KILA MTU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE KATIKA UTAKATIFU NA HESHIMA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno hai la MUNGU aliye hai.
Kama kuna kitu kinawakosesha watu wengi basi ni uzinzi na uasherati. Naomba MUNGU aliyekuumba akupe neema ya kulisoma somo hili lote kwa makini maana nilipewa kama ufunuo ili nimwambie kila mwanadamu nitakayemfikia. Wengi hawapendi masomo kama haya lakini haya ndio muhimu kuliko vyote.
Kila mmoja lazima ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu.

1 Thesalonike 4:3-5 '' Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;  kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;  si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU.''

Kila mmoja ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima.
Kuuweza mwili maana yake kuutiisha na kutokuuruhusu mwili kufanya matendo maovu.
Maana yake kila mmoja ajue kuyaepuka matendo ya mwili  yaliyo machukizo.
Matendo ya mwili ya kuyaepuka yamewekwa wazi sana katika Biblia ili kumsaidia kila mmoja kuuweza mwili wake.
Wagalatia 5:19-21 '' Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.''

Ndugu, usipouweza mwili wako utaanguka dhambini.
Kuna watumishi hudanganya watu kwamba kila mtu ana udhaifu wake. Watu waliofundishwa hivyo hivyo hujichagulia baadhi ya dhambi, wakitenda dhambi hizo kila mara huku wakijisemea kwamba wao udhaifu wao ni huo mmoja tu.
Ndugu mmoja siku moja baada ya mimi kufundisha somo la maonyo alisema kwamba ''Nyinyi watumishi wa kisasa mnajifanya watakatifu sana, je wewe huna dhambi?''
Ndugu yule alisema hayo kwa hasira baada ya mimi kufundisha kwamba wanaosaliti ndoa zao wasipotubu hawataingia uzima wa milele maana ndivyo Biblia inasema.
Mtumishi mwingine akaniambia siku moja kwamba nifundishe tu uzuri wa mbinguni na sio kukemea dhambi maana nikifundisha uzuri wa mbinguni wengi wataelewa na ndipo wataacha dhambi. Nilimwambia ndugu yule kwamba inategemea na ujumbe ambao MUNGU amekupa. Huwezi kuupindisha ujumbe aliokupa MUNGU kwa sababu tu utawakwaza wanadamu watendao hayo maovu. YESU alikemea na mitume walikemea hivyo ukipewa ujumbe wa kuonya, kukaripia na kukemea basi fanya hivyo. Watu wengi ukifundisha ujumbe huo huona kama unawahukumu na kwa jinsi hiyo wanakimbilia andiko linalosema ''Usihukumu usije ukahukumiwa''
Ndugu zangu kila mmoja ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu.
Biblia inasema ''Nakuagiza mbele za MUNGU, na mbele za KRISTO YESU, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;  lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.  Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.2 Timotheo 4:1-5''
Kumkemea mtu sio kumhukumu.
Kumuonya mtu sio kumhukumu.
Kukemea dhambi fulani sio kuhukumu.
Watu katika jamii ya leo wakiambiwa waache dhambi wanasema wanahukumiwa.
Siku moja katika ndoto niliota kuna dada mmoja ninayemfahamu ambaye kanisani kwao ni mwimbaji mzuri sana. Lakini katika ndoto nikamwona anaelekea jehanamu na nikauliza huko ndotoni na kuambiwa kwamba ni kwa sababu siku za karibuni alitoa mimba ya pili na aliyempa mimba hizo zote ni kijana mmoja ambaye naye anasali kanisa lingine. Niliambiwa nimuonye ili ageuke kutoka hiyo safari ya jehanamu na sasa aanze kuelekea mbinguni baada ya kutubu na kuacha uovu huo. Kesho yake nilitafuta namba zake za simu na hakupatikana ila kuna ndugu mmoja anakaa naye ndio akampa simu yake na nikaongea naye. Nilichomwambia ni kwamba nimeona anaelekea jehanamu kwa sababu ya uasherati na kutoa mimba mbili hadi muda huu. Yule Binti aliaanza kulia kwenye simu na akaomba tuonane ili nimuongoze sala ya toba upya. Ni kweli baada ya siku mbili yule binti alikuja Kanisani na akajikuta ananieleza ukweli kama niliouona kwenye ndoto, kisha akaniambia kwamba kwa sasa ana uhusiano wa kimapenzi na wanaume watatu. Alilia sana na kisha nikamuombea na akaapa kwamba kuanzia dakia ile amevunja mahusiano na wanaume hao watatu. Binti yule kwenye Wokovu ana miaka zaidi ya 8 na nilijikuta hadi mimi nataka kulia kwa sababu ya uovu huo alioniambia. Baada ya pale ilipita kama wiki nikampigia simu akasema sasa ana amani na anamshukuru MUNGU maana amerejea kwa upya katika Bwana YESU na hatatenda dhambi tena ya uzinzi. Nilimshukuru MUNGU kwa ajili yake na ni kweli sasa anaendelea vyema kwa YESU huko aliko.
Ujumbe wa leo ambao ROHO wa MUNGU alinipa ni kwamba kila mmoja ajue kuuweza mwili wake katika uatakatifu na heshima.
Usipouweza mwili ujue tu utakuweza, na ukikuweza mwili ujue utatenda dhambi hivyo yakupasa dhambi uishinde.
Mwanzo 4:7 '' Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.''

 Watu wengi matendo ya mwili ndio yamewakamata na kwa njia hiyo wako mbali na MUNGU.
Anayevaa kikahaba huyo hajui kuuweza mwili wake.
Mzinzi na mwasherati huyo hajui kuuweza mwili wake katika utakatifu.
Muongo na mwizi na mchawi hao hawajauweza mwili.
Kila mmoja na ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu.
Kumbuka matendo ya mwili yaliyo maovu ndio hayo yanayowapeleka watu jehanamu kama wakiyatii.
Wako watu pia wamejificha makanisani huku ni watenda dhambi wa kudumu.

 1 Kor 5:9-10 '' Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi. Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.''

Ndugu zangu, ni muhimu sana kila mmoja kuweza mwili wake.
Mwili unatamani dhambi lakini aliyeuweza mwili wake hawezi kuutii mwili hata kufuata tamaa zake.

Usipojua kuuweza mwili wako ujue yafuatayo  yatakuwa yako.

1. Utakuwa ni mtu wa kuanguka dhambini kila mara.

 1 Yohana 2:15-17 ''Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba(MUNGU), bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.''

2. Utatenda dhambi na kuendelea kutenda dhambi na usipopata neema ya kutubu unaweza kukosa uzima wa milele.
Kuna wengine hufa kabisa wakati wakitenda dhambi.

1 Kor 6:9-10 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.'' 

3. Utapata madhara na hasara nyingi katika maisha yako.
Mfano wake ni huu.

Mithali 23:29-30 '' Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu? Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika.'' 
Pombe ni  dhambi na  inaweza kusababisha madhara ya kufanya vitu vibaya na hata kupigwa na kuachiwa jeraha zisizo na sababu.
Kuathirika na magonjwa ya zinaa ni sehemu tu ya hasara ambazo mtu anaweza kuzipata.
Mwizi kupigwa ni mfano hai wa hasara ambazo unaweza kuzipata usipojua kuuweza mwili wako.

 4. Utakuwa muasi kwa MUNGU kila mara.
1 Yohana 3:4  '' Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.''


 5. Utakosa baadhi ya baraka za MUNGU ambazo bila utakatifu huwezi kuzipata.

 Yeremia 5:25 ''Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate. ''
 MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments