KUVUMILIA HUKU UKIOMBA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Uvumilivu kwa Mteule wa MUNGU ni jambo la muhimu sana.
1 Thesalonike 5:14-22 '' Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; VUMILIENI na watu wote. Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya MUNGU kwenu katika KRISTO YESU. Msimzimishe ROHO; msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna.'' 
Uvumilivu ni silaha mojawapo kubwa ya kumshinda shetani na mawakala zake lakini uwe ni uvumilivu unaoambatana na maombi.
Inawezekana unapitia magumu sana lakini naomba utambue kwamba licha ya magumu yako kukulemea lakini magumu hayo hayajamzidi Ayubu ndio maana nakuomba uvumilie ndugu yangu kama alivyovumilia Ayubu maana Ayubu alipitia magumu kuliko wewe ila alivumilia na akashinda, na wewe vumilia.
Ayubu 2:7-10 ''Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru MUNGU, ukafe.
 Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa MUNGU, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.''

 
Ayubu aliugua kuliko wewe lakini kwa kuvumilia na maombi alishinda na kuongezewa miaka ya kuishi duniani.
Ayubu alifiwa na watoto wake saba kwa Siku moja lakini jambo hilo halikumfanya amkufuru MUNGU kama ambavyo wewe kwa kuugulia tu unataka kumkufuru MUNGU.
Ndugu, vumilia huku ukiendelea na maombi na Bwana YESU atakushindia.
Unajiona mgonjwa kwa sababu hujawaona wagonjwa.
Unajiona huwezi kuolewa lakini kuna wenye umri kuliko wako wanaoolewa kila Mara na unashuhudia ndoa zao. 

Unajiona huwezi kupata kazi maana umejaribu mara kumi bila mafanikio, ndugu wapo waliopata kazi  wakiwa na vyeti vya kawaida kabisa, sio kama chako na walivumilia kuliko wewe na sasa wanafurahia kazi nzuri ambazo MUNGU aliwapa.
Unajiona huwezi kuzaa kwenye ndoa yako ya miaka 10 tu hata unataka kuwakimbilia mashetani kwa waganga, Ndugu vumilia maana wapo akina Isaka waliishi miaka 20 ndani ya ndoa bila mtoto na bado MUNGU alikuja kuwabariki uzao uliotengeneza taifa teule la Israeli.
Akina Sarah walizaa hata katika miaka 90, walivumilia na MUNGU hakuwaacha.
Vumilia ndugu na ushindi wako upo tu.
Waebrania 5:13-15 ''Kwa maana MUNGU, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na hivyo KWA KUVUMILIA akaipata ile ahadi.''
 Ndugu inawezekana kabisa MUNGU alishasema na wewe hivyo vumilia na atatimiza.
Usiogope maana Bwana YESU anakuandalia ushindi wako. Waliokucheka wataanza kulia kipindi wewe umekumbukwa na MUNGU.
Vumilia ndugu kama alivyovumilia Ayubu hadi akapata ushindi na baraka double Double.


1 Petro 2:19-25 '' Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka MUNGU, pale ateswapo isivyo haki. Kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi? Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za MUNGU. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana KRISTO naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.''
 
 Inawezekana sana unatamani kuingia katika ndoa lakini kuna vikwazo unapitia, ndugu waliofanikiwa kufunga ndoa hata wao walipitia vikwazo lakini walipomtegemea MUNGU na kuvumilia walishinda.
Naamini hata wewe utashinda na muujiza wako wa kufunga ndoa utafika tu.
Songa mbele na YESU kwa utakatifu na Maombi hakika kesho yako ya baraka ya ndoa itafika tu.
Ipo Siku waliokucheka watanuna huku wewe ndio ukiwacheka.

Ili ufikie baraka zako wakati mwingine inahitaji uvumilivu na maombi.
Usikubali kuzimia njiani.
Usikubali kubadili njia njiani kwa kwenda kwa waganga.
Ndugu wala usikubali kutumia nguvu za giza kutafuta muujiza wako.
Kumbuka shetani kazi yake ni kuiba, kuchinja na kuharibu.
Yohana 10-:10A ''Mwivi(Shetani) haji ila aibe na kuchinja na kuharibu''
Shetani anaweza kuja kwa wema mwanzo kumbe anaandaa uharibifu wako na hata kifo chako, usikubali kumpa nafasi hata moja. Unaweza kwenda kwa waganga ili upate mtoto na mtoto huyo kwa sababu ametokana na shetani basi baadae akawa nyoka na kukuangamiza wewe uliyemzaa.
Mngoje MUNGU ndugu na sio kwenda kwa waganga.
Vumilia huku ukiomba katika jina la YESU KRISTO.
Unapokuwa kwenye Maombi maana yake unajipa moto zaidi kiasi kwamba adui hawezi kukusogelea.
Maombi ni silaha Kuu ya kukupa ushindi.
Maombi katika jina la YESU ndio ushindi wako na uzima wako.

Mathayo 7:7-11 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;  kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana BABA yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?
''

 
 Kumbuka hii ndugu; Kuwakosea watu sio mpaka ufanye mabaya tu, hata ukitenda mema kuna wengine unaweza ukawakwaza kwa kutenda kwako mema, hivyo unaweza pia kuwaomba msamaha watu kwa sababu umetenda mema ili kama kuna mtu umemkosea kwa sababu umetenda mema basi ajue ana wajibu wa kukusamehe, asipokusamehe ni hatari kwake. Kwa sababu umetenda mema basi endelea kutenda mema na usiache kutenda mema hata Siku moja, kama kuna watakaokwazika kwa sababu umetenda mema wambie tu wakusamehe ila endelea kutenda mema.
 Wewe mteule ni mfano wa Mwisraeli katika utu wako wa ndani na kuna taifa unapigana nalo rohoni kila Mara. Nguvu za Giza ni taifa unalopigana nalo. Mawakala wa shetani ni taifa lake nalopigana nalo, N.k
Israel walikuwa wanapigana kila Mara walipokuwa katika safari yao ya kaanani hivyo ndugu endelea kupigana vita ya rohoni na ushindi wako upo kwa YESU Mwokozi wako.

Kumbuka Wanadamu wana maneno lakini MUNGU analo Neno, na Neno la MUNGU lina uponyaji ndani yake
Kufanya wema machoni pa watu ili kupata sifa
Yesu alitoa maonyo makali kwa wafuasi wake wajiepushe na unafiki kwa kutamani kufanya wema wa aina yoyote kwa nia ya kujitafutia umaarufu ''Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya hivyo, hampati thawabu kwa BABA yenu aliye mbinguni.-Mathayo.6:1

 Unaposhinda jaribu MUNGU anakupandisha viwango vingine kiimani, ila liwe ni jaribu ambalo hukusababisha wewe kwa tamaa zako na kiburi chako.
Katika jaribu kama hilo inakupasa sana kuvumilia huku ukiomba.
Inawezekana kabisa wakati mwingine una maadui wengi kuliko marafiki, hiyo idadi kubwa ya maadui kuliko marafiki wala isikuumize kichwa kama YESU KRISTO ni Mwokozi wako na wewe humuomba MUNGU Baba kwa yeye.
Adui hana lolote hata moja kwa Mfalme YESU KRISTO.
Unataka kujua zaidi?
Ahadi ya MUNGU kwa wewe unayeishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO na ni muombaji ni hii.

Isaya 54:15 "Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako."

Ndugu hatuna cha kupoteza hata kimoja, kazi yetu ni
1. Kuishi maisha matakatifu.
2. Kuomba katika ROHO MTAKATIFU
3. Kumtumikia KRISTO kwa moyo.

4. Kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.

Yakobo 5:8 '' Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia.'' 

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments