MAOMBI YA KUHARIBU FARASI NA MPANDA FARASI WA KICHAWI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Leo omba maombi ya kuharibu farasi na mpanda farasi wa kichawi.
Yeremia 51:20-21 '' Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja FARASI, NA YEYE AMPANDAYE; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;''

Bwana YESU atukuzwe.
Ngoja nikupe maarifa kidogo tu ili uombe kwa siku moja hii na kushinda.
Inawezekana umeshawahi kuona farasi kwenye ndoto au maono.
Inawezekana unajua farasi anawakilisha nini katika ulimwengu wa roho.
Leo nasukumwa kukupa maarifa kidogo ya kukusaidia katika maombi.


Kwenye Ulimwengu wa roho farasi huwakilisha mambo yafuatayo.

1. Farasi huwakilisha safari yenye spidi.

Hivyo ukiota umepanda farasi wewe mwenyewe maana yake katika yale unayoyafanya mema kwa wakati huo unatakiwa uongeze spidi maana inahitajika spidi ili kuyakamilisha kwa wakati.

Maana yake kazi ya MUNGU unayoifanya inakupasa sana kuongeza spidi sana wakati huo maana jambo hilo liko ndani ya wakati maalumu.
Kama umeona watu wengine wamepanda farasi basi itategemea na mazingira uliyoona ndipo ujue watu hao na farasi hizo zinawakilisha nini.

2. Farasi huwakilisha mbio zenye spidi.

Katika Biblia farasi ametajwa sehemu nyingi sana.
Kuna farasi katika wema wa MUNGU na kuna farasi wa kipepo kwa kusdi la kishetani.
Kwenye ndoto inawezekana umewahi kuona farasi wa aina mbalimbali.

Naomba nikufafanulie ili kama ni farasi wa kipepo ujue sasa kulitumia jina la YESU KRISTO kuwashinda hao mawakala wa shetani.

1. Farasi mweupe huwakilisha ushindi na haki.
Lakini katika farasi mweupe inakupasa kumuomba MUNGU akujulishe aliyepanda juu ya farasi huyo ni nani na anawakilisha nini maana hata mpinga Kristo Biblia inamuonyesha kuwa atapanda farasi mweupe lakini cha ajabu mpinga Kristo kama roho ya kuzimu atakuwa na uta na mshale.

Ufunuo 6:2 '' Nikaona, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda ana uta, akapewa taji, naye akatoka, ali akishinda tena apate kushinda.''

Anayezungumzwa katika andiko hili ni mpiga Kristo lakini atakuwa amepanda farasi mweupe. Unajua maana yake?
Ni kwamba mpinga Kristo atakuja katika mfumo wa dini fulani iliyo kinyume na Wokovu wa Bwana YESU lakini huyo roho ya kuzimu atakuwa na uta yaani ana upindi na mshale, maana yake ni dini lakini dini hiyo kuua watu ni jambo la kawaida tu. Hilo tukio la mpinga Kristo ndilo tukio la kwanza kabisa la wapingaji wa Wokovu wa Bwana YESU.
Lakini tukirudi katika somo langu la leo.
Unadhani kwanini apande farasi na sio mnyama mwingine? Ni kwa sababu ya maana za kiroho za farasi. Kwahiyo mpinga Kristo ni mkusanyiko wa dini zote na na madhehebu yote ya dini ambazo zinakataa Kuokolewa na Bwana YESU na kumkataa ROHO MTAKATIFU na kukataa kuitii Biblia katika kusudi la MUNGU BABA.

2. Farasi mwekundu katika ulimwengu wa roho huwakilisha vita, mateso na kuondoa amani.
Ufunuo 6:4 '' Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.''

Unaweza ukaona katika ndoto au maono mtu amepanda farasi mwekundu na anakushambulia au anafukuza kitu chako au mwana familia au familia. Tambua kwamba kutatokea vita hivyo yakupasa sana uwe muombaji ili kuharibu vita ya kipepo uliyoiona itakayoondoa amani kwako au katika ndoa yako au katika ukoo au jamii.

3. Farasi mweusi huwakilisha njaa.
Ufunuo 6:5 '' Na alipoifungua muhuri ya tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. ''
Kuna umasikini mwingine huwa una chanzo katika ulimwengu wa roho kutokana na mashambulizi ya kipepo.
Kuna ukata mwingine unaweza kukukumba kwa sababu tu huombi na adui anakuwa ameshakuwekea maroho ya kishetani ya kukufilisi.

4. Farasi wa kijivujivu huwakilisha roho ya mauti.
Ufunuo 6:8 '' Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi. ''
Wengi wanateswa sana na roho za mauti.
Nimewahi kufundisha somo kuhusu kuharibu roho za mauti(Unaweza uka-seach google utalipata na utafahamu kwa upana sana maana roho ya mauti ni katika maeneo mengi mno)

Katika maandiko hayo ya Kitabu cha Ufunuo 6 tunaona ni matukio ya siku za mwisho yaliyoamriwa na MUNGU kuelekea wakati wa kurudi kwa Bwana YESU, lakini kwanini nimekuwekea hapa maandiko hayo? Ni ili ujue maana ya farasi katika ulimwengu wa roho na sio ujue maana ya kitabu cha ufunuo, hivyo kujua kitabu cha ufunuo ni somo linge na hili.
Farasi hao aina nne wametajwa pia katika kitabu cha Zakaria 1:8-9 '' Naliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe.
Ndipo nikasema, Ee BWANA wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonyesha ni nini hawa. ''

Farasi katika ulimwengu wa roho wanaweza wakatumika pia kama silaha za kipepo.

Kwanini leo tunaomba maombi ya kuharibu farasi na mpanda farasi wa kichawi?
Kutoka 15:1-3 ''Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni MUNGU wangu, nami nitamsifu; Ni MUNGU wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake.''

Nataka tujue yafuatayo kuhusu hili.
Baada ya MUNGU kuwaua farasi na mpanda farasi wa kimisri ndipo hatuoni tena vita yeyote kati ya Farao na waisraeli.

Mwisho wa vita kati ya farao na wateule wa MUNGU ni baada ya MUNGU huwaharibu farasi na mpanda farasi.

Kwenye maombi wewe uliyeokoka una mamlaka kuu sana.
Ni mara nyingi umesikia kuna wachawi wanatembea na ungo kwenda kuroga. 

Inawezekana kabisa wachawi wanaokusumbua wewe usiku huwa wanakuja na ungo kukuroga, huo ungo ndio farasi wa kichawi na aliyeanda ungo huo ndio mchawi. 

Ulishawahi kujiuliza ukiomba maombi ya kuteketeza kila ungo wa mchawi anayepanga kuja kukuroga, je mchawi huyo ataweza kusafiri? Jibu ni hapana.
Basi maombi ya kuharibu farasi na mpanda farasi wa kichawi yanaweza kumharibu mchawi na zana zake za kichawi.

 Maombi yako yanaweza kuharibu mchawi na vyombo vyake vya kusafiria kichawi, hivyo vyombo ndivyo farasi wa kichawi.

Mimi P Mabula tangu utotoni kule kwetu usukumani niliwahi sana kusimuliwa jinsi wachawi wanavyokwenda kuroga.

Siku moja usiku tukiwa  nyumbani tuliona moto mbugani kwa mbali na wakubwa wetu wakatuambia hao ni wachawi wamepanda fisi wanaenda kuroga. 
Sasa kama iko hivyo basi ukiomba maombi ya kuharibu fisi wao wa kichawi hakika huyo mchawi hata kama anapanga kuja kukuroga wewe hakika hatakuja maana usafiri wake wa kipepo umeharibiwa kupitia maombi yako katika jina la YESU KRISTO.
Huo usafiri wa kichawi ndio farasi wa kichawi.

Leo usikubali farasi na mpanda farasi wa kichwai wakutese tena.
Omba maombi ya kuharibu mchawi na usafiri wake wa kichawi.
Vita itakoma tu kama utaharibu mchawi na vyombo vyake vya usafiri vya kichawi.

Ni ufunuo mzuri huu leo kwamba uombe maombi ya kuharibu farasi na mpanda farasi.
maombi haya ni muhimu sana na mara ya kwanza mimi nilisikia sauti nikiwa Kanisani kwamba niombe maombi ya kuharibu farasi na mpanda farasi wa kichawi, hakika nilishinda.

Baada ya maombi yale mimi naamini hakika hata kama mawakala wa shetani watataka kutuma maroho ya uharibifu basi hakika maroho hayo hayatasafiri maana usafiri wao wa kipepo nimeshauangamiza kwa damu ya YESU KRISTO.

Kuna farasi wengine kwenye ulimwengu wa roho sio farasi tu wa kawaida hivyo maombi yako katika jina la YESU KRISTO yatakuletea ushindi mkuu.
Ufunuo 9:17-21 ''17 Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao waliokaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti. Theluthi ya wanadamu wakauawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kiberiti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao. Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao; maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa, nao wanadhuru kwa hivyo. Na wanadamu waliosalia, wasiouawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda. Wala hawakuutubia uuaji wao, wala uchawi wao, wala uasherati wao, wala wivi wao.''

Ndugu omba na hakikisha unaishi maisha matakatifu ndipo hakika utakuwa na ushindi wa kudumu dhidi ya mawakala wa shetani.
Omba katika ROHO MTAKATIFU na omba kwa imani.

Jambo la Mwisho naomba uzingatie katika maombi ni kwamba kila unapopambana na maroho ya shetani tambua kwamba inakupasa upigane na maadui wanne ndipo utashinda kwa urahisi sana.

1. Adui wa kwanza ni hiyo roho ya kipepo iliyotumwa kwako.

2. Adui wa pili ni maroho yaliyowekwa kipepo ili kuisaidia hiyo roho unayopambana nayo ikitokea unataka kuishinda ili isitimize lengo la kishetani.

3. Adui wa tatu ni vyombo vya usafiri vya kichawi vilivyobeba hivyo unavyopambana navyo.

Vyombo hivyo vya usafiri wa kichawi ndivyo hivyo mimi nimeita farasi wa kichawi.

4. Adui wa nne ni yule aliyetuma maroho hayo ya kukutesa katika maisha yako.

Katika maombi yako hakikisha hubakizi hata adui mmoja ndipo utashinda vita ya kiroho vyema.

Maombi katika jina la YESU KRISTO ni silaha ya mwisho isiyoweza kushindwa na adui yeyote katika ulimwengu wa roho.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments