MAOMBI YA KUOMBEA SIKU, NYAKATI NA MAJIRA YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu.
Majira ni vipindi mbalimbali ndani ya wakati ulioamuriwa.
Nyakati ni vipindi kulingana na matukio yaliyoamuriwa.
Kuna majira ya kupata baraka fulani katika maisha na mtu, Mtu huyo asiposhirikiana na majira yake ya kupata baraka hiyo kutoka kwa MUNGU basi itamsumbua kupata baraka hiyo majira hayo yakipita.

Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''

Maana yake kila majira yana vitu yamebeba, kila nyakati ina matukio yake.
Unaweza ukang'ang'ana na jambo fulani na ikakusumbua sana kufanikiwa katika jambo hilo kwa sababu tu sio majira yake, majira yake yakifika ukigusa tu unafanikiwa hadi unashangaa.
Ni vyema sana kufanya jambo sahihi katika wakati sahihi.
Niliwahi kukaa Zanzibar kikazi, kuna wakati nikaota nahamia Dar es salaam. Nilijua nitahama lakini kuhama kulikuja ghafla sana kiasi kwamba kuna vitu vyangu nililazimika kuviuza kwa bei ya chini kupita kawaida, kuna vitu vya thamani hadi nililazimika kuvigawa tu kwa sababu nisingeweza kuvisafirisha maana uhamisho ulikuja ghafla mno. Hapo unaweza kujifunza kitu kwamba wakati mwingine huwa unajulishwa kwenye ndoto au maono ili ujue majira hayo na ujue ufanyeje.

Hebu tujifunze Neno hili, Yohana 4:1-4 ''Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake YESU alikuwapo.  YESU naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.  Hata divai ilipowatindikia, mamaye YESUakamwambia, Hawana divai. YESU akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.''
Bwana YESU baada ya kuja duniani kupitia Mariamu alikuwa na mamlaka ya mbinguni lakini hatuoni akifanya muujiza hadi wakati au majira sahihi yaliyoamuriwa na MUNGU yalipofika.
YESU alikuwa na uwezo wa kufanya miujiza yote akiwa na miaka hata chini ya kumi lakini hadi alipobatizwa akiwa na miaka 30 ndipo akaanza kufanya miujiza. Miujiza ambayo Bwana YESU alilifanya kwa miaka mitatu ni mingi kiasi kwamba hata Biblia isingetosha kuandika yote, ndivyo maandiko yasemavyo.
Tukio hili la Kana linaonyesha kwamba wakati wa Bwana YESU kufanya miujiza ulikuwa haujafika ndio maana akasema ''Saa yangu haijawadia''
YESU alikuwa na uwezo wa kufanya miujiza hata kama majira yake ya kufanya hivyo yalikuwa bado, lakini tunajifunza Kanuni ya MUNGU kutoka kwa Bwana YESU kwamba kuna majira ya mambo  fulani ndio maana akasema ''majira hayo yalikuwa bado kufika.
Ninaloweza kusema ni kwamba ukifanya jambo sahihi katika wakati sahihi wa jambo hilo matokeo yake huwa ni makubwa sana kuliko kufanya jambo sahihi lakini ni katika wakati usio sahihi.
Hata mvua zina majira yake, ukiacha kulima wakati wa mvua huku ukisubiri baada ya majira ya mvua kupita ndipo ulime hakika mazao yako yatakauka na hautapata mazao stahiki. Majira ni muhimu sana.
Wakati wako wa kuolewa au kuoa ukifika na wewe ukadharau basi itakuwa vigumu kuoa au kuolewa katika majira mengine. Mfano Kama mama amedharau kuolewa hadi akiwa na miaka 60 ndipo atake kuolewa hakika itakuwa vigumu sana. Majira nayo ni muhimu sana katika maisha yako ndugu.
Watu wengi sana ni waombaji na huomba na kufunga kwa maombi lakini baadhi yao hushindwa kushirikiana na majira yao ya baraka baada ya MUNGU kuwabariki.
Unaweza ukaomba MUNGU akupe kazi nzuri na MUNGU akayaleta majira ya wewe kupata kazi hiyo. Usipoyajua majira yako au usiposhirikiana na majira yako hakika hutapata kazi kwa muda huo.
Nakuomba litafakari sana Andiko tuliloanza nalo kwamba ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''

Ni vyema sana majira yako ya kuanza huduma ukayazingatia.
Ni vyema sana majira yako ya kuingia katika ndoa ukayazingatia.
Ni vyema sana majira yako ya kuzaa watoto ukayazingatia.
Kwa kila jambo kuna majira yake, hivyo ukipishana na majira yako hakika itakusumbua kufanikiwa katika jambo hilo ukiwa katika majira mengine.
Tunapofanya maombi maana yake tunaruhusu MUNGU atukutanishe na majira yetu ya kupokea kutoka kwake.
Hata katika Bustani ya Edeni MUNGU alikuwa na majira yake ya kumtembelea Adamu, MUNGU hakumtembea kila dakika au kila saa bali kila saa tisa alasiri ndipo MUNGU alikuwa anamtembelea Adamu. Ndio maana katika majira hayo siku moja MUNGU akamkuta Adamu hayupo katika eneo alilotakiwa kuwapo, kumbe amejificha baada ya kufanya dhambi ya kula tunda.
Kanisani kwa mfano  huwa najifunza mambo kadhaa na ninagundua ni majira yake hayo.
Kuna wakati mafundisho mengi yanakuwa ni ya kuwataka watu kuomba na kupigana vita ya kiroho. Waliokusudiwa wakiomba katika majira hayo hufanikiwa sana lakini majira ya mafundisho hayo kuna wakati yanakuwa hayapo  kwa muda mrefu Kanisani tena, wakati huo mafundisho labda yanakuwa ni kuhusu Imani.
Unaweza ukashangaa Mchungaji kwa mwezi mzima anakuwa kila somo analofundisha linawataka watu kuvumilia majaribu, baada ya muda kadhaa utashangaa ujumbe mwingi unakuwa ni kuhusu toba. Ninaamini kila majira yana kusudi la MUNGU kulingana na matukio ya majira husika.
Kwanini basi leo nakufundisha somo hili?
Ni kwa sababu shetani na mawakala zake kazi yao ni kuharibu majira yako yaliyokusudiwa na mbingu, hivyo lijue hili na uombe kwa jina la YESU KRISTO utashinda.
Nimewahi kushuhudia dada mmoja ambaye alikuwa na akili darasani lakini wakati wa mitihani kuanza aliugua ghafla na kushindwa kufanya mitihani vyema.
Kwa vyovyote vile yule dada angefaulu na kuendelea mbele lakini mawakala wa shetani walibadili majira yake. Kurudia masomo mwaka mzima ni kwa sababu ya kubadilishiwa majira kipepo au kwa mtu mwenyewe kutokana na uzembe wake katika majira sahihi.
Ukisoma Kitabu Cha Danieli 7:25 Utagundua kwamba kazi mojawapo ya mpingaKristo ni kubadili Majira na sheria(Neno la MUNGU).
Ukitaja mpingaKristo ndani yake lazima ujue kwamba wako wachawi, waganga, wakuu wa giza, washirikna, mizimu na kila roho ya kuzimu.
Hao wanaweza kuyabadili majira ya mtu kama mtu huyo hatajua kuomba.
Hebu leo kataa machawi kukubadilishia majira yako yaliyokusudiwa na mbingu ya kupata kazi, kuolewa, kuoa, kuzaa, kumtumikia MUNGU N.k
Omba leo ili ushirikiane na majira ya MUNGU ya kufanikiwa kwako.
Kumbuka 
Mithali 10:5 '' Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.''
Utumie vizuri wakati wako wa kupokea baraka uliyoomba kwa MUNGU.
 Isaya 49:8-9 ''BWANA asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho.''
Kazi yetu kama watu wa MUNGU ni kuomba na kazi ya MUNGU ni kutupa sawasawa na maombi yetu lakini ni lazima tujue kwamba MUNGU ana wakati wake pia wa kutupatia hizo baraka.
Ukiomba jambo na ukapokea hapohapo maana yake huo ni wakati wake na ni majira yake.
Ukiomba na kupewa wakati huo huo basi tambua kwamba majira yako yalikwisha fika siku nyingi sana ila tu wewe hukufanyia kazi.
Kuna majira mengine MUNGU ameweka kuwa majira ya kudumu kwa watakaomtii MUNGU.
Majira ya kufunguliwa ni ya kudumu, majira ya kuishi maisha matakatifu ni ya kudumu.
Ukiona umefunguliwa sasa kutoka vifungo vya kipepo ni kwa sababu umetambua sasa kwamba YESU anaweza kukufungua lakini ukweli ni kwamba hata kama ungemwendea YESU miaka kumi iliyopita bado angekufungua tu, kwa jinsi hiyo tunagundua kwamba tatizo katika majira ni letu wanadamu.
MUNGU anasema ''Wakati uliokubalika, nimekujibu'' 
Ndugu kuwa na ROHO MTAKATIFU ni muhimu sana maana kuna majira yakifika atakujilisha.
Kuna majira yakifika atakuelekeza jambo la kufanya kumbe ni katika kukusaidia tu ili ufanikiwe katika majira yako.
Unaweza ukapata msukumo wa kuomba sana na kufunga, kumbe hayo ni majira yako ya kufanikiwa katika baraka fulani ambalo ulikuwa umefungwa na sasa utafunguliwa na kupata baraka yako. Wengi huwa wanadharau majira muhimu kama hayo ambayo unajulishwa kuomba.

           KWANINI TUOMBEE MAJIRA, SIKU NA NYAKATI?

1. Kwa sababu MUNGU amepanga kila jambo kwa majira yake na kwa wakati wake.
Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''

2. Maana majira ya MUNGU kwetu yameambatana na baraka zetu.
Zaburi 3:8 '' Wokovu una BWANA; Baraka yako na iwe juu ya watu wako.''

3. Ili tupate kushirikiana na majira yetu yaliyoandaliwa na MUNGU.
Esta 4:14 '' Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?''

4. Ili  ROHO MTAKATIFU atujulishe wajibu wetu katika majira ya MUNGU wakati huu.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''

5. Ili kuyateka majira na nyakati,ili shetani asiyabadili majira ya baraka zetu.
Yeremia 30:1-3 ''Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,  BWANA Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia. Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema BWANA; nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki.''

 Kuna majira yakipita yamepita hivyo ili ufanikiwe katika jambo lako inakupasa usubiri majira mengine.
Ndugu husika na majira yako na wakati mwingine unaweza ukawa unaona katika ndoto au maono kumbe unajulisha nini cha kufanya maana majira yako yamefika.
Unatakiwa uwe mtu wa maombi sana na kujua maana ya ulichoona roho ikusaidie kujua majira yako na ujue ufanye nini.

 Wgalatia 6:9 '' Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.''
Huo wakati wa kupokea na kuvuna ungoje bila kuchoka maana majira hayo yatafika tu.

Je uombe nini juu ya majira, siku na nyakati?

1. Omba ROHO MTAKATIFU akufunulie jukumu lako katika majira yako ya baraka za MUNGU.
Kama huna ROHO MTAKATIFU unatakiwa uokoke na kuishi maisha matakatifu na maombi.

2. Teka majira yako ya baraka zako  ili mawakala wa shetani wasiyaingilie.
Unaweza hata ukafunga na kuomba lakini utakatifu katika KRISTO ni lazima liwe vazi lako la kudumu. 

3.Omba MUNGU akupe kushirikiana na majira yako ya baraka zako.




MUNGU akubariki sana sana na kama ukipenda kunisapoti katika huduma yangu kwa sadaka ya hiari ya kiwango chochote utakachopenda karibu na MUNGU akubariki sana, pia kitabu cha MAOMBI YA KINA kipo na wasiliana nami utakipata na ukifanyia kazi itakusaidia sana.
Hapa chini ni maombi ya kuombea majira, nyakati na siku
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.


MAOMBI YA KUOMBEA SIKU, NYAKATI NA MAJIRA YAKO.

Baba wa mbinguni hakuna kama wewe.
Ninakushukuru na kukuabudu YAHWEH MUNGU wa pekee muumbaji wangu.
Ninakushukuru MUNGU wangu maana uliniumba katika tumbo la mama yangu katika majira yako na ukanipa kuishi katika majira haya.
MUNGU wangu nakuomba unipe kuishi kwa kusudi lako katika majira yako kwangu na nifanye niliishi Neno lako la uzima.
Asante Bwana YESU kwa neema yako na kwa kuniokoa katika majira haya, ni neema yako tu na upendo wako tu wa kipekee.
BWANA niko hapa nikiombea majira yangu, siku na nyakati.
Ninajua kabisa kwa kila jambo katika maisha yangu kuna majira yake kutoka kwako MUNGU wangu.
Ninaomba majira hayo yasiingiliwe na shetani wala wakala wake, kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Nimekuomba MUNGU wangu katika mambo mengi na naomba BWANA nipe kushirikiana na majira yangu ya baraka.
Katika jina la YESU KRISTO ninaomba majira yangu ya kupata Mchumba na kisha ndoa yasiingiliwe na shetani, ninavunja mtego wa giza kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya kupata kazi ni sasa na adui anayenipinga namharibu kwa jina la YESU KRISTO.
Hakuna mchawi atayenizuia katika majira yangu ya kufunga ndoa, hakuna mchawi atanizuia katika majira yangu ya kupata uzao na kupata kazi.
Ngome ya kipepo inayonizuia katika majira yangu ninaiharibu kwa jina la YESU KRISTO.
Kila baraka yangu iliyo katika majira ya MUNGU na ije kwangu katika majira hayo , katika jina la YESU KRISTO.
Najua majira yangu ya kupata biashara yameshafika, najua majira yangu ya kufunga ndoa yameshafika, najua majira yangu ya kupata kazi yameshafika, najua majira yangu ya kupata watoto katika ndoa yangu yameshafika, najua majira yangu ya kupandishwa cheo kazini yameshafika, na kila majira yangu ya baraka za MUNGU yameshafika, adui aliyenizuia katika majira yangu ninamharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
shetani na washawi wako na majini yako achia majira yangu ya kubarikiwa na MUNGU muumbaji wangu.
Hakuna adui atakayenizuia katika majira yangu ya baraka za MUNGU, ninakataa kuzuiliwa na yeyote, katika jina la YESU KRISTO.
ROHO wa MUNGU ninaomba kwa neema yako unifunulie majira yangu ya baraka za MUNGU Baba ili yasinipite.
Kuna majira mengine kibinadamu nashindwa kuyajua lakini wewe ujuaye yote naomba nipate neema mbele zako na unijulishe ili niyafahamu majira haya natakiwa nifanye nini kwa utukufu wa MUNGU na kwa kufanikiwa kwangu.
Sasa nayateka majira yangu kwa jina la YESU KRISTO.
Majira yangu ya kufunga ndoa takatifu nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kupata watoto  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kuinuliwa katika huduma yangu  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kuipeleka injili ya KRISTO mbele  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kujenga nyumba nzuri  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kununua gari  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kufaulu mitihani  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Majira yangu ya kupona na kuwa mzima kila siku  nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
Kila majira yangu ya baraka za MUNGU
nayateka kwa jina la YESU KRISTO na hakuna wakala wa shetani  atakayenizuia.
MUNGU Baba naomba unipe kushirikiana na majira yangu.
Nipe kufanya juhudi sana pale ninapohitajika kufanya juhudi katika majira yangu.
Nipe kuomba sana pale ninapohitajika kuomba katika majira yangu.
Kila kusudi lako Muumba wangu lifanikiwe katika majira yako uliyoyaamuru juu yangu.
Bwana YESU nitetee katika majira yangu na ili adui asiniguse.
Ninakushuru MUNGU Baba Maana wewe unaweza.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi mkuu.
Amen Amen.

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments