MTUMISHI WA MUNGU UWE MAKINI SANA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia kwa sehemu watumishi na utumishi wao.
Tuko katika kipindi cha mambo mengi sana na hayo mengine hayampi MUNGU utukufu na mengine ni machukizo kabisa.
1 Kor 4:1-2 ''Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.'' 

Kwa sababu sisi tuliookoka na tunamtumikia MUNGU tu watumishi wa KRISTO  na mawakili wa siri za MUNGU basi ni muhimu sana tujue kwamba kazi yetu ni kumtumikia MUNGU na kufanya yanayompendeza MUNGU na sio vinginevyo.
Sio watumishi wote leo ni watumishi wa MUNGU.
Sio  watumishi wote leo wanalitimiza kusudi la MUNGU.
 Mfano unaitwa Mwimbaji wa nyimbo za injili au wewe mwenyewe unajiita mwimbaji wa nyimbo za injili lakini ajabu ni kwamba hujawahi kumtaja YESU au huwa humtaji YESU kwenye nyimbo zako. Je unajua kwamba Injili ni ya KRISTO?
Unapoitwa mwimbaji wa nyimbo za injili maana yake unamtambulisha KRISTO na matendo yake.
Sasa wewe humtaji YESU mwenye injili harafu unajiita mwimbaji wa nyimbo za injili.
Jichunguze ndugu maana watu watajiuliza wewe ni mwimbaji wa nyimbo za injili ipi?

 Nyimbo za injili ni mahubiri kwa njia ya uimbaji, lakini tatizo La Leo ni kwamba wanaohubiri kwa njia ya uimbaji ni wachache sana.
Ni heri waimbaji wakahubiri injili kwa njia ya uimbaji wao, hasa waimbaji binafsi maana kwaya nyingi wanajitahidi kuhubiri kwa njia ya uimbaji wao.


Unajiita mhubiri injili lakini kwenye mahubiri yako huwa unamtaja YESU KRISTO Mara moja kwa mwezi.
Wewe ni mhubiri wa injili ipi?
Kwenye mahubiri yako unajitaja wewe Mara kumi lakini YESU wala humtaji.
Unamtaja mkeo au mmeo lakini YESU mwenye injili hata humtaji.
Unataja dhehebu lako na huduma yako Mara nyingi kuliko mwenye injili.
Wewe ni mhubiri wa injili ipi?


Wewe unayejiita Mwinjilisti harafu humhubiri YESU wala kumtaja basi hujui maana ya Mwinjilisti.
Mwinjilisti ni mpeleka Injili, na injili halisi ni ya KRISTO.
Ukiamua kuwa mpeleka injili basi tambua kwamba unampeleka YESU.
Sasa unajiitaje mwana Injili wakati humtaji mwenye injili?
Je unapeleka injili ipi?
Hebu jifunze maandiko haya itakusaidia.

Wagalatia 1:6-12 " Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya KRISTO, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya KRISTO. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au MUNGU? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa KRISTO. Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa YESU KRISTO."

Ndugu kama unaona aibu kumtaja YESU ujue hiyo ni kwa faida ya shetani na ni kwa hasara yako mwenyewe.
Ewe mwana Injili.
Ewe mwimbaji wa nyimbo za Injili.
Ewe mhubiri Injili.
Zingatia Sana kumhubiri mwenye Injili kwenye Injili unayoipelek
a.

Kumbuka pia kwamba waitwao ni wengi lakini Wateule ni wachache.
Wateule hawaishii kuitwa tu Bali huendelea katika Wito na utakatifu hata kufikia katika kuwa wateule.
Wateule ni waaminifu.
Wateule huvumilia huku wakiomba.
Wateule hawachukuliwi na upepo wa mafundisho ya shetani ambayo yana lengo la kuwatoa watu kwa YESU.
Wateule humwabudu MUNGU Baba katika ROHO na kweli.
Wateule wanamtii MUNGU katika mambo yote.
Wateule wanamtii Bwana YESU KRISTO katika mambo yote.
Wateule wanaongozwa na ROHO MTAKATIFU na wanamtii ROHO MTAKATIFU katika mambo yote.
Wateule wanalitii Neno la MUNGU.
Wateule wanaliishi Neno la KRISTO, ndio maana waitwao ni wengi lakini wateule ni wachache.

Mathayo 22:14" Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache."
Kila aliyeitwa katika Wokovu wa KRISTO ana uwezo wa kufanyika mteule wa MUNGU siku zote.
Wengine huishia kuitwa tu, yaani anaokoka wiki moja kisha anarudi kwa shetani.
Ndugu hakikisha ukiitwa fanyika mteule wa KRISTO maisha yako yote.


Mtumishi wa MUNGU ukitoka kwenye nafasi yako aliyokupa MUNGU ujue utakuwa unatoa nafasi kwa virus wa shetani kuchukua nafasi.
Usipokaa kwenye nafasi yako ya kuhubiri injili ya KRISTO ujue wapinga Kristo Utawapa nafasi ya kuwatoa watu kwa YESU KRISTO kupitia mafundisho yao ya uongo.
Usipoimba nyimbo za injili ujue kuna nafasi umeiachia ili watu wasikilize nyimbo za shetani.
Nakuomba kaa kwenye nafasi yako katika injili ya KRISTO.
Tito 2:7-8"katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu,
na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu."


Fanya kazi ya MUNGU bila kujali mazingira na vyeo vya watu.
Kumbuka unaweza ukayafanya mapenzi ya MUNGU na ukachukiwa na waliyo kinyume na mapenzi ya MUNGU.
Unaweza ukafanya mapenzi ya MUNGU na ukawakosea watu walio kinyume na mapenzi ya MUNGU.
Ndugu Usiogope Kamwe.
Mapenzi ya MUNGU maana yake ni Matakwa ya MUNGU.
Ni kile akitakacho MUNGU.
Ndugu yatimize hayo na MUNGU akubariki katika Jina la YESU KRISTO.

1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

Hakikisha unakuwa Mteule wa MUNGU bila mawaa. Labda ngoja tujiulize kidogo ''Mawaa ni nini?''
Mawaa ni alama za tofauti katika kitu halisi.
Mawaa ni kasoro inayojitokeza ambayo haitakiwi iwepo.
Mawaa ni madoa yasiyo sahihi katika kitu.
Kwa kanisa la MUNGU mtu mwenye mawaa ni mtu ambaye haishi maisha matakatifu, ni mtu wa michanganyo.
Mtu asiye na mawaa ni mteule aliye safi bila hatia yeyote.
Mtu asiye na mawaa ni mteule asiye na kasoro yeyote katika maisha yake ya Wokovu.
Mawaa hayo ni madoa yanayochafua Wokovu na kusababisha kanisa litukanwe.
Ni mtu anayeleta fedheha na kuliabisha kanisa.

Watumishi wote wa MUNGU inawapasa kuwa watumishi wasio na mawaa.

2 Petro 2:12-14 '' Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao; Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni MAWAA na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi; wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; ''


Biblia imelitumia Neno hilo mawaa katika maandiko mengi.
Watumishi wote wa MUNGU inawapasa kuwa watumishi wasio na mawaa.  

Wakolosai 1:21-22 ''Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, WATAKATIFU, WASIO NA MAWAA wala lawama;''

Kanisa la KRISTO ni lazima tuwe watakatifu na wakamilifu wasio na uchafu wowote ambao ni dhambi.
Watumishi wote wa MUNGU inawapasa kuwa watumishi wasio na mawaa.  
2 Petro 3:14 '' Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.''

MUNGU anahitaji Kanisa lake lisiwe na mawaa yaani lisiwe na uchafu ndani yake.
Watumishi wote wa MUNGU inawapasa kuwa watumishi wasio na mawaa. 

 Waefeso 5:25 -27 '' Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama KRISTO naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na MAWAA ''

Ndugu unahitaji sana kuwa Mkristo usiye na mawaa.
Ndugu unahitaji kuishi Maisha ya Wokovu yasiyo na mawaa yaani yasiyo na dhambi na yasiyo na michanganyo na yasiyo na uchafu.


Kumbuka pia kufanya kazi ya MUNGU kwa moyo na kwa upendo na hiari, Kumbuka apandaye kidogo atavuna kidogo na apandaye vingi atavuna vingi.
Je wewe ndugu unapanda nini katika ufalme wa MUNGU?
Unapanda nini katika injili ya KRISTO?
Unapanda nini katika Kanisa la MUNGU?
Ndugu, iko wazi kabisa kwamba utakapopanda vingi utavuna vingi, lakini pia ukipanda vichache utavuna vichache.

2 Wakorintho 9:6 "Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu."

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
Ndugu mhubiri KRISTO YESU na sio vinginevyo.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments