USIMDHARAU ADUI YAKO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe Kanisa.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Somo letu leo linasema Usimdharau adui yako. Neno adui  lina maana zifuatazo.
1. Adui ni kiumbe au mtu anayemtendea mwingine uovu.
2. Adui ni jambo lolote linalodhuru au kuharibu.
3. Adui ni mtu unayegombana naye au kushindana naye.
4. Adui ni yule mnayepigana naye vita.
5. Adui ni mtu au kiumbe mwenye mpango mbaya dhidi yako.
Ndugu Usimdharau adui yako.

Zaburi 6:9-10 ''BWANA ameisikia dua yangu; BWANA atayatakabali maombi yangu. Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.'

Baada ya maelezo hayo naomba nianze na jambo moja ambalo watu wengi tunachanganya sana.
 Siku moja nilifundisha somo kuhusu Maombi ya Kuwaharibu maadui wa sirini, Kuna watumishi baada ya kusoma somo hilo walinipinga sana wakisema kwamba Bwana YESU alisema tuwaombee maadui zetu. 
Maadui wa sirini niliowataja ni roho za uchawi, majini, mizimu, wakuu wa giza  na nk. 
Watu wanashindwa kuelewa aina za maadui ambao Bwana YESU aliwazungumzia. 
Ukweli Bwana YESU aliwazungumzia maadui wanadamu tunaoshindana nao katika hali ya kawaida, tunaishi nao, japokuwa wanakusudia kutudhulumu au kutuonea kazini lakini tukimuomba MUNGU wetu anatushindia. Bwana YESU hakuzungumzia adui zaidi ya hapo, hakuzungumzia jini wala mizimu.
Vita yetu tunaipigana kwenye ulimwengu wa roho hivyo huko haijalishi adui ni nani, ni lazima tupigane naye kwa maombi na MUNGU wetu atatushindia.Kumbuka Biblia inasema 
 ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama- Waefeso 6:12-13'' 

Bwana YESU hakuzungumzia kwamba tumuombee shetani au mizimu au wakuu wa giza au majini au mwanadamu anayetumia nguvu za giza kutaka kutuua, hiyo roho ya kishetani ndani yake lazima tuiue kwa damu ya YESU ndipo atabaki yeye akiwa mtu safi, akishupaza shingo MUNGU wetu anaweza kumwangamiza kabisa.
Ni wachawi wengi sana wamewahi kufa baada ya kushindana na watu wa MUNGU.
Kwanini MUNGU awaue? Kama wewe ukimtii na kutembea kwenye kusudi lake hakika yeye atakuwa adui wa adui zako.
Biblia inasema '' Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.-Kutoka 23:22''

Kumkabili Ibilisi na mawakala zake Kunahitaji Uhusiano Mzuri Kati Yetu Na MUNGU Baba Yetu Wa Mbinguni. 
Ndugu Usiwatukane Wachawi Wakati Ukijua Kabisa Kwamba YESU KRISTO Hayuko Upande Wako.
Uhusiano Wa Mtu Na MUNGU Huwa Unaweka Mamlaka Ya Kiungu Ndani Ya Mtu Huyo. 
Chimbuko La Miujiza Sio Kulitaja Tu Jina La BWANA YESU Bali Uhusiano Wetu Na Yeye.
Usimdharau adui yako lakini kabla ya kumsambaratisha hakikisha kwanza upo upande wenye nguvu yaani umeokoka na unaishi maisha matakatifu yanayompendeza Bwana YESU. 
2 Kor 5:17 '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''

 Ndugu una maadui wengi sana katika ulimwengu wa roho, kuwashinda hao unatakiwa uwe muombaji na unaenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Shetani ana mbinu nyingi sana lakini ukiwa na ROHO wa MUNGU shetani na mawakala zake hawana ujanja wowote.
Tabia ya mapepo ni kukunyonya kiroho ili yakupate kimwili. Kataa nguvu hizo za giza na jitenge mbali nazo siku zote za maisha yako. Damu ya YESU pekee ndio inayoweza kukuweka mbali na nguvu hizo za giza. 
Mkimbilie Bwana YESU kwa maombi utashinda.
Bwana YESU anasema ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu.-Yohana 14:13-15''

Bwana YESU ni mshindi na ukimtegemea kwa maombi na utakatifu hakika hakuna adui katika ulimwengu wa roho atakuweza.
Kutoka 15:3 "BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake."
Maana ya andiko hilo ni kwamba MUNGU ni shujaa wa vita, ni shujaa katika vita yote.
Ni MUNGU anayeweza kukushindia muda wowote na popote.
Kutoka 15:26 " akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye."

MUNGU anachotaka ni wewe tu usikie sauti yake na maagizo yake na kuitii hakika utafanikiwa sana.
Yeye MUNGU ni shujaa wa vita na ukitembea kwenye utakatifu wake hakika kupitia maombi yako utashinda kila vita.
Maombi ni vita na Bwana YESU ni wa vita, na katika vita yeye ni mshindi.
Wana wa Israeli walimfahamu MUNGU Kama BWANA wa majeshi maana hajawahi kushindwa katika vita yeyote.
MUNGU aliyewashindia Israeli ndiye MUNGU pia ambaye anaweza kukushindia wewe, Kama ukiomba kwa imani na utakatifu katika KRISTO.

''Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;-Mathayo 7:7''
Ndugu yangu unayo fursa nzuri ya kuomba Leo na kushinda.
Shujaa wa vita yuko tayari kukushindia Leo.
Omba ndugu na kuna ushindi katika hitaji lako hilo.

Maombi Yako Ya Leo Ni Akiba Yako Ya Baadae. Ndugu Omba.
Usidharau Hata Dakika 1 Ambayo Utaitumia Kwenye Maombi Kwani Dakika Hiyo Ni Muhimu Sana Kwako. 
Pia Usikubali Kumpa shetani Hata Dakika 1 Katika Maisha Yako Yote.
Kibali chako kinatafutwa na adui zako kwenye ulimwengu wa roho ili usifanikiwe, usiwadharau bali pambana kimaombi.
Hata kibali chako cha kuamka salama na kukaa salama kinatafutwa na adui.
Kibali chako cha kufanikiwa kinatafutwa na adui,
usiwadharau bali pambana kimaombi. 
Kibali chako cha kupata mchumba kinatafutwa na adui, usiwadharau maadui zako katika ulimwengu wa roho bali pambana kimaombi. 
Kibali chako cha kuhudhuria ibada kanisani kinatafutwa na adui.
Kibali chako cha kuwa mzima Siku zote kinatafutwa na adui,
usiwadharau maadui zako katika ulimwengu wa roho bali pambana kimaombi.
Ndugu yangu nakuomba kwamba husika zaidi na MUNGU kwa maombi na utakatifu ndipo kibali chako kitakaa salama siku zote.
Shetani anaweza kujaribu kukuondolea kibali chako kwa njia nyingi lakini ndugu mtii KRISTO na neno lake utakaa salama.
Shetani anaweza kutaka kukuondolea kibali chako kwa njia ya kukuvunja moyo.
Shetani anaweza kuuharibu ufahamu wako na njia hiyo ikakuondolea kibali chako.
Ziko njia nyingi adui anaweza kuzitumia ili kukuondolea kibali chako ila nakuomba mtii MUNGU na neno lake utashinda.
Labda nikuulize swali,
Je katika hayo unayoyaendea una kibali cha MUNGU?

Ndugu, omba na usiwadharau maadui zako.
Bwana YESU yuko katikati yako ili kukushindia.
Mathayo 18:19-20 ''Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na BABA yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.''

Pambana na maadui zako kiroho na sio kuwaangalia tu.
Kumbuka Tunafunga milango ya nyumba zetu usiku kwa sababu hatutaki upinzani kutoka nje utujie.
Wanyama, wadudu na wezi huo ni upinzani kutoka nje.
Upo pia upinzani kutoka ndani na huo ndio upinzani mbaya zaidi.
Upinzani unaoupata katika ndoa yako huo ni upinzani wa ndani.
Upinzani kwenye familia au ukoo huo ni upinzani wa ndani.
Magonjwa ni upinzani kutoka ndani.
Sijui huwa unaushughulikia vipi upinzani wa ndani.
Zaburi 37:39-40 " Na wokovu wa wenye haki una BWANA; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. Naye BWANA huwasaidia na kuwaopoa; Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa; Kwa kuwa wamemtumaini Yeye."


Ndugu, hata kama unakutana na upinzani kutoka ndani lakini Biblia inasema Wokovu wa mwenye haki una BWANA.
Wokovu wa mwenye haki una MUNGU.
Ushindi wa mwenye haki una MUNGU.
Uponyaji wako uko katika jina la YESU KRISTO.
Mtegemee YESU ndugu hakika utashinda.
Maadui wa ndani wanaweza kukuzuia usifanikiwe katika jambo Fulani ukiambatana na Bwana YESU hakika utashinda.
Ukiamua kuomba huku ukidumisha utakatifu hakika kuna kushinda.

Madui wa ndani ni hatari sana lakini yuko MUNGU anayeweza yote, ukiomba atakushindia.
Nahumu 1:9 " Mnawaza nini juu ya BWANA? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili."


 Hata kama adui ni mdogo usije ukamdharau.
Dhambi ni adui yako maana usipotubu dhambi inaweza kukupeleka jehanamu.
 Inawezekana kabisa unasema una ka dhambi kadogo tu hivyo unawaona wengine kuwa ni waovu sana, lakini napenda kukuambia kwamba dhambi hiyo hiyo ndogo inaweza kukufikisha jehanamu sawasawa na wale wa dhambi kubwa.
Waristo wengi leo humdharau shetani. Ni kweli kabisa shetani hana nguvu kwetu maana tuna YESU KRISTO lakini hatutakiwi kumdharau bali kupambana nae.
Usimdharau adui yako.
Goliathi alimdharau Daudi lakini mwisho alikatwa kichwa na huyu huyu Daudi aliyemdharau Mwanzo.
Watu wengi hulidharau Neno la MUNGU lakini siku zote huwa najiuliza, Kama unalidharau Neno la MUNGU je MUNGU akikudharau wewe itakuaje? 

Mithali 3:34 ''Hakika yake(MUNGU) huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.''
 
Mungu akikudharau ni hatari sana kwako.
Jambo jingine ni kwamba Dharau ni binamu yake kiburi.
Hawa wawili hawafai hata kidogo.
Hawa wawili ni maadui zetu hivyo tusiwadharau bali tuwaondoe maishani mwetu.

 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments