KAZI YA KILA MKRISTO ALIYEOKOLEWA NA BWANA YESU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
 Kila mtu anapompokea  YESU KRISTO kuwa Mwokozi wake mtu huyo anakuwa Mteule wa MUNGU.

Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

Kumpokea YESU kama Mwokozi hutupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU.
Kuwa watoto wa MUNGU ni mwenendo wetu wa utakatifu kwa MUNGU.
Uwezo huo anaotupa Bwana YESU hutufanya pia tuwe na ushirika na MUNGU Muumba wetu.
Kwa sababu tumeingia sasa katika ufalme wa MUNGU kupitia Mwokozi wetu YESU KRISTO, Inatupasa sana kujua wajibu wetu kama watoto wa MUNGU.
Wewe uliyeokolewa na Bwana YESU ni mtu wa thamani sana sana hivyo hakikisha unaionyesha thamani hiyo kwa kutimiza kusudi la MUNGU la wewe kuokolewa.
Ungeokolewa uende tu mbinguni basi ungeokoka na kufa muda huo huo na kwenda mbinguni. Lakini MUNGU amekupa kuishi katika muda maalumu sana na muda huo unatakiwa kufanya sasa yakupasayo katika Injili ya KRISTO Mwokozi aliyekuokoa.
Naomba uujue wajibu wako kama Mkristo uliyeokoka na unayejitambua.
Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU kupitia YESU KRISTO Mwokozi.
Wajibu huo wa Kila MKRISTO katika Wokovu wa MUNGU ni;

1. Kuieneza injili ya KRISTO.

Wafilipi 1:5-6 "kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya KRISTO YESU; "
Injili ya KRISTO inaenezwa kwa njia nyingi sana.
Kuna wanaohubiri mitaani na kwenye semina na makanisa.
Kuna wanaoimba, kuna waombaji wanaoombea watu wanafunguliwa. Kuna wanaoifanya kazi ya MUNGU kwa kutoa pesa zao na mali zao ili wengine waende kuhubiri, kuna wanaosambaza vijitabu na kuna njia nyingi mno za kuieneza injili. Kazi zote hizo za kuieneza injili zinamhitaji MKRISTO na sio mtu mwingine. Katika maisha yako ya Wokovu hujawahi kufanya kitu chochote kwa vitendo cha kuieneza injili hakika inakupasa sana kuipeleka injili maana ndio wito wa MUNGU kwa kila Mteule.
Marko 16:15-18 '' Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao WAAMINIO; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.''
 Ni jukumu lako kuipeleka injili kokote kule.

2. Kuitetea injili ya KRISTO.

Wafilipi 1:7 "vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii."
 Ni lazima Mteule wa MUNGU aitetee injili.
Umeokolewa ili kufanya kazi ya MUNGU na moja ya kazi ya MUNGU ni kuitetea injili iokoayo ya KRISTO YESU.

Jinsi ya kuitetea injili;

A. Kufundisha ukweli wa injili.
 Ili wanaoipindisha injili wakute watu wanaijua kweli hivyo hawataukubali uongo.
Kufundisha ukweli ni kuitetea injili.

B. Kukemea watu wanaofundisha uongo.
Ukikemea wanaofundisha uongo hakika utakuwa umeitetea injili ya KRISTO.

 C. Kuishi maisha matakatifu.
Unapoishi maisha matakatifu moja kwa moja unakuwa unalitimiza kusudi la injili ya KRISTO na kwa jinsi hiyo unakuwa unaitetea injili ili isitukanwe.

D. Kuomba maombi ili wanaotumia uongo katika mahubiri yao MUNGU awaabishe.

E. Kuipeleka injili.
Kuipelekea injili ni kuifanya injili itimize kusudi la MUNGU na kwa jinsi hiyo unakuwa unaitetea kwa watu ambao walikuwa hawaijui kwa usahihi waijue kupitia wewe kuipeleka.
 Wewe ndio mteteaji wa injili ya KRISTO hivyo itetee daima.

3. Kuwa na mwenendo nzuri na kuishindania injili.

Wafilipi 1:27 "Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya KRISTO, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili;"

Kuishindania imani ni jukumu la kila Mteule wa MUNGU.
Kuishindania imani ni kujifunza sana Neno la MUNGU na kuliishi Neno hilo la MUNGU kama linavyotaka.
Kuishindania imani ni kutimiza mwenendo sahihi ukupasao katika injili ya KRISTO.
Kuishindani injili ni kuzaa matunda yatokanayo na injili kama Neno la MUNGU kwako.
Kuishindani imani ni kubaki katika YESU KRISTO huku ukisonga mbele na Wokovu bila kujali kuna nini au unapitia mazingira gani.

Yuda 1:3 '' Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.''

 Ni wajibu wako wa kudumu kuishindani imani ya uzima mabayo ipo moja tu yaani Wokovu wa Bwana YESU.

4. Kuiishi injili ya amani ya YESU KRISTO.

Waefeso 6:14-15 " Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;"

Kuiishi injili ya KRISTO ni kutimiza wajibu muhimu sana wako mteule wa MUNGU.
Iishi injili kwa kuitii na sio kutii tamaduni za kidunia.
Kuishi injili maana yake ni kuishi maisha matakatifu.
Kuiishi injili ni kuiishi kweli ya MUNGU ambayo ni Neno la MUNGU.
Kuiishi injili ni kuipeleka injili na kuwa tayari kuisapoti wakati wote.
Tumeitwa na MUNGU katika wakati wa injili hivyo ni muhimu sana kuiishi injili ya Bwana YESU.
Yakobo 1:22-25 '' Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. ''


5. Kuwakataa waongo waliojiingiza kwenye injili na kufundisho isivyo injili ya KRISTO.

Wagalatia 1:6-9 "Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya KRISTO, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya KRISTO. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe."
Shetani siku zote hujaribu kuipotoa injili ya KRISTO lakini kazi ya wateule wa MUNGU ni kuzikataa hila hizo za giza.
Wapo watu ambao shetani amewapanda kwa siri katika Ukristo ili tu wafundishe uongo na kuwateka wateule wa MUNGU.
Kazi ya kila mteule wa MUNGU aliyeokolewa na Bwana YESU ni kuwabaini watu hao na kuwakataa.
Ni wajibu wako kuwakataa waliojiingiza kwa siri ili kuliharibu kanisa la MUNGU.
 1 Yohana 4:1-3 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. ''

6. Kuwa na utii katika kuikiri injili ya KRISTO.

2 Wakorintho 9:13 "kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza MUNGU kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya KRISTO, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote."

 Mteule wa MUNGU ni wajibu wake kuikiri injili popote aliko.
Ni wajibu wako kabisa kwamba uikiri injili na usiionee haya injili kwa lolote.
Kuikiri Injili ya KRISTO ni kumkiri KRISTO na ni kuwataka watu wamkiri YESU KRISTO awe Mwokozi wao.
Majaribu yapo lakini hakikisha hupunguzi spidi yako ya kuikiri injili ya KRISTO popote uliko.
Inawezekana kabisa ukakosana na watu kwa sababu tu unawahubiria injili ili watoke kwenye tabia zao za dhambi, songa mbele maana huo ni wajibu wako kuwaambia haijalishi wanataka au hawataki.
Tumia Neno la MUNGU kuwasaidia watu.
Tumia Neno la KRISTO kuwafanya watu wamwamini YESU KRISTO na kumpokea kama Mwokozi wao ili wapate uzima wa milele maana nje na KRISTO hakuna uzima wa milele.
Mathayo 10:32-40 ''Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga. Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.''

7. Kutokuionea haya injili ya KRISTO.

Warumi 1:16 "Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa MUNGU uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia."


Ni wajibu wa kila mteule wa MUNGU kutoionea haya injili ya KRISTO.
Haiwezekani wewe mteule hata wakati unaenda kanisani unaficha Biblia ili watu wa dunia wasikuone kama unaenda kanisani watakucheka.
Hakikisha huionei haya injili ya KRISTO maana injili ni uwezo wa MUNGU uletao wokovu kwa wanaoamini.
Hakikisha watu wanaamini kupitia injili ya KRISTO, ni wajibu wako ndugu.

''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana(YESU) sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana(MUNGU).-1 Kor 15:58''

Hata kanisa lote ni muhimu sana kujua wajibu wao.
Ngoja nikujilishe kazi za kanisa katika injili, na kumbuka kanisa sio jengo ila ni watu waliookoka.
Kumbuka Tena kwamba Kanisa ni Mimi na wewe tuliokolewa na Bwana YESU.
1 Wathesalonike 1:4-5 " Kwa maana, ndugu mnaopendwa na MUNGU, twajua uteule wenu;ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika ROHO MTAKATIFU, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.'' 

 Ni muhimu sana kanisa likatimiza majukumu yake katika injili ya KRISTO.

Kazi 4 za kanisa katika Injili.

1. Kazi ya kanisa ni kuhubiri injili ya KRISTO inayookoa.

2 Timotheo 4:5 Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.''

MUNGU huwaita watu kwa injili hivyo yatupasa kanisa kuipeleka injili ya YESU KRISTO kwa watu wote.

2. Kuidhihirisha injili ya KRISTO kwa watu wote.

2 Timotheo 1:10 "na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu KRISTO YESU; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;''

Ni lazima kanisa tuwe na mabadiliko ndani yetu yaliyotengenezwa na injili ya KRISTO tunayoiamini.

3. Kuishi maisha ya Wokovu.

2 Wathesalonike 2:13-14 "Lakini imetupasa sisi kumshukuru MUNGU sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa MUNGU amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na ROHO, na kuiamini kweli; aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu YESU KRISTO.''

Maisha ya wokovu ni maisha ya ushindi dhidi ya dhambi.
Maisha ya wokovu ni maisha matakatifu ambayo kanisa linatakiwa kuyaishi.


4. Kudumu katika imani.

Wakolosai 1:23 "mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake."

Kanisa ni lazima sana kudumu katika KRISTO.
Ni muhimu sana kudumu katika utakatifu na utumishi.
Kuna hukumu kwa waasi wote.
Wakolosai 3:5-6 " Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;"


Kanisa ni lazima sana kujitenga na mabaya yote maana kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU.

1 Petro 4:17 "Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya MUNGU; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya MUNGU utakuwaje?"

 MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments