MATOLEO NI UFUNGUO WENYE NGUVU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu Yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kwa matoleo mtu humkaribia MUNGU wake. Unapomtolea MUNGU sadaka na zaka ni tendo mojawapo la kumkaribia MUNGU.
Sadaka ni tendo la ibada.

Matoleo ni ufunguo wenye nguvu sana kama mtoaji anamtoleo MUNGU wa mbinguni na huku ameweka tumaini lake kwake MUNGU nabkuliishi kusudi la Wokovu wa YESU KRISTO.
Kwa jinsi gani sadaka inaweza ikawa ufunguo wenye nguvu?
Hebu ngoja tujifunze kutokana na waliotutangulia.


Mwanzo 8:20-22 "Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma."


Sadaka ya Nuhu ikawa ufunguo wa kufungwa kwa gharika.
Gharika baada ya hiyo ya Nuhu, MUNGU alisema haitatokea tena gharika ya kuua watu wote duniani.
MUNGU alisema hivyo moyoni mwake baada ya sadaka safi ya Nuhu.
Sadaka hiyo ikamfanya MUNGU kubariki na kufuta mabaya ikiwemo gharika.
Sadaka ikamfanya MUNGU kusema kwamba hatailaani tena nchi kwa ajili ya mwanadamu.
Ndugu, sadaka yako inaweza ikawa ufunguo wa kufuta laana katika maisha yako.
Laana ni kitu kinachokushikilia kiroho ili usifanikiwe katika baadhi ya vitu, matoleo yako mazuri yanayoambatana na maombi yanaweza kufuta laana hizo zote.
Sadaka yako njema inaweza inaweza kuleta harufu njema kwa MUNGU hata vitu vingi vizuri vikazuiliwa kwako.
Jambo la kujua ni kwamba sadaka njema hutoka katika moyo wa kumpenda MUNGU, asiyempenda MUNGU hawezi kumtolea MUNGU sadaka njema.


Kutoka 25:1-3 "BWANA akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba,"


MUNGU akasema kwamba watu watoe sadaka lakini ni wale ambao mioyo yao inapenda kumtolea MUNGU sadaka. Lakini pia MUNGU anasema sadaka anazohitaji watu wamtolee ni vitu vya thamani kabisa na vyema.
Dhahabu, fedha na shaba ni madini ya thamani sana.
Utoaji wako wa sadaka nzuri na moyo wa unyenyekevu na utii kwa MUNGU Unaweza ukaifanya sadaka yako kuwa katika daraja au kiwango cha dhahabu.
Matoleo yana matokeo makubwa sana kwa anayetoa.
Mtumishi asipowafundisha watu kumtolea MUNGU hakika mtumishi huyo hawatakii mema watu wake anaowapa Neno la MUNGU.
Unaweza ukaomba sana lakini kuna baadhi ya mahitaji Unaweza ukafunuliwa na ROHO MTAKATIFU utoe na sadaka ndipo unapokea.


Rafiki Yangu mmoja yuko morogoro alikaa miaka zaidi ya 4 kwenye ndoa bila mtoto. Aliomba sana lakini majibu ya MUNGU yalikuja yakimhitaji atoe sadaka nzuri, alipotoa sadaka mwezi uleule mwaka uliofuata alipata mtoto kwenye ndoa yake.
Sio vitu vyote tunavyoviombea tutavipata kwa kutoa sadaka lakini kuna vitu pia sadaka hujitajika ndipo unapata.
Sadaka ni muhimu sana katika kutengeneza mambo yako katika ulimwengu wa roho lakini pia sadaka njema lazima itoke katika moyo safi.
Ni lazima uwe unaishi maisha matakatifu katika Wokovu wa Bwana YESU ndipo uambatanishe na sadaka nzuri katika baadhi ya mahitaji.


Ndugu mmoja alipata ufunuo wa ajabu.
Ndugu yule katika ukoo wake walikuwa wanazika kila mwaka, walikuwa watoto zaidi ya kumi katika familia yao, jambo la ajabu walirogwa na kila mwaka wakawa wanazika mmoja, yaani ikifika December kama hajafa mtu wanaanza kuishi kwa mashaka maana ni lazima mmoja afe kabla mwaka mwingine haujafika. Ndugu yule alikuwa ni mtu wa kuumwaumwa tu kila Mara na ni mlemavu. Mwishoni mwa Mwaka 2015 alijua anakufa yeye, ghafla akaanza kutafuta masomo mtandaoni ya kumsaidia kujinasua kwenye janga hilo la kuzika kila mwako kwenye uzao wa familia yako. Alipotafuta alikutana na somo langu na akapata ufunuo wa kutoa sadaka niiombee sadaka na nimuombee na yeye ili mambo ya kuzika kila mwaka yafutike kwenye ukoo wao. Nalimshangaa kwa sadaka yake na Imani yake kwa YESU, nikamuombea na sadaka ile ikanisaidia katika kuchapishia kitabu. MUNGU alimfungua yule ndugu na alifungua ukoo wote. Mwaka ule 2015 hawakuzika, 2016, hawakuzika, 2017 hawajazika na hadi Leo wanafurahi japokuwa hadi anatoa sadaka hiyo walikuwa wameshakufa ndugu zaidi ya 8 kwa miaka 8 mfululizo na wote ni wa familia moja.
Kwa tukio hilo niligundua kwamba sadaka ikiambatana na maombi sahihi na utakatifu hufanya kazi kubwa sana. Ndugu yule alikuwa ameshaombewa sana lakini ufunuo wa sadaka ndio ukabeba ushindi wake, utukufu kwa MUNGU Baba juu mbinguni.
Ndugu mmoja siku moja alinifurahisha sana. Alinipigia simu jioni moja akisema hapo alipo ameshika sadaka, ilikuwa ni jumamosi na akasema niiombee sadaka hiyo maana ni ya kuvunja maagano na kesho yake ataipeleka Kanisani kwao na kuitoa madhabahu. Niliomba na kesho yake akaipeleka Kanisani kwao na maagano husika yakafutika na tangu siku hiyo huwa tunawasiliana akisema anamshangaa MUNGU kwa ufunuo huo aliopewa na ndio ikawa kufanikiwa kwake. Ndugu huyo kabla ya hapo alishaombewa sana, lakini ilihitajika sadaka ndipo akashinda.
Kuna siri kubwa katika kutoa sadaka.
Shetani anajua nguvu za sadaka ndio maana ukienda kwa mganga lazima sadaka iwepo, shetani alijifunza kwa MUNGU kazi za sadaka ndio maana akaiga na kuanza kuwafunga watu kwa sadaka za kipepo kupitia kutoa kwa waganga na wachawi.
Sadaka ni ya muhimu sana lakini mtoaji anatakiwa kuitoa kwa MUNGU huku akiishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU.
Sadaka njema uitoayo kwa Bwana YESU inaweza kusababisha jambo kubwa sana katika ulimwengu wa roho kukuhusu.
Ona mambo makubwa yaliyotoka baada ya Ibrahim kutoa sadaka nzuri na sadaka inayouma sana.


Mwanzo 22:15-18 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu."


Hadi Leo wazawa wa Ibrahim wanamiliki milango ya adui zao kwa sababu tu ya sadaka njema ya Ibrahim.
Sadaka ya Ibrahim ilileta baraka hadi kwa watoto wake na uzao wake hadi Leo hii ninapoandika Ujumbe huu muhimu wa kukusaidia.
Ndugu usipende kumwangalia Mtumishi unayempa sadaka yako Bali mwangalie JEHOVAH MUNGU wake anayemtumikia katika kweli ya KRISTO YESU.

Watu wengine wanatoa hela kanisani badala ya kutoa sadaka kwa MUNGU. MUNGU hahitaji hela yako kwani kila kitu ni mali yake (Zaburi 24:1)
Hivyo usitoe sadaka kwa sababu tu umehimizwa na mhubiri au kanisa ila toa kwa sababu umepata maagizo kutoka ya utoaji kwa MUNGU. MUNGU anaweza kumtumia mhubiri kukupa maelekezo jinsi ya kutoa lakini hakikisha kuwa yanaendana na neno lake.
MUNGU hawezi kukupa ujumbe nje ya Neno lake. Hivyo ukiona mhubiri anakupa maelekezo ya utoaji sadaka ambao haupo kwenye biblia hiyo hiyo sauti ya ROHO MTAKATIFU. Kuna watumishi wanakuambia toa kiasi fulani ili MUNGU afungue milango ya baraka na usipotoa huwezi kubarikiwa, huo ni utapeli.
Lakini Kumbuka kuna wakati usiende mikono mitupu kwa MUNGU.
Kuna mahitaji mengine yanahitaji sadaka, lakini sio mtumishi kukulazimisha sadaka Bali wewe rohoni mwako kufunuliwa ya kutoa sadaka.
Hebu ona mfano huu.


Kumbu 16:16-17 " Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; WALA WASITOKEE MBELE YA BWANA(MUNGU) MIKONO MITUPU. Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya BWANA, Mungu wako, alivyokupa."


Sijui ndugu Yangu, ni katika mahitaji yako yapi ambayo ulimwengu wa roho unatakutaka hadi utoe sadaka ndipo ufanikiwe?
Sijui ni katika hitaji lako Leo pi ambalo uditende mikono mitupe mbele za MUNGU ndipo utapokea?
Hayo asikuambie tu mtumishi wa MUNGU Bali akuambie ROHO MTAKATIFU au wewe mwenyewe uone rohoni au kupata msukumo
Usiwe chini ya sheria kwamba ni lazima utoe sadaka ndipo uombe na kupokea, lakini yako mengine sadaka itahitajika kwa sababu ya mazingira yako ya ulimwengu wa roho.
Na mengine sadaka itahitajika ili kumlazimisha shetani kukuacha.
Sadaka inaweza kuwa ufunguo wa kufutwa kwa madai ya shetani kukuhusu.
Lakini kwa muhimu kujua kwamba utoaji bila utakatifu na kumtii
MUNGU ni hasara.
Usitoe sadaka kidini au kidhehebu ila toa sadaka kwa imani na utakatifu halisi.
Sadaka bila kuokoka ni hitilafu kubwa.


Mathayo 6:19-21 " Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako."


MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments