KANISA LISILOONEKANA NA KANISA LINALOONEKANA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Shalomu Mteule wa MUNGU upendwae sana na MUNGU BABA.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kanisa ni mwili wa KRISTO na KRISTO ndio kichwa cha kanisa.
Ukiangalia Kamusi ya Kiswahili utaona Maana mbili za Neno kanisa.
1. Kanisa ni jumuia ya wakristo.
2. Kanisa ni jengo linalotumiwa na wakristo kufanya ibada.
 
Kibiblia Neno  KANISA maana yake ni  “kusanyiko” au “walioitwa.” hii ndio maana kuu ya Kanisa ambayo kila mwanadamu anatakiwa kufahamu.
Maana ya Kanisa Kibiblia  sio  jengo, bali ni watu. 
Hebu ona mfano huu ambao Mtume Paulo anasema ''Nisalimie Kanisa lililomo katika Nyumba''
 Warumi 16:4 '' waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia; NISALIMIENI NA KANISA LILILOMO KATIKA NYUMBA YAO ''
Unapoona Kanisa liko kwenye Nyumba maana yake Kanisa sio jengo bali ni watu. 
Ndani ya watu ambao ni Kanisa anatakiwa kukaa ROHO wa MUNGU.
1 Kor 3:16 ''Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la MUNGU, na ya kuwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu?  ''
ROHO MTAKATIFU hakai katika jengo bali anakaa katika Moyo.
Hivyo akikaa kwenye hekalu maana yake kwenye moyo wa mteule wa KRISTO anayeishi maisha matakatifu.
Kanisa lipo kwa ajili ya KRISTO. 
Kanisa linatakiwa liwe chini ya mamlaka ya KRISTO na sio vinginevyo.
Waefeso 1:20-23 ''aliotenda katika KRISTO alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya KANISA; ambalo ndilo MWILI wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote. ''

YESU KRISTO ndiye kichwa cha Kanisa la MUNGU.
Hakuna anayeweza kuondoa kichwa katika mwili kisha akaweka kichwa kingine harafu ule mwili ukawa hai.
Kanisa bila kusimama katika kweli ya KRISTO haliwezi kuwa kanisa hai la MUNGU.
Anayelidharau Kanisa hai la MUNGU huyo anakuwa pia anamdharau KRISTO ambaye ndiye mwenye kanisa. Na kumdharau KRISTO ndio kumdharau MUNGU, na kumdharau MUNGU ni kujipeleka mwenyewe katika ziwa la moto. Kanisa la MUNGU lazima lisimame katika nafasi yake daima. 

Ubarikiwe wewe uliyeokoka na Ubarikiwe sana wewe unayemwabudu MUNGU Baba katika ROHO na kweli.
Kwa Uchunguzi wangu mimi Peter Mabula ni kwamba Neno ''Kanisa'' katika Biblia  linapatikana zaidi ya mara mia na limeandikwa Mara nyingi zaidi katika vitabu hivi; Waraka wa kwanza wa Wakorintho, Matendo ya mitume na  kisha Ufunuo wa Yohana.
Kwanini maana ya Kanisa Kibiblia ni ''Walioitwa'' au ''Kusanyiko''?
 Naweza nikasema hivi. Kanisa ni walioitwa kutoka katika dhambi na sasa wanaokolewa na Bwana YESU ndipo wanakuwa Kanisa hai la MUNGU.
Kanisa ni kusanyiko wa wanaomtii KRISTO na kutimiza kusudi la MUNGU la Wokovu.
Lakini maneno hayo ya ''Walioitwa'' na ''Kusanyiko'' yana msingi Katika Kanisa la kwanza.
Kanisa la Kwanza ni Waisraeli walipookolewa na MUNGU kutoka utumwani Misri na kuanza safari ya Kaanani.
Kanisa pia linasafiri kwenda mbinguni.
Hayo tunayajuaje ya kwamba Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri ndio walikuwa Kanisa la Kwanza?
Matendo 7:37-38 ''Musa huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, BWANA Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye. Yeye ndiye aliyekuwa katika KANISA jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi.'' 

Bwana YESU ndiye aliyetabiriwa na Musa pamoja na manabii wote ya kwamba yeye ndiye Mwokozi na zaidi yake hakuna Mwokozi mwingine.
 YESU KRISTO Ndiye Pekee Rafiki Wa Kweli Maana Atakuwa Na sisi Kanisa lake  Hadi Ukamilifu Wa Dahari.
Mathayo 28:19-20 '' Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. ''
Ni heri sana kuwa na rafiki huyo mwenye uzima wa milele.
 Ndugu Achana Na Hao Marafiki Wazinzi Na Ambao Urafiki Au Uhusiano Wenu Utaishi Tu Kaburini.


Baada ya hayo  sasa naingia katika kiini cha somo langu.
Nielewe kwa makini sana itakusaidia.
Kuna aina mbili za Makanisa.

KANISA LINALOONEKANA.


Kanisa linaloonekana ni kanisa la mahali ambamo watu hukutanika na kujifunza Neno la MUNGU. 
1 Kor 11:18 ''Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; ''
Anaposema kwamba ''Mkutanikapo Kanisani'' Maana yake hapo kanisani ni kwenye jengo la Kanisa, ambalo nalo linaitwa Kanisa, Hivyo Kanisani linaloonekana linaweza kuwa jengo pia.
Ninaposema Mfano kwamba mimi nasali PAG au EAGT au KKKT au ANGLIKANA n.k hayo ni makanisa yanayoonekana ila hayawezi kuamua kuingia uzima wa milele kwa mtu.
MUNGU hana madhehebu maana madhehebu ni mipango ya kibinadamu tu lakini pia ni muhimu sana tujue kwamba madhehebu yanayohubiri kweli ni ya muhimu sana sana.
Madhehebu ni mwamvuli wetu tu wa kutufanya tuutangaze ufalme wa MUNGU.
Madhehebu yanasajiliwa na serikali na sio na MUNGU.
Kanisa linaloonekana linaweza kuwa jengo ambamo watu hukutana kumwabudu MUNGU.
Kanisa linaloonekana wanaweza kuwa ni wakristo katika jamii zao zote.
Tena kanisa linaloonekana ni dhehebu ambalo limeundwa na kutumia kanuni ya imani na katiba  huku muongozi ukiwa neno la MUNGU.
1 Kor 4:17 '' Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika BWANA, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.'' 
Inaposemwa ''kila Kanisa'' Maana yake sio kanisa moja tu bali ni makanisa mengi ya sehemu tofauti tofauti.
 Hivyo wewe ambaye ni muumini wa Kanisa fulani au dhehebu fulani, wewe unasali Kanisa linaloonekana lakini naomba ujue kwamba huwezi kuingia uzima wa milele kwa sababu tu wewe ni mshirika wa Kanisa hilo au dhehebu hilo.

Mathayo 16:18 '' Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. ''
YESU alisema atalijenga Kanisa lake lakini ni vyema tukatambua kwamba Kanisa la YESU sio majengo wala madhehebu bali ni watu waliompokea Kama Mwokozi wako na wanaishi maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye.
 

                   KANISA LISILOONEKANA.
 
Kanisa lisiloonekana ni muunganiko wa wateule wote ulimwenguni ambao wana sifa za kuingia katika uzima wa milele.
Tumeitwa katika makanisa yote mawili yaani Tumeitwa katika kanisa linaloonekana na kanisa lisiloonekana. Neno la MUNGU tunajifunza katika kanisa linaloonekana lakini matendo yetu ndiyo yatakayotufanya tuwe kanisa lisiloonekana ambalo linangoja kunyakuliwa na Bwana YESU.
Mathayo 5:8 ''Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU.'' 
Wenye Moyo safi ndio wateule wa KRISTO waliookoka na wanaishi maisha matakatifu.
Usafi wao huanzia hapa,  '' Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.-Warumi 10:9''
Tukio la kumpokea YESU kama Mwokozi huambatana na toba ya kweli.
Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;''
 Kumpokea YESU kuna umuhimu gani?
Biblia ina majibu sahimi mno, Inasema
 '' Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.-1 Yohana 1:5-10 ''
Kwa maneno hayo tunagundua kwamba kumbe Kuokoka ndio mwanzo wa kumwabud MUNGU katika kweli yake.
 Biblia hailiachi hewani tu Kanisa la MUNGU lisiloonekana ambalo ni mteule mmoja mmoja bali Biblia inatoa hata majibu ya baada ya Kanisa kuchakuliwa na siku ya mwisho kuisha.
Biblia inatoa uhakika huu baada ya mwisho wa dunia.
 ''Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha MUNGU na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia;  nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao. Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa BWANA Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele.-Ufunuo 22:3-5 ''
Ninachoweza kukuambia ndugu ni kwamba, usikubali tu kubaki kanisa linaloonekana bali fanyika kanisa lisiloonekana ambalo ni watakatifu watimilifu wa MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele.
Usikubali tu kuwa mshirika wa dhehebu fulani au mshirika wa kanisa fulani bali fanyika mtakatifu timilifu ndio utakuwa Kanisa hai la MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele.
Kumbuka Kanisa lisiloonekana ambalo ni watakatifu wa KRISTO wote popote waliko ndilo litanyakuliwa na sio madhehebu wala majengo na makanisa.
Ili ufanyike Kanisa hai la MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele ni lazima uachane na machukizo yote ''1 Thesalonike 1:9 Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia MUNGU mkaziacha sanamu, ili kumtumikia MUNGU aliye hai, wa kweli;''
 Kumbuka Kanisa hai la MUNGU litanyakuliwa.
1 Thesalonike 4:16-17 ''Kwa sababu BWANA mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika KRISTO watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki BWANA hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na BWANA milele.''
Kwanini nimesema litakalonyakuliwa ni Kanisa lisiloonekana na sio kanisa linaloonekana?
Ni kwa sababu Kanisa lisiloonekana sio dhehebu.
Ni kwa sababu Kanisa lisiloonekana sio jengo.
Ni kwa sababu Kanisa lisiloonekana sio makanisa haya tunayoyafahamu na kuyataja sana.
Ni kwa sababu Kanisa lisiloonekana sio kuwa tu sehemu ya kusanyiko fulani la dini.
Kanisa lisiloonekana ni wateule wa KRISTO waliookoka na wanaishi maisha matakatifu katika yeye huku wakimwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli.

Mambo haya 7 muhimu sana kuhusu Kanisa naomba uyajue.

1. Kanisa litakalonyakuliwa ni lile kanisa lisiloonekana yaani kila mteule wa KRISTO anayeishi maisha matakatifu haijalishi anasali local church ipi au  Dhehebu gani.

2. Kuna watu hudhani kwamba dhehebu lao tu ndilo watakaoingia uzima wa milele hivyo ukiwa nje na dhehebu hilo wewe huhusiki na uzima wa milele. huo ni uongo wa mchana peupe. Halitachukuliwa dhehebu hata moja ila atachukuliwa mtu binafsi anayeishi kwa kumtii KRISTO na neno lake, Huyo Mteule ndiye Kanisa lisiloonekana.

3. Tumeitwa katika makanisa yote mawili yaani Tumeitwa katika kanisa linaloonekana na kanisa lisiloonekana. Neno la MUNGU tunajifunza katika kanisa linaloonekana lakini matendo yetu ndiyo yatakayotufanya tuwe kanisa lisiloonekana ambalo linangoja kunyakuliwa na Bwana YESU.

4. Kuna makanisa yanayoonekana ambayo mafundisho yao kama muumini akiyashika na kuyatii yanaweza kumfanya asiwe katika kanisa lisiloonekana hivyo kuikosa mbingu mpya.
Usiridhike tu kuwa mwana kanisa fulani bali hakikisha kanisa hilo au dhehebu hilo wanafundisha Kweli ya KRISTO katika kanuni ya Biblia.

5. Ni muhimu sana kila mtu akawa katika kanisa linaloonekana maana katika kanisa linaloonekana ndiko tunakopata kila kitu cha ki-MUNGU na huko ndiko tunakojua lipi tufanye ili tumpendeze MUNGU wa mbunguni.
Kwa hiyo usikubali kukaa bila kuwa na sehemu ya kuabudu.

6. Sio kila kanisa linaloonekana ni kanisa sahihi mtu kwenda. maana kuna mafundisho mengine ni kinyume kabisa na KRISTO mwenyewe hivyo ukiyashika sana utakuwa sio mhusika wa kanisa lisiloonekana na kukosa uzima wa milele.

7. Sio kila aliye katika kanisa linaloonekana ni mhusika wa kanisa lisiloonekana ambalo ni jumuiko la watakatifu wote.

Baada ya hayo naomba niseme yafuatayo.
Kanisa la MUNGU tunatakiwa tuwe wamoja na tunie mamoja, maana huo ndio mpango wa MUNGU kwetu.
Biblia inasisitiza tuwe na nia moja na nia hiyo ni nia ya jinsi ya KRISTO na tupange mipango ya injili katika umoja na tuitekeleze mipango hiyo katika umoja na kupatana nia zetu.

Warumi 12:16-18 ''Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili. Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.''
Nia ni kitu cha muhimu sana.
Nia ni dhamira ya kukamilisha jambo.
Nia zetu katika kazi ya MUNGU tukiwa pamoja tutafanikiwa sana.
Kanisa halitakiwi kuwa na nia nyingine ila kutangaza ufalme wa MUNGU.
Madhehebu ni mwamvuli wetu tu  wa kutufanya tuutangaze ufalme wa MUNGU, ni lazima tuwe na nia moja ndipo tutafanikiwa.
Kanisa halitakiwi kulipa uovu kwa uovu bali kazi ya kanisa ni kufanya mema machoni pa watu wote.


Katika Kanisa la Leo mimi Binafsi naona  wakristo makundi  mawili.
1. Kikundi cha kwanza kinaitwa waenda kanisani au wahudhuria kanisani.
Hawa  ni wakristo wa kawaida tu.
Wanachanganya ukweli na uongo.
Wanachanganya dhambi na utauwa wa muda tu.
Hunywa pombe, huenda kwa waganga wa kienyeji, wanatumia mizimu ya ukoo, huoa wake zaidi ya mmoja, wanashika baadhi tu ya siku huku hawataki wokovu.
Hubadili Kanuni ya Biblia na hujitungia uongo. 
Husujudia sanamu, huabudu vitu au waanzilishi wao wa madhehebu yao.
Hawamhitaji ROHO MTAKATIFU.
Huwamini zaidi waanzilishi wa madhehebu yao kuliko hata KRISTO.
Wametekwa wakati mwingine na elimu ya uongo hivyo humwacha YESU.
hulipa kisasi n.k

2. Kikundi  cha pili Kinaitwa waliozaliwa mara ya pili Kwa maji na kwa ROHO(Yohana 3:5).
 Hawa huhudhuria kanisani na kulifanyia kazi Neno la MUNGU walilofundishwa.
Wameokoka na wanaenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Ni watakatifu wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
Ndugu hakikisha unafanyika mteule wa KRISTO unayeishi maisha matakatifu na uko tayari kwa ajili ya uzima wa milele.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments