BAADA YA KUMPOKEA YESU UNATAKIWA UJITAMBUE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mteule wa KRISTO uliyezaliwa Mara ya pili inakupasa sana kujitambua, kwamba wewe ni nani katika kazi ya MUNGU na ujitambue wajibu wako kwa MUNGU na kwa wanadamu.
Bwana YESU alituletea Neno lake ili tujitambue na tumtambue MUNGU Muumba wetu, na tutambue haki zetu na nafasi zetu.
Yapo mengi unayotakiwa kujitambua lakini jambo kuu na muhimu sana ni kujitambua kwamba wewe ni mpitaji, mgeni na msafiri tu duniani maana wenyeji wako ni mbinguni.
Siku moja Bwana YESU alikuwa anazungumza na MUNGU Baba na katika maombi yake hayo alijulisha kwamba sisi wateule wake sio wa dunia hii.
Bwana YESU alisema Yohana

"Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.-Yohana 17:14-17"

Kama mteule hutaishi kama mgeni, msafiri na mpitaji duniani hakika utaishi kama mwenyeji wa dunia hii unayeipendeza dunia na maovu yake.
Siku zote msafiri yuko makini ili asiachwe na basi muda wa kusafiri ukifika.
Mpitaji hawezi kuwekeza pasipo kwao maana yeye anapita tu.
Mgeni hawezi kufuata mila za taratibu za ugenini Bali atafuata taratibu za kwao.
Tu wapitaji duniani na wenyeji wetu ni mbinguni kwa MUNGU maana tumechagua huko kupitia kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi, kutubu na kuacha dhambi.
Ndugu mteule wa MUNGU hakikisha unaishi kama mpitaji, mgeni na msafiri uliye tayari kwa safari muda wowote.


1 Petro 2:11-12 " Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.
Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa."


 MUNGU hajakuita bure, Ukilijua hilo hakika utamtumikia Bwana YESU kwa uaminifu na juhudi sana.

Baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake anatakiwa mtu huyo ajitambue.

Warumi 12:1-2 " Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu."


Biblia katika kumjulisha mtu aliyeokoka ili ajitambue inamsaidia kwa kusema yafuatayo;

1. Kwa sababu sasa umeokoka basi Usifuatishe namna ya machukizo ya dunia hii.

2. Kwa sababu umeokoka basi geuza nia yako kutoka kuwaza mabaya na sasa nia yako igeuzwe kwa kufanywa upya kwa jinsi ya KRISTO.
 
Nia yako itageuzwa kutoka katika mabaya kwa kufanya yafuatayo;

1. Kulisoma Neno la MUNGU, kulitafakari na kulitendea kazi katika ROHO MTAKATIFU.

2. Yajue mapenzi ya MUNGU ya kumpendeza kwa ukamilifu.
Mapenzi ya MUNGU ni mambo ambayo MUNGU anataka ufanye.


Waefeso 5:8-11 " Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana(YESU); enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;"

Kumbuka Neno hili ya kwamba waliojitambua kwa kuokolewa na Bwana YESU na wakaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake hakika yeye Bwana YESU atakuja kuwachukua.
Katika kujitambua unahitaji sana utakatifu na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Wanaojitambua humwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli.
Wanaojitambua wameacha dhambi zote na sasa wanamtumikia MUNGU katika kweli ya injili.
Wanaojitambua ni watauwa, wacha MUNGU na wamefanyika viumbe wapya waliosamehewa dhambi zao zote.


2 Wakorintho 5:17 "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya."

Ndugu Yangu, kama kweli umezaliwa mara ya pili, umeokoka, umetubu dhambi zote na kuziacha hakika wewe ni mteule wa KRISTO unayejitambua.

Kuokoka ni kumwamini Bwana YESU na na kumpokea rohoni mwako kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wake.
Kuokoka ni kuchagua kumtumikia Bwana YESU.
Kuokoka ni kuchagua ROHO MTAKATIFU akae ndani yako ili akutumie katika kazi ya MUNGU.
Kuokoka ndio mwanzo wa kumwabudu MUNGU katika kweli yake.
Kuokoka ni kumpokea YESU KRISTO huku ukijitenga na shetani na kila kazi ya giza.
Kuokoka ni kuchagua kufanyika mtoto wa MUNGU.
Kuokoka ni kufanyika mwenyeji wa mbinguni unayesubiri tu muda wa kuondoka hapa ili uende huko.
Kuokoka ni Kufanyika mrithi wa uzima wa milele.
Kuokoka ni kuchagua kuacha dhambi zote na sasa unamcha MUNGU na kumtumikia na kumwabudu katika Roho na kweli.
Kuokoka ni kuchagua uzima wa milele.
Kuokoka ni kuzaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho.

Yohana 3:5-7 ''YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa ROHO ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. ''

Hongera sana ndugu kwa kuokoka.
Na wewe ndugu ambaye hujaokoka napenda kukuambia kwamba YESU KRISTO anaokoa, ukimpokea leo hakika unaokoka.

 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments