MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUTANGULIE KATIKA BARAKA YAKO IJAYO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la maombi.
Siku moja ijumaa usiku  Roho wa MUNGU alinijulisha juu ya kufundisha ujumbe huu wa kumwambia MUNGU atutangulie katika katika matukio ya baadaye yanayotuhusu.  ROHO wa MUNGU akanipa ujumbe huu na andiko la Mwanzo 39:21 Linalosema '' Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.''

Kila Mteule wa MUNGU  kuna matukio mengi mbele yake ambayo yanahitaji MUNGU awe pamoja na mteule huyo ndipo huyo ndugu atafanikiwa.
Inawezekana mbele yako kuna kupata Mchumba, kuna kufunga ndoa na kuna kuishi maisha ya ndoa.
Inawezekana mbele yako kuna kuanza shule.
Inawezekana mbele yako kuna kuomba kazi.
Inawezekana mbele yako kuna kusafiri.
Inawezekana mbele yako kuna kukutana na watu fulani wa ofisini.
Inawezekana mbele yako kuna kuajiriwa.
Ni mambo mengi mno yako mbele yako ndugu lakini naomba nikuambie kwamba unahitaji kumwambia MUNGU Baba akutangulie katika baraka yako hiyo itakayokuja.
Hata kama baraka hiyo unataka uipate miaka 15 ijayo bado unahitaji kumwomba MUNGU ili akutangulie, na hakika MUNGU atakutangulia na kukufanikisha maana yeye hasahau wala hachoki.
Unaweza ukaomba maombi leo na maombi hayo yakaja kukuvusha katika baraka yako ya miaka 20 ijayo.
Katika andiko hilo la Mwanzo 39:21 nililopewa tunajifunza mambo yafuatayo;
1. Ili Yusufu afanikiwe ni lazima MUNGU awe pamoja na yeye.
2. Ili Yusufu afanikiwe ni lazima MUNGU amfadhili.
3. Ili Yusufu afanikiwe ni lazima MUNGU ampe kibali kwa wanadamu.
Katika baraka yako ijayo unahitaji MUNGU awe pamoja na wewe, unahitaji MUNGU akufadhili na unahitaji Kibali cha MUNGU.
Hayo yatafanyika vyema kipindi MUNGU akikutangulia, akawa pamoja na wewe kuanzia sasa hadi utakapoipokea baraka yako na hadi ukiwa na baraka yako.
Akikutangulia MUNGU atakuwa pamoja  na wewe katika wakati huo wa kupokea baraka yako.
Akikitangulia MUNGU atakufadhili ili upokee hitaji lako uliloomba kwake.
Akikutangulia MUNGU hakuna atakayekupinga.
Akikufadhili MUNGU hakuna atakayekupinga.

Zaburi 136:26 '' Mshukuruni MUNGU wa mbingu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.''
 Akikufadhili MUNGU, wachawi wanaotaka kukuzuia ili usipate baraka yako hawatakuona wakati wa kupokea baraka hiyo.
 Ni muhimu sana kumuomba MUNGU akutangulie katika matukio yajayo yanayokuhusu.
Akikutangulia MUNGU atakupa kibali mbele ya wanadamu ambao watahusika na kufanikiwa kwako katika baraka yako.

Yakobo kabla hajaanza safari ya mbali ambayo ingempa mke, watoto na familia alihitaji kumuomba MUNGU amtangulie katika yote.

Mwanzo 28:20-22 ''Yakobo akaweka nadhiri akisema, MUNGU akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa MUNGU wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya MUNGU; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.''
 Safari ya Yakobo ilikuwa na mambo mengi ndani yake, na hayo yote Yakobo aliomba MUNGU amtangulie na kumfanikisha.
Yakobo alikaa ugenini kwa miaka 21 na jambo la ajabu ni kwamba alienda akiwa hata chochote lakini alirudi akiwa na familia kubwa na mali nyingi sana.
 MUNGU alimtangulia Yakobo na kumbariki sana kuliko hata wenyeji wake.
MUNGU alimpa familia na kumlinda na kumbariki kwa kila jambo.
Ndugu, Katika mambo muhimu unayohitaji kwa MUNGU ni pamoja na MUNGU kukutangulia katika matukio ya baadae yanayokuhusu.
Inawezekana kabisa una mpango wa kuwa mfugaji au mkulima, hapo pia unamhitaji MUNGU akutangulie.
Inawezekana kabisa unataka kugombea nyadhifa serikalini, unamhitaji MUNGU akutangulie.
Inawezekana kabisa una mpango wa kwenda kuishi mji fulani, unamhitaji MUNGU akutangulie.
Maombi yako ya leo yanaweza kumfanya MUNGU akutangulie na kukufadhili na kukupa kibali na utastawi sana.
MUNGU akikutangulia ndugu yangu hakika utashinda kirahisi sana sana.
Wewe Binti ukiomba MUNGU akutangulie katika uchumba unaotegemea kuingia, ukidumu katika utakatifu hakika MUNGU atakuwa pamoja na wewe na kukufanikisha kirahisi sana.
Wewe kijana ukimuomba MUNGU akutangulie katika Interview ya kazi iliyoko mbele yako hakika utafanikiwa kirahisi maana MUNGU atakuwa pamoja na wewe, atakufadhili na kukupa kibali kwa watu wote.
Ni muhimu sana kumuomba MUNGU akutangulie.
Mbele yako kuna mambo mengi sana  na hayo yote unamhitaji MUNGU akutangulie.
Inawezekana mbele yako kuna kusomesha.
Inawezekana mbele yako kuna kujifungua.
Inawezekana mbele yako kuna mkutano
Inawezekana mbele yako kuna kesi ya kusingiziwa na hapo unahitaji kuvuka salama.
Inawezekana mbele yako kuna  kusubiri matokeo.
Inawezekana mbele yako kuna Kujenga Nyumba.
Inawezekana mbele yako kuna Kununua gari n.k
Ndugu, katika mambo yote yaliyoko unamhitaji MUNGU akutangulie ili ufanikiwe.
MUNGU aliwatangulia wana wa Esraeli, hivyo na wewe mwambie akutangulie katika safari yako na hatua zako.


 FAIDA ZA KUMUOMBA MUNGU AKUTANGULIE KATIKA TUKIO LAKO LIJALO.

1. MUNGU atakuwa na wewe hata wakati wa kupokea baraka yako.
Zaburi 50:15 ''Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.''
Wakati wa Kumwita MUNGU ni tofauti na wakati wa kupokea, Ukimwita MUNGU atakuwa na wewe hadi wakati wa kupokea kwako na ndipo utamtukuza.

 2. MUNGU atakutangulia na kufuta vikwazo vya kukuzuia kupokea.

Kutoka 13:21-22 ''BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.''

3. MUNGU ataitunza baraka yako hata uimiliki.
Habakuki 2:3 '' Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.''

 4. MUNGU atakulinda wewe ili uifikie baraka yako na kuimiliki.
Hesabu 6:24-26 '' BWANA akubarikie, na kukulinda;
BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili;
BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.''

5. Utafanikiwa kwa urahisi.
Mathayo 7:7-8 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.''

6.  Inaongeza Imani na  uhakika wa kufanikiwa, Maana kwa imani utabaki ukijua kwamba MUNGU amekutangulia.
1 Samweli 2:1-5 '' Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;  Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.  Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.  Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.''
 Hana aliomba kwa imani kwamba MUNGU atampa watoto saba.
Wakati anaomba Hana alikuwa tasa lakini ni kweli baadae MUNGU alimpa watoto 6.

7.  MUNGU atakuongoza kuifikia baraka yako uliyoomba kwake.
Isaya 49:10 '' Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.''

 Ndugu, Inawezekana kabisa ukakutana na vikwazo vingi sana, lakini kama una uhakika kwamba MUNGU yuko pamoja na wewe hata katika baraka unayoiendea hakika hutaogopa wala kukata tamaa.
Naomba ulijue pia jambo hili ya kwamba hivi ndivyo vikwazo vikubwa vinavyoweza kumfanya MUNGU asiambatane na wewe hata kama  uliomba akutangulie.
1. Dhambi.
2. Kutokumwamini MUNGU.
3. Kukataa maongozo ya ROHO MTAKATIFU.
4. Kutokumwomba ROHO MTAKATIFU akufundishe nini cha kufanya au kuongea wakati wa kupokea baraka yako.
5. Kutokulitii Neno la MUNGU.

Jitenge na mambo hayo matano baada ya maombi yako ya kumwambia MUNGU akutangulie katika baraka yako ijayo.
MUNGU akupe ushindi mkuu katika maombi yako ya leo.
Kwa leo sitaandika maombi maana ni vigumu mno kujua malengo ya kila mtu ya baadae lakini nakuomba ndugu omba MUNGU katika kila hitaji lako la baade ili MUNGU akutangulie, awe pamoja na wewe hadi wakati huo, akufadhili na akupe kibali.
 
 
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments