JE, UNAFANYA KAZI YA MUNGU AU UNAFANYA KAZI PAMOJA NA MUNGU?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Leo naomba ujifunze jambo hili muhimu sana sana, Naomba ujumbe huu ukiweza wape hata na watumishi wa MUNGU unaowafahamu ili iwasaidie katika kutenda vyema katika utumishi wao.
Watu wengi tu hufanya kazi ya MUNGU lakini sio wote wanafanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU mwenyewe.
Kuna tofauti kubwa sana kati ya kufanya kazi ya MUNGU na kufanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.

Kufanya kazi ya MUNGU ni nini?
Kufanya kazi ya MUNGU ni  kufanya kitu chochote ambacho kipo kwenye kazi ya MUNGU lakini sio lazima MUNGU aambatane na wewe.
Kufanya kazi ya MUNGU ni MUNGU kuambatana na wewe katika kazi yake. Zaburi 32:8 ''Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''

Kila mtu duniani anaweza kufanya kazi ya MUNGU lakini sio kila mtu anaweza kufanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
Hata mtenda dhambi yeyote anaweza kufanya kazi ya MUNGU lakini huyo hawezi kufanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
1 Kor 3:9-14 ''Maana sisi TU WAFANYA KAZI PAMOJA NA MUNGU; ninyi ni shamba la MUNGU, ni jengo la MUNGU. Kwa kadiri ya neema ya MUNGU niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu.''

Kama mtumishi wa KRISTO usikubali kufanya kazi ya MUNGU tu bali fanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
Andiko hapo juu linaanza na kitu cha muhimu sana sana kwamba Sisi tu wafanya kazi pamoja na MUNGU.
Kumbe hatutakiwi kuwa wafanya kazi katika kazi ya MUNGU tu bali tunatakiwa tuwe tunafanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
 Unaweza ukafanya kazi ya MUNGU ili watu wakuone lakini MUNGU hayuko pamoja na wewe na hajakuagiza chochote.
Hili ni jambo la muhimu sana sana la kufanya kazi pamoja na MUNGU.
Mathayo 7:22-23 '' Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.''
 Unaweza ukafanya kazi ya MUNGU hata bila kumtii lakini huwezi kufanya kazi pamoja na MUNGU kama humtii MUNGU.
Kuna watu kazaa wamewahi kunijulisha mambo ambayo nilishangaa na kutafakari sana kuhusu kumtumikia MUNGU na kumtumikia MUNGU ukiwa pamoja na yeye.
Ndugu wa kwanza alikuwa ni mtumishi wa MUNGU lakini alikuwa anafanya uasherati kwa siri. Aliendelea na tabia hiyo kwa muda lakini akifika kanisani analia sana na kutubu sana, lakini baada ya ibada anaenda kuendelea na uzinzi wake. Kisha akajua kwamba MUNGU sasa hawezi kumsamehe maana anatubu na kuendelea na uasherati. Kwa sababu kila jumapili na katikati ya wiki lazima asimame kuhudumu basi aliamua kuwa anatubu na kisha anaombea watu na kama watu wakiponywa mapepo kwa maombezi yake basi hicho kinakuwa ni kipimo chake kwamba MUNGU yuko pamoja na yeye kwamba hata akiendelea na uasherati wake basi upako bado utakuwa na yeye tu. Ndugu huyo kwa muda mrefu alijisahau kabisa kama anachofanya ni dhambi. Ni Neema ya MUNGU tu baadae alikosana na mzinzi mwenzake waliokuwa wanafanya dhambi wote ndipo akabadilika na kutubu na MUNGU akamwambia arudi katika kanisa la kwanza alikokuwa anahudumu huku anafanya uovu, akarudi na kumweleza Mchungaji wake kiongozi ndipo akaongozwa sala ya toba upya na akaanza sasa kumtumikia MUNGU pamoja na MUNGU.
Unaweza ukajiuliza kwanini alikuwa anafanya dhambi kila leo na mapepo yanaondoka akiyakemea?
Luka 10:19-21 ''Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.''
 
Ndugu zangu, kutoa mapepo sio kipimo cha kwenda uzima wa milele. Kutoa mapepo sio ndio ishara ya kwamba unafanya kazi pamoja na MUNGU. 
Unaweza ukafanya kazi ya MUNGU kwa sababu tu una muda wa kuifanya kazi hiyo lakini MUNGU asiwe pamoja na wewe maana humtii.
MUNGU anaweza akatenda miujiza mingi kwa ajili ya utukufu wake na sio kwa sababu yako wewe mtumishi unayetenda kazi yake lakini bila yeye.

 Ndugu wa pili aliniambia kwamba alikwenda kwenye maombezi kwa Nabii mmoja ambaye alikuwa anajitangaza sana. Yule mama baada ya kufika huko Mtumishi badala ya kumwombea alianza kumvua nguo ili azini naye, kilichomsaidia yule mama  ni kupiga kelele akiomba msaada ndipo yule mtumishi alimwacha. Yule mama aliniambia kwamba tangu siku hiyo aliapa kwamba hatakwenda kwenye maombezi yeyote. Mama huyo baada ya miaka kadhaa aliendelea kuteseka na nguvu za giza, anatamani kwenda kuombewa lakini moyoni anakumbuka tukio la nabii yule. Yule mama aliniambia kwamba baadae alikutana na dada mwingine aliyemwambia kwamba tabia ya yule nabii inafahamika ni hiyo maana ameshafanya uchafu huo na watu wengi na inasemekana ana ukimwi pia huyo nabii. Nililia baada ya mama yule kunisimulia kwa njia ya simu. Baadae nikamuuliza kuhusu huduma ya huyo nabii, akasema ana upako sana na miujiza mingi sana inatendeka katika kanisa lake. Baada ya kuniambia hivyo nilikumbuka kwamba mtu anaweza akafanya kazi ya MUNGU lakini asifanye kazi pamoja na MUNGU. Ndio maana Bwana YESU alisema kuna  ''Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.''

 Ndugu mwingine aliniambia habari za ajabu sana.
Alisema katika kwaya yao ya kanisa kulikuwa na mwimbaji muhimu sana wa kiume lakini alikuwa ni shoga. Mwimbaji yule alikuwa anawatongoza hadi wanakwaya wenzake na Mchungaji alijua kabisa kwamba yule Mwimbaji wa viwango ni shoga. Haikuniingia akilini maana kwaya ile ni kubwa sana na maarufu na wako vizuri kiuimbaji na Kanisa pia lina waumini zaidi ya 700 lakini katikati ya kundi kuna Mtumishi anafanya kazi ya MUNGU lakini hafanyi kazi pamoja na MUNGU, Ni hatari.
MUNGU hawezi kufanya kazi yake pamoja na mwovu.
 Mithali 6:16-19 '' Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu. ''

Ndugu mwingine akaniambia ya kwamba alikwenda kuombewa katika huduma fulani mkoani kwao. Alipofika kuombewa alishangaa Muombeaji ambaye ni Mchungaji anampapasa na kumvua nguo kisha siku hiyo hiyo wakazini ofisini kwa Mchungaji. Yule dada alikuwa na ukimwi  na aliyeenda kuombewa na alimweleza Mchungaji yule kabla hata ya uzinzi ule lakini hata sijui kama Mchungaji yule alikuwa na mapepo kama alivyokuwa muombewaji maana walijikuta wanafanya uzinzi  na kisha yule Mchungaji baada ya fahamu zake kumrudia alilia sana sana na kumwomba msamaha yule dada huku akisema hata hajui imekuwaje. Tukio hilo lilimfanya yule Binti kuogopa maombezi na aliapa kutokwenda kuombewa ila neema ya MUNGU ikamgusa baada ya kusoma somo mtandaoni ndio ikapelekea kuombewa na kupona kabisa.

Mama mmoja kwa uchungu sana aliniambia kwamba kuna Mchungaji huwa anamaliza hata miezi miwili akiwa kwa hawara huku ana mke na watoto, na ni Mchungaji maarufu tu na ana upako na ni mhubiri mzuri sana. Yule mama aliniuliza ''Kwanini MUNGU anendelea kumtumia yule mtumishi?''
Nilimwambia kwamba Biblia inasema kwamba karama za MUNGU hazina majuto hivyo kama karama MUNGU hakuondolei hata kama unafanya uovu lakini karama haipimi mtu kama anaenda mbinguni. Mtu anaweza akamtumikia MUNGU na kufanya mambo mengi lakini kama haishi maisha matakatifu jina lake halimo katika kitabu cha uzima. Alisema kwamba yule Mtumishi huaga Kanisa na familia yake kwamba anakwenda kufanya huduma kumbe anaenda kwa mahawara zake kufanya uzinzi. Jambo hilo ndilo lilisababisha yule dada Kuhama kanisa lile maana hata yeye alikuwa ameponapoa kidogo tu kunasa katika mtego wa Mtumishi Yule.

Leo katika baadhi ya makanisa kuna watu wanamtumikia MUNGU na huku  wakiendelea kufanya uovu huku wakijifariji ujinga.
Kuna waimbaji ni wadhambi tu na hawaoni hata aibu.
Kuna wahubiri ni wadhambi tu na hata chembe ya hofu hawana.
Ndugu zangu ni hatari sana sana.
Mtumishi wa MUNGU unahitaji kuwa makini sana sana.
Usifurahi tu kuona watu wanakushangilia  japokuwa katika uharisia wewe ni mtenda dhambi mkubwa.
Itakusaidia nini wewe ufanye kazi ya MUNGU na kisha ukose mbingu?
Unatoa mimba na bado unajiita mtumishi wa MUNGU.
Unakunywa pombe na bado unajiita mtumishi wa MUNGU.
Ni mzinzi na Mwasherati na bado unajiita mtumishi wa MUNGU.
Ni mwizi na tapeli na bado unajiita mtumishi wa MUNGU.
Unafanya maovu mengi huku unajiita Mtumishi wa MUNGU.
MUNGU hafanyi kazi na wewe sasa ndio maana hata kwenye nyimbo zako wala humtaji tena Bwana YESU.
MUNGU hafanyi kazi na wewe sasa ndio maana unahubiri baraka tu huku hukemei dhambi maana hata unaofanya nao zao wanakuona hivyo kwa kuwahofia wao huwezi kukemea dhambi.
Ndugu tubu na rejea sasa katika kweli ya Bwana YESU.
Watumishi wa kweli wa Bwana YESU wapo na wanamtumikia MUNGU pamoja na yeye kwenye kazi yake, waeleze hao itakusaidia.

Kwanini nimesema kwamba kuna tofauti katika ya  kumtumikia MUNGU na kutumika pamoja na MUNGU?
Ni kwamba ili utumike pamoja na MUNGU unatakiwa uwe na ROHO MTAKATIFU na ukubali kumtii huku ukiishi maisha matakatifu.
Wagalatia 5:25 ''Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''

 Kuna tofauti ya kufanya kazi ya MUNGU na kufanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
Kila mtu anaweza kufanya kazi ya MUNGU lakini sio kila mtu anaweza kufanya kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
Unaweza ukafanya kazi ya MUNGU hata bila kumtii lakini huwezi kufanya kazi pamoja na MUNGU kama humtii MUNGU.
Kutumika pamoja na MUNGU kutakufanya usiangalie aliyeko mbele yako wala aliyeko nyuma yako au pembeni, bali utamuangalia MUNGU.
Huwezi kuacha kukemea dhambi kwa sababu tu watenda dhambi wakubwa kanisani ni wale ambao hukutegemeza.
Kama watumishi wa MUNGU inatupasa sana kuwa makini sana.
Ni kweli kabisa tumeagizwa na Bwana YESU Mwokozi kwamba tuipeleke injili kote lakini hata sisi ni lazima tuwe watakatifu ndipo tutafanya kazi yake pamoja na yeye.
Mathayo 28:19-20 ''Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.''

Katika kuipeleka injili ya KRISTO inakupasa uende pamoja na KRISTO mwenyewe.
Yeye Bwana YESU yuko katika utakatifu na yuko katika Neno lake.
Ukihubiri Neno lako na sio lake unakuwa unafanya kazi bila yeye.
Leo kuna watu wanaogopa hata kuombewa ili wafunguliwe vifungo kwa sababu tu kuna watumishi ambao hawafanyi kazi ya MUNGU pamoja na MUNGU.
Wengi wanafanya kazi ya MUNGU na matundo yao tu na kwa faida za kimwili tu na kwa dhambi.
Biblia inaagiza kwamba ukitaka kumtumikia KRISTO basi mtii kwanza yeye hata kabla ya kumtumikia, tii Neno lake na ishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.
Kumbuka hii ya kwamba '' Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.-Yakobo ''
 Sio kwamba MUNGU hataki watumishi wawe wengi bali anataka kila Mtumishi afundishe ukweli huku yeye mwenyewe akiwa kielelezo chema katika matendo yake yote, hapo ndipo atafanya kazi pamoja na MUNGU.
Kumbuka MUNGU anahitaji watenda kazi, lakini hao watenda kazi ni muhimu sana wakajifunza kanuni za kutenda kazi pamoja na MUNGU, Nje na hapo ni hatari.
Luka 10:2-3 ''2 Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu.''

Ndugu yangu nakuomba usiogope kumtumikia MUNGU ukiwa pamoja na yeye bali ogopa kumtumikia MUNGU ukiwa peke yako bila yeye MUNGU.
1 Timotheo 4:15-16 ''Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.''
Naamini sasa utafanya vyema katika MUNGU huku ukiwa pamoja na yeye.
Kama wewe ni mmoja wa watumishi ambao wanafanya dhambi kwa siri nakuomba tubu na acha mara moja.
Kama wewe ni mtumishi unayetumika kipepo nakuomba okka upya na sasa anza kumtii Bwana YESU.
 
  MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments