MAOMBI YA KUOMBEANA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe wateule wa MUNGU.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la zamu ya muda huu.
Maombi ni mteule wa KRISTO kuzungumza na MUNGU.
Maombi ni faragha njema ya mwanadamu kuzungumza na muumba wake.
Maombi ni muhimu sana, na kama watu wa MUNGU ni muhimu sana kubebeana mizigo wakati mwingine kwa njia ya maombi.
Yakobo 5:15-16 " Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na BWANA atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii."


Kwanini kubebeana mizigo katika maombi, yaani kuombeana?
Ni kwa sababu.


1. Kwa sababu si wanadamu wote wana Imani ya kuomba na kupokea kutoka kwa MUNGU Baba.

 
Kuna wenye Imani haba, wenye Imani kidogo na wenye Imani kubwa.

Mathayo 9:29 ''Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate.''
 Kumbe utapokea kwa kadri ya imani yako.
 Wenye Imani kubwa akiomba kwa Imani ni anaweza kupokea mapema kuliko wa Imani ndogo,japokuwa MUNGU anataka wateule wake wote tuwe na Imani kubwa.
Imani pia imegawanyika; kuna Imani ya kuomba na Imani ya kupokea. Kuna watu wana Imani kubwa ya kuomba lakini hawana Imani ya kupokea ndio maana hawapokei au majibu huchelewa kwa sababu ya Imani zao.

Maandiko mengi yanajulisha jinsi watu walivyokuwa wanaombeana tangu zamani.
Wakolosai 1:3 ''Twamshukuru MUNGU, Baba yake Bwana wetu YESU KRISTO, siku zote TUKIWAOMBEA;''


2. Sio wanadamu wote wana haki inayoweza kuleta majibu sahihi na haraka.

Waebrania 12:14 '' Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao;'' 
 
Haki ni utakatifu na kuzijua kanuni za MUNGU na kutembea katika hizo, japokuwa lengo la MUNGU wateule wote wawe wenye haki mbele za MUNGU.

Ili kujibiwa maombi vyema ni muhimu sana kuitafuta haki ya MUNGU kwanza.
Sio wote wanaweza kutembea katika haki ya MUNGU hivyo kuombeana kunaweza kuwafanya wapokee kutoka kwa MUNGU, Si kwa sababu ya maombi yao ila kwa sababu ya maombi ya wenye haki wa MUNGU waliowaombea
Unaweza kuwa na ndugu ambao hawajaokoka hivyo hawana haki kwa MUNGU lakini maombi yako yanaweza kuwasaidia hadi wakati ukafika wakaokoka na kuwa na haki mbele za MUNGU za kuomba na kupokea.
Biblia inaonyesha maombi ya wenye haki walivyoomba na kuponya taifa zima.
Hesabu 21:7 ''Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia MUNGU, na wewe; UTUOMBEE kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa AKAWAOMBEA watu.''

 
3. Sio wote wana uwezo wa kuomba katika wakati sahihi wa kuomba.

1 Wafalme 13:6 '' Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa MUNGU, Umsihi sasa BWANA, Mungu wako, UKANIOMBEE, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa MUNGU AKAMWOMBA BWANA mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.''
Huo ni mfano wa mtu ambaye alikuwa hawezi maana inawezekana alikuwa kwenye maumivu makubwa akaomba msaada wa kuombewa. 
MUNGU akamsikia mtumishi wake na kumponya yule ndugu. 
Yapo mambo mengi yanaweza kumfanya mtu asiombe katika wakati sahihi.
Mfano mtu aliyepatwa na mabaya mfano kufiwa au ajali mbaya hawezi kuomba kama mtu asiye katika matatizo, ndio maana kubebeana mzigo kwa njia ya maombi ni muhimu sana.

 Biblia inaonyesha majibu mengi pia yalitokana na kuombeana.
Ayubu 42:10 '' Kisha BWANA akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.''


4. Kuna watu hawajafunguliwa yaani wako kwenye vifungo mfano vifungo vya dhambi, uabudu shetani na walio na mapepo ndani yao.
 Mashetani Yale yamewakamata kiasi yamewaondolea hata akili ya maombi na kujifunza Neno la MUNGU, ni jukumu letu kuwaombea walio katika maeneo yetu ili kwanza wafunguliwe na Bwana YESU ndipo wapate kuomba wao kama wao.

Mathayo 10:7-8 ''Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.''
Agizo la Bwana YESU kwetu sisi wateule wake ni kuipelejka injili yake.
Katika kuipeleka injili ya Bwana YESU kwa watu wote kuna agizo pia la kuwaombea ili wafunguliwe.
Ndio Maana Bwana YESU akatuagiza kuombea wagonjwa ili wapone, waliokufa wafufuke, waliona ukoma wapone, mapepo yatoke na mengine mengi. Hivyo vitu havitafanyika bila maombi ndio maana kuombea wengine ni muhimu sana.
Isaka alimuombea Mkewe ili apate ujauzito na MUNGU akajibu hakika.
Mwanzo 25:21 '' Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.''
 
Wako watu wako katika vifungo mbalimbali na wanahitaji tu neema ya MUNGU ili watoke katika mabaya hayo.
Wako watu wako dhambini kiasi kwamba ili watubu wanahitaji maombi ya kuwafanya wajitambue, maana wakati huu hawajitambua.
Kuna watu usiposimama wewe muombaji na kuwaombea hakika wataharibikiwa.
Bwana YESU siku moja aliwaambia wanawake kulia kwa ajili ya watoto wao na nafsi zao maana kuna hukumu mbeleni kwa waovu wasiotubu, hivyo kulia kimaombi kwa ajili ya wengine ili MUNGU awahurumie ni muhimu sana.
Luka 23:28-30 '' YESU akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. ''

5. Kuwaombea wengine ni upendo wa ki MUNGU. 

Waefeso 6:18 '' kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;'' 
Biblia hapa inatutaka tudumu katika sala, maombi na kusali lakini tusidumu kujiombea sisi tu bali kuwaombea na watakatifu yaani waaminio wenzetu katika kweli ya KRISTO.
Kuombea wengine ni dalili njema kwamba tuna upendo sahihi. Ni upendo mkuu  pale tutakapoweza kuwaombea wengine.
Ayubu alikuwa anawaombea watoto wake na kutoa sadaka kwa ajili yao.
Musa aliwaombea waisraeli ili wasiangamizwe kwa sababu ya kuabudu ndama.
Bwana YESU alimuombea Petro ili asirudi kwa shetani kwa sababu ya jaribu lakini asonge mbele katika wokovu na kuwasaidia wengine kwa kuwafundisha  kumcha MUNGU.
Luka 22:31-32 '' Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.'' 
 

6. Tunaombeana kwa sababu ni agizo la MUNGU kupitia Biblia kwamba tuombeane.

Yakobo 5:16 ''Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.''
Biblia inasema tuungame dhambi zetu sisi kwa sisi pia Biblia inaagiza kuombeana maana kuna faida kuu katika kuombeana.
Kuungama maana yake ni kukubali ukweli wa uovu ambao mtu ameufanya, hivyo anahitaji msaada wa MUNGU na kuombewa na watumishi na kusaidiwa kiroho ili asirudie dhambi ile.
Kuungamia ni kuombea mtu msamaha.
Kuungamisha ni kumfanya mtu aombe msamaha kwa MUNGU. Hivyo unaweza kumuombea  mtu msamaha kwa MUNGU ili MUNGU ampe kutubu mtu huyo. Jambo la kukumbuka ni kwamba unamuombea mtu aliye hai tu na sio aliyekufa.
Aliyekufa hata ukimuombea miaka 10 mfululizo hakuna utakalokuwa unamsaidia hata moja, hivyo kama mtu unampenda na yuko katika uovu basi muombee wakati akiwa hai ili MUNGU ampe moyo wa toba na atubu na kuacha uovu wake.
Baada ya kifo Biblia inasema ni hukumu(Waebrania 9:27)
 Jambo jingine kujua ni kwamba Tunaombeana ili kuondoa ubinafsi ndani yetu, na tukumbuke kwamba sio watu wote wana bidii ya kuomba, hata kama agizo la MUNGU kila mtu aombe.

7. Tunaombeana kwa sababu tumejulishwa kwa ufunuo kwamba tuombe.
 
Mfano unaweza ukaota ndoto juu ya mabaya yanayotaka kumpata mtu Fulani. Jambo la kwanza wewe kujua ni kwamba katika hilo umepewa jukumu la kumuombea huyo mtu haijalishi ni mtesi wako au sio ndugu yako au hakuhusu kwa lolote.
Kuna watu hulia kwa ajili ya taifa au jamii kwa sababu kuna vitu wameviona katika ulimwengu wa roho sio vizuri, hivyo yanahitajika maombi, huko ndiko kubebeana mizigo katika maombi.


Wakolosai 1:9 "Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni;"

Points hizi pia ni muhimu sana kuzijua katika maombi.
 
=Narudia tena, ni kwamba, Muhimu kujua ni kwamba tunaombea walio hai tu, sio waliokufa.
Hata ungeombaje juu ya aliyekufa huwezi kumsaidia kwa lolote, labda tu kama hajafa ila amechukuliwa msukule, huyo unaweza kumwombea.
=Wa kumuomba ni MUNGU tu katika utatu wake na sio kuwaombea wanadamu au watakatifu wa zamani.
Maombi ni muhimu sana kwa kila mtu.
=Tangu Adamu hadi Leo nafasi ya kuomba kwa MUNGU ipo kwa kila mwanadamu.
=Maombi ya kuombeana ni muhimu sana haijalishi anayeomba ni nani, muhimu tu muombaji awe ameokoka na anaishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO YESU.


Waefeso 6:17-18 "Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa ROHO ambao ni neno la MUNGU; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;"


=Tukumbuke kwamba katika maombi tunazidiana nguvu za kiroho kulingana na ufahamu wetu wa Neno la MUNGU, kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na Imani, hivyo kuombeana ni muhimu sana.
Muhimu kujua ni kwamba kila mtu anatakiwa kuwa muombaji na anayewaombea wengine pia.
=Hakutakiwi kuwa na kundi la waombaji na kundi la waombewaji.
Wote tunatakiwa kuwa waombaji na wote pia tunatakiwa kuwaombea wengine.
Mtu ambaye yeye huwa haombi Bali husubiri tu kuombewa hakika huyo hajitambui na imani yake huyo haiwezi kuongezeka.


FAIDA ZA WEWE KUOMBEA WENGINE.

1. Kujibiwa maombi hayo.
2. Unapoombea wengine ndivyo pia unavyotoa nafasi ya wengine kukuombea wewe.
3. Unakuwa umeshiriki kuwaokoa wengine, kuna thawabu mbinguni kwa kazi hiyo.
4. Unakuwa umemtumikia MUNGU kwa njia hiyo ya kuombea wengine.

Ona mfano wa kanisa la kwanza jinsi walivyokuwa wanaombeana.
1 Wathesalonike 1:2 "Twamshukuru MUNGU siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu."


Ndugu yangu nakuomba sana hakika unakuwa muombaji na hakikisha unaombea wengine kila Mara.
Ukiacha maombi unakuwa umeacha kitu cha muhimu sana sana.
YESU kama kiongozi wetu alipokuwa duniani alikuwa muombaji na aliweka kipaombele maombi, na kwa njia hiyo alitupa kielelezo chema cha kuwa waombaji, hivyo yatupasa sana na sisi kuwa waombaji.
=Kumbuka maombi yetu ni katika jina la YESU KRISTO tu.
=Maombi yetu ni katika ROHO MTAKATIFU pekee.


MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari  katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments