TENDO LA NDOA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze.
Leo inawezekana kabisa kichwa cha somo kikawa kinaleta mshtuko kidogo lakini acha tujifunze.
Tendo La Ndoa Huitwa Hivyo Kwa Sababu Hufanyika Tu Katika Ndoa, hilo ndilo jambo muhimu zaidi kujua.
Tendo ni kitendo na kitendo ni kitu kinachofanyika na kitu kicho kwenye ndoa  kinaitwa Tendo la ndoa.
Waebrania 13:4 '' Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu.'' 
Katika andiko hilo kuna mambo makuu matatu ambayo nataka tuyajue ndani ya somo la leo.
1.Kuna ndoa.
2. Kuna wazinzi
3. Kuna waasherati.
Ndani ya ndoa ndimo kunapatikana pia tendo la ndoa.
Nje ya ndoa kuna wazinzi na waasherati kwa watu wale wanaohusiana kimwili wakiiga Ndoa.
Kwa ambao ni vijana na muda wao wa kuoa au kuolewa haujafika Biblia inawaamuru kuzikimbia tamaa za ujanani ambazo wakizitii zitawafanya wawe waasherati, hivyo kuzikimbia tamaa za ujanani matokeo yake ni pamoja na kuukimbia uasherati.

2 Timotheo 2:22 '' Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi.''

Kwa walio ndani ya ndoa Biblia inawataka kuziheshimu ndoa zao maana wakitoka nje ya ndoa zao watakuwa wazinzi na Biblia katika andiko la kwanza imejulishwa kwamba wazinzi na waasherati MUNGU atawahukumu yaani wasipotubu na kuacha uovu wao wataenda jehanamu.
Ndio maana Biblia inayaunganisha mambo mawili hayo yaani uasherati na uzinzi ni uzinifu na MUNGU anaonya akimwambia kila mwanadamu kwamba asizini.
Hiyo iko  Kutoka 20:14 ''Usizini''
 Ukiambiwa usizini maana yake usifanye uasherati wewe kijana na usifanye uzinzi wewe mwanandoa.
Wazinzi ni akina nani?
Wazinzi ni wanandoa ambao wanatoka nje ya ndoa zao na kufanya ngono na watu wa aina yeyote.
Waasherati ni akina nani?
Waasherati ni ambao hawajaingia katika ndoa lakini huwa wanashiriki ngono iwe na wachumba zao au hata watu wowote wale.
Najua kabisa kila mmoja anajua tendo la ndoa ni nini lakini ujumbe wangu hasa  umelenga haya yafuatayo.
Nje Ya Ndoa Hakuna Tendo La Ndoa Ila Kuna Tendo La Ngono Tu. Nje Ya Ndoa Kuna Tendo La Uasherati.
 Nje Ya Ndoa Kuna Tendo La Uzinzi. 
Nje Ya Ndoa Kuna Tendo La Uzinifu. 
Nje Ya Ndoa Kuna Ukahaba Na Umalaya Tu.
Makundi hayo yote Biblia inasema kwamba watu watendayo mambo ya aina hiyo wajawaurithi uzima wa milele.
1 Kor 6:9 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,'' 
 
Neno la kigiriki lilitafsiriwa kumaanisha uasherati ni neno linaloweza kumaanisha kila aina ya uchafu wa kimapenzi kama zinaa, uasherati, ukahaba na kadhalika.
Kama Kuna Mtu Hudhani Anafanya Tendo La Ndoa Wakati Hayuko Katika Ndoa Huyo Anajidanganya Nafsi Yake. Japokuwa Vitendo Vya Tendo La Ndoa Vinafafana Na Vitendo Vya Tendo La Ngono Au Vitendo Vya Uzinifu Lakini Tendo La Ndoa Sio Dhambi Lakini Uzinifu Ni Dhambi Mbaya Na Uzinifu Umewapeleka Wengi Kuzimu. 
Kwa kanisa la MUNGU Biblia inashauri kwamba '' Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;  si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU-1 Thesalonike 4:3-5''

Kama Binti Unatembea Na Mume Wa Mtu Na Kujiona Umefanya Tendo La Ndoa Nakupa Pole Sana Maana Usipotubu Na Kuacha Uchafu Huo Ujue Jina Lako Halimo Kwenye Kitabu Cha Uzima. 
 Ufunuo 21:8 '' Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.''

Kama Kijana Unatembea Na Mchumba Wako Na Kujiona Umefanya Tendo La Ndoa Nakupa Pole Sana Maana Kuna Waliowahi Kufanya Kama Wewe Na Hawako Mbinguni Baada Ya Kufa Kwao. 
Masomo  Kama haya  Huwa yinaamsha Hasira Za Watu Ila Mwenye Sikio La Kusikia Na Asikie Leo. 
YESU Anaokoa Ukiamua Wewe akuokoe na utijenge na maovu yote ikiwemo uzinzi na uasherati.
Biblia Ndio Inayosema Kwamba Hakuna Mbingu Ya Wazinzi Wala Waasherati Ikiwa Na Maana Kwamba Mzinzi Akiokoka leo Na Akaacha Uzinzi Wake, Huyo Haitwi Tena Mzinzi. 
 Kama Inakuhusu Mpendwa Ni Muhimu Tu Kutubu Na Kumpokea YESU Na Kujitenga Na Uzinzi Au Uasherati. 
Jambo Jingine Ni Kwamba Tunahubiri Mtandaoni Kwa Sababu MUNGU Ametuambia Tufanye Hivyo, Hizo Ni Huruma Za MUNGU Hakika Na MUNGU Alisema Kizazi Kijacho Chote Kitakuwa Busy Mtandaoni Tu Ndio Maana MUNGU Akataka Neno Lake Liwatangulie Watu Hao Ili Asiwepo Mwenye Uzuru.
 Wagalatia 5:19-21 '' Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.''
 
Nini kinazaliwa katika tukio la kufanya mapenzi?

1. Kunatengenezwa agano.
A. Agano la ndoa  kwa wanandoa waliofunga ndoa takatifu.
 Mwanzo 2:24 '' Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''
Watu wawili tofauti wa jinsia mbili tofauti kufanyika mwili mmoja ni agano. Agano hilo hufanyika baada ya kufunga ndoa yao takatifu mbele za MUNGU.
Kuwa mwili mmoja ni agano
B. Agano la kipepo kwa wazinzi na waasherati.
1 Kor 6:16 ''Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.'' 
Aliyeunga na kwa sababu ya uzinzi na uasherati ni mwili mmoja na ni agano lakini ni agano baya.
Hata kufanya mapenzi na majini ni agano lakini la kipepo.
Ni lazima mtu wa MUNGU avunje maagano hayo ndipo itamsaidia hata kuingia katika ndoa takatifu.

2. Kama ni majira ya uzao  Mimba hutungwa wakati huo.
Mwanzo  4:1 '' Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA.''
Adamu akamjua mkewe yaani Adamu na Eva wakafanya tendo la ndoa na tukio hilo likapelekea Eva kupata Mimba na kisha kuzaa mtoto. 
Hiyo ni moja ya matokeo ya tendo la ndoa.

 Tendo la ndoa sio ndoa lakini haiwezekani ndoa bila tendo la ndoa. Wanandoa kama wanavyothamini tendo la ndoa basi na maisha ya ndoa yote wanatakiwa kuyathamini.
Tendo la ndoa ni haki ya kila mwanandoa kutoka kwa mwenzi wake pekee waliofunga naye ndoa.
Tendo na ndoa ni ndani ya ndoa tu.
Wachumba Kufanya Mapenzi Mara Baada Ya Posa Ni Dhambi. Posa Haihalalishi Ngono.  Neno la  Mungu ni taa humulika kote hivyo kwa wewe unayefanya uasherati kwa kujihalalishia nakuomba acha dhambi  hiyo na utubu.
 Wagalatia 6:7 '' Msidanganyike, MUNGU hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.''

Ukipanda uzinzi utavuna uharibifu.
Ukipanda uasherati utavuna jehanamu usipotubu na kuacha.
Ukipanda uzinifu utavuna jehanamu ya moto usipotubu.

 Kwa wanandoa mlio katika ndoa takatifu nina neno moja pia kwenu la mwisho; wivu unaotengeneza kutengana, ugomvi, faraka na vita ni wivu uliotengenezwa na shetani.
 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments