MWAMBIENI ARKIPO AIANGALIE SANA HUDUMA ALIYOPEWA NA BWANA HATA AITIMIZE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu popote ulipo.
Kwa furaha nyingi nakukaribisha tujifunze Neno la MUNGU.
Wakolosai 4:17 ''Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika BWANA, ili uitimize.''
Mtume Paulo alikuwa katika moja ya huduma zake za kuihubiri injiliya KRISTO. Akiwa mbali na kolosai aliandika Waraka au Barua kwa Knaisa la Kolosai akiwaelekeza Neno la MUNGU.
Baada ya Barua hiyo kuiangika, Mtume Paulo aliwapa Waraka huo Tikiko na Onesimo ili waipeleka Barua hiyo Katika mji wa Kolosai ambako kulikuwa na Kanisa la MUNGU. Katika Waraka huo Mtume Paulo ameandika mambo mengi ya kulisaidia kanisa,  Katika kumalizia yaani Mstari wa pili kutoka Mwisho  Mtume Paulo aliagiza kwamba Aambiwe Mtumishi mmoja aitwaye
Arkipo kwamba Aiangalie sana huduma aliyopewa na MUNGU ili aitimize.
Ndugu zangu Neno la MUNGU ni hai milele na ndio maana naomba ujue wewe mwenye huduma, wewe uliyeokoka na wewe Mteule wa KRISTO ya kwamba wewe ndio Arkipo wa leo katika maeneo yako na kwamba unatakiwa uiangalie sana huduma uliyopewa na MUNGU katika kazi ya MUNGU ili uitimize.
Naomba kukueleza mambo haya machache wewe Arkipo wa leo ili ikusaidie kumtumikia KRISTO kwa usahihi na umakini na uhakikishe unatimiza huduma yako uliyopewa.
Kila Mkristo anayo huduma MUNGU amempa na huduma kuu ni kuwaleta kwa YESU wanadamu wote.
Nisikilize sasa Arkipo wa leo ili utumike kwa usahihi kwa MUNGU;

 =Watu wengi kadri wanavyokuwa na miaka mingi katika wokovu ndivyo wengi sana katika wao huota viburi na mazoelea mabaya.
Ni mbaya hiyo, kama inakuhusu badilika maana MUNGU hataki kiburi wala mazoelea, Tumika kwa KRISTO kwa usahihi na uaminifu ili utimize huduma yako.

1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA. ''

=Ni muhimu sana kujua kwamba Wewe sio wa wewe bali wewe ni wa KRISTO.
Ishi maisha matakatifu ayatakayo KRISTO, maana huko ndiko kuwa mali ya KRISTO na ndiko kuwa mteule aliye tayari kwa uzima wa milele. Unamtumikia MUNGU sasa lakini baada ya kumaliza wito wako ufuate uzima wa milele.
Usitumike tu mradi unatumika bali tumika huku wewe mwenyewe ukiwa kielelezo katika kuishi maisha matakatifu.
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''

=Matendo yako ndio yanaweza kuwaonyesha watu kwamba unampenda MUNGU au humpendi.
Matendo huongea zaidi kuliko maneno.
Matendo yako yote yanatakiwa kuongea mbele za watu kwamba unampenda Bwana YESU.
Kuna watu kwa maneno yao husema sana kwamba wanampenda Bwana YESU lakini kipimo cha kuwajua kama wanampenda ni matendo na sio maneno tu.
Kumbuka Biblia inathibitisha kwamba wapo pia watu ambao humpenda MUNGU kwa vivywa vyao tu lakini mioyo iko mbali na yeye.
Jitahidi wewe usiwe katika kundi hilo.
Mathayo 15:8" Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami."

Wewe mpende MUNGU katika kweli.
Maneno yao yathibitishwe na matendo yako kwamba unampenda Bwana  YESU.


=Mambo matatu yanayoweza kuondoa ujasiri ndani ya Mkristo ni.
1. Dhambi.
2. Kutokujifunza Neno la MUNGU na kulitii.
3. Kuipenda dunia na maovu yaliyomo.
Kumbuka 1 Yohana 2:15 "Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake."
Hutakiwi kufanya dhambi na hutakiwi kuacha kujifunza Neno la MUNGU na hutakiwi kuipenda dunia na mambo mauvu yaliyomo.

=Kuna kuwa kwa MUNGU na kuna kuwa kwa shetani, hakuna sehemu ya katikati.
Ukimuona mtu hayuko kwa YESU maana yake moja kwa moja yuko kwa shetani

Hakuna falme tatu bali ziko mbili.
Kuna ufalme wa MUNGU na kuna ufalme wa shetani, hakuna zaidi ya hapo, hivyo mtu akiwa nje ya ufalme wa MUNGU maana yake moja kwa moja yuko kwenye ufalme wa shetani.
Mfalme wa ufalme wa MUNGU ni Bwana YESU KRISTO.

Ukiona mtu yeyote anatawala au ni mfalme tambua kwamba anatawala ama kwa msaada wa ufalme wa MUNGU au kama ni mwovu anatawala kwa msaada wa ufalme wa shetani.
Ndugu yangu ni muhimu sana uwe katika ufalme wa MUNGU.
Yakobo 1:22-25 '' Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. ''


=Tunakwenda kanisani ili tupate Neno la MUNGU la kutusaidia katika safari yetu ya mbinguni.
Ndugu mpendwa wa KRISTO YESU  na Mtumishi unayetumika kwa MUNGU nakuomba:
1. Usiende kanisani ili Ubarikiwe tu na watu.
2. Usiende kanisani ili watu wakuone.
3. Usiende kanisani ili kuwahadaa watu.
4. Usiende kanisani ili kuwaona watu uwapendao mfano wachungaji na waimbaji maarufu.
5. Usiende kanisani ili kujaza kanisa.


 1 Petro 2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa(Neno la MUNGU), ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ''

Nenda kanisani ili kupata Neno la MUNGU la kukusaidia jinsi ya kumpendeza MUNGU, ili uhusike na uzima wa milele kama ukilitii Neno la MUNGU.
Katika ibada Neno la MUNGU ndilo la muhimu kuliko chochote.
Ukienda ibadani kisha ukaliacha neno kanisani hakika wewe hukwenda kuabudu kwa faida Bali kwa hasara.
Neno la MUNGU ndio muhimu kuliko yote.
Ukienda ibadani kisha usilizingatie Neno la MUNGU na kulitii katika maisha yako hakika kwenda kwako ibadani hakukuwa na matokeo yaliyokusudiwa.
Usipoenda ibadani hakika unakuwa unakosa nini MUNGU anataka utende na kujua ili kukusaidia katika safari yako.
Ibada ni muhimu sana lakini pia ni lazima uzingatie neno la MUNGU sana sana.


= Usichoke kutenda mema huku ukiishi Maisha matakatifu maana kuna faida baadae.
2 Thesalonike 3:13 ''Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.''
Usipoipata faida hapa duniani basi utaipata mbinguni.
Ukitenda jambo jema kwa MUNGU au kwa mwanadamu kuna faida.
Rahabu aliwatendea mema watumishi wa MUNGU waliokuwa wakiipeleleza nchi, kwa wema huo Rahabu na familia yake hawakuuawa wakati wa Vita, kwa wema ule ikawa ndio sababu ya Rahabu kuungana na watakatifu wa MUNGU na kwa tendo hilo jema akawa mteule wa MUNGU.
Chanzo cha yote ni mema aliyowatendea Israeli.
Ndugu tenda mema na usikubali kuchoka kutenda mema.


 =Usikubali kulegea katika kile ambacho MUNGU amekuagiza utende.
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments