JINSI YA KUIJUA KARAMA YAKO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Je unakijua kipawa chako?
Je unakitumia kipawa chako katika kusudi la MUNGU?
Kila mmoja wetu kuna kusudi la MUNGU kuwepo kwaka Wokovu wa Bwana YESU.
Kila mmoja kuna hatima njema ya MUNGU aliyomkusudia kama akimtii MUNGU.

Hakuna aliyezaliwa kwa bahati mbaya.
Hakuna mtu aliyezaliwa kwa matakwa tu ya mwanaume na mwanamke.


Karama ni nini?
Kipawa anachokuwa nacho mtu kwa
sababu ya kumwabudu sana MUNGU.

Kipawa ni uwezo mtu aliozaliwa nao
ambao humwezesha kufanya jambo Fulani vizuri.

Kwa sababu kuna kuzaliwa upya kiroho baada ya kuokoka basi kuna vipawa pia huzaliwa baada ya sisi kumpokea Bwana YESU na ROHO MTAKATIFU kuingia ndani mwetu, maana ROHO ndiye anayetoa karama na vipawa.
 Kwa lugha ya Kiingeleza Neno karama ni ''Gracious gifts'' likiwa na maana ya  ''zawadi za neema''  na kumbuka maana ya Neema ni kustahilishwa bila kustahili. Kwa hiyo zawadi za neema au karama ni zawadi ambazo mtu anazipata kutoka kwa ROHO MTAKATIFU bila kustahili au kuzigharimia.
Karama za ROHO MTAKATIFU ni zawadi
ambazo
ROHO MTAKATIFU huwapa wateule wa KRISTO kwa neema na ndiye huamua ampe nani na ampe nini na Mteule Mwingine apewe karama gani  bila kujali anapenda au hapendi.
Ndugu inakupasa sana kumtii MUNGU katika maisha yako yote.
Wewe mteule wa MUNGU Katika kanisa huwa rohoni mwako unatamani umtumikie MUNGU kwa huduma Ipi? au huwa unasukumwa rohoni kutumikia kanisani katika nini?
Kuna wengine hutamani kuwafariji watu na kuwatia moyo. Wengine Kuwa waimbaji wa Sifa na kuabudu, wengine ualimu na usafi wa kanisa, wengine Kuombea watu, wengine uiinjilisti wengine Kuombea wagonjwa na kufungua watu watoke katika giza na kutoa mapepo kwa jina la YESU KRISTO wengine maombi na usafi wa mazingira ya kanisa. Njia rahisi zaidi wakati mwingine wa kuijua karama yako kwenye injili ya KRISTO ni kile kinachokusukuma zaidi kufanya kama mfano wa hivyo nilivyovitaja. 

1 Kor 12:4-11 ''Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule.  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ''
 
Binafsi Mimi nimewahi kuulizwa maswali mengi na watu wakitamani wajue karama zao na vipawa walivyopewa na MUNGU kwa ajili ya kazi yake.

Njia 4 za kuijua karama yako.
 
1. Njia rahisi ni kile unachokitamani zaidi kuliko vingine katika kazi ya MUNGU hiyo ndio karama yako unayotakiwa kuifanyia kazi katika kazi ya MUNGU.

2. Watu wengine Katika Kanisa wanaweza kukujulisha karama yako watakapokuona unamtumikia MUNGU, Hivyo kwa urahisi zaidi utajua karama yako na utatenda vizuri zaidi.


3. Maombi ni ufunguo wa  kila kitu hivyo kwa maombi ROHO wa MUNGU anaweza kukujulisha karama yako.

4. Jambo la kujua jingine ni kwamba MUNGU akikupa karama katika kanisa lake huanzia na msukumo wa ndani yako wa kutamani kitu hicho na wakati mwingine unaweza ukafanya huduma nyingi lakini kuna huduma ukiifanya unajisikia amani na furaha zaidi kwa sababu hiyo ndio karama yako.

1 Kor 12:31 ''Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.''
 
Pia kumbuka kwamba Kama mtu hatafanyia kazi karama yake kwa muda mrefu anaweza kujikuta hata msukumo tena wa kufanya huduma unaondoka maana ameshindwa kuzaa matunda kupitia huduma yake hiyo. Ni muhimu kuipalilia karama yako na kuifanyia mazoezi na Maombi ili ukipata nafasi ya kutumika katika karama hiyo hasi utatumika kwa viwango.

Watu wengi hudharau vipawa vyao ambavyo ROHO MTAKATIFU amewapa ili wamtumikie MUNGU katika Kanisa.
Ngoja niseme machache kuhusu kipawa au karama kwa jina lingine.

Kipawa kinaweza kikakuinua hata ukakaa meza moja na wakubwa ambao isingekuwa kipawa hicho usingekutana nao hata siku moja.
Kipawa kina nguvu sana.
Adui akitaka kukitumia kipawa chako usikubali.
Nakuomba kaa sawa kwa YESU na mruhusu ROHO MTAKATIFU akutumie vyema katika kipawa au karama aliyokupa.

Ngoja nikupe ushuhuda mfupi ili ikusaidie kuchochea karama yako aliyokupa MUNGU katika Kanisa.
Siku moja nilipigiwa simu na mtumishi wa MUNGU mkubwa na anayeheshimika Afrika mashariki nzima na zaidi ya hapo. Mtumishi yule alinisalimia na kunitia moyo sana na kumihimiza sana niendelee kumtumikia MUNGU kwa kuwafundisha watu mtandaoni.
Akanialika pia kanisani kwake nikafundishe vijana zaidi ya 1000 kuhusu ujana, uchumba na ndoa.
Muda wote kipindi mtumishi huyo anaongea nilikuwa sina hata neno la kumjibu maana nilikuwa tu nimeduwaa. Wewe jiulize unaongea na mtu ambaye huwa unamuona YouTube tu na huwa unamuona kwenye Vitabu tu maana nilikuwa na kitabu chake.
Ndugu naomba nikuambie kwamba kipawa chako kinaweza kukukutanisha na wakuu, endelea mbele kumtumikia Bwana YESU bila kuangalja watu wanasema nini.

Nimewahi kupigiwa simu hadi na waheshimiwa wakihitaji maombi, nilimshangaa MUNGU hata kwa hilo. Nakumbuka hayo yalitokea wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ndugu palilia karama yako kwa maombi na utakatifu maana karama yako kwa MUNGU inaweza ikakupa kufika pahali usingefika Kama isingekuwa hiyo karama.
Mwezi wa 11 mwaka 2015 niliduwaa siku moja nilipopigiwa simu na mhariri wa gazeti akiniomba somo langu Fulani liwekwe gazetini. Na kweli kwa wiki 4 mfululizo somo langu lilikuwa linawekwa gazetini. Mimi nilikuwa namshangaa MUNGU tu na kumshukuru.
Kuna watumishi wangapi hadi nipate nafasi Mimi?
Ndugu, palilia karama yako maana karama hiyo inaweza kukukutanisha na watu ambao isingekuwa karama hiyo hata kama ungewapigia simu mwaka usingewapata.
Endelea kunyenyekea kwa MUNGU na endelea na utakatifu huku ukimtumikia Bwana YESU kupitia kipawa alichokupa.

1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

Achia moyo wako utumiwe na MUNGU.
 Usikubali moyo wako utumiwe na majini bali kubali na uuachie moyo wako ili utumiwe na MUNGU.
Mchungaji mmoja alisikia kwa sauti akiambiwa kwamba "Umekubali kuifanya kazi yako na umeacha kazi ya MUNGU?"
Mchungaji huyo aliambiwa neno hilo kwa sauti ikitokea angani baada ya mchungaji huyo kuacha kazi ya uchungaji ili akaajiriwe serikalini.
Hakuitii hiyo sauti Bali aliendelea na kazi mpya nzuri serikalini huku hana wasiwasi.
Baada ya miezi 6 akiwa kazini alipata mapigo ya kiroho ndipo akakumbuka kazi ya MUNGU na akaacha kazi ya serikali na kurudi kumtumikia MUNGU.
Hata wewe kama umeacha kazi ya MUNGU kwa tamaa zako nakuomba rudi kumtumikia MUNGU.
Inategemea na wito aliokuitia.
Kuna wito unaweza ukafanya kazi zako na huku ukifanya na kazi ya MUNGU.
Lakini pia kuna wito unatakiwa ufanye kazi ya MUNGU tu na MUNGU atakubariki huko huko kwenye wito wake.
Kama MUNGU akikuambia uache kazi Fulani au vitu Fulani na umtumikie basi mtii MUNGU.
Kama MUNGU hajakuagiza kuacha kazi basi endelea na kazi yako huku ukimtumikia MUNGU.
Ila akikuambia acha kazi ili ufanye kazi yake usikubali moyo wako kuwa mgumu.

Endelea kumtumikia Bwana YESU kwa moyo na uaminifu.  
Akisema ROHO MTAKATIFU amesema MUNGU.
Usipomsikiliza ROHO MTAKATIFU humsikilizi MUNGU.


1 Petro 4:9-11 ''Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika; kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za MUNGU. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya MUNGU; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na MUNGU; ili MUNGU atukuzwe katika mambo yote kwa YESU KRISTO. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.'
 
Baada ya hayo naomba nikushauri mambo yafuatayo;
=Ukizaa kubali kulea.
Karama na vipawa alivyokupa MUNGU vinatakiwa vimletee MUNGU matunda mema.
Inawezekana kabisa umehuduma na watu wameokoka hivyo usiwatelekeze tu tu bali walee katika misingi sahihi ya injili ya KRISTO.
Ukizaa watu kiroho ni muhimu uwalee katika wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.

=Ukipewa talanta usiifiche uvunguni, Bali itumie katika kazi ya injili ya KRISTO.
 
Inawezekana kuna watu wanaangamia kwa sababu tu wewe uliyeokoka umeikalia karama yako uliyopewa na MUNGU.

=Watu wanashuhudia nini kuhusu wewe?
Je kwako unatoka ushuhuda mzuri au mbaya.
Ndugu, Unatakiwa kuwa ushuhuda mzuri kwa watu wote. 



=Usikubali kupoteza uwezo wako wa kumiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Uwezo ni nguvu hivyo usikubali kupoteza nguvu zako za kumiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Wewe Mteule wa YESU ni mtu hatari sana katika ulimwengu wa roho, tatizo lako tu wakati mwingine hujitambui ndio maana mapepo ukikosea tu kidogo yanakuchapa kwa sababu hujitambui na huzitambui haki zako kama mteule wa KRISTO.
Ndugu, usikubali kupoteza uwezo wako wa kumiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Dhambi inaondoa ujasiri.

Ukimuona mtu wa Kanisa anatenda dhambi huku akiwa na ujasiri basi tambua kwamba huyo kama hajavamiwa na mapepo basi amejitenga na Neno la MUNGU na hamtii MUNGU hata kama huhudhuria kanisani.
Huyo anahitaji kusaidiwa kiroho.


=Ukilipokea Neno halisi la MUNGU basi tambua kwamba umepokea Ufalme wa MUNGU.
Kwa Neno la MUNGU hakika ukilitii utakuwa mtu wa tofauti sana.

Naomba pia ujue kwamba kuna tofauti kati ya kustawi na kufanikiwa.
Watu wengi wamefanikiwa kiroho ila hawajastawi kiroho.
Hebu ona mfano huu ambapo Mtumishi wa MUNGU Joshua aliambiwa jinsi ya kustawi.

Yoshua 1:8 '' Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.''
Ili Joshua astawi kiroho ilimpasa kufanya haya;
1. Neno la MUNGU lisiondoke kinywani mwake.
2. Atafakari Neno la MUNGU usiku na Mchana.
3. Atende sawa sawa na Neno la MUNGU linavyotaka.

Kwa hayo matatu ndipo njia yake itafanikiwa sana na kisha atastawi sana kiroho.
Hata wewe kama unataka kufanikiwa hakikisha;
1. Neno la MUNGU lisiondoke kinywani mwako.
2. Tafakari Neno la MUNGU usiku na mchana.
3. Tenda sawasawa na Neno la MUNGU la injili ya KRISTO YESU linavyotaka.
Kwa hayo hakika utafanikiwa sana.
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments