CHANZO CHA KUSINZIA WAKATI WA IBADA NA WAKATI WA KUSOMA BIBLIA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Unajisikiaje Neno La MUNGU Linapohubiriwa Wewe Unasinzia? Lakini Mahubiri Yakiisha Tu Na Wewe Unaamka. Na Jambo Hilo La Kusinzia Wakati Wa Neno Ni Jambo Endelevu Kwako.
Unajisikiaje wakati wa mahubiri Kanisani wewe umelala, ukiambia simama tuombe dakika moja huwezi kusimama, na mambo hayo wewe huwa unayafanya kanisani tu. Ukitoka nje ya Kanisa unaweza kupiga story ukiwa umesimama kwa masaa 2 tena huku unatamani story ziendelee.
Ndugu Mmoja Aliniuliza mimi Peter Kama Nimewahi Kusinzia Kanisani Nikamjibu Haijawahi Wala Haitakuja Kutokea Hata Siku Moja, Ndugu Yule Alishangaa Sana Na Kusema Kwamba Yeye Ni Jambo la Siku Zote Kulala Wakati Neno Likihubiriwa, Tusiwalaumu Watu Hawa Ila Tuwasaidie. 

Vyanzo vya Watu Kusinzia Kanisani;
 1. Mtu kutawaliwa na nguvu za giza/Mapepo.

 Mathayo 13:19 '' Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.''

Kazi mojawapo ya shetani ni kuliondoa Neno la Ufalme ndani ya mtu anayelisikiza hilo Neno la MUNGU.
Kazi ya kulinyakua Neno la MUNGU ndani ya mtu wakati mwingine ni kwa njia ya kumuondolea utulivu wa kulisikia.
Wakati mwingine mapepo humletea mtu usingizi ili asielewe Neno muhimu la kumsaidia.
Watu wanaoteswa na nguvu za giza ni rahisi sana kuwajua wakati mwingine.
Ukiona mtu kila Neno la MUNGU likianza kuhubiriwa yeye anasinzia basi tambua kwamba huyo amevamiwa na nguvu za giza au ndani yake kuna nguvu za giza zinazopingana na Neno la MUNGU siku zote.
Mtu anayesumbuliwa na mizimu ya ukoo na yeye wakati mwingine anaweza kuwa anasinzia wakati wa mahubiri au anakuwa mzito sana hata haelewi Neno la MUNGU.
Mapepo yakiwa ndani ya mtu humteka fikra zake kiasi kwamba humuondoa kimawazo katika kulisikiliza Neno la MUNGU litakalomsaidia.
 Mwabudu sanamu naye lazima awe mzito katika kulielewa Neno la kweli la MUNGU.
Kila nguvu za giza ndani ya mtu kazi yake kuu ni kumfanya mtu huyo asielewe Neno la MUNGU la kumfungua, hivyo mtu anayeteswa na nguvu za giza ni rahisi sana kusinzia wakati wa Neno la MUNGU likihubiriwa.
Kuna wengine hata akiwa nyumbani akisoma tu Biblia anapata usingizi ghafla na anakuwa mzito sana hata anaacha kusoma Biblia, chanzo cha hayo ni nguvu za giza kumvamia mtu au anazo kabisa ndani yake.
Maombi Ya Kuharibu Vitu Hivyo  vya giza Ni Muhimu Sana Na Mtu Huyo Atakuwa Huru. 
shetani Hataki Watu Wajue Kusudi La MUNGU Ndio Maana Anawaletea Usingizi Wakati Wa Kitu Kizuri Yaani Wakati Wa Neno.
Kusinzia wakati wa neno ni mpango wa shetani kusudi usisikie neno la MUNGU ukaamini na kuokoka na kufunguliwa. Ni lazima kuzikemea hizi roho isiyo ya kawaida kwa mkristo unayeenda mbinguni.
shetani anawateka watu kwa pepo la usingizi ili wasisikie MUNGU anasema nini juu ya maisha yao na kuwafanya wasifunguliwe.
Kusinzia kanisani ni kuvamiwa na kapepo asilimia 100%
Ni pepo Mchafu huyo. Wengne hata kusoma Biblia anasinzia lile pepo lina mletea usingizi.
Hii haikubaliki ni lazima kabla haujaingia kanisani kumsihi MUNGU wa rehema roho hizi za kuleta usingizi ili tusisikie neno ziyeyuke nasi tulisikie neno ili tuwe wanafunzi wazuri wa YESU KRISTO
Kumbuka Ibada njema inaanzia nyumbani Omba sana MUNGU akufungue.

2. Uvuguvugu wa kiroho.
 Ufunuo 3:15-17 ''Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.''

Mtu aliyevuguvugu kiroho ni yupi?
Biblia inatoa majibu katika maandiko hapo juu kwamba;
= Mtu anayejiona ni tajiri maana yake hana uhutaji wa mambo ya MUNGU maana anayo mengi na anaamini yale aliyonayo tayari yeye ni tajiri hivyo hahitaji msaada zaidi.
Mtu kama huyo wakati wa Neno la MUNGU anaweza akamwangalia mhubiri kisha akakosoa moyoni mwake maana yeye anajua zaidi ya mhubiri kisha hajishughulishi na Fundisho la mhubiri huyo na shetani anachochea uzito na mtu huyo anaweza kujikuta anasinzia au anakuwa ni mtu wa kusinzia kidogo kisha anaangalia saa maana anatamani mhubiri amalize kufundisha maana haoni jipya.
Lakini Ukweli ni kwamba Neno la MUNGU ni jipya kila leo, halichoshi na wala halijawahi kumkinai mtu yeyote ila wanadamu tu ndio hulikinanai Neno.
= Anajiona hana haja ya kitu maana anavyo.
Mtu akijiona hana haja ya Neno la MUNGU basi huyo hata kusinzia hataona tatizo.
Mtu kama huyo hawezi hata kuzingatia kuandika ujumbe wa Neno la MUNGU.
Usiporuhusu Neno la MUNGU ndani yako wakati wa mahubiri basi utaruhusu mambo mabaya kukuvamia, na usingizi ni wakati huo ni moja ya mambo yasiyotakiwa.
Kumbuka hakuna mtu hata mmoja asiyelihitaji Neno la MUNGU.
 Kila siku inatupasa sana kujifunza Neno la MUNGU.
1 Kor 8:2 '' Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.'
Mtu akiwa vuguvugu atajiona kama amekamilika lakini ukweli ni kwamba huyo anahitaji sana Neno la MUNGU.
 

3. Kutawaliwa na mambo ya kidunia yanayoambatana na matumizi mabaya ya muda.

1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.''

Mambo ya kidunia yamechochoea sana watu kuwa mbali na MUNGU na kuwafanya wengi hadi kusinzia ibadani bila sababu za Msingi.
Jiulize kijana siku ya jumamosi ameenda kuangalia mpira katika mabanda ya kuonyesha ligi za Ulaya, Mechi imeanza saa tano usiku na saa saba na nusu ndio huyo kijana amerudi nyumbani, alipofika nyumbani ikabidi amalizie Marudio ya tamthilia fulani anayoipenda kisha saa tisa alale kidogo kisha saa kumi na mbili aamke na kujiandaa kwenda kanisani. Huyo kwa kupenda kwake sana mambo ya kidunia anaweza kujikuta amesinzia  wakati wote wa mahubiri.
Biblia inasema tusiipende sana dunia na mambo yaliyomo.
Kuna watu usiku huwa hawalali na kesho yake wanakuwa Kanisani, Mtu kama huyo kusinzia ibadani sio jambo la ajabu kabisa. Na kusinzia huko kunamkosesha mambo mengi mazuri ya ki MUNGU.

Mengineyo ni 
=Kusinzia kwa sababu ya umri mkubwa.
Angalau ni heri mzee kusinzia ibadani kuliko kijana lakini jambo la ajabu ni kwamba wenye umri mdogo ndio wanaongoza kwa kusinzia.
Mtu wa miaka kuanzia 60 na kuendelea basi hata akisinzia ibadani sio tatizo kubwa sana. Lakini sio kusinzia kila ibada.

=Mtu kama ni mgonjwa.
Mtu kama anaumwa ni kweli hawezi kuwa sawa na mtu mzima.
Mgonjwa akisinzia kama ni kwa sababu ya ugonjwa wake tu basi hiyo sio tatizo.

 Tatatizo lililopo ni kwamba wanaosumbuliwa na kusinzia ibadani wengi wao ni wanaohusika tu na mambo matatu ya kwanza hapo juu.
Wanaosinzia ni wale wale kila siku kwa sababu nguvu za ngiza hazijawaachia.
 Ndugu, Kwanza YESU  mengine baadae.
Kwanza utakatifu katika KRISTO, mengine baadae.
Kwanza maombi, mengine baadae.
Kwanza kujifunza Neno la MUNGU, mengine baadae.
Mengine ni kazi zetu, muda wetu wa kupumzika, safari zetu, biashara zetu na mengine mengi tuyapendayo.
Hayo mengine hayatakiwi kutufanya tusiende ibadani, tusimwabudu JEHOVAH na hayo hayatakiwi kutufanya tusiombe na kujifunza Neno la MUNGU.
1 Petro 2:2-3 " Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili."


 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments