SABABU 7 ZA KWANINI HUWA TUNATOA SADAKA NA ZAKA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tena karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna aina mbili(2) Za matoleo ambayo wateule  wa KRISTO humtolea   MUNGU.
Aina hizo mbili za matoleo ni  Fungu la kumi(Zaka) na sadaka. Sadaka nayo imegawanyika katika makundi zaidi ya saba kulingana na mtoaji alichokusudia. Inawezekana ikawa ni sadaka ya shukrani kwa MUNGU, Inawezekana ikawa ni sadaka ya amani, inawezekana ikawa ni sadaka ya agano n.k
Sadaka sio fungu la kumi na ni vitu viwili tofauti na vyenye matokeo tofauti.
Zaka ni moja katika kumi ya kipato cha mtu ambacho mtu huyo humtolea MUNGU kwa hiari na upendo Kanisani.
Neno kuu katika kutoa zaka ni upendo kwa MUNGU.

Kuna madhara mengi sana kama humtolei MUNGU fungu la kumi.
Kwa uzoefu wangu nimegundua kwamba watu wengi sana wasio waaminifu katika kutoa fungu la kumi ndio hao hufa kiroho sana.
Chanzo kimojawapo kikuu cha mteule kufa kiroho ni kutokuwa mwaminifu katika kutoa fungu la kumi. 
Kuna ajabu nyingi katika fungu la kumi ila watu wengi sana hawajui.
Alichoagiza MUNGU huwa kina maana sana sana.



Sadaka ni kitu au fedha ambazo hutolewa na mtu kwa kuwapa wanaostahili kwa ajili ya kujipatia thawabu kwa MUNGU.
Katika Kanisa la MUNGU ni muhimu sana kutoenda mikono mitupu, Bali nenda na sadaka lakini ni muhimu kutoa kwa upendo na sio kulazimishwa au kujilazimisha ndipo utapata dhawabu kwa MUNGU.

Thawabu ni malipo mema anayoyapata mtu kutoka kwa MUNGU baada ya kutii Neno la MUNGU juu ya jambo husika.
Hagai 1:5-7 ''
Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. ''
Kwa ujumla sadaka ni hiari lakini ni ya muhimu sana kwa MUNGU na kwa mtoaji na ina matokeo makubwa kulingana na moyo wa mtoaji na jinsi ilivyotolewa ikiambatana na maombi sahihi katika YESU KRISTO.
Zaka ni jambo la lazima kwa wateule wa MUNGU, ni matoleo ya aina yake na ambayo ni kipimo kikuu cha MUNGU kama unampenda na ni jambo pekee katika Biblia ambalo MUNGU amesema tumjaribu tuone kama hatatubariki.
 

SABABU 7 ZA KWANINI TUNATOA SADAKA NA ZAKA.

1. Kwa sababu ni agizo la MUNGU .

Kumb 16:16-17 ''
Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu. Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako, alivyokupa''
Huu ni mfano wa agizo la MUNGU la utoaji wa matoleo, ni agizo la kila mteule wa MUNGU.
Ni agizo la hiari lakini likiwa limebeba ushindi mkuu kwa mtoaji.


2. Kwa sababu tunampenda na kumweshimu MUNGU hata kwa vitu vyetu.

Mithali 3:9-10 ''
Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.''

Huwezi kumheshimu MUNGU kama humpendi, upendo huileta heshima sahihi.
Kama tunampenda MUNGU na kumweshimu basi hakika utoaji wa zaka na sadaka wala hautakuwa mzigo kwetu.
Wanaompenda MUNGU na kumweshimu humtolea matoleo yao kwa upendo.


3. Kwa sababu sadaka na zaka ni hitaji la madhabahuni.

Kumb 14:22 ''Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.''
Madhabahu ni daraja kati ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili. Sisi tuko katika ulimwengu wa mwili na ili tufanikiwe katika ulimwengu wa roho basi wakati mwingine matoleo yetu ni muhimu sana.
Pia ni muhimu tujue kwamba matoleo ni hitaji la madhabahuni kwa sababu kila kitu kanisani kinahitaji pesa. Vyombo, umeme, viti na kila kitu kinahitaji pesa. Wachungaji nao MUNGU amewapa fungu lao kutokea madhabahuni, ni agizo la MUNGU kabisa.
Ni mambo mengi sana kanisani yanahitaji tutuoe sadaka nzuri ili huduma iende vizuri, sadaka ni hitaji la kimadhabahu hivyo watu wa MUNGU inawapasa sana kuzingatia kumtolea MUNGU zaka na sadaka. 

4. Tunatoa ili kuonyesha shukrani zetu kwa MUNGU na ni sehemu katika kumcha MUNGU.

Zaburi 50:5 ''
Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.''

Kumbe matoleo hutengeneza agano na MUNGU.
Kama agano hilo utalitengeneza na MUNGU ujue agano hilo litavunja maagano ya kipepo yaliyokufunga.
Kuna watu wengi sana hufunguliwa baraka zao na hufunguliwa maagano kwa sababu ya uaminifu wao kwa MUNGU.
Matoleo huonyesha shukrani kubwa kwa MUNGU.
Matoleo huonyesha ni MUNGU amekulinda na kukubariki hivyo unapotoa matoleo ni kuonyesha shkrani kwa MUNGU na ni njia mojawapo ya kumcha MUNGU.


5. Tunatoa ili kutengeneza hazina zetu mbinguni.

Luka 12:31-34 ''
Bali utafuteni ufalme wa MUNGU, na hayo mtaongezewa. Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu. ''

Maandiko haya yamejitosheleza kabisa kwamba matoleo ni njia mojawapo ya kumtafuta MUNGU, Tena jambo kuu ni kwamba pale ambapo hazina yako ilipo mbinguni na wewe utakuwa hapo.
Hazina yako ya mbinguni inakuwakilisha wewe na siku ukifika huko kama ukishinda ya dunia kwa kuishi maisha matakatifu hakika utaungana nayo hiyo hazina yako.
Hazina ahaitengenezwi kwa matoleo tu lakini hata matoleo hutengeneza sana hazina ya Mtu.
Kama huna hazina mbinguni huwezi kwenda huko.
Hazina yako utaitengeneza kwa;
a. kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO. 
b. Kumtumikia Bwana YESU. 
c. Matoleo sahihi 
Matoleo yana faida nyingi sana kwa mtoaji, moja ya faida hizi ni kutengeneza hazina yako mbinguni.
Ukiishi maisha ya Wokovu matakatifu hakika utaikuta mbinguni hazina yako.
Lakini ni muhimu kujua kwamba wapo watu pia walitengeneza hazina zao mbinguni kwa matoleo lakini baadae walimwacha YESU na kuacha utakatifu hivyo hawakwenda mbinguni bali kuzimu na mema yao ikiwemo hazina yao iliyotokana na matoleo haikukumbukwa tena. Hivyo ndugu uwe mtojai wa matoleo lakini pia hakikisha maisha yako yote unaishi maisha matakatifu katika Bwana YESU.

6. Tunatoa ili tupate thawabu au baraka za MUNGU.

Malaki 3:8-11 ''
Je! Mwanadamu atamwibia MUNGU? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu ''

Hakuna mtu asiyependa kubarikiwa na MUNGU.
Matoleo ni njia mojawapo kuu ya kubarikiwa na MUNGU hivyo unavyomtolea MUNGU kwa usahihi na uaminifu hakika atakubariki sana sana kwa baraka zote za rohoni na mwilini.
Kumbuka pia baraka za MUNGU ziko katika makundi haya:
a. Baraka za kiuchumi.
b. Baraka za kutamalaki.
c. Baraka za ndoa.
d. Baraka za uzao.
e. Baraka za afya.
Wengi humtoleoa MUNGU wakitarajia tu baraka za kiuchumi lakini MUNGU anaweza kukubariki kwa baraka zote tano.
Baraka hizo 5 zimeunganisha kila mahitaji ambayo mwanadamu anahitaji katika maisha yake.
Shetani huwapiga watu wengi katika kundi mojawapo la baraka. Kuna ambao shetani anawatesa katika baraka ya ndoa, kuna wengine kwenye baraka ya ndoa wako vizuri lakini katika baraka ya afya wanateseka. Kuna ambao kwenye afya wako vizuri lakini kwenye uchumi adui anawatesa sana. Siku moja nitafafanua zaidi juu ya baraka 5 ambazo MUNGU hutubariki.
Utoaji una faida sana.


7. Tunatoa kwa sababu vyote ni Mali ya MUNGU hivyo hatuwezi kumzuilia MUNGU chochote.

Zaburi 24:1 ''Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake. ''

Kwanza MUNGU hatuwezi kumzuilia chochote maana hata mali zetu zote ni zake pia na ana uwezo wa kuziondoa, kuziongeza au kuzifuta; hivyo kwa wanadamu mwenye akili lazima ajue kwamba vitu vyote ni mali ya MUNGU, hivyo unaopomtolea matoleo unamfanya MUNGU ailinde mali yake uliyonayo wewe, ni neno gumu lakini ni heri kuwa mtoaji mzuri wa zaka na sadaka.
Ndugu mmoja alisikia kabisa sauti ya ikimwambia kwamba amtolee MUNGU, Alipogoma alifilisika akawa hana mali hata moja. Baade aligundua kosa na kutubu uovu wake huo wa kumzuilia MUNGU ndipo akaanza kupata mali tena.
 
 
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments