MTUMISHI WA MUNGU KUWADHARAU WATUMISHI WENZAKE WA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno muhimu sana.
Njia mojawapo ya kukufanya uwe uwe mtumishi mzuri wa MUNGU ni wewe kumtumikia Bwana YESU kwa moyo wa upendo huku ukiwahesabu watumishi wenzako kuwa ni bora kuliko nafsi yako.


''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; -Wafilipi 2:3-5''


Kuwaona watumishi wenzako ni bora kuliko wewe itakusaidia ili usiwe na kiburi na utakuwa unatimiza kusudi la MUNGU na mpango wa MUNGU maana MUNGU huwapinga wote wajikuzao.

Yakobo 4:6 '' Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.''


Hivyo Mtumishi wa Bwana YESU ni lazima kumtumikia MUNGU kwa moyo na jambo la pili ni ni wewe kuwahesabu watumishi wenzako kuwa ni bora kuliko nafsi yako.
Ukimdharau mtumishi mwenzako wa MUNGU maana yake unamkosoa MUNGU aliyempa wito wa kutumika.
Unapomdharau mtumishi mwenzako wa KRISTO maana yake unamdharau MUNGU aliyemuita.
Inawezekana kabisa kuna watumishi hawana upako kama wewe.
Inawezekana kabisa kuna watumishi hawana karama nyingi kama wewe.
Inawezekana kabisa kuna watumishi wanajua kufundisha tu lakini sio kuombea.
Hao wote kama ni watumishi wa Bwana YESU inakupasa sana kuwaona ni bora kuliko wewe hata kama unatumika sana.
Kumbuka mnamtumikia YESU KRISTO yule yule hivyo kila mmoja amhesabu mtumishi mwenzake kuwa ni bora kuliko yeye.


''Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.-1 Samweli 2:3''


Tatizo kubwa la baadhi ya watumishi ni kuwadharau watumishi wenzao katika mwili ule ule mmoja yaani Mwili wa KRISTO. Unaweza ukawagundua hata katika mafundisho yao kama wanadharau watumishi wengine.
Ni hatari sana wewe mtumishi wa MUNGU kumdharau mtumishi wenzako wa MUNGU.
Kumbuka ni MUNGU mmoja mnayemtumikia
Kumbuka ni Mwokozi YESU yule yule ambaye wote mnamtumikia.
Kumbuka ROHO MTAKATIFU ni mmoja tu na humgawia kila mmoja vile apendavyo yeye ROHO MTAKATIFU, hivyo hakuna anayeweza kujichagulia karama za kumtumikia MUNGU bali ROHO MTAKATIFU ndiye hutoa karama, vipawa na huduma.


1 Kor 12:4-11 ''Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.''


Hivyo Mtumishi mmoja wa MUNGU kuwadharau watumishi wengine wa MUNGU ni udhaifu mkubwa sana sana.
Kila Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU anapaswa sana kuwahesabu watenda kazi wenzake kuwa ni bora kuliko nafsi yake.
Inawezekana wewe huduma yako imeinuliwa sana, hiyo isiwe sababu ya kuwadharau watumishi wenzako wa KRISTO.
Inawezekana wewe ni mwimbaji ambaye ukishika mic tu kanisa zima wanazizima kwa furaha sana kwa sababu ya uimbaji wako, hiyo isikufanye ujione ni bora kuliko waimbaji wengine, hiyo isikufanye ujione wewe ni bora kuliko wengine.
Kumbuka kila mmoja hupewa kipimo chake cha utumishi hivyo kwa sababu wote mnamtumikia Bwana YESU basi haipasi mwenye kipimo kikubwa awadharau wenye kipimo kidogo. Ukimdharau mtumishi wenzako wa Bwana YESU maana yake umeota kiburi.
Agizo la MUNGU ni kwamba ''Kila mtumishi awahesabu watumishi wenzake wa KRISTO kuwa ni bora kuliko yeye.
Kumbuka hii ''Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.- Mithali 13:10''
Kumbuka pia na hii ''Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.-1 Wakorintho 10:12 ''

 
Katika kumtumikia MUNGU kila mmoja amepewa sehemu yake ya kutumika.
Ukiwa unamtumikia Bwana YESU mjini na una kundi kubwa basi usijione ni wa thamani kuliko wanaomtumikia Bwana YESU vijijini huku watu wakiwa ni wachache tu.
Ukiwa mfano ni Askofu una pesa wewe isiwe kigezo cha kufundisha watu ili wasitoe zaka na sadaka.


''Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.- 1 Petro 5:5-7''


Katika utumishi nimejifunza jambo hili; Kadri MUNGU anavyokuinua kihuduma ndivyo inakupasa kuongeza sana unyenyekevu.
Wapo watu kwa sababu ya roho za viburi hujiona wao ndio pekee watumishi wa MUNGU huku wakiwaona wengine kuwa ni watoto tu kuitumishi.
Siku moja nilikuwa nafuatilia mahubiri ya mtumishi mmoja wa MUNGU alikuwa nahubiri kwa majigambo mengi.
Katika mahubiri hayo alisema kauli ambazo zilinishangaza sana. Yule Mtumishi alisema kwamba yeye ndio mtumishi wa MUNGU na wengine watabaki kuwa wainjilisti tu.
Nilishangaa sana maana kwa mtazamo wake ni kwamba ukiwa na huduma kubwa wewe ndio mtumishi wa MUNGU na wengine wenye huduma ndogo ndogo ni wainjilisti tu.
Kwa haraka haraka nikagundua kabisa kwamba huo ni udhaifu mkubwa sana sana.
Leo baadhi ya watumishi wanaweza kuhubiri redioni au kwenye Tv na muda mwingi hata hawamzungumzi KRISTO tena bali wanajitangaza wao na kujipa sifa kubwa kubwa tu, ni hatari hakika.
Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.- Isaya 66:2''

Ndugu mtumishi wa Bwana YESU mwenzangu nakuomba wahesabu watumishi wenzako wa Bwana YESU kuwa ni bora kuliko wewe ili hiyo ikusaidie kumpendeza MUNGU na ikusaidie usiwe na roho za kiburi.
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments