NJIA SABA(7) ZA KUPIGANA VITA YA KIROHO KWA MAOMBI YA VITA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kabla hatujaangalia Njia 7 za kupigana vita ya kiroho nataka kwanza uyajue yafuatayo.
Katika maombi ni muhimu sana kujua mambo yafuatayo.

1. Kuomba kwa imani na utakatifu

Waebrania 11:6 '' Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.''
Hautakiwi kuomba kwa imani tu bali omba kwa imani ukiwa msafi kwa MUNGU.
 Mathayo 5:8 '' Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU. ''
Wenye moyo safi ni watakatifu waliosafishwa kwa damu ya YESU KRISTO, hao ndio wakiomba kwa imani wanaweza kumwona MUNGU vyema katika maisha yao.
 Waebrania 12:14 '' ....... na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; ''
Yaani pasipo imani huwezi kumwona MUNGU akikutendea muujiza.Yaani pasipo imani huwezi kupokea muujiza wako kutoka kwa MUNGU.
Jambo la pili hapo hapo ni kwamba pasipo utakatifu huwezi kumwona MUNGU maana yake huwezi kuingia uzima wa milele na maana ya pili pasipo utakatifu huwezi kumwona MUNGU  akikutendea muujiza. 
Hivyo wewe Muombaji shika kanuni hiyo ya kiroho kwamba ''Pasipo imani siwezi kumpendeza MUNGU na pasipo utakatifu siwezi kumwona MUNGU''
Kumbuka Biblia inasema katika Yohana 1:18 '' Hakuna mtu aliyemwona MUNGU wakati wo wote; MUNGU Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba(MUNGU), huyu ndiye aliyemfunua.'' 
Kumbe Hakuna mwanadamu awezaye kumwona MUNGU kwa sura lakini Mathayo 5:8 inasema wenye moyo safi yaani watakatifu watamuona MUNGU, Yaani watakatifu wataingia uzima wa milele na kumwona MUNGU lakini pia watakatifu watasikiwa na MUNGU na kutendewa muujiza.
 Ndio maana leo unaweza ukasikia mtu nasema kwamba ''Hakika nimemuona MUNGU'' Je amemuonaje?
Jibu ni kwamba ametendewa muujiza na MUNGU yaani amemuona MUNGU kupitia alichokifanya MUNGU kwenye maisha yake.

2. Kuomba katika jina la YESU KRISTO.

Kuomba katika jina la YESU KRISTO inajumuisha mambo mawili.
A. Kuomba ukilitaja na kulitegemea jina la YESU ili ushinde.
Yohana 14:13 ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu(YESU KRISTO), hilo nitalifanya, ili Baba(MUNGU) atukuzwe ndani ya Mwana. '' 

B. Kumtii YESU KRISTO na Neno lake.
Kumtii YESU KRISTO ni kibali cha kupokea hitaji lako.
Yohana 15:16 ''Si ninyi mlionichagua mimi(YESU), bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba(MUNGU)kwa jina langu awapeni. '
Ndio maana Biblia inasema kila alitajaye jina la YESU KRISTO na auache uovu.
2 Timotheo 2:19 ''Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana(YESU) na auache uovu.''

3. Kuomba katika ROHO MTAKATIFU.

Kuomba katika ROHO MTAKATIFU inajumuisha mambo mawili.
A. Kunena kwa lugha katika ROHO MTAKATIFU.
 Marko 16:16-17 "Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; WATASEMA KWA LUGHA MPYA;"

2. Kuomba kwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU au kujulishwa na ROHO MTAKATIFU.
 Yuda 1:20 "Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU,"

Mfano ROHO wa MUNGU anakujulisha ili umuombee mfu fulani, ukitii kwa kumuombea mtu huyo huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU hakika majibu yake ni makubwa na hapo utakuwa umeomba katika ROHO MTAKATIFU.
Ngoja nikupe ushuhuda kidogo.
Mwaka 2012 Mwishoni nilikuwa katika mazingira magumu sana kutokana na jaribu baya sana maishani mwangu. Nilikaa siku 5 Bila kula huku nikishindwa hata kuomba zaidi ya kutaja maneno mawili tu kwamba ''MUNGU wangu nisaidie'' na ''MUNGU wangu nisamehe''
Nikiwa katika hali ile niliona roho ya mauti lakini maombi yangu niliomba ni heri MUNGU anichukue mbinguni yaani nifariki.
Sikuiogopa roho ya mauti niliyokuwa naiona maana nilitamani MUNGU anichukue kwenda paradiso.
Sikupanga kujiua mwenyewe kwa sababu nilikuwa najua kabisa kwamba hakuna mtu anayejiua hata mmoja anayeenda mbinguni, maana Biblia inasema '' Usiue-Kutoka 20:13''  Hivyo inapokataza kuua basi hata wewe ukijiua hakika umeua hivyo hata kama ulikuwa mtakatifu kiasi gani huwezi kwenda uzima wa milele maana uliua. Nilijua kabisa japokuwa nilitamani MUNGU BABA anichukue lakini sio mimi kujiua maana sikutaka kupishana na uzima wa milele. 
Nilimkumbuka Nabii Eliya pale ambapo alifikia hatua ya kuomba afe.
1 Wafalme 19:2-8 '' Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.  Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.  Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule.  Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena.  Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.  Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa MUNGU.'' 

Kwa upande wangu Nilijitenga na watu muda huo na sikutaka mtu ajue yaliyonisibu roho yangu kwa sababu ya kuvunjika uchumba katika hali ya fedheha kubwa sana sana sana. Lakini ajabu ni kwamba ni kipindi hicho ndipo MUNGU aninifunulia kuhusu huduma yangu na ni kipindi hicho MUNGU kwa njia ya ndoto alinifundisha kutengeneza Blog yangu ya maisha ya ushindi kwa ajili ya kupanua wigo wa injili ili iwafikie watu wengi zaidi. Nilikuwa katika maumivu makubwa sana.
Lakini wakati nikiwa katika mazingira hayo Mchungaji wangu wa Zanzibar alinipigia simu akiniambia kwamba kuna kitu kwangu sio kizuri na ameniombea lakini bado anaona tatizo kubwa sana. Kwa sababu kipindi hicho hicho ndio nilikuwa nimehamia Dar es salaam kutokea Zanzibar na Kanisani ambako MUNGU alinielekeza kuabudu nilikuwa nimeenda mara chache tu huku hata watu hawanijui vizuri. Lakini Dada mmoja alifunuliwa jambo baya liko mbele yangu na ROHO wa MUNGU akamwambia afunge siku 5 kuniombea mimi. Yule dada aliomba ili MUNGU aniepushe na mabaya na roho yake yule dada iliugua sana na akaanza kufanya juhudi za kunitafuta kwa simu lakini ilimsumbua sana. Baadae akaipata kwa Mchungaji na kunipigia simu akiniuliza kama mimi ni mzima. Nilipomwambia kwamba mimi ni mzima akamshukuru MUNGU maana alijua kabisa niko kwenye hatari na wakati mwingine alijua mimi sipo. Baada ya pale ilinisumbua kupona majeraha ya moyo lakini neema ya MUNGU ilinigusa baadae nikapona kutoka kwenye dhambi ya kutokusamehe.
Kwanini nimekuambia haya?
Ni katika kipengele cha kuomba katika ROHO MTAKATIFU.
Mchungaji wa Zanzibar alijulisha na ROHO wa MUNGU akaomba kwa kufuata alichoagizwa na ROHO wa MUNGU, Hayo ni maombi katika ROHO MTAKATIFU.
Dada wa kanisani alibebeshwa mzigo mzito kuniombea na akatii na kuomba huku akiongozwa na ROHO MTAKATIFU ili kunifungua, hayo ni maombi katika ROHO MTAKATIFU.
Kwa hiyo kunene kwa lugha ni kuomba katika ROHO MTAKATIFU lakini pia kufuata maelekezo ya ROHO MTAKATIFU katika maombi hayo ni maombi katika ROHO MTAKATIFU.

Hayo Mambo matatu niliyokufundisha hufanya kazi pamoja na ni kitu kimoja cha kuleta majibu sahihi ya maombi ya Mtu.
Mimi Binafsi kwa kupitia kuomba mara kwa mara na kumsikiliza ROHO MTAKATIFU nimegundua mifumo kadhaa ya maombi ambayo mteule wa KRISTO  anaweza akaomba kutokana na ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Mifumo miwili katika mingi ni hii;

 1. Kuhusika na  MUNGU tu.

Hapa unaomba kwa MUNGU bila kukemea wala kuamuru mamlaka za giza ziachane na wewe. Humtaji mtu wala humfukuzi adui wewe unamwita tu MUNGU ili aje akusaidie.
Kwa maombi hayo kama ni katika ROHO MTAKATIFU hakika MUNGU atawapiga maadui zako na kuwafukuza hata kama hujawataja.
Hapa MUNGU atakuletea msaada kwa sababu umemhitaji yeye.
Hapa MUNGU anaweza kutuma malaika au watu kukusaidia japokuwa hukuita watu wakusaidie ila umemwita MUNGU ili akusaidie.
2 Samweli 22:1-7 ''Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa adui zake zote, na mkononi mwa Sauli;  akasema, BWANA ndiye jabali langu, na ngome yangu, na mwokozi wangu, naam, wangu;  MUNGU wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio yangu; Mwokozi wangu, waniokoa na jeuri.  Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu.  Maana mawimbi ya mauti yalinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka; Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita BWANA, Naam, nikamlalamikia MUNGU wangu; ''

2.Kutumia mamlaka ya KRISTO YESU iliyoko ndani yako.

Maombi haya ni maombi ya vita.
Wafilipi 2:13 ''Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.''
Ni maombi ya kumwamuru shetani akuachie hata kama hataki.
Kwa maombi haya MUNGU atatuma Malaika au  Neno  na maadui zako watakimbia.
Tofauti ya maombi haya ya maombi ya kuhusika na MUNGU tu ni kwamba hapa unawataja wabaya wako na kuwaelekeza wafanyeje, kama wakimbie hakika watakimbia na kama kazi zao zife hakika hizo kazi zao cha kichawi zitakufa.
Yeremia 1:10 ''angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. ''
Yaani maombi ya kwanza ni maombi ya kumsihi MUNGU na maombi ya pili ni maombi ya wewe kutumia mamlaka ya YESU KRISTO iliyoko ndani yako.
Katika maombi haya wewe ndio unaamuru iweje.
Katika maombi haya unaweza kulisemesha tatizo lako ili lisikie na kuondoka na hakika linaondoka.
Unaweza kuusemesha ugonjwa ili ukuachie na hakika ugonjwa huo ukakuachia.
Maombi haya mhusika ni wewe maana unatumia mamlaka ya MUNGU wako iliyo katika KRISTO YESU.
Waefeso 6:10-13 '' Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana(YESU) na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.''
 
Maombi haya hutuonyesha kwamba tuna mamlaka ndani yetu ambayo MUNGU wetu aliyetuokoa ametupa.

Baada ya hayo sasa naingia katika kiini cha ujumbe wangu wa leo.
Sasa ndio tunaingia sasa katika kanuni au njia za kupigana vita ya kiroho kwa maombi. 
Kuna njia kadhaa Biblia inazitaja  kama njia za kupigana vita ya kiroho kwa maombi. Husika nazo itakusaidia.

1. Kukanyaga.
Luka 10:19 '' Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.''

Mhusika hapa sio MUNGU kukanyaga nguvu za giza ili zisifanye kazi bali mhusika ni wewe kwamba ukanyage hizo nguvu za giza.
Bwana YESU amekupa mamlaka ya kukanyaga hivyo itumie mamlaka yako hiyo kukanyaga nguvu za giza.
Maana yake ni kwamba usiwaruhusu mawakala wa shetani kukushambulia, hivyo kabla hawajainua silaha zao wewe muombaji unayejitambua unakuwa umeziharibu silaha zao na hata wao wenyewe.
Kwenye ndoto au maono  wakati mwingine huwa unajulishwa mipango ya kipepo kukuhusu ili unyamazishe mipango hivyo ya shetani iliyokusudiwa juu yako. 
Mfano unaota nyoka anakufukuza. Tukio hilo linakuwa wakati mwingine halijatokea yaani linakuwa ndio liko katika kutekelezwa. MUNGU kwa upendo wake na neema yake amekufunulia ili umkanyage huyo nyoka na kunyamazisha kilichokusudiwa kibaya ili kikupate. Ziada kuhusu mfano huo ni kwamba Nyoka anaweza akawakilisha majini, uchawi, mizimu, shetani mwenyewe, uganga wa kienyeji, kutumia mapepo na nyoka ni roho ya uongo. Hivyo unaweza ukapambana na hayo niliyokutajia ambayo wewe kwenye ulimwengu wa roho umemuona nyoka.

 Ili ukanyage kazi za shetani timia katika haya itakusaidia.
A.  Kwanza unatakiwa uwe unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''

 B.  Unatakiwa kumwamini MUNGU kwamba katika yeye yote yanawezekana.
2 Nyakati 20:20 '' ...............  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. ''
 
 C, Uombe kwa imani katika jina la YESU KRISTO.
Yakobo 1:6-8 '' Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa BWANA.  Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote. '' 

Pia ujue kutumia mamlaka za kiroho za MUNGU za kukushindia.
Mamlaka hizo ni;

1. Jina la YESU KRISTO.
Yohana  14:14 ''Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.'' 

2. Damu ya YESU KRISTO.
 Ufunuo 12:11  '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ''

3. Neno la MUNGU
Zaburi 107:20  ''Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.''

4. Nguvu za ROHO MTAKATIFU.
1 Yohana 4:4 '' Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda(shetani), kwa sababu yeye aliye ndani yenu(ROHO MTAKATIFU) ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia(Shetani).  ''

 Somo hili litaendelea maana bado njia 6 za kupigana vita ya kiroho.
Uendelea kufuatilia na utakuwa muombaji mzuri sana.


MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments