KANUNI 10 ZA KIONGOZI WA KIROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunazungumzia Kanuni za uongozi wa kiroho ambapo kila Mkristo ni kiongozi wa kiroho anayetakiwa kuwaongoza watu kumpendeza MUNGU.
Kanuni za kiroho ni nini?
 Kanuni za kiroho ni taratibu, nguzo au masharti anayotakiwa kuyazingatia kiongozi wa kiroho ambapo taratibu hizo zina msingi katika Neno la MUNGU.
Kanuni za kiroho kwa maana nyingine tunaweza kusema ni taratibu ambazo hazina budi kufuatwa katika mambo ya kiroho.
Kiongozi ni nani?
Kiongozi ni mtu anayesimamia na kuelekeza watu au kikundi cha watu kazi fulani.
Kiongozi ni mtu mwenye madaraka juu ya wengine katika kiukundi au kazi fulani.
Marko 10:42-44 '' YESU akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.'' 
Wakuu wa mataifa maana yake viongozi wasio wa kiroho yaani watawala katika maeneo mengine nje na kanisa la MUNGU.
MUNGU anasema kwamba anayetaka kuwa kiongozi katika kazi ya MUNGU basi inampasa huyo kuwa mtumishi wa wote.
Anayetaka kuwa kiongozi katika kazi ya MUNGU anatakiwa kutumika kuliko wote.
Kuna kanuni za uongozi wa kiroho ambazo mhusika anatakiwa azizingatie ila kumletea MUNGU matunda mema.

                 Kanuni za kiongozi wa kiroho.

1. Kuishi maisha matakatifu ya Wokovu na kuwaelekeza watu kuishi maisha matakatifu.

1 Petro 1:15 '' bali kama yeye(MUNGU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''
Maisha matakatifu sio ya kujipangia tu bali maisha matakatifu yameelekezwa katika Biblia.
Maisha matakatifu kwa mtu yeyote huanza kipindi anampokea YESU kama Mwokozi wake kisha anaanza kuishi kwa kulifuata Neno la MUNGU.
Kiongozi ni kielelezo hivyo anatakiwa awe kielelezo katika kuishi maisha matakatifu.
Kama kiongozi akiwa mlevi hakika jamii nzima itamshangaa, hadi vyombo vya habari vitaandika maana ni ajabu hiyo.
Kiongozi wa kanisa anatakiwa awe anatumia akili sana katika maongezi yake na kauli zake maana yeye ni kielelezo.
MUNGU anataka viongozi wa kanisani tuwe vielelezo katika kuishi maisha mema na matakatifu.
Kazi nyingine muhimu ni kuwafundisha watu kuishi maisha matakatifu.
Tutakuwa na ujasiri wa kuwafundisha watu utakatifu kama tu na sisi tunaishi maisha matakatifu.
Kumbuka jambo la muhimu kujua ni kwamba mafundisho yako yanatakiwa kwanza yakuhubiri wewe unayehubiri kabla ya wengine, hivyo yakupasa sana kuwa kielelezo katika utakatifu.
 Kuwafundisha watu kuishi maisha matakatifu inatakiwa kuwa kanuni ya kiongozi ya siku zote.
Ukiwafundisha watu baraka ni kweli watabarikiwa lakini kama hawana utakatifu utakuwa hujawasaidia kwa lolote.
Ukiwafundisha watu upendo ni kweli watakuwa na upendo lakini kama hawana utakatifu hakika utakuwa hujawasaidia kwa lolote.
Ukiwafundisha watu kuhusu vyakula ni kweli watatii lakini kama hawana utakatifu hakika utakuwa hujawasaidia lolote.
Ukiwafundisha watu utakatifu hakika na mengine yote mema yatawapata maana utakatifu katika KRISTO ni njia inayotengeneza baraka na mafanikio kiroho na kimwili na mwisho ni uzima wa milele.
Hivyo utakatifu ndilo jambo la muhimu kuliko yote kulifundisha katika kanisa la MUNGU.

2. Kuweka hazina mbinguni.

 Luka 12:32-34 ''Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu. ''
Kuweka hazina mbinguni ni jambo la kila mmoja na sio waumini tu.
Kiongozi unatakiwa uwe mfano mzuri katika kuweka hazina mbinguni.
Hazina mbinguni zinawekwa kwa;
=Matoleo safi.
=Maisha mema na ya haki.
=Utumishi wa kweli na kutimiza kila kusudi la MUNGU.
Kiongozi hatakiwi kuwa mtu wa kuwaelekeza tu wengine ili waweke hazina mbinguni huku yeye hazina zake akiweka duniani kwa ujinga wake.
Kuweka hazina mbinguni ni faida ya kila mteule wa KRISTO hivyo haijalishi ni kiongozi au sio kiongozi ni muhimu sana kuweka hazina mbinguni.
Ilipo hazina yako ndipo na roho yako itakuwa, je kama kiongozi huna hazina mbinguni roho yako itakuwa wapi?
Kama mtu wa mfano kiongozi wa kanisa anatakiwa sana kuweka hazina mbinguni kila siku.
Ufahali wa duniani utaishia duniani hivyo yatupasa sana kuweka hazina zetu mbinguni.
Kuweka hazina zetu mbinguni ni kutanguliza kabisa vitu vyetu mbinguni. Kwa anayetarajia kwenda mbinguni awe ni kiongozi au asiwe kiongozi yampasa sana kuweka hazina mbinguni.
Hazina yako ya mbinguni ndio nyumba yako ya mbinguni siku ukifika huko, kama huna nyumba mbinguni unadhani utaenda huko mbinguni?

3. Maneno yako yathibitishwe na matendo yako.

 Mathayo 5:36-37 '' Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.''

Kama kiongozi ni muhimu sana ukajua kwamba unaangaliwa na kila mtu kama mfano.
Ukijikwaa katika maneno yako au matendo yako tambua kwamba unapunguza watu wa kukuamini.
Ukisema uongo hiyo ni dhambi na inakupunguzia watu wa kukuamini.
Maneno yako yanatakiwa yathibitishwe na matendo yako.
Sio unafundisha upendo katika ndoa huku wewe mwenyewe huna upendo katika ndoa yako.
Sio unafundisha utakatifu huku wewe mwenyewe wala huishi maisha matakatifu.
Kiongozi unatakiwa sana kuwa na hofu ya MUNGU katika mambo yote.
Usiongee kuwafurahisha jamii tu au serikali bali ongea kumfurahisha MUNGU katika kweli.
Kanisa linaweza likatukanwa kwa sababu wewe kiongozi humtii MUNGU.

4. Kumtumikia MUNGU kwa usahihi katika mambo yote.

 1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

Kumtumikia MUNGU kwa usahihi kunaanzia katika Kumwabudu katika Roho na kweli.
Kumtumikia MUNGU ni kutimiza agizo la MUNGU la wewe kuokoka na ni kutimiza pia agizo la MUNGU la wewe kuwa kiongozi Kanisani.
=Ni muhimu sana kiongozi wa kanisani kila wakati kujiuliza ''MUNGU anataka nini'' akijua kile atakacho MUNGU basi amtii MUNGU katika hayo.
=Tunamtumikia MUNGU kwa;
A. Kumwabudu katika kweli.
B. Kuwaongoza wengine katika kweli ya Injili ya KRISTO.
C. Kumtolea matoleo pamoja na sisi wenyewe kuitoa Miili yetu sadaka kwa MUNGU ili tutimize mpango wake MUNGU wa kuwapo kwetu duniani.


5. Kumtii MUNGU BABA, YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU.

Umekuwa kiongozi wa kirohoni kwa sababu ni MUNGU amekupa nafasi hiyo kanisani, usipomtii MUNGU hakika wewe hujitambui.
Ni lazima kiongozi wa kanisa akamtii MUNGU katika mambo yote.
Mtendo 5:29 ''Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.'' 
Mitume kama vielelezo kwetu, wao waliamua kumtii MUNGU kuliko wanadanamu.
Hivyo kila kiongozi wa kanisani ni lazima amtii MUNGU na sio vinginevyo.
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''

Jambo jingine muhimu kujua ni kwamba Kanisa ni mali ya KRISTO, ukijitenga na KRISTO maana yake umejitenga pia na MUNGU na umejitenga pia na uzima wa milele.
Kuna viongozi kwa kupotoka hutangaza kwamba wanamtii MUNGU wakati huo huo hawamhitaji Bwana YESU wala ROHO MTAKATIFU. Hao hawajitambui na hawajui kwamba MUNGU hayuko upande wao.
Ukishajua kwamba Kanisa ni la KRISTO hakika unatakiwa kumtii YESU KRISTO katika mambo yote.
Yohana 3:17-18 '' Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''
Usipomtii YESU KRISTO moja kwa moja wewe unahama kutoka kuwa mtumishi wa MUNGU na unakuwa mtumishi wa shetani.
2 Yohana 1:8-9 '' Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye CHEO, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba(MUNGU) na Mwana(YESU) pia. '' 
Jambo muhimu sana kujua pia ni hili; ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu kuliko vyote katika maisha ya kila Mkristo akiwemo na kiongozi wa kiroho.
Bila ROHO MTAKATIFU huwezi kumpendeza MUNGU.
 Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
ROHO MTAKATIFU anatakiwa awe kiongozi wa kiongozi wa Kanisa.
Ukijitenga na ROHO MTAKATIFU wewe unakuwa umeanza kuuchoka uzima wa milele.
Usipomtii ROHO MTAKATIFU maana yake humtii pia YESU na kwa jinsi hiyo humtii MUNGU.
Usipomtii MUNGU wewe sio mtumishi wake.

6. Kuachana na dhambi, kuichukia dhambi na kuikemea dhambi yoyote popote.
Zaburi 34:13-14 ''Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
Kiongozi hatakiwi kuwa mdhambi.
Kiongozi anatakiwa kuichukia dhambi na kuwafundisha watu kuichukia dhambi.
Kiongozi anatakiwa kuikemea dhambi popote pale.
MUNGU anawatarajia viongozi wa kanisa kuikemea dhambi kwenye jamii na hata serikalini. MUNGU anasihi kwa vinywa vya watumishi wake hivyo viongozi wanatakiwa kuikemea dhambi yeyote.
Kama ushoga umekubaliwa katika taifa fulani harafu viongozi wa kanisa wanachekelea jambo hilo, hakika hao hawajitambui hata kidogo.
Kama rushwa imekuwa jambo la kawaida katika taifa na hakuna kiongozi wa kiroho anakemea dhambi hiyo, hiyo haifai kuwako katika viongozi wa kanisa.

7. Kiongozi wake ni Neno la MUNGU yaani Biblia na wajibu wake alitumie Neno la MUNGU kwa halali katika mambo yote.
2 Timotheo 2:15 '' Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. ''
Kila kiongozi wa kiroho duniani ana kiongozi wake pia, na kiongozi huyo ni Neno la MUNGU.
Zaburi 119:105 '' Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.'' 
Ni vyema sana kulitumia Neno la MUNGU kwa halali.
Ndani ya Neno la MUNGU yuko MUNGU, Yuko YESU KRISTO na yuko ROHO MTAKATIFU.
Maana mojawapo ya Neno kiongozi kwenye Kamusi  ni kwamba Kiongozi ni Kitabu chenye maelezo ya Namna ya kufanya jambo fulani, Hivyo Biblia ni kiongozi wa kiongozi wa kiroho.
Kiongozi wa kiroho ni lazima sana na yeye amtii kiongozi wake mkuu ambaye ni Neno la MUNGU.
Katika wakati huu Kibiblia ni wakati wa Kanisa au wakati wa Neema na vyote viwili yaani Kanisa na Neema viko ndani ya kitu kimoja tu yaani INJILI YA KRISTO YESU YA UZIMA WA MILELE.
Hivyo Injili ya KRISTO ndilo fundisho analotakiwa kuwa nalo kiongozi wa kanisa.
Tangu YESU hadi Mitume wote walihubiri jambo moja tu ya INJILI YA YESU KRISTO IOKOAYO.
Injili ya KRISTO ndio vazi analotakiwa kulivaa siku zote kila kiongozi wa Kiroho.
Tunaposema kwamba injili ya YESU KRISTO haina maana kwamba tubague tu baadhi ya vitabu vya Biblia lakini tunatakiwa tutumie vitabu vyote vya Biblia lakini katika kusudi la Wokovu wa KRISTO na sio vinginevyo.

8. Kuwa tayari wakati unaofaa na wakati usiofaa.

2 Timotheo 4:1-2 " Nakuagiza mbele za MUNGU, na mbele za KRISTO YESU, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;
lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho."
Kama mtumishi wakati mwingine kuna kuchoka na wakati mwingine kuna kuzongwa na familia na mambo mengine, lakini kwa nafasi zetu kama viongozi wa kiroho ni muhimu sana kuwa tayari katika Nyakati zote ili kuwasaidia watu kiroho na ili wampendeze MUNGU.
-Kiongozi anatakiwa afundishe Neno, Atatue migogoro ya ndoa za waumini wake au watu wa makanisa mengine na hata wapagani.
Watu wengi hata wasiompokea YESU wakipatwa na matatizo basi pa kukimbilia huwa ni kwa watumishi wa MUNGU.
Misiba ikitokea katika jamii viongozi wa Kanisa hutafutwa ili kuongoza ibada za mazishi na kuwatia moyo wafiwa kwa kuwahubiria Neno la MUNGU, Hata nyimbo zinazoimbwa misibani wakati mwingine huchukuliwa watu wa kanisa kwenda kuimba. Jambo la muhimu kujua katika hilo ni kwamba Kiongozi wa Kanisa hatakiwi kufanya ibada za wafu bali kazi yake ni kuwaonya kwa upole walio hai na kuwakumbusha kwamba hata wao ipo siku wataondoka hivyo wanatakiwa kumpokea YESU KRISTO na kuishi maisha matakatifu maana hakuna aijuaye saa yake ya kuondoka, ila kuondoka ni lazima. Kuwaonya wale wanaopanga kuwa wacha MUNGU wakizeeka kwamba mawazo hayo ni ubatili.
Yako mambo mengi sana yanayomhitaji mtu wa MUNGU kama kiongozi kuwa tayari wakati mzuri au wakati mbaya kwake lakini yote hayatakiwi kufanywa kwa kujilazimisha bali kwa upendo wa kiMUNGU huku pia akitumia nafasi hiyo kuwafanya watu wampokee YESU na kuishi maisha matakatifu.
Kiongozi wa Kanisa ni muhimu sana akayazingatia hayo.
Kiongozi wa kiroho hutakiwi kulipa baya, hiyo ndio Kanuni ya kiongozi pia.
Changamoto zipo sana lakini usikubali kulipa baya.
Mtumikie MUNGU kwa moyo na sio kwa kujilazimisha.
Fuata hata ushauri huu wa Daudi kama kiongozi akimuambia Suleimani aliyekuwa katika kuchukua uongozi.
1 Nyakati 28:9-10 '' Nawe, Sulemani mwanangu, mjue MUNGU wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele. Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.'' 
Wewe MUNGU amekuchagua ufanye nini katika kazi yake?
Ndugu itimize hiyo kwa moyo na sio kwa kujilazimisha.
Uwe tayari wakati unaofaa na hata wakati usiofaa.
9. Kuepuka Mapato ya aibu.

 Tito 1:7-9 '' Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno ,kwa kuwa ni wakili wa MUNGU;asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake,asiwe mwepesi wa hasira,asiwe mlevi wala mgomvi,asiwe mpenda mapato ya aibu. bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.''

Biblia imemtaja Askofu kama mmoja wa viongozi katika kanisa na kutaja sifa zake.
Sifa za Askofu ndizo sifa za kila kiongozi wa kiroho kokote aliko.
Askofu maana yake mwangalizi hivyo na wewe ni mwangalizi katika kazi ya MUNGU au idara au kikundi au popote hivyo unatakiwa kuwa na sifa za mwangalizi.
Kuna viongozi wengi katika kanisa la MUNGU walihusika katika mapato ya aibu lakini wewe nakuomba na kukuonya kwa upole kwamba usikubali kuwa kiongozi anayehusika na mapato ya aibu.
Mithali 4:14 '' Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya.''
Mapato ya aibu ni pamoja na;
1. Pesa ya wizi.
wewe uibe au watu waibe na kukuletea ili tu uwasaidie katika mambo yao.
2. Rushwa ni mapato ya aibu.
Kiongozi wa kanisa usikubali kutoa rushwa ama kupokea rushwa.
Kama mnachagua viongozi fulani katika kanisa basi rushwa haitakiwi kuwako, ukikubali rushwa ili uwape watu fulani nafasi katika Kanisa naomba ujue kwamba umepanda mbingili ambazo zitakuchoma wewe mwenyewe na hakuna pia mbingu ya wapokea rushwa.
3. Kuchangisha pesa ili uzitumie kwa mambo yako nje na kusudi la Kanisa.
4. Kudanganya watu kwamba umefunuliwa ili tu wakupe pesa.
5. Kufanya huduma ya MUNGU kwa pesa, mfano kuombea kwa pesa, hiyo ni haramu kwa watu wa MUNGU.
Mathayo 10:7-8 '' Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.''
10. Kanisa ni la MUNGU na sio la kwako kiongozi.

Matendo 20:28 ''Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.'' 
Jambo muhimu sana kujua ni kwamba Kanisa ni la MUNGU na sio la viongozi.
Viongozi ni wasimamizi tu katika Kanisa.
Jitahidi sana kulifanya kanisa ni la MUNGU na sio la kwako.
Msikilize Mwenye Kanisa ambaye ni MUNGU kupitia YESU KRISTO.
Msikilize na kumtii ROHO MTAKATIFU ambaye ndiye msimamizi wa Kanisa la KRISTO Duniani.
Usijipe mamlaka ya kuhukumu watu na kulaaani watumishi wenzako kwa sababu tu wewe unajiona uko juu kuliko wao.
Mtii MUNGU hata wakati umeinuliwa kihuduma.
Waheshimu watu wote na tenda kwa haki kwa kila mtu ambaye MUNGU amemweka chini yako.
Baki ukimtumikia MUNGU mwenye kanisa na sio wewe kutaka kutumikiwa kama mumiliki wa Kanisa.
Kuna maaneno mengine akifika tu Kiongozi wa Kanisa watu wanamuogopa na kumhofu kama kwamba ana mbingu ya kuwapeleka.
Kuna maeneo mengine akitokea tu mtumishi watu wote wanapewa amri ya kusimama na kutulia hadi huyo mtumishi wa MUNGU atawaambia wakae chini, asikasahau kuwaambia kukaa basi watasimama muda mrefu sana, chanzo cha hayo ni misingi mibaya iliyoweka na kanisa ya kuwahofu viongozi na kuwanyenyekea vibaya.
Kiongozi wa kiroho usiweke mazingira ya watu kukuogopa kuliko hata MUNGU.
Usiweke mazingira ya watu kukunyenyekea wewe kuliko YESU.
Nyenyekea kwa MUNGU na mtumikie MUNGU.
Kumbuka andiko tulilianza nalo ambalo linasema
 '' YESU akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.-Marko 10:42-44''
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments