UNAUJUA WAJIBU WAKO MTEULE KWA WENGINE?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Je unaujua wajibu wako kwa wengine?  
Maana ya neno wajibu ni kama ifuatavyo.
Wajibu ni kuwa na zamu halisi katika kusimamia kitu, watu au vitu.
Wajibu ni nafasi au uwezo wa kutenda jambo.
Wajibu ni nafasi ya kutoa maamuzi peke yako.
Wajibu ni kuitumia nafasi uliyonayo.
Wajibu ni kuwa mhusika wa jambo fulani katika yale yanayokuhusu.

Wakolosai 1:10-15 ''MWENENDE KAMA ULIVYO WAJIBU WENU  KWA BWANA, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya MUNGU; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha;  mkimshukuru BABA, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. ''

Mwenende kama ulivyo wajibu wenu, Nalimpenda sana neno hilo la kwamba tuenende kama ulivyo wajibu wetu katika Bwana YESU.
Ndugu inakupasa sana kuenenda kama ulivyo wajibu wako kwa Bwana YESU.

KUNA AINA TATU ZA WAJIBU.

1.Kuna wajibu wa mtu kwa MUNGU.

Wajibu wako kwa MUNGU ni kulitii Neno lake.
Ni kutimiza kila kazi ya MUNGU.
Kama unayo huduma yeyote unatakiwa kuwajibika katika huduma yako.
Kwa sababu wewe ndio unawajibika kwenye kitengo chako basi naomba ujue kwamba wakusifiwa juu ya huduma yako ni wewe na wa kulaumiwa ni wewe pia.
Ukifanya kwa ulegevu utalaumiwa na ukifanya kwa umakini na kwa juhudi utasifiwa wewe.
Katika kutimiza wajibu wako kwa MUNGU unatakiwa uwajibike wewe bila kuwategemea watu wengine maana umeitwa wewe ili uwajibike kwa MUNGU.

Katika wajibu wako kwa MUNGU umepewa karama ili kukusaidia kutimiza kusudi la MUNGU kwako na kwa wengine.Kwa ufupi Wajibu wa mtu kwa MUNGU ni kama ifuatavyo;

A. Kumwamini MUNGU 
2 Nyakati 20:20b '' mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''
Kumwamini MUNGU ni wajibu wa kila mteule wa KRISTO.
Moja ya vitu vibaya sana ambavyo MUNGU anavichukia ni kutokumwamini.
Wana wa Israeli waliangamizwa jangwani kwa sababu ya kutokumwamini MUNGU.
Ukishindwa kumwamini MUNGU ni lazima tu utamwamini shetani na uongo wake. Wajibu muhimu sana kwa kila mteule wa MUNGU ni kumwamini MUNGU.

B. Kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Yohana 4:24 '' MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.''

 C. Kumtumikia KRISTO kwa moyo.
 1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

D. Kuishi maisha matakatifu katika wokovu wake KRISTO.
1 Petro 1:15-16 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.'' 
 
2. Kuna wajibu wa mtu kwa wanadamu Wengine.


A.Kuwahubiria injili ya KRISTO.
Marko 16:15-16 '' Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. ''

B. Kuwaombea.
Wakolosai 4:2-4 ''Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba MUNGU atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya KRISTO, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena.'' 
''Mkituombea na sisi'' hiyo katika kuwaombea wengine nje na wewe.

C. Kuwasaidia kiroho na kuwashauri mema.
 1 Thesalonike 2:10-12 '' Ninyi ni mashahidi, na MUNGU pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa; vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia; ili mwenende kama ilivyo WAJIBU wenu kwa MUNGU, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake.''

Unatakiwa kuifanyia kazi karama yako katika kuwasaidia watu wengine kuokoka na kuishi maisha matakatifu.
Unapomwinua mwingine hapo unakuwa umetimiza wajibu wako.
Katika wajibu wako naomba ujue kwamba ni Heri kujilaumu mwenyewe kuliko kuwalaamu wengine.

Unao wajibu mkubwa sana kwa watoto wako.
Wajibika kwa watoto wako.
Wajengee ujasiri na usalama wao.
Kuwa muwazi ili kuwapa nafasi watoto wako wajieleze kwako na kwa wengine.


3. Kuna wajibu wa mtu kwake mwenyewe.

A. Kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi wako. 
 Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''
 
B. Kuukomboa wakati kwa kuishi maisha matakatifu na ya haki.
Wakolosai 4:5 '' Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.'' 

C. Kuenenda katika ROHO MTAKATIFU na kumtii yeye katika yote.
Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

Baada ya kumaliza kusema kuhusu wajibu wako mtumishi wa MUNGU sasa naomba nikushauri haya yafuatayo;
Shamba la BWANA ni kubwa sana hivyo hakuna haja ya watumishi kugombania madhabahu kwa ajili ya kuhubiri.
Shamba la Bwana YESU ni kubwa na pana sana hivyo hakuna haja ya waimbaji kuoneana wivu. 
Shamba la BWANA ni kubwa sana, wengine wanahubiri kupitia sauti zao na wengine wanahubiri kupitia karamu zao, kuna wanahubiri masokoni na kuna wanahubiri magerezani, kuna wanahubiri kwa filamu na wengine wanahubiri kupitia pesa zao wanazozitoa kwa MUNGU. 
 Wote hao ni watendakazi katika shamba la BWANA YESU.
 injili inasonga na shetani anaona aibu kila Siku, Watu wanaokoka na JEHOVAH mwenye nguvu anatukuzwa kila Siku.
Ewe mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU nakuomba ongeza juhudi katika kazi yako ya injili. 

Shamba la MUNGU ni kubwa sana na hata hatujalifikia hata nusu yake tu. 
Tumika kwa nafasi yako kwa ajili ya injili ya amani ya Wokovu wa KRISTO YESU, Mwokozi na Mfalme wa uzima.
Timiza wajibu wako kwa wote.
1 Timotheo 5:1-2 ''Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote.''  
 
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments