UKIBARIKIWA USIMSAHAU MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia baraka.
Watu wengi akibarikiwa na hubadilika.
Wengi wakibarikiwa huota viburi hata kwa kanisa au kwa watumishi wa MUNGU au kwa wazazi au ndugu.
Biblia inataka ikusaidie wewe unayesoma somo hili ili ukibarikiwa na MUNGU ubaki na utii wako na unyenyekevu wako kwa MUNGU.


Kumbukumbu la Torati 8:10-20 "Nawe utakula ushibe, utamshukuru BWANA, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa. Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka. Kama vile mataifa yale ambayo BWANA anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya BWANA, Mungu wenu."

Ukipata kazi nzuri usimsahau MUNGU.
Kuna walikuwa watii sana na walikuwa waombaji sana na wahudhuriaji wazuri kanisani lakini walipopata kazi waliacha ibada, ndugu ukibarikiwa usikubali kumsahau Bwana YESU.
Ukipata utajiri usimsahau MUNGU.
Ukipata Baraka ya ndoa usimsahau Bwana YESU.
Kuna watu baada ya kufunga ndoa walilisahau na kanisa kama lipo, ni hatari. Hukuja kanisani ili ufunge ndoa na kuondoka Bali ulikuja ili uwe mshirika ukidumu katika fundisho la KRISTO na ibada na maombi.
Ukipata Baraka ya uzao usimsahau MUNGU.
Kuna watu baada ya kupata mtoto basi na kanisani haendi,ndugu ukibarikiwa usikubali kumsahau MUNGU.
Ukibarikiwa usisahau Neno la MUNGU. Ukibarikiwa usisahau ibada na mikesha ya maombi.
Ukipandishwa cheo kazini usimsahau MUNGU.
Ukipata Mali usimsahau MUNGU.


Mithali 3:9 "Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote."

Njia nzuri za kumheshimu MUNGU baada ya Baraka ni:

1. Kumtolea MUNGU zaka na sadaka kila unapopata.


2. Ni kutoacha ibada.


3. Ni kutokubali kuwa na roho ya kiburi Bali unabaki na unyenyekevu wako kwa MUNGU na kanisa.


Unapobarikiwa usikubali kuwa na kiburi kinachotengenezwa baada ya Baraka kuipata.
Unapobarikiwa inakupasa kutokubadilika.
Unapobarikiwa hakikisha unabaki wewe yule yule mtii na mnyenyekevu, baki yule yule muombaji na mzingatiaji wa ibada.
Kumbuka kipindi unaomba, kumbuka kipindi unafunga na kulia mbele za MUNGU ili akubariki. MUNGU amekubariki hivyo usikubali kumsahau wala usikubali kusahau ibada.
Kumbuka Neno hili 


Mithali 3:33 "Laana ya BWANA i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.
Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema."


MUNGU anawapa neema wanyenyekevu hivyo baki na unyenyekevu wako wa kwanza.
Unaweza kukuta mtu alikuwa muombaji sana kwa MUNGU ili MUNGU ambariki gari. MUNGU akambariki gari hiyo lakini badala sasa awahi kanisani maana hata usafiri anao, yeye ndio kabisa kila siku ana dharula na dharula hizo ni za kwenda kwenye kujirusha, kwenye viwanja. Kabla hajapata gari alikuwa anawahi kanisani lakini baada ya kupata gari anachelewa kanisani au haji kabisa kanisani, au akifika anaondoka mapema akisema kuna mahali anawahi.
Ndugu usimsahau MUNGU baada ya Baraka yako kuipata.
Kanisani kwetu tuliwahi kumwombea ndugu mmoja ambaye alikuwa anaumwa hata kutembea hawezi, ndugu yule nilikuwa nafanya juhudi nyingi kumpitia na kumwombea. Baada ya muda akapona na tukaomba apate kazi na akapata kazi nzuri. Baada ya kupona na kupata kazi akaacha ibada na akageuka kuwa adui na kuna siku hadi alitengeneza profile Facebook na kuanza kunitukana na kuleta uzushi mwingi. Ilinisumbua kidogo lakini nikajifunza kwamba wako watu wakibarikiwa anamsahau MUNGU. Baada ya muda mwingi alifukuzwa kazi ndio siku moja nikamuona kanisani, yaani ilikuwa Kama baada ya miaka miwili tangu kipindi tunamuombea na kumsaidia kusimama akiwa hoi mno.
Ndugu, wewe unayesoma Ujumbe huu nakuomba ukibarikiwa usimsahau MUNGU.
Kadiri unavyobarikiwa nakuomba ongeza unyenyekevu na adabu mbele za MUNGU.
Ukibarikiwa Baraka yeyote usikubali kumsahau Bwana YESU KRISTO na wokovu wake.
Usiache ibada baada ya kupata kazi.
Ukipanda cheo kazini usimsahau MUNGU.
Hakikisha cheo chako hakikuondoi kwa Bwana YESU.
Inawezekana baada ya kubarikiwa ulipata marafiki wapya wa hadhi yako, ndugu marafiki wapya usikubali wakakuondoa kwa Bwana YESU.
Katika Baraka na katika hali zote usikubali kumwacha Bwana YESU mwenye uzima wako wa milele.
Kumsahau MUNGU ni kujiangamiza.
Nakuomba uwe kama mtumishi huyu anayesema katika maandiko haya ya Zaburi baada ya kubarikiwa kwako.


Zaburi 116:12-18 " Nimrudishie BWANA nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la BWANA; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote. Ina thamani machoni pa BWANA Mauti ya wacha MUNGU wake. Ee BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako, Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako, Umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; Na kulitangaza jina la BWANA; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote."


MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments