MAOMBI YA KUOMBEA KIBALI KATIKA KILA ENEO LA MAISHA YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

  Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu.
Kwanza namshukuru MUNGU wa mbinguni maana  bado masomo saba(7) ili nifikishe masomo 700 tangu nianze kufundisha mtandaoni Neno la MUNGU, Utukufu ni kwa Bwana YESU Mfalme wa uzima wa milele.
Katika somo la leo linahusu maombi ya kibali kitakachokuwezesha kuwa mshindi katika maisha yako yote.
Kibali ni nini?
Kibali ni idhini anayopata mtu ili kupata vitu fulani avitakavyo.
Kibali ni kukubaliwa kufanya jambo jema unalolitaka kulifanya.
Kibali ni ruhusa inayovisukuma nje vizuizi vyote.
Kibali ni ridhaa ya kutenda unachotaka kutenda.
Sasa nisikilize kwa maandishi haya  itakusaidia.
1 Samweli 2:26 ''Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.''
 Samweli alikuwa mteule wa MUNGU kama ulivyo wewe ulieokolewa na Bwana YESU.
Samweli alikuwa na  kibali kwa MUNGU na kwa wanadamu.
Kibali kilikuwa kimemtangulia Samweli katika maisha yake, ndio maana alisema naye mara kwa mara.
Kibali kilifanya Samweli awe mtawala wa waisraeli wote bila kuchaguliwa na watu wala kuteuliwa, alikuwa mwamuzi wa mwisho kabla ya mfumo wa ufalme haujaanza katika Israeli.
Biblia inasema watu  walikuwa wanamfuata ili awaamue na kuwafundisha na kuwaelekeza, Kwa sababu ya nini?
 Ni kwa sababu ya kibali.
Baadae Waisraeli walitaka mfalme ndipo MUNGU akasema na Samweli na kwa kupitia Samweli,  Sauli akawa mfalme. Lakini jambo la ajabu ni kwamba Samweli alikuwa na nguvu wakati mwingine kuliko Mfalme maana hata Mfalme alihitaji Msaada kwa Samweli mwenye kibali kwa MUNGU na wanadamu.
Kibali kina nguvu sana sana.
Ukishindana na mtu mwenye kibali itakusumbua sana kumshinda.
Nilichojifunza ni kwamba kila eneo la maisha yako unahitaji kibali cha MUNGU ndipo utafanikiwa na kustawi.
Sio waliosoma wote na kazi nzuri, wenye vibali haijalishi wana elimu ndogo   wana kazi.
Sio mabinti wazuri na warembo wote wamefunga ndoa takatifu, wenye vibali ndio walifanikiwa kufunga ndoa takatifu.
Sio wahubiri wazuri wote wana makanisa makubwa sana, wenye vibali ndio wamefanikiwa.
Nimewahi kukutana na wanaume wenye kazi nzuri na maisha mazuri lakini kila akimchumbia binti anakataliwa, ndugu mmoja mwanaume  alinipigia simu akisema afanye nini ili naye apate mchumba? 
Ndugu yule aliongea kwa uchungu sana huku analia sana.
Nikamuuliza ana miaka mingapi, akasema miaka 42 na amejaribu sana kutafuta mchumba lakini hajafanikiwa kumpata, hana tatizo lolote la maumbilie au uchumi lakini hakuna binti amewahi kumkubali ili wachumbiane kisha wafunge ndoa.
Kibali ni kitu muhimu sana.
 ''Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA.-Mithali 18:22 ''
 Tafasiri ya BHN inasema '' Anayempata Mke amepata bahati njema; Hiyo ni fadhili kutoka kwa MUNGU''
Mke au Mume anayezungumzwa hapa kwamba ukimpata umepata bahati njema inayotokana na fadhili za MUNGU sio kila Mke au Kila Mume bali ni Mke Mwema au Mume Mwema.
Huyo mke mwema au mume mwema ili umpate unahitaji fadhili za MUNGU na fadhili za MUNGU zimebeba kibali cha MUNGU cha kukufanikisha ili umpate huyo Mke Mwema wako au Mume mwema wako.
 Kuna watu wako katika ndoa kabisa lakini hawana vibali kwa wenzi wao. Unakuta mama wa familia hata aongee nini mumewe hawezi kukubaliana naye japokuwa mama huyo anaongea jambo sahihi na muhimu kabisa.
Mama unahitaji kibali cha MUNGU cha kukubaliwa.
Dada unahitaji kibali cha MUNGU na kutendewa mema.
Kuna watu katika ukoo huonekana kama takataka tu maana hawana kibali, ndugu uhahitaji kibali cha MUNGU kwa ndugu zako.
Mtumishi unahitaji kibali cha MUNGU kwa wote unaowaendea ili kuwahubiria injili ya KRISTO.
Jambo muhimu sana kujua ni kwamba kila mwanadamu huumbwa na kibali fulani katika maisha yake, kibali hicho hutolewa na MUNGU hata kabla mwanadamu huyo hajazaliwa.
Ona Mfano huu, Yeremia 1:5 '' Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.''

Yeremia aliumbwa na MUNGU huku akiwa na kibali cha kuwa nabii wa mataifa.
Hata wewe ulipoumbwa na MUNGU katika tumbo la mama yako ulipewa na MUNGU kibali katika vitu fulani katika maisha yako.
Tatizo tu wengi hawajui wamepewa vibali katika jambo gani  kwa utukufu wa MUNGU.
Wengi shetani huwateka mapema sana na kuvigeuza vibali vyao ili badala ya kuvitumia vibali hivyo kwa utukufu wa MUNGU, wao wanavitumia kwa utukufu wa shetani na kujipoteza kabisa wao wenyewe.
Kuna waimbaji MUNGU amewapa kibali cha uimbaji cha kimataifa kabisa lakini wao wanatumia vibali hivyo kumwimbia shetani na sio MUNGU aliyewapa sauti na karama hiyo.
Unakuta kuna mwimbaji wa kidunia alipewa kibali na MUNGU ili amwimbie MUNGU katika kanisa lakini yeye alichagua kumwimbia shetani duniani na kujipoteza kabisa.
Wapo watu wana vibali katika nguvu lakini badala ya nguvu hizo kuzitumia kupeleka injili wao hutumia nguvu zao katika wizi na ujambazi.
Katika Mwili wa KRISTO Kila Mteule wa MUNGU na kibali cha MUNGU lakini wengine vibali vyao vimezibwa kipepo ndio maana hawawezi kusimama katika nafasi zao kiutumishi.
Wengine kwa sababu ya maisha ya dhambi ndio maana vibali vyao havifanyikazi yake.
Vibali vya MUNGU viko vingi sana sana.
Hujawahi kukutana na binti ambaye watu walikuwa wanamwita mbaya wa sura lakini kwa kibali anafunga ndoa takatifu na kuishi maisha ya ndoa ya furaha kuliko hata waliokuwa wanambeza?
Hujawahi kuona mtu anapata madaraka fulani lakini wenye nguvu kuliko yeye na wenye elimu nzuri kuliko yeye wapo tu wanaangalia?
Kuna wenye vibali vya kimataifa kama Yeremia na kuna kuna wenye vibali katika taifa, kuna wenye vibali katika mji na kuna wenye vibali katika maeneo fulani.
Jambo muhimu tu kujua ni kwamba una kibali katika nini?
Ndugu ombea kibali chako ulichoumbwa nacho na MUNGU na kitumie kibali hicho kwa utukufu wa MUNGU.
Shetani anaweza kuharibu kibali  ndio maana kuna watu hufanya baadhi ya vitu bila kibali na watu hao hujikuta wameanguka sana na bila mafanikio
MUNGU ametuumbia kibali na MUNGU pia ametuumbia matendo mema ili tuyaishi tukitumia vibali vyetu kwa kusudi lake.
 Waefeso 2:10 ''Maana tu kazi yake(MUNGU), tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.''

Ndugu una kibali katika nini?
Nakuomba fanyia kazi kibali chako.
Kuna vibali vya aina nyingi sana.
Kuna watu wana vibali katika vinywa yaani matamshi yao yana nguvu kubwa sana inayowafanya watu wengine kuwasikiliza na hata kuwafuata.
Kuna watu wana vibali kuandika, ndugu andika Neno la MUNGU.
Kuna watu wana vibali vya ushawishi.
Kuna watu wana vibali vya kupendwa na kukubaliwa sana katika jamii.
Kuna watu wana vibali vya kuongoza.
Kuna watu wana vibali vya kusikilizwa.
Vipo vibali vingi sana.

Kwanini uombee kibali?
Hebu ngoja nikufundishe kazi za kibali ili upate msukumo wa kuombea kibali chako.

1. Kibali kinafungua macho ya watu kukuona na kukutendea mema.
2. Kibali kinaamrisha watu kukukubali na kukutendea mema, hata kama huna sifa za kukubaliwa
3. Kibali kinawafanya watu kukuheshimu na kukuthamini.
4. Kibali kinawafanya watu kukupenda na kukufanyia mema, hata kama huna sifa za kupendwa.
5. Kila kinawafanya watu wakufuate katika unayoyasema na kuyafanya.
6. Kibali kinakutengeneza ili ufae, hata kama hufai.
7. Kibali kinaleta upendeleo kwako, hata kama hustahili kupendelewa.

Zaburi 106:4- '' Ee BWANA, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. Unijilie kwa wokovu wako, Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako.''

Hujawahi kumuona mtu ambaye watu wengi sana wanamkubali sana sana hata kama hana sifa yeyote njema, huyo mtu ana kibali.
 Omba MUNGU akuletee watu wanaokiona kibali chako kutoka kwa MUNGU na kukithamini.
Jambo kubwa tu kumbuka tuliumbiwa matendo mema ili tuyaishi hivyo kibali alichokupa MUNGU ni kwa mema na sio mabaya.

Endelea kujifunza somo hili itakusaidia.

Dalili za mtu ambaye kibali chake shetani amekiharibu.

1. Hafanikiwa hata kama ana sifa zote za kufanikiwa.
2. Kutumia nguvu nyingi sana hata pale ambapo asingetumia nguvu nyingi  akiwa na kibali.
3. Kukataliwa bila sababu, kuonewa bila sababu wala kosa na kupuuzwa bila sababu za msingi zozote.
4. Kutokufikia lengo la mafanikio yaliyokusudiwa.

Ndugu unahitaji sana kuombea kibali chako.
Kuna watu wana vibali vya kupendwa kwa mfano.
Mtu kama huyo akifungua biashara atafanikiwa sana maana watu wanampenda na hata hawajui kwanini wanampenda.
Kila mtu ana kibali katika jambo fulani.
Ukitaka ujue hivyo chunguza tu katika Kanisa la MUNGU.
Sio wote wana kibali katika uimbaji wao, kuna wenye sauti nzuri za kuimba lakini hawana kibali.
Sio watu wote wana uwezo wa kushawishi, wenye kibali hicho hata akiwa kiongozi mfano wa vijana, anaweza kuwashawishi vijana kushuhudia na ukashangaa sana matokeo yake kuwa makubwa sana.
Ndugu ombea kibali chako.
Unaweza ukawa na elimu nzuri lakini watu wanakuweka katika kundi moja na ambao hawakusoma  kwa sababu tu shetani ameharibu kibali chako na kazini wewe ndio umegeuka mtumwa tu na sio bosi.
Kibali kina nguvu sana.
Kila jambo katika maisha yako omba kibali cha MUNGU cha kukuwezesha.
Watu wengi hawajui kabisa kwamba hata ukiomba jambo fulani kwa MUNGU tambua kwamba unahitaji kibali cha MUNGU ili kupokea baraka hiyo.
Kuna kibali cha kupata Mchumba lakini pia kuna kibali cha kufunga ndoa, tena kuna kibali cha kuishi maisha ya ndoa na hata kuna kibali cha kuishi maisha ya ndoa ya furaha.
Ukiomba tu upate kibali cha kupata mchumba basi unaweza ukampata mchumba na kabla ya ndoa uchumba unavunjika kwa sababu shetani ameshaharibu kibali chako cha kufunga ndoa.
Katika eneo la maisha yako muombe MUNGU akupe kibali.

 Katika maombi yako juu ya kibali omba maombi yafuayato.

1. Omba kibali ulichoumbwa nacho na MUNGU kifanye kazi  sahihi kwa utukufu wa MUNGU.
2. Komboa kibali chako kwa maombi kama mawakala wa shetani wamekiharibu.
3. Omba kibali cha MUNGU katika yote unayoamua kufanya kwa utukufu wa MUNGU.
Mithali 3:3-4 ''3 Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu.''

 MAOMBI YA KUOMBEA KIBALI.

Baba wa mbinguni hakuna kama wewe muumba wangu.
Nakushukuru kwa uzima na kibali chako cha mimi kuishi.
Naomba unisamehe dhambi zangu zote na niwezeshe kuweza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU.
Niko leo mbele zako JEHOVAH MUNGU wa uzima nikiombea kibali katika maisha yangu.
Nimetambua BWANA ya kwamba kuna kibali uliniumba nacho na kwa neema yako naomba kibali changu kifanye kazi sahihi kwa utukufu wako. Kuna mambo nimejaribu kufanya bila kibali chako lakini sikufanikiwa, MUNGU wangu naomba kibali chako.
Nilijaribu kufungua biashara lakini kwa kukosa kibali chako nilifilisika na kumaliza hata mtaji, ninaomba neema yako na kibali chako MUNGU uliyeniumba.
Ninaomba kibali katika kila eneo ninalokanyaga, Ninaomba kibali kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Ninaomba kibali cha kufanikiwa na kustawi. 
Kila kusudi lako MUNGU  uliloweka ndani yangu naomba unipe kibali MUNGU wangu ili nifanikiwe kutimiza kusudi lako MUNGU kwa kibali chako.
Naomba kibali katika kila eneo la maisha yangu. Naomba kibali kwenye ndoa yangu na kwa watu wa familia yangu, Naomba kibali kwa jina la YESU KRISTO.
Naita kibali katika biashara yangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Naomba kibali cha MUNGU cha kufaulu katika masomo yangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
 Naomba kibali cha kupata mchumba, kufunga ndoa na kuishi maisha ya ndoa ya amani na furaha,kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
 Naomba kibali cha kukubalika kazini kwangu, kwa bosi wangu na wafanyakazi wenzangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Naomba kibali cha kushinda kesi, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Naomba kibali cha kuwashinda maadui zangu kiroho wote, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Naomba kibali cha MUNGU cha kuufuta uchawi na uzinzi katika ukoo wangu,kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Naomba kibali cha kufunga nguvu za hiza zote ili zisifanye kazi katika maisha yangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Kila kibali changu katika kila eneo la maisha yangu naomba kifanye kazi yake katika jina la YESU KRISTO.
 Sasa napata kibali cha kuishi bila magonjwa, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Sasa napata kibali cha kuishi bila kuteswa na majini na wachawi,kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Sasa napata kibali cha kuwapiga upofu mawakala wote wa shetani wanaofuatilia maisha yangu, kazi yangu, ndoa yangu na biashara yangu,kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Napokea leo kibali cha kuanza na kumaliza kila kazi ya MUNGU aliyoiweka ndani yangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Napokea kwa jina la YESU KRISTO kibali cha kuoa/Kuolewa, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Napokea kibali cha kupata mchumba na asiniache tena kamwe,kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Napokea kibali cah MUNGU cha kuapata kazi, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Napokea kibali cha MUNGU na kufanikiwa katika maisha yangu,
Napokea kibali cha kuzishinda kila hila za giza, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Kwa jina la YESU KRISTO ninapata kibali cha MUNGU cha kujifungua salama bila upasuaji wowote, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Kwa jina la YESU KRISTO napokea kibali leo cha kuthaminiwa na watu wote, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
Kwa jina la YESU KRISTO napokea leo kibali cha kukubaliwana na kukutendewa mema na watu wote wanaonizunguza,
kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
 Sasa nakomboa kibali changu chochote ambacho mawakala wa shetani walikizuia au kukiharibu.
Nakikomboa kibali changu cha kupata kazi, na sasa nitapata kazi kwa jina la YESU KRISTO.
Nakikomboa kibali changu cha kupata uzao, na nakikomboa kibali changu cha biashara  yenye mafanikio na faida kuu,kwa jina la YESU KRISTO aliye hai nipokee kibali hicho.
 Kila kibali changu katika kila eneo la maisha yangu ambacho majini au wachawi walikizuia sasa nakikomboa kibali changu kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Nakushukuru MUNGU BABA kwa kunishindia katika kila kibali changu.
Nakushukuru Bwana YESU kwa kunishindia.
Asante maana kwako yote yanawezekana na leo kibali changu kitafanya kazi yake.
Hakuna mchawi atakiziba tena kibali changu cha kulitimiza kusudi la MUNGU juu ya maisha yangu.
Asante MUNGU wa Mbinguni uliyeniumba na kibali na sasa kibali changu kitafanya kazi stahiki kwa jina la YESU KRISTO.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi mkuu.
Amen Amen Amen.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments