KUHUSU KUINGIA KATIKA NDOA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo ninazungumzia ndoa takatifu.
Ndoa takatifu Inaitwa ndoa takatifu kwa sababu ni takatifu na inatakiwa kuwa takatifu.
Utakatifu wa ndoa huanzia katika katika ucha MUNGU wa wanandoa hao.
Huanzia katika kumcha MUNGU na kutembea kwenye mpango mtakatifu tangu mwanzo wao.
 Biblia inasema
Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."


Kama wateule wa MUNGU ni lazima Yale tuyafanyayo lazima yafanyike katika Bwana YESU aliye MTAKATIFU.

Jambo la Pili ni kwanini ndoa ni takatifu ni kwa sababu Mwanzilishi wa ndoa ni MUNGU na sifa kuu ya MUNGU ni utakatifu.
Marko 10:7-9 " Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha MUNGU, mwanadamu asikitenganishe."


Kwa maandiko hayo tunagundua kwamba ndoa inapaswa kuwa takatifu
Ndoa MUNGU huwa anaihesabu baada ya ndoa hiyo kufungwa.
Hadi ndoa ifungwe hutokea kwanza
1. Uchumba/posa
2. Kutolewa mahali.

Tukumbuke pia kwamba Hakuna Neno uchumba kwenye Biblia ila tukio la kuonyesha uchumba lipo.
Labda tujiulize uchumba ni nini?
Uchumba ni mahusiano ya awali ambayo wawili (mwanamume na mwanamke) ambao bado hawajaingia katika ndoa wanakubaliana kuoana, na hivyo wanaanzisha mahusiano ya awali, katika utakatifu
Lengo ni ili mteule wa MUNGU asiingie pasipositahili.
Kumbuka Biblia inakataza wateule kuoa au kuolewa na wasiomwamini YESU.
2 Wakorintho 6:14-15 " Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya KRISTO na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?"


Zipo pia ndoa ambazo zimefunga katika mazingira njea na Kanisa.
Mfano ndoa za serikalini, mahakamani au za kimila.
Ndoa za mahakamani ni ndoa halali na ndoa za kimila ni ndoa.
Lakini mteule wa MUNGU ni lazima ukakiki ni nini kinampendeza MUNGU.
Biblia inatuagiza kwamba katika yote tuyafanyayo ni lazima tuhakikishe tunampendeza MUNGU
Waefeso 5:10 " mkihakiki ni nini impendezayo BWANA."


Kunahitajika uchunguzi sahihi kabla ya kukubali kuingia katika ndoa na mtu.
 Kuokoka tu ghafla kwa lengo la kuoana nako kunahitaji umakini mkubwa sana maana Mtu anaweza akaokoka ili mfunge ndoa, lakini huyo mtu anatakiwa aokoke ili kuupata uzima wa milele na sio kuokoka ili apate ndoa. Wengi waliokoka ili wapate ndoa, walipozipata ndoa waliacha wokovu maana hawakuokoka ili waende uzima wa milele Bali waliokoka ili wapate ndoa, ni hatari sana
Kuhusu ndoa pia Tukumbuke pia Harusi ni sherehe ya ndoa. Harusi sio ndoa.
Wapo wanaofunga harusi na sio ndoa kwa sababu ya uovu wao.

'' Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu-Zaburi 34:9''

Suala la kuingia katika ndoa linahitaji pia umakini sana.  Usikubaliwa wakuchagulie mke au mume.
Hii ya kuchaguliana haifai.
Inatakiwa mwanaume achague mwenyewe mkewe na mwanamke achague anayepasa kuwa mumewe, sio kuchaguliwa na watu.

1 Kor 7:2 '' Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.''


  Ni muhimu sana kujua pia kwamba ndoa sio tendo la ndoa.
Binti: Kijana asifanye mbinu za kuzini na wewe kisha uone heri tu kuolewa naye hata kama ni mdhambi mkubwa.
Kijana: Binti asikulaghai kuzini nae kisha uone bora tu kumwoa hata kama ni kahaba 


Kama bado hujafunga ndoa nakuomba  endelea kuisikiliza sauti ya MUNGU na kuitii.
Watu wengi hupenda kusikia kutoka kwa MUNGU vile tu wanavyovitaka kuliko wasivyovitaka.
Wengi hupenda kusikia wanavyovitamani kuliko vile wasivyovitamani.
Kuna watu MUNGU akisema nao hudharau na kupuuza kwa sababu tu hawakutaka aliyoyasema, Lakini huyaacha hayo ya MUNGU wakati hayo ndio bora zaidi kwao kuliko Yale wanayoyatamani.

MUNGU anaweza akamwambia binti avunje uhusiano wake na kijana Fulani ambaye anamuona wa muhimu.
Baada ya kuingia katika ndoa ndipo yule kijana anaonyesha uchawi wake, binti anabaki akijuta tu na kulia.

Rafiki yangu mmoja aliambiwa na MUNGU aachane na binti aliyekuwa amemchumbia ghafla, yule kijana aliendelea na binti kisha wakafunga ndoa. Vita vilivyoibuka kwenye ndoa hiyo vimemwacha kijana akilalamika tu na kulia kila siku.
Siku moja kwa hasira alinipigia simu akiniambia kwamba nikisikia amefunga ndoa nyingine nisimwambie chochote maana ni zaidi ya mwaka na nusu hajawahi kukutana kimwili na mkewe ambaye ni wa ndoa na wanalala chumba kimoja.

Ndugu yangu, wewe nakuomba isikilize sauti ya MUNGU na kuitii, hiyo ni faida kwako kubwa sana.
 Mithali 20:22 ''Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee BWANA, naye atakuokoa. ''

Kwa walio ndani ya ndoa agizo la MUNGU ni ndoa iheshimiwe na watu wote kwa kuanza na wanandoa wenyewe.
Waebrania 13:4 '' Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. ''

Usikubali tamaa ndio iwe imekufanya uolewe au uoe.
Watu wengi miili yao ndio inaongoza roho zao badala ya roho kuongoza mwili.
Tulipokuwa hatujaokoka miili ndio iliyoongoza roho zetu, lakini tulipookoka ROHO MTAKATIFU ndio anatakiwa kutuongoza.
ROHO MTAKATIFU yuko tayari kuwaongoza wateule wanaoamua kuongozwa na yeye.
Ndugu usikubali kuongozwa na kuendeshwa na mwili.
Usikubali hata kuongozwa na roho Bali ongozwa na ROHO MTAKATIFU

Mwili ni dhaifu lakini tunashinda na zaidi ya kushinda kwa sababu hatuenendi kwa mwili.
Mwili wako usikufanye uolewe ili kukidhi matakwa ya mwili.
Usikubali kuoa haraka tu ili kuuridhisha mwili wako.
Ukifanya hivyo utaolewa kweli au ukaoa lakini unaweza ukawa sio uchaguzi wa roho yako bali wa mwili wako na unaweza kuangukia katika madhara usipochunga.
 Labda ngoja nikufundishe kitu wewe unayesumbuliwa na tamaa na tamaa hizo zinakufanya sasa utake kuingia katika ndoa bila hata maandalizi wala ushauri mzuri.

                   Jinsi ya kuutiisha mwili.

1. Maombi, hasa maombi ya kufunga.

Mathayo 17:21 ''[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ''
 Maombi ya kufunga yatautiisha mwili wako hata usiandamwe na tamaa chafu zinazoweza kukufanya kuamua maamuzi mabaya ambayo unaweza kuja kujuta baadae.
 
2. Kulisoma, kulitafakari na kulizingatia Neno la MUNGU.

Yoshua 1:8 '' Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. ''
Neno la MUNGU unatakiwa ulitafakari usiku na mchana na kulizingatia sana ndipo utafanikiwa.
 
3. Kuutumia muda wako mwingi zaidi katika mambo ya MUNGU.

1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.'' 

Ukiwa busy kwa MUNGU hakika hutakuwa na muda wa kuwaza machafu na kuyatenda.

4. Kumtii ROHO MTAKATIFU na kuenenda katika yeye.

Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.''

Ukimruhusu ROHO MTAKATIFU akuongoze hakika atakuongoza katika utakatifu na haki, ukimtii yeye wala shetani na hila zake hazitakugusa.

5. Kuambatana na marafiki wema.

Zabui 1:1-2 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.'' 

Marafiki zako wana mchango mkubwa sana katika maisha yako.
Kama ni marafiki wabaya wasio na hofu ya MUNGU watakufanya na wewe uwe mtu usiye na hofu ya MUNGU.
Kama ni marafiki wema watakufanya umche MUNGU na kwa jinsi hiyo unatakiwa uwaepuke sana marafiki wabaya wasio na YESU ndani yao ili wasikupoteze kwa kukuletea vitu vya kuamsha tamaa za mwili wako hata ukamkosea MUNGU.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments