JINSI YA KUPONA UGONJWA WA DHAMBI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu Yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Dhambi ni ugonjwa mbaya sana.
Watu wengi wanaumwa ugonjwa huu mbaya na hatari kuliko magonjwa yote.
Wanaoumwa ugonjwa huu wakifa bila kupona huu ugonjwa wa dhambi hawawezi kwenda uzima wa milele.

Ndugu unayeumwa ugonjwa huu uitwao dhambi hakikisha unamfuata Daktari YESU KRISTO ili akuponye.
Yeye YESU anaitwa tabibu wa ajabu maana anaponya magonjwa yote ukiwemo na ugonjwa huu wa dhambi ambao hakuna mwingine yeyote anayeweza kuuponya.


Luka 5:31-32 " YESU akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi.Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu."

Kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi wako na kutubu kisha unaacha dhambi zote ndio kupona ugonjwa wa dhambi.
Ugonjwa wa dhambi una virusi vibaya kuliko virusi vyote hivyo kwa mtu anayetaka kwenda uzima wa milele inampasa tu kumfuata Bwana YESU ili amponye ugonjwa wa dhambi.
Kumbuka hakuna dhambi kubwa wala ndogo na hakuna dhambi isiyoponyeka kwa MUNGU hivyo kumpokea Bwana YESU na kutubu ndio kupona ugonjwa wa dhambi.

Tunajua tabibu maana yake Daktari na YESU ndio tabibu wa ajabu maana anaponya hadi ugonjwa sugu wa dhambi.
Ndugu hakikisha unapona Leo.

Kupona ugonjwa wa dhambi ni.


1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.


2. Kutubu dhambi zote na kuziacha.


3. Baada ya toba ishi maisha matakatifu ya Wokovu wake Bwana YESU.


Ndugu tubu kwa Bwana YESU na acha dhambi zote utakuwa umepona hakika ugonjwa huu hatari na mbaya sana wa dhambi.
Baada ya kupona dhambi kwa mfupi sana kutokana na wewe kumfuata Bwana YESU ngoja sasa nikishauri mambo muhimu sana ili ugonjwa huo usikurudie.

Mithali 23:23 " Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu."

1. Inunue kweli wala usikubali kuiuza.

Kuiuza kweli maana yake kuachana nayo au kujitenga nayo.
Kweli ni Neno la MUNGU la Wokovu wa YESU KRISTO.
Hakikisha unalitendea kazi Neno la MUNGU na litii hilo itakusaidia maana Neno la MUNGU ndio kweli.


Yohana 17:17 "Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli."


2. Inunue hekima na wala usikubali kuiuza.

Hekima ni Elimu ya maarifa sahihi yatokayo katika Neno la MUNGU.


Mithali 1:2-5 " Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu; kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili. Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari; mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia."

Kazi ya elimu ni kuondoa ujinga ndani ya mtu.
Mjinga ni mtu asiyeelewa kitu lakini akifundishwa anaelewa na ujinga unafutika ndani yake.
Maarifa ya neno la MUNGU hutuondolea kutokuelewa kwetu na sasa tunakuwa tunaelewa kujua yatupasayo kujua.
Tuna mambo mengi sana tunatakiwa tujifunze kujua.
Hekima ya Ki MUNGU ndio elimu inayotujulisha kila kitu kama wateule wa MUNGU ambao tumepona ugonjwa wa dhambi.
Tunahitaji kuwa na maarifa ya kujua kuisikiliza sauti ya MUNGU na kuielewa, tunahitaji kujua kanuni za Kibiblia juu ya maombi na utoaji.
Tunahitaji kujifunza mambo mengi sana ndani ya Biblia ambayo hayo ni hekima ya MUNGU ya kutuondolea ujinga na sasa tunakuwa tunafahamu.


3. Nunua mafundisho ya Neno la MUNGU.

Kununua mafundisho ya Neno la MUNGU ni kutumia gharama za muda wako ili kujifunza Neno la MUNGU.
Fundisho la Neno la MUNGU ndilo litakufanya ukue kiroho.
Kwenda ibadani kila Mara kwenye mafundisho ya Biblia ni njia mojawapo muhimu sana ya kukufanya ukue kiroho.


Waebrania 5:12-14 "Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya MUNGU; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya."


Unatakiwa upande kiwango chako kiroho kutoka mtoto mchanga na kuwa mtu mzima kiroho.
Hizo hatua kila mmoja katika KRISTO huzipitia hivyo hakikisha unahusika kila Leo na mafundisho ya Neno la MUNGU.


4. Nunua ufahamu wa Ki MUNGU.

Ufahamu wa Ki MUNGU unaletwa na ROHO MTAKATIFU pekee.
Neno la MUNGU ni ufahamu lakini hatuwezi kuuelewa vyema huo ufahamu bila ROHO MTAKATIFU.
Katika kipengele hiki unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ndipo utashinda dhambi siku zote.
ROHO MTAKATIFU katika kutupa ufahamu wa Ki MUNGU hutufundisha, hutukumbusha na kutujulisha ndipo tunajua.


Yohana 14:26 " Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."

ROHO MTAKATIFU ndiye anayejua siri zote za mbinguni na duniani hivyo kwa mapenzi yake hutufunulia na sisi tunajua yatupasayo kujua.
Kupambana kiroho na mawakala wa shetani kunahitaji ufahamu wa Neno la MUNGU tupewalo na ROHO MTAKATIFU ndipo tutashinda.
Kila kitu chetu cha kufanikiwa kwetu tunahitaji ROHO MTAKATIFU atusaidie kwa kutupa ufahamu ndipo tunaelewa.
ROHO MTAKATIFU hutufumbulia mafumbo ya MUNGU tunaelewa na kujua mpango wa MUNGU Muumba wetu.


1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU. ''


Kumbe ni muhimu sana kujazwa ROHO MTAKATIFU baada ya kupona ugonjwa wa dhambi.

Ndio maana Biblia inasema hivi;
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''


Kumbe kuwa Mkristo bila ROHO MTAKATIFU ni kama gari bila mafuta na gari hilo linasafiri.
Unamhitaji ROHO MTAKATIFU sana sana ndipo utashinda ya dunia yote.


MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu, pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments