SABABU NANE(8) ZA KWANINI UMSAMEHE ALIYEKUKOSEA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunaziangalia sababu za kuwasamehe watu waliokukosea.
Kusamehe/msamaha ni nini?
Msamaha ni tendo la kuwia mtu radhi kwa makosa aliyokutendea.
Kusamehe ni kuachilia moyoni mwako yale uliyokosewa na kuyafuta ili yasiwe makosa tena.

Leo watu wengi pia husema wamewasamehe watu waliowakosea lakini kiuhalisia watu hao wanakuwa hawajasamehe.
Watu hao wanakuwa wamesamehe kwa kinywa ila mioyo bado haijasamehe.
Ndugu, Sio vizuri kuweka moyoni jambo ambalo ulisema umemsamehe ndugu yako au mwenzi wako au rafiki yako. 
Naomba ujue kwamba kama jambo hilo ukiliwaza tu unakosa amani au unachukia jua tu kwamba hujasamehe hata kama unadhani umesamehe. 
Msamaha halisi huambatana na kuachilia, kama hujaachilia maana yake pia hujasamehe.
Kuna wengine kwa kutamka ni kama kweli wanakusamehe lakini ukiwangalia usoni unagundua kabisa kwamba hapo hakuna msamaha uliotoka.

 Waefeso 4:32 '' tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.''

Je unamsamehe mtu kwa sababu gani?

1. Unamsamehe mtu kwa sababu ni agizo la MUNGU kuwasamehe. Waliokukosea.

Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''

Ni agizo la MUNGU kuwasamehe watu wanaokukosea.
Usipowasamehe huwezi kuingia uzima wa milele hata kama unajiona ni mtakatifu kiasi gani.
Msamaha ni jambo la lazima kwa wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Usikupokuwa mtu wa kusamehe watu hakika hata wewe hautasamehewa na MUNGU.
Kusamehe ni sheria ya rohoni ya lazima kwa wateule wa KRISTO.
Ni MUNGU ametuagiza tuwe watu wa msamaha hivyo ni lazima tutekeleze agizo la MUNGU.
Usiposamehe watu wewe ni muuaji na wauaji hawana sehemu katika ufalme wa MUNGU wasipotubu na kuacha dhambi hiyo.
 1 Yohana 3:15 ''Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. ''
 
2. Unamsamehe mtu kwa sababu unampenda. Upendo husitiri wengi wa dhambi.

1 Petro 4:8 '' Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.''

 Mtu mwenye upendo kwa watu wote ni rahisi sana kusamehe ili asijinajisi kwa kushindwa kusamehe.
Watu unaowapenda ni lazima uwasamehe, ukikosa msamaha hakika wewe huna upendo.
Lakini ni lazima tujue kwamba sio upendo katika dhambi, nikiwa na maana ya kwamba, kwa mfano  kama kuna mtu amekudanganya na mkajikuta mumefanya uasherati, kisha akakuomba msamaha akikutaka muendelee na mahusiano. Wewe msamehe lakini kuendelea na dhambi ni jambo lingine na usikubali hata siku moja.
Binti mmoja alikuwa na mahusiano ya ngono na kijana mmoja kisha binti yule akazalishwa na kuachwa. Baada ya muda yule kijana akaja akiomba msamaha ili asamehewe, Yule binti akamsamehe lakini kijana yule alisema kwamba kama kweli amesamehewa basi waendelee na mahusiano. Binti yule alimkubalia na hatimaye akajikuta amezalishwa watoto watatu(3) na kuacha tena. Kisha akampata kijana mwingine ambaye naye alimbebesha mimba na kumwacha. Baadae yule kijana alirudi na kuomba msamaha na kusamehewa lakini naye alitaka mahusiano yaendelee maana ndio kipimo chake cha msamaha, yule binti alikubali na akazalishwa mtoto mwingine na kuacha, Ndipo akanipigia simu akilia huku akiomba ushauri. Ana watoto watano na baba za watoto hao walimwacha na kuoa kwingine. Binti yule aliniuliza ''Je nilikosea kusamehe?'' Nikamwambia hakukosea kusamehe ila alikosea kufanya dhambi.
Ndugu zangu, msamaha ni muhimu sana lakini sio msamaha unaotengeneza dhambi mpya.
Ukiwa na upendo kwa watu wote utawasamehe lakini sio kufanya kitu cha kipepo cha kuonyesha umesamehe, haitakiwi kuwa hivyo.
Kumbuka hii  "Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, mabaya hayataondoka nyumbani mwake-Mithali 17:13''

3. Unamsamehe kwa sababu hakuna faida hata moja katika kutokumsamehe.

Mathayo 5:7 '' Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.''

Wenye rehema maana yake ni watu wenye kusamehe na kuachilia.
Hao wanaitwa heri na Biblia inasema kwamba hao na wao watapata rehema.
Unapowasamehe watu unakuwa umetoa nafasi ya wewe kusamehewa kama ukitubu.
Hakuna faida hata moja kama hutamsamehe mtu.
Usipomsamehe wala hatakonda au kupungua.
Usipomsamehe wala hatafilisika au kuumwa.
Usipomsamehe bado yeye atabaki kuwa ni yeye tu hivyo hautampunguzia lolote.
Unahitaji kusamehe tu ndugu maana hakuna faida katika kutokuwasamehe watu, zaidi sana wewe ndio utakonda kwa uchunga na unaweza hata kupata magonjwa kwa sababu ya uchungu unaotokana na kutokusamehe kwako.
Hakuna faida katika kutokusamehe hivyo inakupasa tu uwasamehe wanadamu wanaokukosea.
 ''Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.-Walawi 19:18''

4. Unamsamehe kwa sababu ya kulinda afya yako.

Mathayo 18:21-22 ''Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? YESU akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.'' 

Wanafunzi wa YESU walikuwa wanataka kujua zaidi kuhusu kusamehe na idadi ya kusamehe ya mwisho.
Bwana YESU akawajibu kwamba inawapasa kusamehe saba mara sabini. Msamaha huo una maana ya kwamba msamaha ni jambo lisilo na ukomo.
Hakuna mtu ambaye anaweza akakosewa na mtu mmoja mara 490 ili ahitaji kumsamehe mara 490. Sana sana wewe mtu amekukosea mara moja au mara mbili au zaidi sana mara kumi au mara 40 lakini katika makosa hayo yote anayokukosea unahitaji sana kumsamehe.
Kwanini nimesema kumsamehe mtu ni kulinda afya yako?
Ni kwamba yapo madhara makubwa sana kiroho na kimwili kama hutakuwa mtu wa msamaha.
Usiposamehe maana yake utakuwa na uchungu na maumivu mengi kiasi kwamba hata kuomba utashindwa zaidi ya kulia tu, na kumbuka ukikosa maombi afya yako ya kiroho itayumba tu.
Usiposamehe utakuwa na hasira nyingi na taharuki nyingi rohoni mwako kiasi kwamba huwezi kuwa na muda wa utulivu ili kumsikiliza ROHO MTAKATIFU, Huwezi kuwa na uwezo mzuri na kulisoma Neno la MUNGU na kulielewa. Hayo ndio yanaweza kuifanya afya yako kiroho iwe mbaya, hivyo msamaha unakusaidia katika mengi sana.
Hata afya ya mwili inaweza ikateteleka kwa sababu ya kutokuwasamehe watu.
Kumbuka usipomsamehe mtu lazima utakuwa una hasira naye, utakuwa una uchungu, utakuwa na maumivu na n.k. Hayo yote ni mapando ya shetani ili kukudhoofisha kiroho.
Unahitaji sana kuwa mtu wa kusamehe watu ili ulinde utulivu wako wa ndani, ulinde afya yako kiroho na kimwili pia.
 Biblia inakusahauri ikisema ''Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu.-Mithali 3:3-4 ''

 Rehema ni kusamehe na kuachilia hivyo hayo mawili yasifarakane na wewe bali yaweke moyoni mwako ndipo utakapopata kibali  na akili nzuri mbele za MUNGU na mbele za wanadamu.

5. Unamsamehe ili na wewe usamehewe na MUNGU.

Marko 11:25 ''Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.''
Kipimo kingine cha MUNGU kukusamehe ni pale ambapo na wewe unasamehe wengine.
MUNGU atakusamehe ukimuomba msamaha lakini pia unahitaji sana kuwasamehe na watu waliokukosea wewe.
Usipowasamehe watu utakuwa una dhambi ya kutokuwasamehe watu  na dhambi hiyo haifutiki hadi uwasamehe watu waliokokosea kisha utubu kwa MUNGU kwa sababu ya moyo wako wa kutokusamehe.
Kama unavyotamani kutubu kwa Bwana YESU ili akusamehe basi na wewe wasamehe wanaotubu kwako kwa sababu ya makosa waliyokutendea.
''mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.-Wakolosai 3:13''

Usipokuwa mtu wa kuwasamehe watu hakika hiyo ni hatari kwako na unaweza ukaukosa hata uzima wa milele.
Ndugu unahitaji sana kuwa mtu wa kusamehe watu wanaokukosea.
Waachilie na wewe utaachiliwa.
''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.-Luka 6:37


6. Unamsamehe ili kulifuta jambo hilo moyoni mwako na ili lisikusumbue tena.

 Waebrania 12:15 ''mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.''
Shina la uchungu linatokana na kutokusamehe.
Ukisamehe waliokukosea unakuwa unatoa nafasi ya uchungu kuondoka kwako.
Unaweza ukawa unateswa na vifungo vya kipepo kwa sababu tu ya kutokuwa na moyo wa msamaha hivyo unapoamua kusamehe unakuwa unatoa nafasi ya jambo hilo lisikusumbue tena.
Kuna watu wanateswa sana na nguvu za giza kwa sababu tu ya kutokusamehe, kwanini uteseke kwa sababu ya jambo hilo dogo?
Kutokusamehe ni mlango wa mawakala wa shetani kuingia kwako na kukutesa maana wakati huo ulinzi wa MUNGU utaondoka kwako.
Unahitaji sana kuwa mtu wa kusamehe watu wanaokukosea.
Haijalishi ni makosa makubwa kiasi gani, unahitaji kusamehe maana msamaha huo ni kwa faida yako mwenyewe.



7. Unamsamehe kwa sababu kusamehe ni wajibu wa watu wa MUNGU.

 Waefeso 4:32 ''tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.''
Kusamehe ni wajibu wa wateule wa KRISTO.
Huhitaji mpaka uombwe msamaha ndipo usamehe bali samehe hata usipoombwa msamaha.
Jiulize, kama unasubiria mtu aliyekokosea aje akuombe msamaha ndipo msamehe, je ukifa kabla hajafika kukuomba msamaha utaenda wapi?
Maana utakuwa hujasamehe bado.
Ndugu unahitaji sana kuwasamehe watu muda wowote hata wasipokuomba msamaha. Msamaha ni wajibu wa wateule wa MUNGU.
Kama ambavyo wewe ukiungama dhambi zako MUNGU anakusamehe basi na wewe hakikisha unakuwa na tabia ya kusamehe watu muda wowote.
 
 ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.-1 Yohana 1:19 ''

8. Unamsamehe ili kupisha kisasi cha MUNGU.

 Warumi 12:19 "Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena BWANA" 
Watu wengi sana hawaijui siri hii.
Unaweza ukakosewa sana sana lakini kusamehe ni kupisha kisasi cha MUNGU.
MUNGU amesema kwamba usilipe kisasi, kutokumsamehe mtu ni sehemu ya kulipa kisasi na kama unatarajia MUNGU awaadhibu waliokukosea hakika MUNGU hatawaadhibu kamwe.
Ukiwasamehewe basi hapo umeipisha ghadhabu ya MUNGU ili MUNGU akulipie kisasi kwa waliyokutendea watu hao japokuwa wewe tayari umeshawasamehe.
Wengi sana MUNGU huwa anawapiga kwa sababu waliowakosea wateule wake, lakini ni hadi mteule huyo awasamehe.
Kutokusamehe ni kulipa kisasi na kwa njia hiyo MUNGU hawezi kuwapiga watu hao waliokukosea kosa ambalo linahitaji wapigwe.
samehe ndugu maana ni kwa faida yako mwenyewe.
 
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments