MAOMBI YA KUHARIBU ROHO YA MAUTI ILIYOTUMWA MAISHANI MWAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
 Bwana YESU KRISTO apewe sifa ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunazungumzia roho ya mauti ambayo ni silaha kubwa sana ya shetani anayoitumia kuwaharibia watu wa MUNGU.

Roho ya mauti ni roho ya uharibifu ya kipepo.

Neno Mauti Kibiblia limetumika katika mambo matatu au maeneo matatu.

1. Kuna mauti yaani mwili kutengana na roho.

Kila mwanadamu atakufa kifo hiki cha mwili kutengana na roho.
Ayubu 14:1-2 '' Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.''

Hii inaitwa mauti ya kwanza ambayo kila mwanadamu itamuhusu.
Ukisikia kuna mtu amefariki maana yake roho yake na mwili wake vimetengana.
Kifo hiki kinapotokea kwa mtu kinaweza kikawa ni mpango wa MUNGU baada ya muda wa mwanadamu kuishi duniani kuwa umeisha kulingana na ratiba ya MUNGU.
Lakini pia kifo hiki kinaweza kumpata mtu kutokana na mipango ya wanadamu au ya mawakala wa shetani. Ndio maana MUNGU anawakataza wanadamu wote wasiue.
Kutoka 20:13 ''Usiue.''
Andiko hili ndilo andiko fupi kuliko yote katika Biblia lakini ni agizo la MUNGU lenye maana kubwa sana.



2. Kuna mauti ya pili yaani mwili na roho kutengana na MUNGU milele.

Hii inawahusu tu watakaokwenda jehanamu au ziwa la moto.
Hawa ni ambayo hawakutubu dhambi zao na kuziacha, hawakumpokea Bwana YESU kama Mwokozi wao na hawakuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU.
Mauti yao hao kibiblia inaitwa mauti ya pili.
Ufunuo 21:8 '' Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.''

Hao watateseka milele katika jehanamu.
Mauti ya pili haiwahusu wateule wa KRISTO waliookoka na kuishi maisha matakatifu duniani.
Wateule wa MUNGU wakifa kifo chao kinaitwa tu kulala.
1 Thesalonike 4:13-14 '' Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya kwamba YESU alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika YESU, MUNGU atawaleta pamoja naye.''

Wateule wakifa kifo cha kwanza ni kama wamelala tu maana wanaamka na baada ya hapo hawatateseka tena.
Bwana YESU alisema juu yao kwamba hata wakifa sasa watakuwa wanaishi yaani watakuwa paradiso mbinguni wakifurahi.
Yohana 11:25-26 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?''

Mauti ya pili ni kwa waliomkataa YESU kama Mwokozi wao na hawakutaka kuishi maisha matakatifu.


 3.Mauti ya tatu ni roho ya mauti.
Hii ndio hasa kiini cha somo langu.
Hii ni roho ya shetani ya uharibifu, ikiingia katika eneo la maisha yako usipoomba  lazima iue maana ni roho ya mauti.
 Ufunuo 6:8 ''Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.''

Hii roho ya mauti ni roho ya shetani ambayo husimamiwa na mawakala wa shetani ambao ni majini, mizimu, waganga wa kienyeji, wachawi na wakuu wa giza wote.

Nimekuwa nikitafakari jinsi watu wa MUNGU wanapoota baadhi ya ndoto mbaya za vitisho ndipo  hugundua kwamba hiyo ni roho ya mauti inawafuatilia na ndipo huanza kuomba wakiharibu roho hiyo ya mauti.

Lakini wengi sana ni mpaka waote ndoto za kutaka kuuawa ndipo hujua kwamba kuna roho za mauti zinawafuatilia, lakini ni vyema kujua kwamba roho ya mauti sio ile inayotaka kukuua tu bali roho ya mauti inaweza ikatumwa katika maeneo yako mengi ili kuua vitu vyako.

Watu wengi huharibu roho za mauti za aina moja tu yaani inayotaka kuua mwili lakini roho za mauti kwenye maeneo mengine huwa hawafuatilii.

Siku moja  miaka ya karibuni tulikuwa tunamuombea dada mmoja kanisani wakati wa ibada, tuliombea kwa muda kidogo bila mapepo kumwachia. Katika maombi yale tulikuwa tunatamka mapepo ya aina mbalimbali lakini jini ile halikutoka, Baadae Mchungaji kwa ufunuo ndipo akaanza kutamka ''Ewe roho ya mauti nimekuona na sasa toka kwa jina la YESU KRISTO'' Aliposema tu neno hilo yule dada aliruka juu kwa nguvu na mapepo yale yakamtoka yakisema msingetujua tusingetoka. Nilijifunza kitu siku hiyo kwamba adui uzipomjua wakati mwingine hawezi kutoka, alipotajwa tu ndipo alitoka. Watu tulikuwa tuko busy kusema ''Ewe makata, ewe pepo la uzinzi na usingizi'' Kumbe adui alikuwa anaitwa jini mauti au kaburi akiwa na ajenda kabisa za kuua.

Nilipanuka ufahamu siku hiyo maana mimi ni mtu wa kujifunza na siku hiyo nilijifunza. Niligundua kwamba ni heri ukaomba mapepo yatoke bila hata kuyataja lakini ukiyataja na huna uhakika hayatatoka kama hukuyataja kwa majina yao labda tu Neema ya MUNGU itumike kuyaondoa, labda tu nguvu za MUNGU ziwe kubwa ndipo watatoka bila hata kuwataja majina.
Roho ya mauti inaweza kutumwa katika maeneo mengi ya maisha ya mwanadamu, hilo ndilo muhimu naomba tujue.
Roho ya mauti inaweza kutumwa kwenye afya ili tu mtu asip ones ugonjwa anaoumwa. Wagonjwa wenye roho ya mauti wanaweza kuwa wanaumwa sana lakini wakipima Hospitali ugonjwa hauonekani, wanaweza kuwa wanaumwa kwa msimu, wakinywa dawa wanapona lakini baada ya muda wanaumwa tena.
Unaweza kuwa una roho ya mauti iliyokuletea kisukari au presha kiasi kwamba unakuwa unapona kwa muda lakini baada ya siku kadhaa ugonjwa unarudi, usipojua kumtafuta Bwana YESU kwa maombi hakika roho hiyo ya mauti inaweza ikasababisha kifo kabisa.
Zaburi 116:3-5 '' Kamba za mauti zilinizunguka, Shida za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni;  Nikaliitia jina la BWANA. Ee BWANA, nakuomba sana, Uniokoe nafsi yangu.  BWANA ni mwenye neema na haki, Naam, MUNGU wetu ni mwenye rehema. ''

Unaweza ukapata taabu kwa sababu ya roho ya mauti.
Unaweza ukapata shida zisizoisha kwa sababu ya roho ya mauti waliyokurushia wabaya wako.
Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye Bibashara yako ili iue biashara hiyo.
 Mwenye roho ya mauti katika biashara hakika kila akifungua biashara inakufa au anafilisika katika hali ambayo sio ya kawaida.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye uchumba wako ili huo uchumba ufe au uvunjike. Wapo watu kila akipata mchumba wakikaribia tu kufunga ndoa uchumba unakufa. Ndugu mmoja wiki ya kufunga ndoa na mchumba wake huyo mchumba akafa, akapata mchumba mwingine na walipokaribia kuoana tu yule mchumba akamkataa, akapata mchumba tena na walipokaribiana kuoana yeye mwenyewe katika hali ambayo sio ya kawaida akaamua kuvunja uchumba akisema tu sijisikii kuingia kwenye ndoa. Iliendelea kwa muda mrefu sana akiachana wa wachumba kwa sababu ambazo sio za kawaida. Kumbe ni roho ya mauti ya kuua uchumba ilikuwa iko naye, tunahitaji kuwa makini sana na kuomba sana sana.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye ndoa yako ili hiyo ndoa ife na msipokaa sawa kwa MUNGU hakika ndoa yenu itakuwa na migogoro isiyoisha hadi itakufa kabisa, mnaweza mkawasumbua sana wasimamizi wa ndoa yenu na wachungaji kumbe mlimfungulia mlango shetani na akawatumia roho ya mauti ya kuua ndoa yenu.
Leo kwa jina la YESU KRISTO amka na omba maombi ya kuiharibu kila roho ya mauti katika maeneo yako, yataje maeneo ambayo unahisi kuna roho ya mauti.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye akili ili tu iharibu akili yako kiasi kwamba huwezi kuwaza jema na hata ukiliwaza jema ukipata pesa unalisahau. Unaweza pia ukawa unahisi kuchanganyikiwa katika baadhi ya muda katika mambo nyeti ili usifaulu mitihani.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye uchumi wako kwa ujumla.
Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye kazi yako ili ufukuzwe kazi au usifaidike na kazi yako.
Kumbuka kazi ya shetani ni kuua na kuchinja na ndio maana Bwana YESU akaja ili ukiomba kwa MUNGU kupitia yeye uwe huru.
Yohana 10:10 ''Mwivi(shetani) haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi(YESU) nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.''

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye ukoo wenu  au familia yenu ili tu mchukiane hata umoja katika ukoo au familia ufutike na muwe maadui mnaotafutana kuuana.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye kipato chako ili kila ukipata pesa nzuri basi matatizo makubwa yanatokea ili kuifuta pesa hiyo, yaani matatizo yale ni kama mfuko wa kuwekea kila pesa yako unayoipata.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye nafsi yako kiasi kwamba unakuwa unapanga uharibifu tu au mambo ya kishetani tu.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye Kanisa wasioomba ili tu kutawanya waumini, ni roho ya mauti ya kuua Kanisa.

Roho ya mauti inaweza ikatumwa kwenye kikundi chenu ili kife.
Ni katika maeneo mengi sana roho ya mauti inaweza ikatumwa.

Unaweza ukawa unaota pesa zako zinapeperuka au zinaibiwa, mara unaota kuna vitu vinakufa, kumbe unajulishwa kwamba roho ya mauti imetua katika eneo hilo.

Roho ya mauti ni roho ya uharibifu ya shetani na kazi yake ni kuharibu hivyo vitu vingi vinavyoharibika kwako katika mazingira ambayo sio ya kawaida wakati mwingine chanzo kinaweza kuwa ni roho ya mauti.
Unaweza ukawa unaugua magonjwa ya ajabu ajabu kumbe chanzo ni roho ya mauti.
Roho ya mauti inaweza ikakaa katika kizazi  kukuzuia kuzaa au inaweza ikakaa katika kizazi ili kukuletea kansa ya kizazi.

Inaweza ikakaa katika titi ili kukuletea kansa. Inaweza ikakaa katika tumbo ili kukuletea uvimbe.
Roho ya mauti inaweza kutegwa barabarani ili magari yapate ajali ufe.
Roho ya mauti inaweza ikategwa kwenye leso au chakula.
Leo haribu roho za mauti katika maisha yako.
Zaburi 18:4-5 '' Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.  Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. '

Ashukuriwe MUNGU maana Bwana YESU alishinda kifo na mauti ili atushindie na sisi wateule wake.
Wakolosai 1:18-19 '' Naye(YESU) ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.  Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; '

 Ndio maana kwa jina lake leo tunaomba na kushinda.
Leo roho zote za mauti hakikisha zinakufa kwa jina la YESU KRISTO.
YESU anaturuhusu tuombe ili kwa jina lake tushinde.
Yohana 14:14 '' Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.''

 Jambo moja ambalo Bwana YESU hahitaji kwetu ni dhambi hivyo ni muhimu sana kuachana na dhambi zote na kuanza kuishi maisha matakatifu ndipo kila pando ambalo hakulipanda MUNGU Baba litang'olewa.
Mathayo 15:13 '' Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa.''

 Roho za mauti ni mapando ya shetani ambayo ni lazima tuyang'oe kwa jina la YESU KRISTO, lakini kwanza ni lazima tuwe watakatifu na wanaoishi maisha matakatifu.
Roho za mauti zinaweza kutegwa popote lakini maombi katika jina la YESU KRISTO ni silaha ya ushindi mkuu.

Zamani za Elisha Nabii kuna watu waliikuta mauti ndani ya sufulia ya chakula ili wakila wafe, neema ya MUNGU iliwagusa hawakula hadi maombi ya Nabii Elisha, Hiyo iko 2 Wafalme 4:39-41
Hiyo inatufundisha kwamba roho ya mauti inaweza kutegwa popote  lakini maombi katika jina la YESU KRISTO yanaweza kuifuta roho ya mauti hata isiwepo kwetu tena.
Zaburi 68:20-21 ''MUNGU kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana. Naam, MUNGU atakipasua kichwa cha adui zake, Utosi wenye nywele wa mtu afulizaye kukosa.''

 DALILI ZA MTU ANAYETESWA NA ROHO YA MAUTI.

1. Kushambuliwa na magonjwa kila mara.

2.Kupata ajali mara kwa mara.

3. Kila Biashara anayoianzisha inakufa.

4. Kuwa na uoga usio wa kawaida.
Anaweza akaogopa hata kuingia hata chumbani kwake tu.

5. Mikosi na balaa zisizoisha.

6. Hasira isiyo na kiasi inayoweza kuleta madhara makubwa.

7. Mtu wa kujihisihisi bila sababu.

8. Kuwa na maamuzi ya haraka baadae anajuta.

9. Kila akipata Mchumba anaachwa bila kosa lolote.

10. Kila janga na yeye lazima limpate.

Hizi ni baadhi tu ya dalili za mtu anayeteswa na roho ya mauti.
Ndugu yangu omba leo maana kuna ushindi, hata unaweza kufunga na kuomba ili tu kuharibu roho za mauti.
Ezekieli 13:18-20 '' useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege. ''

Somo hili litakuwa pia katika kitabu siku moja kwa ufafanuzi zaidi.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu  ubarikiwe.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.
Mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments