MAOMBI YA MUOMBAJI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Imani katika KRISTO ni mtaji wako wewe muombaji.
Mtaji usipozalishwa huwezi kupata faida wala kufanikiwa.
Usiwe na Imani kwa maneno tu bali uwe na imani katika KRISTO kwa matendo.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kazi ya muombaji ni kuomba ili apewe.
Kila Mtu naamini nalo hitaji lake na ili kupokea inatupasa tuwe waombaji.
Kama Muombaji hakikisha unaomba kwa MUNGU katika kweli yake.
Mombaji katika Kanisa ni mlinzi, ni askari anayetakiwa kuwa zamu muda wote.
Kama vitu ukikaa kimya wewe muombaji hakika adui anaweza kupanda magugu.
Ndugu Usimwache MUNGU akakaa kimya.
Isaya 62:6-7 ''Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.''
Ndugu usimwache MUNGU akae kimya, mkumbushe mahitaji yako unayotaka akutendee, omba na utashinda kwa jina la YESU KRISTO.
Haijalishi umeomba miaka mingapi, leo pia ni wakati wako wa pekee sana, mkumbushe MUNGU juu ya mahitaji yako na utapokea.
Sio kwamba MUNGU husahau bali hasahau lakini anachotaka wewe uombe na uishi maisha matakatifu na ya haki.
Mkumbushe MUNGU leo, usimwache akae kimya.
Ukitaka akae kimya hakika atakaa kimya na wewe hutapokea hitaji lako lakini leo ni moja ya siku ambazo nakuomba mkumbushe MUNGU juu ya mahitaji yako, omba na hata fanya tendo la imani na MUNGU atakupa iliyo haki yako.
yeye anasema
''Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.-Isaya 43:26''

 
Ahadi za MUNGU zilizo katika yeye ni ndio na hakika.
Ndugu songa mbele na Bwana YESU mwenye uzima wako wa milele, omba kwa MUNGU na utapokea.
Aliyeahidi ni mwaminifu na wa haki.
Usimwache akae kimya bali mkumbushe kwa maombi yako.


Ukiwa uko katika maombi ya kufunga.
Mtu mwingine Anaweza ajue na pia anaweza asijue.

Muhimu kujua hatufungi ili watu wajue tumefunga Bali tunafunga ili MUNGU atujibu maombi yetu.
Ukizingatia hiyo ni vyema sana na maombi yako ya kufunga yataleta majibu.
Kumbuka  ''Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.-Mathayo 17;21''


Huyo ndio ndiyo muombaji yaani anaomba na hata kufunga kwa maombi nafunga.
Katika Kanisa waombaji ni muhimu sana na ni muhimu zaidi hata kuliko hata baadhi ya viongozi wa Kanisa.

Sifa za Muombaji Kama Askari anayepigana vita vya kiroho na kushinda.
 Waefeso 6:10-12 '' Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika BWANA na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.''
 
1. Ni hodari na mwenye bidii na maarifa katika kupambana kiroho.

2. Ni shujaa na ana imani atashinda bila kujali ukubwa wa jeshi la adui.

3. Anamtii kiongozi wake ambaye ni ROHO MTAKATIFU katika maombi na maisha yake.

4. Anatumia vyema na kwa usahihi silaha za kiroho na mamlaka za kiroho alizopewa na MUNGU.
Mamlaka/Funguo za kiroho kwa muombaji ni;
A. Jina la YESU KRISTO.
B. Damu ya YESU KRISTO.
C. Neno la MUNGU.
D. Nguvu za ROHO MTAKATIFU.


5. Amevaa vazi halisi ili aweze kushinda. 
Vazi la kuvaa muombaji linaitwa Wokovu wa KRISTO.
Vazi hili linahitaji utakatifu na kutembea kwenye kusudi la MUNGU la injili ya KRISTO.


6. Ana umri sahihi wa kuwa askari wa kiroho.
 Umri wake ni kukua kiroho hata asiwe mchanga kiroho tena.
Mchanga kiroho huchukuliwa na upepo wa elimu isiyo ya MUNGU na kupoteza ujasiri wake.
Mchanga kiroho anaweza kuwa haziamini hata silaha za kiroho anazotakiwa kuzitumia kupambana na kushinda.


7. Ana mbinu sahihi za kivita.
Mbinu hizo hutokana na ufahamu wake kwenye Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU ndio lina ramani na maarifa yote hata uweze kushinda.


Wateule wa KRISTO wote ni askari kwenye ulimwengu wa roho, lakini sio wote hushinda vita.
Uwezo wa kushinda vita unatokana na sifa nilizotaja hapo juu.

Biblia inasema " ombeni bila kukoma; jitengeni na ubaya wa kila namna.-1 Wathesalonike 5:17,22"

Kama maaskari wa kiroho yaani waombaji  ni muhimu pia tuwatambue maadui zetu tunaopambana nao.
Biblia inawataja maadui wengi lakini baadhi ya maadui wakuu ni hawa ikisema " Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.-Waefeso 6:12-14"


Baada ya kuzungumza hayo maarifa ya Nno la MUNGU nataka leo uombe maombi yafuatayo ambayo ndiyo maombi ya Muombaji leo.

Maombi ya Leo omba mbingu zako zifunguke.
Kumb 28:23 "Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma."

Andiko hilo linaonyesha madhara ya laana kwa mtu lakini wakati mwingine mbingu za mtu zinaweza kufungwa na wabaya wa mtu.
Mimi najua wewe huna laana lakini fungua mbingu zako kwa maombi.
Mvua ya baraka bila kufunguliwa kwako haiwezi kunyesha.
Kama mbingu yako ni chuma ifungue kwa damu ya YESU.

Masaa machache yaliyopita nilikuwa namwombea rafiki yangu mmoja kwa njia ya simu.
Katika maombi yale nikawa namuombea kwamba baraka zake ambazo watu wamezilalia waziachie, baraka zake ambazo watu wabaya wamezilalalia waziachie. Nilipokuwa naendelea na kuomba hivyo ghafla nikaona nyoka Mkubwa amelalia vitu kama mayai meupe sana  ambapo sauti ikasema kwamba roho ile ya kipepo imekalia baraka za ndugu huyo. Nikaanza kuomba kwa spidi kali nikiharibu roho ile ya shetani iliyokalia baraka za ndugu yule.
Ndugu, hata wewe shetani anaweza akakalia baraka zako, dawa ni kuliita jina la YESU KRISTO na damu ya YESU KRISTO ili kumharibu wakala huyo wa shetani aliyekalia baraka zako.
mbingu zako zinaweza zikafungwa na wachawi.
Kumbuka mvua hunyesha baada ya mbingu kufunguliwa, hata baraka huja baada ya mbingu za baraka kufunguliwa.
Lakini pia  mbingu za baraka  zinaweza kufungwa na mawakala za shetani ili baraka hizo zisikufikie wewe muombaji.
Leo omba maombi ya kuzifungua mbingu zako kwa jina la YESU KRISTO.
 Kumb 28:7-8 ''BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.''
Maombi yako yanaweza kuwatawanya maadui zako na wakakimbia kwa njia saba wakiziachia baraka zako.
Watawanye maadui hao walioshikilia baraka zako, watawanye kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Amuru baraka ya MUNGU ikufuate kwa jina la YESU KRISTO.
Changamoto ya waombaji wengi ni kushindwa kuishi maisha matakatifu hata majibu ya maombi yao yawe dhahiri mapema.
Ndugu hakikisha unaomba sana na hakikisha unaishi maisha matakatifu siku zote.
Maombi na utakatifu ni vitu viwili ambavyo huwezi kuvitenganisha.
Ukitenganisha maombi na utakatifu hakika unakuwa unatenganisha baraka zako na wewe hivyo huwezi kuzipokea baraka hizo.
Omba na hakikisha unaishi maisha matakatifu ndipo utamuona MUNGU kupitia maombi yako.
Waebrania 12:14-15 ''Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.''
Maombi ya mwombaji yanatakiwa yaambatane na;
1. Kuomba kwa imani.
2. Utakatifu na maombi.
3. Kuomba kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO.
4. Kuomba sawasawa na Neno la MUNGU.
5. Kuomba katika ROHO MTAKATIFU.
 
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments