USIKUBALI KUPOTEZA NAFASI YAKO KWA SABABU YA DHAMBI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna watu hupoteza nafasi zao kwa sababu tu ya mambo madogo madogo.
Mtu anaweza akasababisha jina lake lisiwemo katika kitabu cha uzima kwa sababu tu ya maovu anayoyaona kuwa ni mdaogo madogo.
Kwanini unapoteza nafasi yako kwa mambo madogo madogo?
Mwanzo 39:2-9 '' BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. NIFANYEJE UBAYA HUU MKUBWA NIMKOSE MUNGU? ''

Yusufu angekubali kutembea na mke wa bosi wake hakika angepoteza nafasi yake ya kuwa waziri mkuu katika taifa la ugenini Misri.
Inawezekana kabisa Yule mama ambaye ni mke wa Potifa baada ya kutembea na Yusufu angeweza kumjengea Nyumba Yusufu na kumpa mali nyingi, Lakini Yusufu hakutaka kuipoteza nafasi yake aliyopangiwa na MUNGU baadae.


Vitu vidogo vidogo vinawapotezea nafasi zao za baadae watu wengi sana.


Ndugu nakuomba usikubali kitu chochote kikuondolee nafasi yako uliyopangiwa na MUNGU kwako baadae.


Inawezekana hujanielewa vyema bado, Ni kwamba;

Mwanafunzi unaweza ukaiba sasa na kukamatwa na kufungwa, na ndoto yako ya kusoma ili uje uwe kiongozi inafia hapo hapo.

Binti unaweza kufanya dhambi ya uzinzi na kupewa mimba au magonjwa na hatima yako inakuwa imepinda kwa sababu ya mambo madogo madogo.

Mfanya kazi wa serikali unaweza ukala rushwa mara moja tu na kukamatwa na kazi unafukuzwa, na kwa njia hiyo unakuwa umepishana na nafasi yako ya baadae uliyopangiwa.


Unaweza ukaaminiwa na kukabidhiwa biashara nzuri lakini wizi kidogo unaweza ukakusababishia ukarudi kwenu kijijini ukilia na hujui pa kuanzia.


Unaweza ukawa na huduma kubwa na ukawa na watu wengi chini yako lakini dhambi kidogo inaweza ikakufanya ukapoteza nafasi yako.


Yusufu hakukubali kabisa nafasi yake ya kuwa mkubwa baadae iondolewe na uzinzi wa mwanamke kahaba.

Hata wewe unaweza kuyaepuka mambo madogo madogo na kwa njia hiyo unakuwa umeiponya nafsi yako.
Unaweza ukapoteza hata maisha kwa sababu ya mambo madogo madogo tu unayoyaendekeza.
Ndugu yangu, nakushauri fanya mema siku zote na sio dhambi.


Kwa Neno au kwa tendo fanya mambo yanayompendeza MUNGU.


Wakolosai 3:17 '' Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye. ''


Usikubali mambo madogo madogo yakakuondoa kwenye wokovu wa Bwana YESU.

Kuna mambo mengi yanaweza kumuondoa mtu katika kusudi la MUNGU, Mojawapo wa mambo hayo ni mazoelea katika mambo ya MUNGU.

Mazoelea katika kazi ya MUNGU ni mabaya sana.
Mazoelea yanaweza kukufanya uwe unachagua vitu vya kufanya katika Kanisa.


Mazoelea yanaweza kumfanya mtu hata katika mahubiri Kanisani  awe anachagua wa kumfundisha na awe anachagua masomo ya yeye kuhitaji kufundishwa.


Niliwahi kufundisha siku moja kwenye group juu ya maisha ya Wokovu na mtu mmoja akaniambia kwamba "Masomo kama haya ni ya kuwafundisha watu waliookoka Leo na sio watu kama sisi"

Baada ya siku kadhaa yule ndugu alikuwa zamu kufundisha somo na ajabu akahubiri somo lenye kichwa na maelezo kama somo langu alilolikataa. Wakati yeye hakujua wala kukumbuka yaliyotokea miezi michache kabla, japokuwa Mimi niliupenda Ujumbe wake maana Neno la MUNGU li hai siku zote na linaweza kumfaa mteule yeyote haijalishi ana miaka 40 kwenye Wokovu .

Neno la MUNGU lililo na nguvu za ROHO MTAKATIFU hata kama somo lile lile likifundishwa mwezi mzima bado litakuwa hai tu na lenye kumsaidia mhitaji. 


Ndugu, katika maisha yako yote usikubali kuwa na mazoelea ya Neno la MUNGU.

Mazoelea ya Neno la MUNGU wakati mwingine ni mpango kabisa ya kipepo ili kukufanya Usiisikie sauti ya MUNGU wala kuifanyia kazi.
Yeremia 9:4-5 '' Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huko na huko na kusingizia.  Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoeza ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu.''

Mambo madogo madogo kama ni uovu kwa MUNGU basi yanaweza sana kumkosesha mtu. 
Kama umempokea YESU KRISTO kuwa Mwokozi wako na unaishi maisha matakatifu hakika nafasi yako wewe ni uzima wa milele. Lakini wapo ambao huanza vyema na YESU lakini baadae kwa sababu ya mambo madogo madogo huacha ibada na kuanza kutenda dhambi.
Kwao hakuna umuhimu tena wa ibada wala kujifunza Neno la MUNGU. 
Ndugu naomba kukujulisha kwamba ukianza kuichoka ibada katika KRISTO hakika unaanza kuichoka pia mbingu. Inakupasa sana kuzingatia ibada na ishi maisha matakatifu.

Kwanini tunaenda Kanisani?

1. Tunaenda Kanisani ili kumwabudu MUNGU.

2. Tunaenda Kanisani ili kukutana na MUNGU muumba wetu.

3. Tunaenda Kanisani ili MUNGU aseme nasi.

MUNGU akubariki wewe ambaye huwa unahudhuria ibada Kanisani na unamwabudu MUNGU katika Roho na kweli huku ukiishi maisha halisi yaliyo matakatifu tu.
Yohana 4:24 '' MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. ''

Usikubali  mambo madogo madogo yaliyo maovu yakakukosesha.

Usikubali kunywa pombe kidogo  kwa siri huku ukiona kuwa ni jambo dogo.

Usikubali kufanya uzinzi na uasherati kwa siri huku ukiona kuwa ni sawa tu, ndugu unaweza ukapishana kabisa na uzima wa milele kwa sababu tu ya  dhambi hiyo unayoiona wewe  ni ndogo.

Rushwa mara moja tu inaweza ikakupotezea nafasi yako.

Wizi kidogo tu au kuhonga ili usaidie kunaweza kabisa kukupotezea nafasi yako kwa MUNGU.

Inakupasa sana kuwa makini. Hakikisha unakuwa na sifa halisi za mteule wa KRISTO aliyeokolewa kwa neema.

Ishi na alama za mteule wa kweli wa MUNGU.
Alama za mteule wa kweli wa MUNGU ni hizi hapa;

1. Ameokoka.
Waefeso 2:8 ''Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;'' 

2. Anaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
 
3. Anatumia kwa haki Neno la MUNGU.
2 Timotheo 2:15 '' Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. ''
 
4. Anaenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''

5. Anamtumikia Bwana YESU.
1 Kor 5:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.''

6. Ni mtu wa maombi siku zote.
 Waebrania 4:16 ''Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.''

7. Anachukia dhambi na amejitenga mbali na anasa za kidunia zilizo machukizo kwa MUNGU.
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
 
Ndugu hakikisha una alama za mteule wa kweli wa MUNGU.
Ndugu usikubali kuuza uzima wako wa milele kwa pesa.
Usiuze uzima wako wa milele kwa tamaa ya kuolewa au kuoa.

Kwa walio kwenye ndoa Kuacha mke wako au mume wako ili umpate mwingine kwa tamaa zako ni kinyume na Neno la MUNGU.

Usiuze uzima wako wa milele kwa kujiunga na makundi maovu.

Usiuze uzima wako wa milele kwa kuabudu sanamu.

Usiuze uzima wako wa milele kwa kuabudu shetani.

Usikubali kubadili dini kwa kumwacha YESU ili uolewe au uoe.
Kumbuka huyo anayekudanganya ili uache wokovu hatakuwa na wewe milele.

Ndugu usikubali katika hali yeyote ile kumwacha Bwana YESU.
Bwana YESU alisema '' Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za BABA yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za BABA yangu aliye mbinguni.-Mathayo 10:32-33 ''

Ndugu usikubali mambo madogo madogo yakakuondolea nafasi yako ya uzima wa milele.

Moja ya mambo madogo madogo ambayo yanawapotezea watu nafasi zao kwa MUNGU ni KUTOKUSAMEHE.
 Neno la MUNGU liko wazi kwamba Amchukiaye ndugu yake ni muuaji.
Muuaji wa kwanza alikuwa Kaini na alilaaniwa kwa sababu ya uuaji wake(Mwanzo 4:8-11)
Watu wengi Leo ni wauaji kwa maana wanawachukia ndugu zao.

1 Yohana 3:15-Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake."

Je unamchukia ndugu yako? 
Unaweza ukaliona hilo kuwa jambo dogo sana lakini kiroho ni jambo hatari sana maana linaweza kukupotezea nafasi yako kwa MUNGU.

Je unamchukia jirani yako?
Unaweza ukaliona hilo kuwa jambo dogo sana lakini kiroho ni jambo hatari sana maana linaweza kukupotezea nafasi yako kwa MUNGU.

Je unamchukia mfanyakazi wako au mfanyakazi mwenzako?
Biblia inasema amchukiaye ndugu yake ni muuaji.
Unaweza ukawa muuaji kwa sababu tu ya chuki zako kwa watu wa MUNGU.

Ndugu usimchukie ndugu yako Bali msaidie kiroho na muombee.
Ukimchukia ndugu yako wewe ni muuaji na wauaji majina yao hayamo katika kitabu cha uzima.

Kama unaonyesha furaha kwa ndugu yako au rafiki yako na kumbe moyoni unamchukia basi wewe ni muuaji, tubu na acha chuki.

Kama unajifanya una furahi na wafanyakazi wenzako na kumbe rohoni unawachukia hakika wewe ni muuaji, tubu na geuka kutoka katika uovu huo.
Kama unajifanya una hasira sana tambua na hii ya kwamba "Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.-Mhubiri 7:6"


 MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana  YESU.
+255714252292.

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu kama ulivyo bila kubadili chochote.

Comments