibada akamwambia yule mtumishi rafiki yangu kwamba MUNGU atampa uzao. Baada ya Ibada yule Mtumishi rafiki yangu akamkaribisha yule Mchungaji wa Malawi na Yule Mchungaji aliwaombea yeye na mkewe na kuwaambia kwamba ''Mwakani majira kama haya mtakuwa na mtoto wa kiume'' baada ya maneno hayo yule Mchungaji wa Malawi alimwambia rafiki yangu kwamba aende Kanisani na akatoe sadaka ya Shukrani kwamba MUNGU amempa Mtoto. Yule Mchungaji wa Malawi akaondoka na kuendelea na safari yake ya huduma. Ni kweli baada ya Mwaka walikuwa na mtoto.
Mtumishi huyu alikuwa anaombea watu sana na alikuwa yuko vizuri lakini hitaji lake la uzao MUNGU aliweka kwa Mchungaji wa Malawi na alipoomba yule hakika utasa ulifutika.
Watumishi hawa walikuwa na uwezo wa kujihesabia haki kwamba watajiombea wenyewe lakini kwa kumwelewa MUNGU kwamba hutumia watumishi wake hakika walipokea.
 Biblia inasema 
Mithali 3:7 '' Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.''


Unaweza ukajiona unaweza yote na huhitaji msaada wa mtu yeyote lakini  Majibu ya maombi yako kwa MUNGU yanaweza kuja kwa njia nyingi na njia zingine zikikutaka kuwaomba ushauri watu wengine.
 1 Kor 10:12 ''Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke''

 Siku moja rohoni kwangu nilijikuta nimegundua kwamba mchungaji fulani rafiki yangu yuko kwenye hali ngumu. Sikuambiwa na mtu , nilikosa raha na jambo hilo likasababisha nimpigie simu Mchungaji yule, akaniambia tangu asubuhi hawajala chakula chochote  na muda huo ilikuwa Saa 11 jioni hakika niliamua kununua mchele na nyama na kumpelekea.
Mchungaji yule bila kumwambia hitaji langu lakini aliniombea jambo lililotimia haraka na ajabu sana. Niligundua kwamba kwenye kupokea hitaji langu nilitakiwa kumbariki mtumishi wa MUNGU na maombi yake yangekata utebe wa baraka yangu ili niipate na nilipata hakika.
Imani ya kupokea ni muhimu sana.

MUNGU anasema ''Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.-Waebrania 10:38''


Ni muhimu sana kuomba na ni muhimu sana kuwa na na maombi ya kufunga lakini Imani ya kupokea nayo ni muhimu sana.
Unafunga kwa sababu unamtaka MUNGU na nguvu zake na mapenzi ya MUNGU
-Wengine wanafunga ili waonekane wa kiroho zaidi.
-Watu wengi hawawezi kufunga kwa ajili ya wengine.

=Funga ambayo MUNGU anaitaka ni ile ya kuutafuta ufalme wake 

Kubarikiwa Wakati Mwingine Kunaleta Kiburi Kwa Huyo Aliyebarikiwa. 
Ni Muhimu Kuwa Makini Sana.
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments