KWANINI UNAENDELEA KUTESEKA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Ulishawahi kujiuliza kwanini unaendelea na mateso hata baada ya wewe kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako?
Naomba ujifunze leo ikusaidie kusimama imara na njia za kuyafuta mateso hayo.
Kuna tofauti kati ya kuokoka na kukombolewa.
Kuokoka ni tiketi ya uzima wa milele lakini kukombolewa ni baada ya kuokoka, kukombolewa ni juhudi ya mhusika katika maombi na utakatifu.

Waefeso 2:8 Biblia inajulisha juu ya kuokoka ambapo inasema hivi '' Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;''
Kumbe tumeshaokolewa tayari na sio tutaokolewa baadae.
Kila mtu baada ya kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi hakika mtu huyo anakuwa ameokoka na jina lake linaandikwa katika kitabu cha uzima.
Kukombolewa ni jambo jingine kabisa.
Kukombolewa huja baada ya kuokoka, kukombolewa ni matunda ya mtu kuokoka, Kukombolewa kunahitaji aliyeokolewa kuitumia nafasi yake kiroho ili kuhakikisha anakombolewa.
Kukombolewa ni jambo linaloendelea kulingana na juhudi ya mhusika katika maombi, utakatifu na kulijua Neno la MUNGU na kulitumia.
Wakolosai 1:13-14 '' Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;'' 
Mteule inakupasa uhamishwe kutoka utawala wa giza na sasa uwe tu katika utawala wa nuru wa Bwana YESU.
Kuna wengine huwa wanahama jumapili tu lakini kuanzia jumatatu wanarudi utawala wa giza.
Ni muhimu sana ukachunguza chanzo cha kuteseka kwako wakati sasa una mamlaka na nguvu za kushinda kila nguvu za giza.
Leo unaweza kukuta mtu aliyeongozwa sala ya toba akaokoka lakini bado mtu huyo anateswa na wachawi na mapepo na kila nguvu za giza kwa sababu tu ya mambo yafuatayo:
1. Kuna mlango wa shetani katika maisha yake bado hajaufunga.
 Waefeso 4:27 ''wala msimpe Ibilisi nafasi.''
Kumpa shetani nafasi ni jambo baya sana maana huo ni mlango wa mateso kwako.
Kufanya dhambi ni mlango wa nguvu za giza kukutesa.
Kuwa na uchungu mwingi na kutokusamehe ni mlango ambao nguvu za giza zinaweza kuingia kwako na kukutesa.
Kushirikiana na watu ambao hawajaokoka katika mambo ya kimila yaliyo machukizo kwa MUNGU ni mlango wa nguvu za giza kuingia kwako na kukuonea. Inawezekana umeokoka lakini matambiko ya ukoo unahudhuria, kama wanachinja mbuzi na kuninenea na wewe unakula na kushiriki basi hayo maagano hayo yanaweza kukukamata.
Katika maisha yako hakikisha hakuna mlango wa kipepo ambao haujaufunga ndipo nguvu za giza hazitaendelea kukutesa.

2. Kuna tabia za kidunia alizokuwa anatenda zamani hajaziacha.
1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.'
Usikubali tabia zako chafu za kabla hujaokoka uendelee nazo hata baada ya kuokoka.
Kama ulikuwa mtu wa kwenda disko na kuimba nyimbo za kidunia, unaweza kuwa ni mlango huo wa mapepo kuingia kwako na kukutesa.
Kama ulikuwa unakunywa pombe acha maana huo ni mlango wa nguvu za giza kuingia kwako na kukutesa.
Kama marafiki zako ni watu wanaokuingiza katika mitego ya kipepo jitnge nao maana huo unaweza kuwa ni mlango wa shetani kuendelea kukutesa hata kama umeokoka.
Kama unaendelea kujichubua na kuvaa mawigi huo tu unaweza pia kuwa mlango wa adui kukutesa.
Kuna tabia nyingi sana za kidunia ambazo zinaweza kuwa mlango wa nguvu za giza kukuvamia, hivyo ni muhimu sana kuziacha tabia hizo chafu.

3. Kutokuwa mtu wa maombi.
 1 Yohana 5:14-15 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake(MUNGU), ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.''

Jambo kuu sana ambalo linaweza kusa sababu ya shetani kukutesa hata kama umeokoka ni wewe kukosa maombi.
Biblia inaagiza kuomba na kudumu katika maombi.
Maisha ni kanuni ya ushindi katika maisha ya mteule wa MUNGU aliyeokolewa na Bwana YESU, Hivyo ukidharau maombi utakuwa huhitaji kushinda nguvu za giza.
Wakati mwingine unahitaji kuomba maombi ya kufunga na wakati mwingine unahitaji kukesha katika maombi.
Ukimuona mtu ameshinda na anaendelea kushinda ni kwa sababu ya maombi.
Usipokuwa muombaji utaendelea kuteswa hivyo hakikisha unakuwa muombaji na tena muombaji uliye na Neno la MUNGU.
 
4. Kutokulitii neno la MUNGU na kuacha utakatifu.
Zaburi 119:11 ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''
Kutokutii Neno la MUNGU ni kikwazo kikuuu cha mtu wa MUNGU kuendelea mbele.
Kutokulitii Neno la MUNGU ni kutenda dhambi.
MUNGU anaweza mambo yote isipokuwa jambo moja tu.
Jambo moja tu ambalo MUNGU hawezi kulifanya ni dhambi.
MUNGU hawezi kufanya dhambi yeyote lakini mengine yote MUNGU anaweza.

Usije hata siku moja ukamhusisha MUNGU katika maovu yako.
Kuna watu hufanya maovu na kudai walimuomba MUNGU ili awalinde katika uovu wao, huko ki kumhusisha MUNGU na uovu, watu kama hao Mimi na wewe tuwasaidie tu kiroho. 
Katika maisha yako hakikisha hufungui mlango wa adui kukutesa
Hakikisha huziachi kanuni za MUNGU ziwapasazo wateule wote wa KRISTO.
Usikubali Kuwa mtu wa michanganyo.
Usikubali Kumtii shetani katika kitu chochote ndipo hakika mawakala wa shetani hawataweza kuingia kwako.
Mteule wa MUNGU anapaswa kuwa mtii kwa MUNGU na neno lake na ajitenge na kila kazi ya shetani.
Jilinde sana katika maisha yako usijitie unajisi.
Unajisi unaondoa nguvu za MUNGU ndani ya mtu .
Unajisi unafuta kusudi jema la MUNGU kwako.

Unajisi unakufanya ukose baadhi ya vitu vya ki MUNGU.
Marko 7:21-23 " Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.
Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi."

Najua kupitia maandiko hapo juu umejua ni mambo gani yanaweza kukutia unajisi.

Lakini pia naomba kukujulisha yafuatayo ili ikusaidie kuwa mteule halisi wa KRISTO.
Kuna makundi mawili ya waaminio hivyo kaa katika kundi la washindi.
Aina za wakristo.
1. Waoga.
-Hawa wana Imani haba.
-Wanatetemeka katika baadhi ya vitu kuhusu imani yao.
-Wakitangaziwa maombi ya kufunga watasema hawawezi.
-Wakitangaziwa mkesha watasema wana usingizi.
-Hutoa zaka na sadaka mpaka lifundishwe somo kuhusu utoaji.
- Husitasita.
-Hawa ni waongo waongo.
-Sio makini
-Hujichanganyachanganya.


2. Wakristo makini.
-Hawa ni makini katika Imani.
-Wanajua wanachokifanya.
-Wanamtii ROHO MTAKATIFU.
-Wanajifunza neno la MUNGU na kulitendea kazi.
-Husamehe na kusahau na kusonga mbele na Wokovu.
-Ni waombaji
-Huishi maisha matakatifu ya haki.

Yakobo 1:19-25 '' Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya MUNGU. Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.
 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.''


Ndugu ngoja nikujulishe mlango mwingine hatari sana ambao kwa huo watu wengi huvamiwa na nguvu za giza.
Kuna watu wengi tu wamepata mapepo kwa njia ya uzinzi na uasherati.
Kuna watu wamepata mapepo baada ya kutembea na wenye mapepo.
Kuna watu wamepata mapepo baada ya kutembea na mawakala wa shetani.
Mtu unaenda kwa mganga na analala na wewe na kukuwekea mapepo na mikataba ya kishetani.

Ndugu zangu, MUNGU anapokataza uzinzi na uasherati ni kwa faida yako ndugu.
Unaweza ukatembea na maroho ya shetani miaka yako yote na ukakosa mbingu kwa sababu tu ya kuruhusu uzinzi na uasherati.

Ndugu, funguliwa Leo kutoka katika hilo, tubu na acha dhambi hiyo.
Tubu kwa jina la YESU KRISTO.

 2 Kor 6:14-18 '' Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya KRISTO na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la MUNGU na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la MUNGU aliye hai; kama MUNGU alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, ''
 MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments