MSHIKE YESU NA SIO KUSHIKA SABATO YA SIKU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Ngoja nimalizie hoja yangu kuhusu sabato maana baadhi ya ndugu hudhani kwamba uzima wa milele umekaa katika siku iitwayo jumamosi, siku zingine wanaita za shetani lakini jumamosi ya MUNGU.

Kwanza ni muhimu kuyajua haya.

1. Ukiisoma Biblia kidini ujue ROHO MTAKATIFU hatakusaidia kujua maana unao msimamo wako tayari ambao hakuna awezaye kuubadili.

2. Katika Agano la kale lote hakuna Neno Sinagogi Bali kuna Hekalu tu tena moja katika nchi nzima, Anza Kule kwa kuhani Elly, kisha Samweli na kisha Hekalu la Solomon. Akina Hana walikuwa wanaenda mwaka baada ya mwaka kuabudu.

1 Samweli 1:1-3 " Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili KUABUDU, na kumtolea BWANA wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa BWANA, walikuwako huko."
 
Yaani mwaka hadi mwaka ndipo Elkana na familia walienda hekaluni. Hakukuwa na sinagogi. Je kila jumamosi waliabudu wapi?
Mfano hapo kwenye maandiko tunaona Elkana alikuwa na wake wawili. Kila mtu anajua kwamba kuoa wake wawili ni dhambi lakini kwa nini hoja iwe jumamosi tu?


3. Katika agano jipya hakuna andiko ambalo linatuagiza Kanisa la MUNGU kuishika sabato ya siku ya jumamosi.
 
Wapo walioshika sabato kabla ya Yohana mbatizaji lakini hilo sio agizo kwetu. Sio kwamba kila waliofanya watakatifu wa zamani ni lazima tuyafanye. Daudi alioa wake wengi, je tumuige na tufuate matendo yake?
Kwanini nimesema habari za Yohana mbatizaji?
Ni kwa sababu kuna vitu vilitakiwa kukoma tangu wakati wa Yohana kuja sasa. Kwa sasa Ufalme wa MUNGU wanaupata wenye nguvu, Ni pia ni muhimu kujua kwamba nguvu hizo sio za mwili.
Mathayo 11:12-13 " Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana."


4. MUNGU aliitakasa siku ya saba kindi cha Adamu, ikapitia miaka maelfu hadi torati ya Musa ilipokuja na agizo la kuitunza sabato, na tena sio sabato moja bali sabato nyingi. 
Leo kuna watu wamebakiza kushika sabato ya jumamosi huku wakijifariji kwamba sabato zingine zilifutwa huku hawana ushahidi hata wa andiko moja.
Wengine hulisingia andiko hili la Hosea 2:11 kwamba ni kweli sabato zote zilifutwa isipokuwa sabato ya jumamosi, sasa hilo andiko linalosema kwamba zilifutwa sabato zote ila sio sababto ya jumamosi wanalipata wapi? Ukweli hakuna andiko linalosema hivyo.
Hebu ngoja tulipitia andiko hilo linalojulisha kwamba MUNGU alizifuta sabato zote wanazozishika watu huku hawataki kuokolewa kwa Neema ya KRISTO.
Hosea 2:11 "Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa."


Biblia ya kiingeleza inaonyesha kwamba ni sabato zote zitakomeshwa na MUNGU.
Biblia inasema hivi,

"I will also cause all her mirth to cease, her feast days, her new moons, and her sabbaths, and all her solemn feasts."

Baada ya hayo nataka niseme kiini cha ujumbe wangu wa kuwasaidia washika siku Wokovu hawautaki.
Wagalatia 2:14 "Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?"


Hapa tunaona makundi mawili.
Desturi za wayahudi na desturi za wasio wayahudi.
Sisi wala sio wahahudi hivyo hatuwezi kuhukumiwa kwa desturi za wayahudi.

Tumeokolewa na KRISTO kwa imani na sio kwa sababu ya matendo ya sheria za musa mfano kushika Sabato.
Ndugu hutaenda mbinguni kwa sababu unaiheshimu jumamosi.
Kumbuka kuna walioiheshimu sabato kuliko wewe lakini kwa kukataa kuwekwa huru na YESU walichukua sifa ya kuwa watoto wa Ibilisi, japo walishika sabato.


Yohana 8:43-44 " Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo."


Ndugu tunaokolewa kwa Neema kwa njia ya kumwamini YESU kama Mwokozi.
Wala usije ukajiita mtakatifu kwa sababu ya kushika matendo ya sheria ikiwemo sabato.
Biblia inakukataza 


Waefeso 2:8-9 " Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; WALA SI KWA MATENDO, mtu awaye yote asije akajisifu."


Unajua maana ya "WALA SI KWA MATENDO?"
Point kuu ya ujumbe wangu ni hii.
Wagalatia 2:15-16 "Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wakosaji wa Mataifa, hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya KRISTO YESU; sisi tulimwamini KRISTO YESU ili tuhesabiwe haki kwa imani ya KRISTO, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki."

Unajua maana ya maandiko haya?
Maana yake hakuna mtu hata mmoja ataingia uzima wa milele kwa sababu alikuwa anashika Sheria(Torati)
Hatuupokei uzima wa milele kwa sababu sisi tumeshika Sheria za Musa.

Torati(Sheria za Musa) zilikuwa ni kivuli tu cha Kitu halisi.
Waebrania 10:1 "Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao."


Sasa kitu halisi kimekuja, je uendelee kushikilia kivuli cha kitu halisi wakati hicho kitu halisi kipo tayari?
Sheria za Musa(Torati) zilikuwa kiongozi wa kutupeleka kwa YESU.
Tumeshafika sasa kwa YESU hivyo hatuwezi kuwa chini ya kiongozi ambaye kazi yake ilikuwa tu kutuleta kwa YESU.
Torati ilikuja na mwisho wake ni kuja kwa KRISTO.
Baada ya hapo Torati haifanyi kazi tena Bali imani katika KRISTO ndio inafanya kazi.
Torati ni kiongozi aliyetuleta kwa YESU kisha sisi tukabaki na YESU Mwokozi wetu.
Wagalatia 3:23-27 " Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa KRISTO, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa MUNGU kwa njia ya imani katika KRISTO YESU. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika KRISTO mmemvaa KRISTO."


Kuja kwa YESU ndio mwisho wa sheria za Musa.
Warumi 10:3-5 "Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya MUNGU, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya MUNGU. Kwa maana KRISTO ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo."


Mimi nilikuwa mbishi sana nilipoanza kumjua MUNGU.
Nilitaka kushika sabato na kushika kila agizo la Torati lakini andiko hili lilinifanya niogope na kuhitaji tu msaada wa ROHO wa MUNGU.


Wagalatia 3:10 "Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye."

 
Niliogopa mno maana niligundua kwamba sikuweza kushika hata robo tu ya sheria za Musa.
Hata Leo hakuna Mwanadamu anayeweza Kuzishika sheria zote za Torati.
Wasabato wote hata nusu tu ya sheria hawazishiki.
Na ukipungukiwa hata moja tu uko chini ya laana.
Ni mambo magumu mno haya.

Ukweli ni kwamba Torati ni Kongwa ambalo liliwashinda Waisraeli na hata sasa limewashinda wote wanaojiweka chini ya torati.
Matendo 15:5-10 "Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo. Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza MUNGU alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini. Na MUNGU, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa ROHO MTAKATIFU vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu MUNGU na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua."


Ndugu usimjaribu MUNGU kama maandiko yanavyosema hapo juu.
Washika dini wengi Leo wamebaki watu wa kuhukumu tu watu ambao hawaishi jumamosi.

Mathayo 7:1-2 "Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa."


Labda ngoja niseme kitu hiki.
Ndugu mmoja aliniuliza swali.
Je unaabudu siku ya Sabato? nikamjibu ndio.
Sasa mbona wewe ni mlokole na sio msabato?
Nikamjibu kwamba kama suala ni kuabudu jumamosi hakuna Mkristo asiyeabudu maana kuabudu maana yake ni kumtolea MUNGU ibada.
Sasa maombi hata Kama ya dakika moja ni ibada, sadaka ni ibada, kijifunza Neno ni tendo la ibada hivyo sheria ya kuabudu jumamosi haiwezi kukuweka hatiani kwa sababu hata unapomuomba MUNGU asubuhi kabla ya kwenda kwenye kazi ni ibada hivyo sheria haikufungi.

Kibiblia kinaitwa hiki tulichopo ni kipindi cha Neema au kipindi cha Kanisa.
Kipindi hiki MUNGU anaabudiwa kila siku na sio siku moja kwa wiki.
Hakuna dhambi katika kuabudu siku yeyote ile ila makosa ni kama humwabudu JEHOVAH MUNGU muumbaji.
Hata wachawi wanaweza kumwabudu shetani jumamosi, je na wao tuwaone wako sahihi maana wameitunza siku hiyo kwa ajili ya mungu wao?
Ndugu zangu ni heri kujua kwamba MUNGU anaabudiwa katika Roho na kweli(Yohana 4:24) na sio tu katika baadhi ya siku.
Yohana 4:24 "MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli."


Ndugu mwingine akaniuliza.
Kama wewe ni uzao wa Ibrahimu mbona hushiki sabato?
Nikamwambia mbona na Ibrahimu hakushika sabato?
Ngoja nizungumze kidogo kuhusu hilo la sisi wateule wa KRISTO kama uzao wa Ibrahimu.
Wagalatia 3:13-18 "KRISTO alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika YESU KRISTO, tupate kupokea ahadi ya ROHO kwa njia ya imani.
Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno . Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, KRISTO. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na MUNGU, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini MUNGU alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi."


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
Ndugu mhubiri KRISTO YESU na sio vinginevyo.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments