MTU ANAWEZAJE KUOKOKA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Mtu anawezaje kuokoka?
Niliulizwa swali hilo na ndugu mmoja aliyezoelea dini bila Wokovu.
Swali kama hilo limekuwa sana katika baadhi ya mioyo ya baadhi ya watu.
Ukweli ni kwamba kuokoka kuko sana na inawezekana kabisa.
Mtu anaweza kuokoka kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake, akatubu na kuacha dhambi zote, kisha tangu siku hiyo anaanza kuishi maisha matakatifu akihudhuria ibada, maombi na kujifunza Neno la MUNGU huku akilitendea kazi neno hilo na MUNGU.
Baada ya hayo hakika umeokoka na Biblia inakuambia kwamba.

Waefeso 2:8 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;"

Mtu anawezaje kuwa Matakatifu?
Mtu anaweza kuwa mtakatifu kwa kukubali kufanyika mtakatifu, kukubali kufanyika mtakatifu ni Kumpokea YESU kama Mwokozi wako Binafsi.
 1 Petro 1:14-19 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO."

Hatua za utakatifu ni pamoja na;

1. Kuliishi Neno la MUNGU katika kweli ya Injili ya KRISTO.

 Waebrania 4:12 ''Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''
Neno la MUNGU wakati mwingine ni kali sana kwa mtu anayeenda kinyume lakini Neno la MUNGU ndilo pekee linaloweza kutufanya tujue tofauti ya maisha ya dhambi na maisha ya utakatifu.
 Ukitaka udumu katika maisha ya utakatifu inakupasa tu kuishi maisha ya kulifuata Neno la KRISTO linavyotaka.
Walioshinda ni wale waliolitii Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU ndilo hutufanya tumtii MUNGU.
Kulitii Neno la MUNGU ndio pia Kuitii sauti ya MUNGU.
 
2. Kuenenda na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.'' 
Jambo la muhimu sana na la lazima sana kulitii kila mteule wa MUNGU ni Kuenenda na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU ndiye MUNGU ndani yetu wateule.
Tukitaka tushinde ya dunia inatupasa tu kumtii ROHO MTAKATIFU.
Ukimtii ROHO MTAKATIFU utaishi maisha matakatifu moja kwa moja.
Ukimtii ROHO MTAKATIFU utatembea katika Neno la MUNGU kwa usahihi.
Ukimtii ROHO MTAKATIFU hauwezi kuona Wokovu mgumu hata siku moja.
Nguvu za wateule za kusonga mbele zina ROHO wa MUNGU hivyo maisha yetu yote ni lazima yaambatane na ROHO MTAKATIFU.
 Wagalatia 5:25 ''Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''
ROHO MTAKATIFU atakufanya Kuishi maisha ya toba na ushindi.

3. Kukataa dhambi zote na kuziacha daima.

Mithali 1:10 '' Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.''
Mteule wa MUNGU ni lazima aache dhambi zote na kujitenga mbali na mazoelea ya mwanzo yote.
Dhambi ndio jambo la kwanza kabisa ambalo linaweza kumfanya mtu aone Wokovu ni mzigo mzito.
Waefeso 4:22-24 ''mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli.''
 
Dhambi ni kitu ambacho hakina faida hata moja.
Dhambi lazima ikae mbali na wateule wa MUNGU walioamua kumpendeza MUNGU.
Kama umeamua kumpendeza MUNGU basi chukia dhambi.
Kama unataka ROHO MTAKATIFU akutumie katika kazi ya MUNGU basi kataa dhambi na maovu yote.
Ukitaka Bwana YESU awe ni Bwana na Mwokozi wako basi hakikisha hutendi dhambi.

1 Kor 6:9-11 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu.''

4. Kutimiza kusudi la kuitwa kwako na MUNGU.

 1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana(YESU) sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana(YESU)''
Moja ya kusudi la kuitwa kwako mteule wa MUNGU ni kumtumikia Bwana YESU. 
Utumishi na utakatifu ni mambo mawili tofauti lakini kwa anayejitambua basi utumishi unaweza kumsogeza karibu na MUNGU na kumfanya awe mbali na maeneo ambayo yatamletea vishawishi vya shetani.
Moja ya matatizo ya watu wengi kuanguka dhambini ni kwa sababu ya matumizi mabaya ya muda hasa kuwa na muda mwingi katika mambo ambayo hayampi MUNGU utukufu.
Kutimiza kusudi la wito wako kunaweza kukufanya usifanye dhambi bali udumu sana katika utakatifu huku ukimtumikia MUNGU katika Kanisa.

5. Kuishi maisha matakatifu na  ya haki.

2 Kor 4:2 ''lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU.''

Kuishi maisha matakatifu ya Wokovu jambo la lazima kwa kila mteule wa MUNGU.
Wokovu ni mpango wa MUNGU kumwokoa Mwanadamu ili huyo mwanadamu sasa aanze kuishi maisha yanayompendeza MUNGU, hivyo kuishi maisha matakatifu ni jambo la muhimu sana na la lazima kwa kila mcha MUNGU.

Watu wote ni watu wa MUNGU maana waliumbwa na MUNGU, lakini sio wote ni watoto wa MUNGU.
Mwana wa MUNGU ni mtu yeyote aliyezaliwa mara ya pili.
Ni mkristo aliyeokoka.


Yohana 1:12-13 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

Ni rahisi tu kuelewa kwamba kabla hujaokoka ulikuwa sio mtoto wa MUNGU. Lakini wokovu wa KRISTO ndio hukupa haki ya kuwa mtoto wa MUNGU.
Kabla hujawa mtoto wa MUNGU ulikuwa mtoto wa nani?
1 Yohana 3:10 " Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU, wala yeye asiyempenda ndugu yake."

Kumbe kuna kuwa mtoto wa shetani na kuna kuwa mtoto wa MUNGU.
YESU anapokuokoa anakupa haki ya kuwa mtoto wa MUNGU.
Hakikisha unakuwa mtoto wa MUNGU kwa kumpokea YESU kama Mwokozi wako na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.

Ndugu hakikisha unaokoka na kuanza kuishi maisha ya wokovu katika Bwana YESU.
 
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments