MAKUNDI SABA(7) YA WATOAJI ZAKA NA SADAKA KANISANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe dugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe huu ni muhimu sana na maombi yako ufunguliwe katika hili na uanze kuona baraka za MUNGU kupitia matoleo yako.
Zaka ni nini?
Zaka ni moja katika kumi ya kipato cha mtu ambacho mtu huyo humtolea MUNGU kwa hiari na upendo Kanisani.
Neno katika kutoa zaka ni upendo kwa MUNGU.




Sadaka ni nini?
Sadaka ni kitu au fedha ambazo hutolewa na mtu kwa kuwapa wanaostahili kwa ajili ya kujipatia thawabu kwa MUNGU.
Katika Kanisa la MUNGU ni muhimu sana kutoenda mikono mitupu, Bali nenda na sadaka lakini ni muhimu kutoa kwa upendo na sio kulazimishwa au kujilazimisha ndipo utapata dhawabu kwa MUNGU.

Thawabu ni malipo mema anayoyapata mtu kutoka kwa MUNGU baada ya kutii Neno la MUNGU juu ya jambo husika.
Hagai 1:5-7 ''B
asi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.''

Ni siku moja jioni nikiwa nyumbani ndipo nilipopewa kiufunuo Ujumbe huo kuhusu zaka na sadaka, niliandika muda mwingi hadi familia Yangu wakaanza kunishangaa maana tulikuwa na safari lakini nikawaambia waniache hadi nimalize kuandika. Nilipomaliza kuandaa somo hili kwenye notebook Yangu ndipo tukaondoka kwenda hiyo safari na ajabu tuliwahi sana sana kabla ya chochote kuanza.


Makundi saba ya watoaji wa fungu la kumi na sadaka kanisani.

1. Wanaojaribu kumpa MUNGU rushwa.

1 Samweli 15:22 '' Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.''
 
Watu wa kundi hili huwa hawatoi matoleo vyema hadi pale watakapobanwa na matatizo makubwa. Mfano watakapoteseka na magonjwa, watakapofilisika, watakapokuwa na kesi mahakamani au watakapokuwa na migogoro mikubwa kwenye familia zao au ndoa zao ndipo wataanza kutoa zaka sahihi na sadaka nzuri ili MUNGU awatoe katika magumu yao.

MUNGU hawezi kukuponya kwa sababu ya matoleo. 
 Kwanini nimesema kwamba ni kama wanataka kumpa MUNGU rushwa kitu ambacho hakiwezekani?
Ni kwa sababu wakishatolewa kwenye matatizo hutawaona tena wakitoa vizuri hadi watakapobanwa tena.
Utoaji matoleo wa mtu wa aina hii hauwezi kumletea baraka stahiki za utoaji wake katika maisha yake.

MUNGU anapenda matoleo  yetu pamoja na kumtii na utoaji ni agizo lake hivyo ukiwa unatoa matoleo kipindi tu una tatizo wewe hakika humtii MUNGU.
Dawa ni kutubu na kuanza kutoa kama MUNGU atakavyo.
Mithali 15:8 ''
Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.''

2. Kundi la pili la watoaji wa sadaka na zaka ni wale wanaotoa kwa kufuata mkumbo tu.

Kutoka 25:1-3 '' BWANA akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba,''
 
Maandiko yanaonyesha kwamba mtoaji sahihi atoe kwa moyo wa upemdo na sio mkumbo.
Watu wa kundi hili hawatoi zaka sahihi au sadaka nzuri hadi watakapoona wengine wanatoa vizuri.
Kwenye michango ya kuahidi mtu wa kundi hili hawezi kuahidi hadi atakapoona watu kadhaa wameahidi ndipo na yeye ataahidi. Ahadi yake haitoki moyoni Bali ni kufuata mkumbo.
Mtu wa kundi hili wakati wa kutoa sadaka yeye hawezi kwenda kutoa hadi atakpoona wengine wameenda kutoa.
Wakati mwingine aliokaa nao karibu Ibadani Kama hawajapeleka sadaka na yeye huacha kupeleka hata kama anayo mfukoni sadaka hiyo.
Wao hawawezi kutoa hadi waone wengine wanatoa, hata kama ROHO MTAKATIFU atawasukuma kutoa wao hawatatoa.
Mtoaji wa namna hii hawezi kubarikiwa vizuri na MUNGU hadi atakapotibia jambo hilo ndio aache kutoka vile atakavyo MUNGU.



3. Kundi la kutoa kwa kulazimishwa.

Kumb 14:22 ''Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.''

Hawa hutoa tu kwa sababu ni sheria kutoa zaka kamili na sadaka.
Hawa hutoa kwa sababu tu wanakwepa kuabika mbele za watu kwamba hawatoi zaka kamili na sadaka.
Hawa hulazimika kutoa kwa sababu kuna watu wanaowaheshimu sana hivyo kwa kulinda heshima kwa watu hao hutoa zaka na sadaka.
Watu hawa kutoa zaka kamili na sadaka nzuri ni hadi mchungaji au kiongozi wa Kanisa afundishe kuhusu utoaji ndipo watatoa.
Hawa jina lingine tunaweza kuwaita ni wanafiki katika utoaji.
Mathayo 23:28 ''
Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi. ''
 
Hawa hutoa zaka kamili na sadaka nzuri hadi mchungaji atakapowasomea maandiko mengi sana ya kuwaonya kuhusu kutokutoa kwao, ndipo wataanza kutoa ila kwa kujilazimisha tu au kwa sheria walioisikia.
Mtu wa aina hiyo hawezi kupokea baraka sahihi kutoka kwa MUNGU kutokana na utoaji wake hadi atakapotubia uovu huo na kuanza kutoa zaka kamili na sadaka nzuri kana atakavyo MUNGU wa mbinguni.

4. Kundi la kutoa ili kupata thawabu za wanadamu.

Mathayo 6: 1-4 ''
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa BABA yenu aliye mbinguni.  Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu.  Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume;  sadaka yako iwe kwa siri; na BABA yako aonaye sirini atakujazi. ''
 
Hawa hupenda kutoa tu mbele za watu wengi kwa lengo la kupata heshima kwamba wametoa.
Mtu wa aina hiyo anaweza akaalika hata marafiki au kama ana uwezo anaweza akaalika hata waandishi wa habari ili wakaone jinsi anavyotoa sadaka yake kubwa kwa ajili ya kazi ya MUNGU.
Kutoa mbele za watu wala sio dhambi lakini kama mhusika ana lengo la kujionyesha kwa watu hakika hayo ni makosa makubwa.
-Watu wa kundi hili hutoa zaka kamili na sadaka nzuri ili waheshimiwe na watu.
-Hutoa ili wapendwe na watu.
-Hutoa ili wapendelewe na watu.
-Hutoa ili wapigiwe makofi na kushangiliwa kwamba wanatoa zaka kamili na sadaka nzuri.
Hawa hutoa wakiwa hawana moyo wa toba au wa unyenyekevu kwa MUNGU.
Baadhi yao hutoa ili kuficha uovu wao ili watu waanze kuwahesabu kwamba wao ni watu wema kumbe wala sio wema.
Kumbuka MUNGU anachunguza kila moyo hivyo moyo kama hila wakati wa utoaji MUNGU anajua.
Yeremia 17:10 ''
Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.''
MUNGU wa aina hii anatakiwa atubu na kuacha Tabia hiyo na aanze sasa kumtolea MUNGU zaka kamili na sadaka nzuri katika kusudi la MUNGU.


5. Kundi la wanaotoa kwa bajeti.

Jambo la kwanza kujua ni kwamba vitu vyote ni Mali ya MUNGU hivyo hatuna jinsi yeyote ya kumzuilia akivitaka.
Zaburi 24:1 ''
Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.''
 
Watu wa kundi hili sadaka zao huwa ni zilezile siku zote.
Kama kila jumapili hutoa Tsh 1000 basi ni hiyo hiyo siku zote maana amejiwekea bajeti ya kutoa hiyo kila ibada.
Hata ikitokea anasikia msukumo rohoni wa kutoa zaidi, hawezi kutoa kwa sababu ameshajiwekea bajeti.
Watu hawa anaweza akaugawa mshahara wake.
Mfano kama anapokea laki 8 kwa mwezi anaweza akatenga Elfu 50 ya sadaka kwa mwezi.
Hivyo kama ana mke na watoto basi kila mhusika wa familia hiyo atakuwa na kiwango chake cha kutoa sadaka kila wiki, kama ni 200 basi itakuwa hivyo na ya kudumu.
Kuhusu zaka ni muhimu kujua kwamba ni asilimia kumi ya kipato hivyo huwezi kuweka bajeti ya zaka kwa kupunguza kiwango halisi cha zaka. Yaani haitakiwa uwe unapokea milioni moja kisha uweke bajeti ya zaka kuwa elfu 50.
Mtu wa kundi hili hawezi kubarikiwa na MUNGU baraka stahiki hadi atakapotubia uovu huo na kuanza kutoa vile atakavyo MUNGU.


6. Kundi la kutoa kwa kujihurumia kwa sababu ya umasikini.

Luka 21:1-4 '' Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina. Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili.  Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo. ''
Mama anayezungumzwa katika maandiko haya alikuwa masikini lakini hakutaka kutokumtolea MUNGU hata kama alikuwa masikini.
Lakini leo wako watoaji ambao huacha kutoa kwa sababu tu ya kujiona ni kundi wasiotakiwa kutoa.
Watu wa kundi hili hutaka kanisa zima lijue kwamba wana matatizo mengi sana hivyo hutaka huruma za viongozi wa Kanisa ili wasitoe zaka na sadaka. Katika mazingira hayo ndiko kunafungwa Kabisa milango ya baraka zao, lakini wao hawafahamu hilo kwa muda mrefu sana.
Katika maandiko hayo juu yanamuonyesha mwanamke aliyekuwa masikini sana na alitoa matoleo yake kidogo sana lakini kwa kipimo cha mbinguni alionekana ametoa sahihi kuliko matajiri waliotoa sadaka za thamani lakini wako katika makundi mengine haya niliyokutajia kwenye somo hili.
Watu wa kundi hili hutaka watu wawahurumie.
Akili zao zimejengwa juu ya kupokea tu misaada na sio wao kutoa zaka na sadaka.
Watu wakitoa michango Kanisani au kwenye kikundi kanisani, wao hujitenga wakidhani michango hiyo haiwahusu maana hata Kanisa linajua hawana uwezo.
Hata wakisikia msukumo rohoni wa kutoa hata kidogo walichonacho wao hwatatoa maana fahamu zao zimekubali kwamba watoaji ni watu wengine na sio wao.
Kila mtu anayetaka kubarikiwa na MUNGU ni lazima awe mtoaji, haijalishi mtu huyo ni tajiri au maskini.
Kanuni ya kibiblia ni heri kutoa kuliko kupokea tu.
Matendo 20:35-36 ''Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana YESU, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote.''
 
Mama wa sarepta alikuwa masikini aliyebakiza chakula cha mlo mmoja tu ili ale yeye na mtoto wake kisha wajiandae kufa maana hawakuwa na chakuka kingine chochote, lakini utoaji wake katika mazingira ya umasikini huo huo alibarikiwa na MUNGU.
1 Wafalme 17:7-16 '' Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.  Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya. ''
Hata Leo masikini anaweza sana akabarikiwa sana kwa utoaji wake.
Kumbuka utoaji wa Ki MUNGU haupimwi kibinadamu ndio maana Bwana YESU alijulisha kwamba mama mmoja aliyetoa akiba yake ndogo alionekana ametoa zaidi kuliko wote ibadani.
Pesa ya kiwango chochote ukitoa kwa kujihurumia huwezi kubarikiwa.
Hakikisha unatoa vile atakavyo MUNGU.

7. Wanaotoa atakavyo MUNGU.

Mwanzo 22:15-18 ''Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni  akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.''
 
Hili ndilo kundi pekee ambalo mtoaji anayetaka kumtolea MUNGU zaka na sadaka anatakiwa awe.
Kumbuka kutoa zaka ni jambo la kudumu kwa mteule wa KRISTO, wala sio jambo la muda tu.
Kutoa sadaka ni jambo la kudumu katika maisha ya mteule wa MUNGU.
Na kumtolea MUNGU sio hadi pesa tu Bali hata vitu Unaweza kumtolea MUNGU na ukabarikiwa, hata mazao pia unaweza ukamtolea MUNGU, hata mifuko n.k
Jiepushe sana na makundi 6 ya kwanza ambayo nimekujulisha.
Watu wa kundi hili hutoa kwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU, hawana sheria ndani yao wala hawana kiwango maalumu siku zote.
Hutoa kwa kulitii Neno la MUNGU na kwa upendo sahihi usio na unafiki ndani yake.
Hutoa kwa sababu wanampenda MUNGU.
Hutoa kwa sababu wanataka kujiunganisha na madhabahu ya MUNGU aliye hai.
Wanatoa kwa upendo wakionyesha shukrani za dhati kwa MUNGU mwenye vyote.
Wanatoa kwa moyo mweupe.
Wanatoa kwa upendo wa Ki MUNGU ili kuweka hazina zao mbinguni, maana hazina zao zitakapokuwa ndipo na roho zao zitakuwa, wanalijua hilo na wanatoa kwa moyo wa upendo siku zote
Sio mpaka wafundishwe somo la utoaji ndipo watoe vizuri.
1 Nyakati 29:9 ''Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu.''
 
Wanajua ni wajibu wao kwa MUNGU kumtolea Zaka na sadaka.
Hawatoi kama watoa msaada.
Hawatoi kama watoa zawadi kwa MUNGU.

 Hawa wana sifa nyingi na katika ya sifa hizo ni hizi;
a. Wao wanajua wajibu wao kwa MUNGU ndio maana wanamtolea kwa moyo wa upendo huku wakitambua kwamba vyote walivyonavyo ni Mali ya BWANA.

b. Wanatoa kwa furaha na moyo wa kuchangamka
2 Kor 9:7 '' Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.''
 
c. Wanatoa kilicho bora
 Mwanzo 4:4 '' Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;''
 
d. Wanatoa zaka kamili na sio nusu.
Malaki 3:10 '' Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.''
 
e. Wanatoa kilicho safi na sio kile ambacho hata wao wakipewa hawapokei.
Hawatoe matoleo ya dhambi, wizi au rushwa Bali wanatoa kilicho safi.
Mwanzo 8:20 '' Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.''
 
Wanatoa bila manung'uniko wala hila ndani yao.
Ni wakamilifu na hata matoleo yao ni makamilifu.
Hawatoi sadaka kilema na wala hawatoi ziada zao.
Wanaishi maisha matakatifu na hata utoaji wao uko sawa kwa MUNGU.
1 Petro  1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; '' 
Mwenendo ni pamoja na  katika utoaji.
Wanatoa zaka kamili na sadaka safi.
Jambo la mwisho nataka kusema ni hili.
MUNGU huwa hahitaji pesa zetu au mali zetu lakini utoaji wetu ni kipimo kwetu kimojawapo kama tunamcha MUNGU.
MUNGU kupitia utoaji wako anaangalia unyenyekevu wako kwake , upendo wako kwake, imani yako na kujali kwako kazi yake.
Kwa njia hiyo atakubariki na sadaka yako itakuwa ukumbusho mbele zake.
Ukiwa unatoa zingatia haya.
1. Usitoa kama unatoa zawadi, MUNGU haihitaji zawadi yeyote ya mwanadamu yeyote.
2. Usitoe kama unatoa msaada kwa watumishi wa MUNGU au Kanisa, MUNGU hakuna andiko hata moja anahitaji msaada wowote wa mwanadamu yeyote.
Hakikisha pesa yako inakuwa sadaka na sio zawadi au msaada.
 MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments