MAOMBI YA TOBA NI UFUNGUO WA KUFUNGUA MLANGO WA CHUMBA CHENYE MAJIBU YA MAOMBI YAKO KWENYE ULIMWENGU WA ROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana wetu YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Soma hili ni muhimu sana hivyo nakuomba soma mpaka mwisho.
Maombi ya toba ni maombi ya muhimu sana na yanahitajika sana katika kutuunganisha na majibu ya maombi yetu mengine.
Toba maana yake ni kujuta na kuomba msamaha kwa ajili ya yaliyotokea ambayo yako kinyume na MUNGU.
Sio kila mabaya yaliyokukuta ni mpango wa MUNGU, Hapana mengine ni wewe ulisababisha hayo yakukute ndio maana ili utoke kwenye tatizo sio kuomba tu kwa imani kwamba utoke bali wakati mwingine unahitaji kutubu kwa ajili ya chanzo cha tatizo ndipo uombe kutoka katika tatizo.
Kutubu maana yake ni  kuomba msamaha kwa makosa yaliyofanyika.
Isaya 57:15 ''Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.'' 

Kuna watu wameokoka na hawatendi dhambi na kwa hali ya kawaida hawahitaji kutubu lakini naomba kuwaambia kwamba katika mahitaji ambayo tunaomba kwa MUNGU tutendewe mengine kuna uovu ulifanyika kabla ndio maana tatizo likaja na sasa tunahitaji MUNGU atutoe kwenye tatizo, hapo toba inahitajika sana hata kama aliyesababisha tatizo sio wewe binafsi.
Ukijua kinachozaliwa na toba ya kweli basi hakika ungeona umuhimu sana wa kutubu.
Unaweza ukaingia katika matatizo yanayohitaji msaada wa MUNGU ili utoke na matatizo hayo wala hukusababisha wewe lakini ili utoke toba ya kweli inahitajika kwanza, Nimesema kwamba kutubu ni kuufungua mlango wa chumba kilichobeba majibu ya maombi yako mengine.
Inawezekana kabisa uko katika matatizo ambayo aliyesababisha ni wazazi wako au serikali katika eneo lako au idara yako.
Inawezekana kabisa tatizo lilisababishwa na wachawi au waganga au wanadamu wabaya, Njia rahisi ya wewe kutoka katika matatizo hayo inaanza na kutubu kwa ajili ya chanzo cha tatizo kisha ndipo uombe kutoka katika tatizo hilo.
Unapotubu unakuwa unamruhusu MUNGU ili akuangalie kwa huruma na kukusaidia.
Unapotubu maana yake unauruhusu ufalme wa MUNGU kukusaidia.
Mathayo 3:2 '' Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''
Ufalme wa MUNGU maana yake ni serikali ya mbinguni inayotawala kote.
Sasa ili System ya mbinguni ikusaidie kushinda pahali uliponasa basi toba ni muhimu sana.
Kumbuka pia huwa kuna hati za mashtaka na dawa ya kuzifuta hati hizo ni kuomba toba juu ya jambo husika haijalishi lilifanyika zamani kiasi gani.
 Katika mahitaji yako ambayo yameshindikana kujibiwa kwa muda mrefu basi toba kwa ajili ya kilichosababisha tatizo na kilichosababisha usijibiwe inahitajika sana, hata kama unadhani huna kosa katika hilo hata utubu.
1 Yohana 1: 7-10 '' bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.  Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.''
 Kumbuka toba ndio inafungua mlango wa chumba chenye majibu ya mahitaji yako.
Hata kama unadhani huna dhambi lakini ili upokee hitaji la maombi yako wakati mwingi sana inahitajika toba kwanza.
Mfano kama unaomba ndugu zako wafunguliwe kutoka vifungo vya pombe na uchawi unapaswa kwanza kutubu kwa ajili ya kilichosababisha ndugu zako wakaingia kifungoni, baada ya hapo wafungue kwa maombi yako yenye mamlaka katika jina la YESU KRISTO.
Biblia inasema hata kwetu sisi wahubiri kwamba wakati mwingine tusiwawekee watu mikono na kuwaombea haraka haraka maana wakati mwingine hapo hakuhitajiki kufunga na kubomoa bali kunahitajika kutubu na Neno la MUNGU.
Hiyo iko 1 Timotheo 5:22 ''Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.''

Toba ni muhimu sana na iwe ni toba ya kweli ndipo itakuwa rahisi maombi ya mahitaji kujibiwa.
Isaya 55:6-8 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.  Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA.''

Kama mfano unateswa na umasikini inakupasa kwanza kutubu kwa ajili ya kilichosababisha huo umasikini ndipo uombe kufunguliwa.
Kama huzai inakupasa utubu kwa ajili ya hicho kilichosababisha usiwe na kizazi, uliumbwa na kizazi lakini kikaondoka baadae kwa sababu ulisababisha wewe mwenyewe au watu wengine walikusababishia, iwe kwa kukuroga au vinginevyo, baada ya kutubu kwa ajili ya chanzo basi ndipo uombe maombi ya mamlaka ili kuondoa zuio la kiroho la kukuzuia kuzaa ndipo utapata uzao. Inawezekana kabisa ulionywa rohoni kwamba acha uovu au omba na wewe hukuzingatia kumbe ndicho kipindi  wachawi wanakuroga ili kukufunga uzao ili usizae, baada ta toba kwa ajili ya chanzo basi omba sasa MUNGU akufungue na upate uzao.
Ufunuo 2:5A '' Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu,''
 Kuna mengine inawezekana ulijichanganya  ndio maana mabaya yakakupata.
Dawa sio kusema tu navunja na kuharibu bali kwanza toba kwa ajili ya kilichosababisha ndipo uanze sasa kuvunja, kuharibu na kuangamiza kila kilichokuzuia usifanikiwe.
Na toba ni lazima iwe toba ya kweli.
Katika kila eneo ambalo adui amekuzuia usifanikiwe unatakiwa kwanza utubu kwa ajili ya kilichosababisha tatizo ndipo kisha uombe kufunguliwa, inawezekana ulilala badala ya kuomba ndio maana adui akapata nafasi ya kukutesa.

Inawezekana kabisa wewe ni mdhambi mkubwa na unataka muujiza wa MUNGU.
Inawezekana kabisa wewe uko ndugu huyu anayeambiwa katika Matendo 8:22-23 kwamba '' Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe BWANA, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.''
Ndugu, dawa ni kutubu kwanza toba ya kweli na kuachana na maovu yote uliyayatenda mwanzo ndipo uombe kupokea hitaji lako.
Kumbuka toba ya kweli katika Bwana YESU huleta nyakati ya kuburudishwa.
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''
Kuburudishwa au kufurahishwa huja baada ya kujibiwa maombi, lakini Biblia inasema ili kuja nyakati cha kuburudiswa basi toba kwanza ndio jambo la lazima.

Hebu ngoja tuone mifano ya watu wa MUNGU walitubu hata pale ambapo hawakuwa na uhakika kama kuna uovu umetendeka.

1. Ayubu alitubu siku zote kwa ajili ya watoto wake.

Ayubu 1:4-5 ''4 Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru MUNGU mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.''

Inawezekana Ayubu hakuwa na dhambi lakini alijua ili wanawe wasaidiwe na MUNGU na kusamehewa basi toba ilihitajika sana.

 2. Mfalme Hezekia aliomba ili aupate msamaha wa MUNGU wa kukizuia kifo na hakika kikazuiliwa.

Isaya 38:1-5 ''Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.  Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA,  akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema,  Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.''

Inawezekana kabisa Hezekia hakuwa au hakujua kama  ana dhambi lakini unyenyekevu wake kwa MUNGU na toba yake iliondoa ugonjwa uliotaka kumwua na MUNGU akampa kuishi miaka mingine 15.
Je wewe umewahi kuumwa ukaomba toba kwa ajili ya kulichosababisha uumwe?
Wengi hulalalimika tu kwanini wanaumwa wakati wao ni watoaji sahihi wa sadaka na zaka.
Ndugu toba haitakiwi kuangalia unafanya nini au umefanya nini, kutubu ni muhimu sana ndugu.
Je wewe umewahi kutubu kwa ajili ya kwanini hujaolewa/Hujaoa hadi sasa kwa sababu ya kukosa Mchumba?
Je Umewahi kutubu kwa ajili ya matatizo yaliyokupata? Au unajihesabia tu haki kwamba wewe huna dhambi na ni mtakatifu sana tena huwa unamtumikia MUNGU sana.
Ndugu kumtumikia MUNGU ni muhimu sana, kutoa matoleo ni muhimu sana sana lakini na toba nayo ni muhimu sana pia.
Ninachoweza kusema ni hiki; Tubu kwanza kwa ajili ya kilichosababisha tatizo ndipo uombe kutoka katika tatizo na hakika utatoka kwa jina la YESU KRISTO.
Warumi  2:4-8 '' Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa MUNGU wakuvuta upate kutubu?  Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya MUNGU,  atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;  wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele;  na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;   '' 

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments