KUTII AGIZO LA MUNGU KUNA FAIDA KUU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Wewe umepewa agizo na MUNGU?
Je unatimiza agizo hilo?
Je unajua faida za wewe kutimiza agizo hilo?

2 Timotheo 4:1-2 " Nakuagiza mbele za MUNGU, na mbele za KRISTO YESU, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;
lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho."


Huwa kuna agizo la MUNGU kwa wateule wote lakini wewe hutakiwi kuliona kama tu agizo la MUNGU kwa wakristo wote, Bali libebe kuwa ni agizo la MUNGU kwako binafsi.
Lizingatie agizo hilo kwa sababu ni package yako binafsi.
Kuna faida nyingi katika kutii agizo la MUNGU kwako.
Faida baadhi katika nyingi zinazotokea baada ya kutii agizo binafsi la MUNGU kwako ni.


1. Utapata thawabu ya MUNGU kutokana na kutii wako.
 Ufunuo  11:18 '' Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi. ''
MUNGU atatoa thawabu kwa watakatifu siku ya hukumu.
Waebrania 10:35 ''Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu.''
Thawabu  ya MUNGU ni malipo mema anayoyapata mtu baada ya kufanya kazi ya MUNGU na baada ya kutii maagizo ya MUNGU.
1 Kor 3:8-9 '' Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na MUNGU; ninyi ni shamba la MUNGU, ni jengo la MUNGU.''


2. Utalindwa na nguvu za MUNGU ili utimize agizo hilo.
Isaya  54:17 '' Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.'' 
MUNGU amesema kwamba urithi wa watumishi wake ni ulinzi. 
MUNGU atakulinda ili utimize kazi aliyokuitia.

3. Agizo hilo linaweza kuwa ndio ufunguo wako wa kufanikiwa katika maisha yako ya kiroho na kimwili.
Kumb 28:1-6 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.'' 
Kumtii MUNGU hutengeneza mlango wa baraka zako.
Kuitii sauti ya MUNGU ni kukaribisha baraka za MUNGU kwako.

4. Utakuwa umefanyika msaada kwa wanadamu wanaohusika katika agizo hilo.
Yakobo 5:14-16 ''Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. '' 
Kumuombea mtu ili aponywe ni njia mojawapo ya kumtumikia MUNGU na jambo hilo litaleta faida kwa waliopona.
Muombaji wewe utakuwa umefanyika msaada mkubwa sana.
Ukisoma kitabu cha waamuzi kwa mfano utaona watu wachache walioitii sauti ya MUNGU na maagizo ya MUNGU na MUNGU akawatumia hao kuokoa taifa zima. Ona mifano ya kina Gedioni na Yeftha jinsi ambavyo walimtii MUNGU na kupelekea waisraeli kutoka utumwani, hiyo ni faida ya kumtumikia MUNGU.
 

5. Utakuwa unanitimiza kusudi la MUNGU la kuitwa kwako.
Wafilipi 2:13-14 ''Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,''
Ukifanya kazi ya MUNGU unakuwa unatimiza kusudi la MUNGU.
Ukitii magizo ya MUNGU unakuwa unatimiza makusudi ya MUNGU ya kuitwa kwako katika Wokovu.

Ni vyema sana kujua kwamba Mawazo ya MUNGU sio mawazo ya mwanadamu.
Ndugu fuata mawazo ya MUNGU na sio mawazo ya mwanadamu.
Kwanini uyafuate mawazo ya MUNGU na sio ya mwanadamu?
Ni kwa sababu
1. Mawazo ya mwanadamu hayana ulinzi.

2. Mawazo ya mwanadamu hayana ukombozi.
3. Mawazo ya mwanadamu hayajakamilika vyema.
4 Mawazo ha mwanadamu yanaweza kupotosha.
5. Mawazo ya mwanadamu yanaweza kuangamiza.
Ni heri sana ukafanyia kazi mawazo ya MUNGU.
Yeremia 29:11 "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho."

Mawazo ya MUNGU yako katika Neno lake, hivyo fanyia kazi Neno la MUNGU na sio maneno ya watu.
Timiza mwito wako katika injili ya KRISTO. 

Ukilisikia Neno la MUNGU, litunze moyoni mwako kisha litii ndipo utafanikiwa, kanuni hiyo iko 
 Kumb 28:1 " Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;"
Faida 4 za ziada zinazotokana na  kuisikia sauti ya MUNGU na kuitii ni hizi;
1. Kuisikia sauti ya MUNGU ni mlango wa wewe kuinuliwa.
2. Kusikiliza sauti ya MUNGU kutakuweka katika nafasi nzuri katika eneo lako kiroho.
3. Uwezo wa kuisikiliza sauti ya MUNGU na kuitii, huo Ni ufunguo kufungua mafanikio yako.
4. Kama hufanikiwi katika jambo Fulani inakupasa sasa uisikie sauti ya MUNGU.
Lakini pia Ni lazima uongozwe na ROHO MTAKATIFU ili uepuke makosa.
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

Baada ya kuitwa katika kazi ya MUNGU ni vyema pia ukayajua haya.
Yatakakiwayo kufanywa na mhubiri wa injili katika kuhubiri injili.
2 Timotheo 4:2 " lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho."
1. Hubiri Neno la MUNGU na sio vinginevyo.
2. Uwe tayari kuhubiri wakati unaofaa na hata wakati usiofaa.
3. Karipia pale panapohitaji karipio.
4. Kemea pale panapohitaji kukemea.
5. Onya watu pale panapohitaji maonyo.
Onya kwa neno la MUNGU na uvumilivu.


Mwisho naomba niseme hivi kwa baadhi ya watu "Enyi mnaokataa Wokovu, mwapotea kwa sababu hamuyajui maandiko wala uwezo wa MUNGU"
Mathayo 22:29 "YESU akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa MUNGU."

Maombi kwa ajili ya marafiki zangu wote wanaosoma masomo yangu na kuzingatia Neno la MUNGU.
  BABA wa mbinguni pokea sifa milele. Nakushukuru kwa ajili ya rafiki yangu huyu. Ee MUNGU naomba umpe uzima na ushindi.
Kila ratiba ya kishetani iliyopangwa juu ya maisha yake na mwili wake, naifuta ratiba hiyo kwa damu ya YESU KRISTO.
Kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO Namkomboa ndugu huyu fahamu zake na mwili wake.
Namkomboa roho yake na nafsi yake na pia mwili wake.
Ninaufunga ukurasa wa kuteswa na sasa Naufungua ukurasa wa ushindi.
Kila mpango wa kuzimu juu yake naufuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila kitu cha kipepo kilichoambatanishwa kwenye jina lake ili kimtese, nakifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Na sasa damu ya YESU KRISTO imuandike huru huyu ndugu.
Katika jina la YESU KRISTO Mfalme wa uzima.
Amen Amen Amen

 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments