MRUHUSU MUNGU AKUTENGENEZE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Naongea sasa kwa njia ya maandishi haya na mtu ambaye MUNGU amemkusudia.
Karibu ndugu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza namna ya kumruhusu MUNGU akutengeneze ili uwe mteule halisi wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Kuna njia kadhaa MUNGU huzitumia kumtengeneza mteule wake na wewe naomba uzizingatie njia hizi ambazo ziko katika Ezekieli 36:26-28 ambazo ni kazi ya MUNGU katika maisha yetu sisi tuliomtii kwa kumpokea Mwanaye YESU KRISTO awe Mwokozi wetu.  Hata wewe fuata utaratibu huu wa MUNGU na utatengenezeka na kuwa mteule safi wa MUNGU. Maandiko haya  ya unabii yanalizungumzia agano jipya ambalo MUNGU atalileta ili lichukue nafasi ya torati na agano hilo ni kazi ya MUNGU kumkamilisha mteule wake aliye tayari kwa uzima wa milele.

Ezekieli 36:25-28 '' Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa MUNGU wenu.''

 Mambo hayo ambayo unatakiwa umruhusu MUNGU akutengeneze sawasawa na Ezekieli 36:25-28 ni haya;

1. Pokea maji safi ya MUNGU ili uwe safi.

Ezekieli 36:25 '' Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.''
 MUNGU yuko tayari kukunyunyuzia maji safi ya kukuosha na kukufanya uwe safi.
Maji ya MUNGU ni kukufanya uwe safi ni wewe Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi maana YESU ndiye mletaji wa Maji hayo aliyoyaahidi MUNGU zamani za manabii. 

Yohana 4:10-15 ''YESU akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya MUNGU, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai?  Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake? YESU akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.''

YESU ana maji ya uzima.
YESU ana maji yaliyo hai.Maji hayo yaliyo hai ni kumpokea YESU na kutubu ndipo mtu anakuwa safi aliyesafishwa na kwa damu ya YESU KRISTO.
Maji huwakilisha toba na damu ya YESU inawatakasa na kuwaondolea uchafu wote hivyo wanakuwa safi sawasawa na Neno la MUNGU linalosema Kwamba ''Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.''

Kuwa safi huko huanza na kumwamini YESU kisha kumpokea kama Mwokozi na kutubu hakika unakuwa safi bila uchafu wowote. Uchafu ni dhambi na kila mashitaka ya rohoni ya zamani lakini mpango wa MUNGU ni kukufanya safi usiye na doa lolote la uchafu. 
Biblia inaendelea kusema
1 Yohana 5:5-6 ''Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU?  Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, YESU KRISTO; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. Naye ROHO ndiye ashuhudiaye, kwa sababu ROHO ndiye kweli.''

Maji hayo ni utakaso unaotokana na fundisho la KRISTO, kisha kumpokea KRISTO kama Mwokozi kunakoambatana na toba inayofuta uchafu wote.
Dhambi ni uchafu.
Mambo ya zamani uliyoyafanya kabla ya kumpokea YESU ni vinyago, hivyo baada ya kumpokea YESU na kutakaswa hakikisha unaachana na vinyago , achana na uchafu, Kubali MUNGU akutakase.
Kubali kwamba wewe unahitaji kutakaswa na MUNGU , Kubali kutubu  na kubali kubadilika kwa kuacha vinyago na uchafu.
Ili uwe safi ni lazima ukubali Bwana YESU akuokoe na kukutakasa.
Hakikisha unaishi maisha ya utakaso.
 Wenye kiu ya kunywa maji hakika huyatafuta maji hayo na kunywa ili kuondoa kiu.
Wenye kiu ya uzima wa milele humpokea YESU na kutubu.
Hakikisha unakuwa ni wewe.
Ufunuo 22:17 ''Na ROHO na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.'


 2. Kubali MUNGU akuumbie moyo mpya.

Ezekieli 36:26 '' Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.''
 Moyo mpya ambao MUNGU ukimruhusu akuumbie ni moyo unaolitii Neno lake.
Zaburi 26:2 '' Ee BWANA, unijaribu na kunipima; Unisafishe mtima wangu na moyo wangu.''
Moyo mpya ni moyo wa unyenyekevu na adabu mbele za MUNGU.
Ni maamuzi binafsi ya mtu kukubali kuumbiwa moyo mpya na MUNGU.
Kuna watu wako makanisani miaka mingi lakini hawajawahi kuumbiwa mioyo mipya maana hawataki.
Moyo mpya ni moyo wa toba.
Moyo mpya  ni moyo wa unyenyekevu na mwanana.
Moyo mpya ni moyo unaosamehe watu na kusahau.
Mwambie MUNGU akuumbie moyo mpya kama ahadi yake inavyosema.
MUNGU yuko tayari siku zote kukuumbia moyo mpya lakini hadi ukubali kuumbiwa moyo mpya.
Wengi wako makanisani lakini wamejaa viburi tu na dharau, hao hawajaumbiwa mioyo mipya, ndugu usiwaige wao bali wewe kubali kuumbiwa moyo mpya na MUNGU.
Moyo mpya ni moyo unaochukia dhambi.
Moyo mpya ni moyo unaompenda MUNGU kuliko chochote.
Moyo mpya ni moyo ulio tayari kumtumikia Bwana YESU .
Moyo Mpya ni moyo unaoishindania imani ya uzima ambayo iko moja tu yaani Wokovu wa Bwana YESU.
Moyo mpya ni moyo wa toba uliojikana na uliopondeka kutokana na Neno la MUNGU.

  Zaburi 51:10 '' Ee MUNGU, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu ''

Ahadi ya MUNGU kwako ni kwamba ukikubali atakuumbia moyo mpya na kuuondoa moyo wa jiwe uliokuwa ndani yako.
Moyo wa jiwe ni moyo ambao hautaki kuokoka.
Moyo wa jiwe ni moyo wa kiburi na dhambi.
Moyo wa jiwe ni moyo unaopenda shetani na mambo mabaya yote.
Mruhusu MUNGU akuondolee moyo wa jiwe na kukuumbia moyo wa nyama na uliotengeneza na Neno la MUNGU pamoja na maongozi ya ROHO MTAKATIFU.

3. Mruhusu ROHO MTAKATIFU akuongoze na kukufundisha.

Ezekieli 36:27 '' Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.''
 Ni maamuzi yako tu ndugu kwamba unahitaji MUNGU akuwekee Roho yake ndani yako.
Roho ya MUNGU ndani yetu wateule ni ROHO MTAKATIFU.
Bila ROHO MTAKATIFU huwezi kumpendeza MUNGU.
Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

 Wana wa MUNGU au kwa jina lingine watoto wa MUNGU ni wale waliozaliwa mara ya pili na MUNGU(Yohana 1:12-13)
Ahadi ya MUNGU kwa watii ni MUNGU kuwapa ROHO wake MTAKATIFU ili ROHO atuongoze na kutuendesha katika sheria ya MUNGU.
Sheria ya MUNGU inaitwa Biblia takatifu.
Sheria ya MUNGU inaitwa Neno la KRISTO.
Neno la KRISTO  ni injili iokoayo.
Usipomruhusu ROHO MTAKATIFU akutengeneze hakika huwezi kumpendeza MUNGU.
ROHO MTAKATIFU ukimruhusu akusaidie  na akutumie hakika utakuwa mshindi daima.
Ndugu yangu, yasafishe maisha yako kwa kumtii ROHO MATAKATIFU.
Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''


4. Kaa katika Kanisa la MUNGU na katika fundisho la KRISTO YESU.

Ezekieli 36:28 ''Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa MUNGU wenu.''
Kuokoka ni kunamfanya mtu aingie taifa lingine ambalo ni taifa la ufalme wa MUNGU.
Unapompokea YESU unaingizwa katika taifa la watu wa MUNGU yaani jumuia yote ya waaminio.
1 Petro 2:9-10 ''Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.''


Waliookolewa na Bwana YESU wote sasa ni taifa moja tena taifa takatifu.
MUNGU ametuweka katika nyumba yake ambayo ni Kanisa kwa fundisho la KRISTO.

2 Yohana 1:9 ''Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba(MUNGU) na Mwana(YESU) pia.''

Ndugu jitahidi sana kudumu katika fundisho la KRISTO.
Fanyia kazi Neno la MUNGU.
 ''Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa MUNGU wenu-Ezekieli 36:28 ''
Kumbuka fundisho la KRISTO linakutaka ufanye mambo yafuatayo;
1. Umwabudu MUNGU katika kweli yake.
2. Ujue mpango wa MUNGU juu ya maisha yako.
3.Utubu na kufunguliwa.


Wakolosai 1:23 ''mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake.''

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka yako ya hiari katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments