IBADA KANISANI NA IBADA YA FAMILIA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.

Ukikosa ibada umekosa haki yako ya kitu chako cha thamani kutoka kwa MUNGU.
Ibada hiyo ni ibada katika KRISTO YESU pekee.

Neno "Ibada" ni neno linalotokana na Neno "kuabudu"
Maana ya kuabudu ni kumsujudia na kumtumikia unayemwabudu.
Neno kusujudu halina maana tu ya kuinamisha mgongo Bali Neno Kusujudu maana yake ni kushuka, kunyenyekea kwa heshima za kiroho.
Kushuka huku sio kuinama tu Bali ni kukubali kuwa chini ya unayemwabudu.
Kwanini nasema unayemwabudu?
Ni kwa sababu sio wote wanaofanya ibada basi ni ibada kwa MUNGU Baba wa mbinguni.
Sio wote wanaoabudu humwabudu JEHOVAH MUNGU pekee wa kweli.
Lakini kwa Kanisa la KRISTO ibada ni jambo la muhimu sana.


Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."

MUNGU alipotuumba Wanadamu alituumbia moyo wa ibada lakini wengi shetani amewapofusha na kuwaondolea moyo wa ibada.
Kuna wengine kwa sasa shetani amewageuzia ibada, badala ya kumwabudu MUNGU wa mbinguni wao wanamwabudu shetani kupitia mawakala zake.
Ewe mteule wa MUNGU uliyeokolewa na Bwana YESU hakikisha unakuwa na moyo wa ibada maana kumwabudu MUNGU ni jambo la lazima kwa Kanisa la KRISTO.


Hakikisha pia unaabudu katika kweli maana pia kuna aina mbili za ibada.
1.Ibada yenye maana.
2. Ibada isiyo na maana au ibada feki.
Warumi 12:1-2 " Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu."


Kwanini hutakiwi kukosa ibada?

1. Ni kwa sababu MUNGU hulituma Neno lake ili kukusaidia hivyo ukikosa ibada umekosa kitu chako cha thamani sana kutoka kwa MUNGU.
Zaburi 107:20 " Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao."

2. Katika ibada MUNGU hujulisha yaliyo ya kwake.
Zaburi 96:7-9 " Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake. Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote."

3. Katika ibada utajifunza na kujumuika na wateule wengine katika kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Yohana 4:23 "Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba(MUNGU) katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu."

Ndugu usikubali kukosa ibada bila sababu.
Usikubali kwenda kwenye mambo ya kidunia muda ambao ni wa ibada Kanisani.

Jifunze kitu kutoka katika Ushuhuda wangu wa Kabla sijaokoka.
Ushuhuda huu ni wa tukio la mwaka 2002.
Kipindi hicho nilikuwa nyumbani kwa Mzee Mabula(Baba yangu mdogo) huko Misungwi Mwanza.
Ulikuwa hivi: kulikuwa na ibada kila baada ya chukula cha usiku.
Sijui nilikuwa Nina nini maana moja ya vipindi nilivyokuwa sivipendi ni ibada hiyo.
Kilichosababisha nisipende ni kuogopa kuambiwa kwamba niongoze ibada na kuhubiri kwa ufupi.
Niliogopa kuambiwa niimbishe wimbo wa kuabudu au niongoze wimbo wa tenzi za rohoni.

Baba alikuwa anaongoza Mara kwa Mara baadae mama akawa anaongoza pia. Baadae Samweli Kaka yangu ninayemfuata akaongoza na taarifa ikatoka kwamba na wengine tujiandae kuongoza, hapo ndipo nilikua natamani ibada isiwepo au Baba Na Mama wawe wamealikwa sehemu hivyo usiku tusiwe na ibada.
Nilikuwa nakosa raha sana muda wa msosi ukifika maana baada ya msosi ni ibada ya familia, nilikuwa natamani kuombewa lakini sio Mimi kuomba, kuongoza nyimbo za kuabudu au kuhubiri.
Nilifanya kila mbinu za kukwepa kuingia zamu lakini siku moja Baba akasema ghafla kwamba "Leo zamu ya Peter kuhubiri" Nilitetemeka hadi watu wote isipokuwa Baba na Mama walicheka.
Nilipewa Biblia huku nikitetemeka sana na huku sina cha kufanya maana ilikuwa wakati wa Mahubiri na mhubiri ni Peter. Nilichofanya ni kushika Biblia huku nikiazimia kwamba nitakapofungua kwa Mara ya kwanza ni hapo hapo nitasoma Bila kufafanua chochote.
Nilipofunua niliangukia kitabu cha Waefeso 5 na nikasoma maandiko yafuatayo;


Waefeso 5:1 Hivyo mfuateni MUNGU, kama watoto wanaopendwa;
Waefeso 5:2 mkaenende katika upendo, kama KRISTO naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa MUNGU, kuwa harufu ya manukato.
Waefeso 5:3 Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;
Waefeso 5:4 wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru.
Waefeso 5:5 Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU.
Waefeso 5:6 Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya MUNGU huwajia wana wa uasi.''


Nilisoma maandiko hayo kwa kukatakata na kutokujiamini huku hata sielewi kama nilikuwa sahihi au kama walikuwa wananielewa.
Nilipomaliza Mzee Mabula alinipongeza huku akicheka kwa jinsi nilivyokuwa nimeogopa, kisha yeye akafafanua vizuri na watu wakaelewa Neno la MUNGU.

Kesho yake Samweli alienda Shule wilayani Magu nikajua sasa nitakuwa sana zamu kuongoza ibada, lakini Baba naye alisafiri kikazi hivyo nikajisemea Angalau.
Kwanini nakujulisha haya Leo?

Nimekumbuka sana kipindi hicho na jinsi ambavyo nilisoma hiyo Waefeso 5 na kuikariri hadi Leo.
Japokuwa kipindi hicho nilikuwa sipendi ibada ya baada ya chakula cha usiku lakini kwa utaratibu huo tulijengewa msingi mzuri sana na hata nilipopata familia yangu niliendeleza.
Kumbuka wazazi au walezi wa watoto wana mchango muhimu sana Bali za watoto wao baadae.
Biblia inasema
"Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.-Mithali 22:6"


Ni vyema sana kuwa na ibada za familia ili watoto wajengwe katika msingi wa Neno la MUNGU.
Mimi binafsi kipindi kile nikiwa mdogo niliona ni mzigo kuwa na ibada za familia baada ya chakula cha usiku lakini baadae niliona niligundua kwamba nilikuwa nafundishwa jambo la muhimu sana sana.
Leo nimeshaandaa masomo zaidi ya 700 lakini kati ya hayo zaidi ya masomo 50 ROHO wa MUNGU alinisemesha nikiwa katika ibada hizo za familia.
Ni ibada muhimu sana hata kama itakuchukua dakika 10 tu au chini ya hapo.

Leo wazazi wanaweza wakasema neno hili "Sina furaha iliyo kuu kuliko hii, kusikia ya kwamba watoto wangu wanakwenda katika kweli.-3Yohana 1:4   kwa sababu ya ile kweli ya KRISTO waliyoipanda ndani yetu.
Hata kama wakati wa kufundishwa sikupenda lakini natambua faida kuu sana iliyotokana na nilichofundishwa zamani.
Ilichukua miaka zaidi ya 7 hiyo mbegu kuota ndani yangu lakini iliota na inafanya kazi Leo, ndio maana ninaujasiri wa kuwaambia rafiki zangu kwamba ibada za familia ni njema sana sana.
Ndugu zangu wote mlio na familia tuuendelezeni utaratibu huu wa ibada za familia.

 MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka. Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments