MAOMBI YA KUIFUNGUA MIKONO ILIYOFUNGWA KICHAWI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kama ilivyo katika ulimwengu wa mwili kwamba mtu akifungwa mikono yake kwa pingu au kamba hawezi kufanya baadhi ya vitu hata kama kutembea anatembea, na hata kukimbia kidogo anaweza ila kwa sababu amefungwa kamba basi kuna vitu hawezi kuvifanya hadi atakapofunguliwa mikono yake.
Mika kadhaa iliyopita niliona katika maono nikiwa nimefungwa mikono yangu kipepo, baada ya maono nilijikagua sana mikono yangu na sikuona chochote lakini kwa kujifunza Biblia mwenyewe niligundua kabisa kwamba adui alikuwa amenifunga mikono yako ya rohoni ili nisifanikiwe lakini kwa Neema ya MUNGU nilitambua na kuomba maombi ya kuifungua mikono yangu. Ndio maana leo ninapokuletea somo hili ninajua kwa ukubwa sana jinsi ambavyo mawakala wa shetani wanaweza kumfunga mtu na jinsi ambavyo mtu akiamua kufunguliwa kupitia jina la YESU KRISTO hakika inawezekana na mafanikio atayaona.
Kuna mikono ya rohoni na hiyo mawakala wa shetani wanaweza kumfunga mtu.
Kuna watu wamefungwa kichawi mikono yao ili wasifanikiwe katika kazi zao, hata kama kazi hizo  wanazifanya kwa juhudi kubwa na kwa nguvu kubwa sana.
Wachawi wana mbinu nyingi sana za kumfunga mtu asiye muombaji na asiyeishi maisha matakatifu ya Wokovu wa YESU KRISTO.
Kuna watu wamefungwa mikono yao kwa kupitia Pesa za kichawi au pesa walizozishika mikononi mwao kutoka kwa watu wabaya zikiwa zimenenewa vifungo kwa atakayezishika wa kwanza.
Kuna watu kwa sababu tu ya wivu wa watu wabaya wamerogwa mikono yao na kufungwa mikono yao.
 
Kiroho Mikono huwa sio tu hii tunayoiona bali Kuna mikono ya kiroho pia ambayo inaweza kufanya kazi kupitia  Mikono ya kimwili.
Hebu tujifunze zaidi.
Kutoka 17:11-12 '' Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda.
 Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa.'' 

Huo ni mfano wa kwanza.
Tunaweza tukajiuliza  kwanini hadi hadi Musa anyooshe mikono yake juu ndipo Israeli Washinde vita?
Kwanini Musa aliposhusha Mikono Israeli walipigwa lakini alipopandisha mikono Walishinda?
Je hiyo ilikuwa ni mikono tu hii ya kawaida au kulikuwa na ziada ya KiMUNGU ndani ya mikono hiyo?
Ukweli ni kwamba ndani ya mikono ya Musa kulikuwa na Mkono wa MUNGU wa kuwashindia.
Sasa katika jamii ya leo wachawi wanaweza kumroga mtu badala ya kuwa na mkono wa MUNGU wa baraka katika mikono yake wao wachawi wanaweza wakamwekea mkono wa shetani ndani ya mikono yake hata asiweze kufanikiwa.

Mfano wa pili ni huu.
Marko 16:17-18 ''Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.''
Watumishi wa KRISTO wataweka mikono juu ya wagonjwa na wagonjwa hao watapona ndivyo Biblia inasema.
Kama Mtumishi wa MUNGU amefungwa mikono yake kipepo hakika ni ngumu kumwekea mtu mkono na kumuombea na akapona.
Unadhani ni mikono tu ikiwekwa kichawni ndipo wagonjwa wanapona?
Ukweli ni kwamba ni lazima ndani ya mikono ya watumishi wa KRISTO kuwe na mkono wa MUNGU wa uponyaji ndipo tukiweka mikono juu ya wagonjwa nao watapona.
Mimi Peter Binafsi nimewahi kuombea wagonjwa wengi sana kwa njia ya simu na wakapona hadi magonjwa ya ajabu sana.
Nimewahi kumwombea Dada mmoja kwa njia ya simu akajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU  kule aliko.
Ndugu zangu, mikono kiroho sio tu hii tuliyonayo kila mmoja wetu.
Ili tufanye mengi ya baraka ni lazima tuwe na mkono wa MUNGU ndani ya mikono yetu.
Isaya 62:8 ''BWANA ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi.''

Waisraeli wakiwa wanatoka Misri kulikuwa na nguvu nyingi ya MUNGU iliyokuwa nao.
Farao na Wamisri waliona mikono ya Musa lakini kumbe ndani ya Mikono ya Musa kulikuwa na mkono wa MUNGU.
Je ndani ya mikono yako kuna mkono wa MUNGU?
Kumb 34:11-12 '' katika ishara zote na maajabu yote, ambayo BWANA alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.'
Kwa mikono ya Musa, MUNGU alitenda ajabu nyingi sana, ndani ya mikono ya Musa kulikuwa na Mkono wa MUNGU.
Tunajuaje?
Kutoka 3:20 ''Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.''
MUNGU ndiye anayetamka katika andiko hilo kwamba ataunyoosha mkono wake na kuipiga Misri lakini Ilionekana Mikono ya Musa ikitenda ajabu zote hizo kumbe ndani ya Mkono wa Musa kulikuwa na mkono wa MUNGU wenye nguvu.
Leo kuna watumishi wengi wa MUNGU ambao Mkono wa MUNGU uko ndani yao ukitenda kazi.
Shetani naye kuna watu amewafunga ili wasifanikiwe.
Mtu kama hana mkono wa MUNGU ndani yake basi shetani humvamia na kumfunga mikono yake.
Leo kuna watu wamefungwa kipepo mikono yao kiasi kwamba hata akipewa mtaji wa Milioni 50 bado hawezi kupata faida bali kufilisika.
Kuna mtu anaweza akapewa mtaji wa Milioni 20 lakini baada ya mwaka mzima utamkuta hana hata elfu kumi, amefilisika na hata yeye hajui kwanini amefilisika maana hata hajui pesa yake imeishaje.
Kuna watu wamefungwa Mikono yao hivyo hata akipewa mtaji bado hawezi kufanikiwa maana bado mikono yake ya kiroho  imefungwa kipepo. Yaani ni kama mtu yuko gerezani kisha umkabidhi Pesa nyingi umwambie fanya Biashara, hawezi kufanya chochote hadi atakapofunguliwa mikono na kutoka gerezani. Ukimrushia mtu Pesa akiwa amefunga mikono na umwambie kwamba adake hiyo itamsaidia hakika huyo ataishia kuiona tu kwa macho lakini hataipokea mikononi mwake maana mikono yake imefungwa, hadi afunguliwe ndipo atafanikiwa.
Kuna watu hata sio walegevu katika kufanya kazi, wana juhudi kubwa lakini ajabu ni kwamba kazi zao hazijawahi kuwapa faida.
Kuna watu ndani ya mikono yao shetani amewawekea miokono ya kipepo ya madeni.
Ndugu, kama mikono yako imefungwa kipepo hata huwezi  kufanikiwa leo vunja kamba za kichawi zilizokufunga, fungua pingu za kipepo zilizokufunga, fungua minyonyoro kwa damu ya YESU KRISTO ili uwe huru.
 Mikono yako inatakiwa iwe na silaha za MUNGU na sio silaha za shetani.
2 Kor 6:7 '' katika neno la kweli, katika nguvu ya MUNGU; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto;''

BAADHI YA DALILI ZA MTU ALIYEFUNGWA MIKONO KIPEPO.

1.Mkono wa MUNGU hauko pamoja naye.
Luka 1:66 '' Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.''
Yohana Mbatizaji ni mfano wa watu waliokuwa na Mkono wa MUNGU ndani yao.
Kinyume cha mtu ambaye ana mkono wa MUNGU ni mtu ambaye hana mkono wa MUNGU.
Mtu aliyefungwa kipepo mikono yake huwa hana mkono wa MUNGU ndio maana kila analoshika kuanzisha ili afanikiwe huwa anaishi kutokufanikiwa.

2. Ni Mlegevu katika kufanya kazi ya kumpatia faida.
 Waebrania 12:12-13 '' Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.''
Kuna ulegevu huwa ni pando la shetani kabisa baada ya mikono kufungwa kipepo.
Ukiona una juhudi sana katyika mambo yasiyo na faida lakini ukawa ni mlegevu sana katika mambo muhimu ya kukupatia kipato basi tambua kwamba umekuwa mlegevu kwa sababu umefungwa mikono yako kiroho.
Kwa wateule wa KRISTO walio waombaji ahadi ya MUNGU ni hii.
Sefania 3:16 ''Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.''


3. Hata apewe Mtaji mkubwa sana hawezi kufanikiwa.
Isaya 35:3 ''Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.''
Ukiwa dhaifu ni vigumu kufanikiwa.
Ukiwa sio imara hakika ni vigumu kufanikiwa.
Kila kitu kina chanzo chake katika ulimwengu wa roho hivyo wakati mwingine kwa sababu ya kufungwa mikono kipepo basi kila ukianza biashara au kazi basi hakuna kufanikiwa maana umefungwa kiroho.
Bishara wakati mwingine hufa au kudumaa kwa sababu ya kufungwa mikono kipepo.


4. Kamba za madeni na machukizo humkamata.
Mithali 22:7 '' Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.'' 
Mtu huyo huwa ni mtumwa wa madeni na kwa njia hiyo anatenda dhambi ya kudhulumu watu maana anashindwa kurudisha pesa au mali za watu alizokopa.
Ni Mtu wa kukopa kila siku.
Mikono yake ya kiroho inamuongoza kufanya machukizo tu.
Zaburi 37:21 '' Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. ''


5. Roho ya umasikini humfuatilia hata kama ana kazi nzuri au mshahara mkubwa sana.
Mithali 14:20 '' Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi.''
Sifa mojawapo ya umasikini ni kuchukiwa.
Kuna watu hawana hata pesa ya kula kwa siku moja lakini mishahara yao ni zaidi ya laki 8 kwa mwezi.
Wakati mwingine hali hiyo hutokea baada ya kufungwa mikono kipepo.
Bdugu nakuomba leo omba ili uvuke salama katika jambo hilo linalokutesa la kuwa na kazi nzuri, mshahara mzuri lakini umasikini ni mkubwa kuko kawaida.
Zaburi 86:1 ''Ee BWANA, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji ''
Leo ikomboe mikono yako kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Leo fungua kamba za kipepo zilizofunga mikono yako.
Leo futa mkono wa shetani wa madeni ulio ndani ya mikono yako.
Ifute mikono ya shetani ya umasikini na uharibifu iliyo ndani ya mikono yako.
Leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO omba kwa MUNGU Baba kwamba Mkono wake wa baraka na ushindi uwe ndani ya mikono yako.
Omba leo na utafanikiwa na utaona mabadiliko makubwa sana.
Kumbuka Mikono yetu kama hatutairuhusu ivamiwe na shetani hakika inaweza ikatunza nguvu za MUNGU.
Ayubu 4:3 '' Tazama, wewe umewafunza watu wengi, Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge.''
Kuomba katika jina la YESU KRISTO na utakatifu kunaweza kukufanya uchanue ukiwa kwenye kitanga cha mkono wa MUNGU.
Isaya 49:16 '' Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.''
MUNGU anao ushindi mkuu kupitia mikono yako mteule, ila hakikisha kwanza mikono yako inafunguliwa kwa damu ya YESU KRISTO.
Kumb 2:24 ''Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano.''
MUNGU anaweza kukubariki kupitia mikono yako, hakikisha tu mikono yako imefuguliwa kwa jina la YESU KRISTO.
MUNGU akubariki sana ukiomba leo.
N.B. (Zamani nilikuwa naweka maombi chini ya somo ili kumsaidia muombaji mchanga lakini kuna watu wabaya wamekuwa wanachukua maombi hayo na kuwatapeli watu mbalimbali, wakijiita jina langu. Kwa jinsi hiyo nimeamua kutokuweka maombi ila somo hili litakuwa katika kitabu na huko litakuwa ni somo lenye ufafanuzi na maombi mengi pia, naomba nisamehewe kwa hilo ila sitaki watu waibiwe pesa na matapeli waliojikinai huku wakitumia masomo yangu ya maombi ambayo ninayo mengi mno)
Bado na-Plan nitawezejae kuweka maombi na yasidukuliwe na waharifu wasio na lengo zuri.
Lakini pia kwa muombaji mzoefu naamini kabisa baada tu ya kusoma somo hili umejua uombe nini kwa kupitia maelekezo niliyotoa.
Wa waombaji wachanga naomba tu endeleeni kujifunza kuomba na na ombeni kwa jina la YESU KRISTO hakika mtapokea ushindi.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments