JE UMESAMEHE NA KUSAHAU?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe sana ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kusamehe kwa watu wengi imekuacha changamoto kubwa.
Wengi wamekosa uzima wa milele kwa sababu tu walishindwa kuwasamehe waliowakosea.
Wengi MUNGU hakuwasamehe kwa sababu tu walishindwa na wao kusamehe waliowakosea.
Mteule wa KRISTO kusamehe ni sehemu ya maisha yake na ni kanuni ya kiroho kabisa.
 Mathayo 6:14-15 " Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.
Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu."

 Siku moja nilikuwa nasoma kitabu cha Historia ya Askofu Moses Kulola na nilikutana na vitu vya ajabu sana sana lakini nikajifunza kitu muhimu sana yaani msamaha.
Katika kitabu kile kuna wakati Askofu Kulola alikamatwa na kuteswa muda mfupi tu kabla ya yeye kuhubiri katika mkutano wa injili. Waliomtesa waliingia kwa siri katika mkutano wake ili tu wamsikie akihubiri kuhusu wao ili wapate sababu zaidi ya kumkamata. Lakini jambo la ajabu ni kwamba Askofu Kulola hakuwahi kuhubiri waliomtesa kabla ya mkutano bali aliposimama jukwaani  alihubiri Neno la MUNGU bila kusema lolote juu ya alivyotendewa kabla hajaingia kuhubiri. Jambo hilo la kukamatwa na kuteswa kabla ya kuhubiri halikutokea mara moja tu bali mara nyingi lakini Mtumishi yule hakuwahi kusema hayo wakati akihubiri. Leo la waliomkamata lilikuwa ni kwamba atatumia muda mwingi siku hiyo kuwataja wao lakini hata hakuwataja.
Hakuwa amekosea Askofu Huyo lakini alisamehe mapema kabisa ili asinaswe na uchungu na mambo ambayo yatampa hasira ili asihubiri Neno la MUNGU. Huo ni ujasiri wa kipekee sana na ambao watumishi wengi wa MUNGU hawana.
Mtumishi akipata tatizo kidogo tu unaweza kushangaa mahubiri yote ya siku hiyo analalamika tu kuhusu alichokosewa.
Kama watu wa MUNGU wote inatupasa kusamehe na kusahau.
Ni Kanuni ya MUNGU kwamba ukisamehe wewe basi hata ukimuomba MUNGU msamaha na wewe atakusamehe.
Kama wewe huwezi kusamehe hakika na wewe MUNGU hatakusamehe ukimuomba msamaha, hilo ndilo jambo ambalo linawapeleka wengi jehanamu.
Ndugu yangu, inakupasa usamehe na kusahau kabisa maana na wewe MUNGU anakusamehe.
Waefeso 4:31-32 ''Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.''

Kusamehe/msamaha ni nini?
Msamaha ni tendo la kuwia mtu radhi kwa makosa aliyokutendea.
Kusamehe ni kuachilia moyoni mwako yale uliyokosewa na kuyafuta ili yasiwe makosa tena.
Kusamehe na kusahau ni pale ambapo hata ukilikumbuka jambo ulilokosewa hutaumia
Kuna watu akikumbuka tu jambo alilokosewa jasho humtoka.
Mwingine akikumbuka tu alivyokosewa mwili unasisimka na na nywele zinacheza hiyo ni dhambi ya uchungu na mtu kama Huyo anakuwa hajasamehe

''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Luka 6:37 ''


Kusamehe kunahitaji sana maombi na maamuzi magumu sana . niliwahi kukosewa jambo ambalo haikuwa rahisi kusamehe ila nilisamehe japo sio Kwa siku moja wala mwezi mmoja

Nilijigundua nimesamehe baada kama ya miezi 9, japo mwanzo kila siku nilikuwa nasema nimeshasamehe
Kama kuna wakati ROHO MTAKATIFU alikuwa na kazi kubwa ya kunisaidia ni wakati huo.
Wakati huo ungeniambia nifungwe jela miaka 20 au nisamehe ningechagua kufungwa sio kusamehe

Lakini ni muhimu kujua kwamba kusamehe Kwa mkristo ni sheria ya lazima.
Kuna wakati inahitajika Neema ya MUNGU ndipo mtu asamehe na kusahau
Mathayo 5:7 ''Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.''
Rehema ni kusamehe na kuachilia.
Biblia inawaita wana heri wale wanaosamehe na kuachilia.
Sasa utajuaje kama umesamehe?
Utakapopata uchungu kila ukikumbuka jambo hilo
Utakapopata hasira kila ukikumbuka jambo hilo.
Utakapojiona hukutendewa haki kila ukikumbuka jambo hilo na unaanza kuwaza kuitafuta haki hiyo hata unajua huwezi kuipata.

Walawi 19:18 ''Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.''

Usimsamehe mmoja aliye kukosea Bali samehe wote waliokukosea.
Usichague watu wa kuwasamehe wakikikukosea Bali samehe wote wanaokukosea.
Ukiwasamehe ni kwa faida yako mwenyewe.
Kuna Baraka huwezi kuzipata kwa sababu tu hujasamehe.
Kuna mambo makubwa MUNGU hawezi kukusemesha kwa sababu tu hujasamehe.
Huwezi kusema kwamba umeshawasamehe waliokukosea kumbe umesamehe baadhi tu ya waliokukosea.
Agizo la MUNGU uwasamehe wote waliokukosea.
Hata kama umesamehe 100 waliokukosea lakini Kama una deni la mtu mmoja kumsamehe hakika unaweza ukakosa mbingu kwa sababu ya mmoja huyo ambaye hujamsamehe.

Kuna watu unakuta ameshawasamehe watu wengi wanaomkosea lakini moyoni mwake yuko mtu amemwahidi kwamba "Sitakusamehe hadi naingia kaburini"
Ndugu ukiingia kaburini hujasamehe ni kwa hasara yako mwenyewe na sio ya mwingine, kwanini upate hasara kwa sababu ya mtu mmoja?
Kwa nini ukose uzima wa milele kwa sababu ya kutokumsamehe mtu mmoja tu katika wengi Sana waliokukosea?

Ndugu nakuomba usibakize deni la kutokusamehe Bali samehe wote waliokukosea.
Kuna mtu anaweza akasema "Wewe mtumishi unatufundisha sisi kusamehe kwa sababu hujawahi kutendwa vibaya" ndugu Mimi mama yangu mzazi alitaka kunitoa sadaka kwa wachawi ili wale nyama yangu lakini MUNGU wa mbinguni akaniokoa na nikasamehe.
Hivyo na wewe samehe hata kama ulitendwa jambo baya kiasi gani.
Wengi huwa wanashindwa kusamehe kwa sababu ya kusalitiwa lakini kwanini ukose mbingu kwa sababu ya mwanadamu?
Ndugu, kwani huyo aliyekusaliti ndio mwanaume pekee duniani anayetakiwa kuwa mchumba wako?
Kwani huyo dada ndio mwanamke pekee duniani mrembo anayetakiwa yeye tu kuwa mchumba wako?
Ndugu, Mimi nilitendwa katika hayo na kikaa wiki nzima bila kula, nikilia na kusema maneno mawili tu kwa muda huo wote yaani "MUNGU wangu nisamehe na MUNGU wangu nisaidie" lakini nilisamehe na kusahau lakini MUNGU alinibariki kuliko type ya mwanzo na nikajikuta kumbe nilifanya vyema kuachana na mchumba yuleeeeeeee.
Nilitaka kutokamehe mwanzo lakini baada ya kusamehe kwa sasa namtukuza MUNGU na kumshukuru kwa kutokuniruhusu kujichanganya zamani ili nisipate Baraka iliyotimia ya sasa.
Ndugu Ujumbe wangu kwako ni kwamba samehe watu wote waliokukosea.
Kumbuka huwezi kuingia uzima wa milele usiposamehe watu.
Neno la MUNGU ni nyundo, naomba nyundo hii ikugonge na kukusaga kukufinyanga ili uwe na moyo wa toba na msamaha.
Lishike na kulitii hili neno itakusaidia.

Mathayo 18:21-35 ''Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? YESU akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na BABA yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, MSIPOWASAMEHE  kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake. 

Ndugu Samehe ili uruhusu baraka mpya kwako.
Ndugu, kama kuna kitu muhimu unahitaji katika maisha yako ni kusamehe na kusahau.
Wasamehe wote waliokukosea na omba msamaha kwa MUNGU kwa kutokusamehe kwako.
 Kuna baraka inawezekana kabisa zimeshazuiliwa kwako kwa sababu tu hujui kuwasamehe waliokukosea.
Unaweza ukang'ang'ana sana bila mafaniko, unaweza ukadhani MUNGU hakupendi kumbe huna roho ya kusamehe ndio maana ungali unataabika.

Wakolosai 3:13 '' mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.''
 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments