MISINGI YA MAISHA YA UTAKATIFU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna njia za kumfanya mtu wa MUNGU aliyeokolewa na Bwana YESU aendelee na utakatifu na kumpendeza MUNGU siku zote.
Kuna misingi muhimu sana ambayo kila mtu anatakiwa kuifuata ili adumu katika utakatifu.


Misingi hiyo ya maisha ya utakatifu kwa mteule wa KRISTO ni.


1. KUZALIWA UPYA.


1 Yohana 3:9 '' Kila mtu aliyezaliwa na MUNGU hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na MUNGU. ''

Ni lazima mtu azaliwe mara ya pili.
Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na kisha unaanza kuliishi Neno la MUNGU huko ndiko kuzaliwa upya.
Ni kuzaliwa kwa Neno la MUNGU.
Ni kuzaliwa na MUNGU kwa kuanza kuwa na tabia ya kiungu inayotokana na Neno la MUNGU.


2. KUENENDA KWA ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO ''
 
Kila mteule wa MUNGU inampasa kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Kila mteule wa KRISTO natakiwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU katika maisha ya Wokovu.
Unapozaliwa mara ya pili kubali kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.


Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''


3. KUISHI MAISHA YA MAOMBI.

Yuda 1:20-21 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele. ''

Maombi ni kanuni ya kudumu ya maisha ya mteule wa KRISTO.
Maombi ndio huyafanya maisha ya Wokovu kuwa mepesi na rahisi.
Maombi hufanya kazi nyingi sana ikiwemo kazi ya kuutiisha mwili ili mteule asitende dhambi.
Maombi yanafuta mipango ya kipepo ya dhambi inayopanga na shetani.
Maombi ni jambo la muhimu sana kwa mtu anayetaka kuishi maisha matakatifu siku zote.


4. KUISHI KWA KULITII NENO LA MUNGU.

1 Petro 2:2-3 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili.''

Neno la MUNGU ndio ramani ya kuifuata ukitaka kuishi maisha matakatifu siku zote.
Neno ndilo hutaja dhambi ili mteule asizitende dhambi hizo.
Neno la MUNGU ndilo hutaja kazi za mteule ili ampendeze MUNGU.
Neno la MUNGU ndilo dira ya mteule ili ampendeze MUNGU siku zote.
Tukitaka tumpendeze MUNGU basi ni lazima tulijue Neno lake na kulitii.
Ukilitii Neno la MUNGU umemtii MUNGU.
Neno la MUNGU linatakiwa likae moyoni na sio kwenye daftari yako tu.


''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.- Zaburi 119:11''


5. KUDUMU KATIKA KUSANYIKO LENYE FUNDISHO SAHIHI LA NENO LA KRISTO.

Waebrania 10:24-25 ''tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.''

MUNGU hutaka kukusaidia katika ibada kanisani.
MUNGU anataka akusaidie katika semina ya Neno lake na mikutano ya injili.
Kuwa mtu wa ibada ni jambo la muhimu sana sana kwa mtu anayeishi maisha matakatifu.


6. KUISHI MAISHA YA UPENDO WA KWELI.

Wakolosai 3:12-14 ''2 Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.''

Upendo una siri kubwa sana.
Upendio ndio tabia ya wateule wa MUNGU.
Kuishi maisha ya upendo ni kumpendeza MUNGU.
Watakatifu ni watu wa upendo kwa watu wote.
Mfano mmoja ni kwamba ukiona mtu anaenda kuwashuhudia injili watu ujue huyo ndugu kwanza amejaa upendo wa MUNGU ndio maana anawahurumia na wengine na anatamani Bwana YESU awaokoe.


7. KUKATAA DHAMBI ZOTE NA ZA KILA NAMNA.

1 Kor 5:9-11 ''Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi. Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.''

Dhambi ndio kitu pekee kinachoweza kufuta utakatifu wa mtu.
Kanisa la MUNGU ni lazima tukatae dhambi zote na tusishirikiane na watenda dhambi katika dhambi zao.


MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments