UMAKINI KABLA YA NDOA UNAHITAJIKA SANA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu kujifunza Neno la MUNGU.
Katika jamii ya leo kuna changamoto nyingi sana ujana na  za uchumba na kuna mitazamo mingi sana juu ya suala la kuoa au kuolewa.
Ngoja kwa sehemu kidogo nizungumzie kidogo mambo fulani kuhusu vijana na kuhusu uchumba ambayo kwa yatawafaa wengi.
Kuna tofauti kati ya kufikiri kwa mtu mmoja na mtu mwingine juu ya jambo moja na ndio maana kuna tofauti ya maisha kati ya mtu mmoja na mwingine kwa sababu kila mmoja anajua anavyofikiri. Kufikiri kwako ndiko kumekufikisha hapo ulipo.
Kufikiri kwako ndiko kumekupa maisha hayo uliyonayo sasa.
Kama binti ulifikiri vibaya ukapewa mimba na kuharibiwa future yako basi hayo unayoyaishi sasa yalisababishwa na kufikiri kwako.
Kijana kama umekuwa teja hiyo inatokana na ulivyofikiri.
Kama nguvu za Giza zimekufunga ni kwa sababu ufahamu wako hukuuruhusu umfuate KRISTO ili uwe salama na hivyo kuteseka kwako huko na nguvu za giza hiyo imechochewa na kufikiri vibaya kwako kila siku.
Ndugu yangu ni muhimu sana sasa uanze kufikiri vyema ili uishi maisha sahihi matakatifu mbele za MUNGU.
Kumpokea YESU ndio kufikiri vyema zaidi na baada ya hapo fikiri kumtumikia MUNGU na kisha fikiri kumpendeza MUNGU siku zote.

1 Yohana 2:14-17 '' Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la MUNGU linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba(MUNGU), bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''


Kumpenda MUNGU humtengeneza kijana ili afae katika mambo mengi sana.
Kumpenda MUNGU kunamfanya kijana kuishi maishi matakatifu ya wokovu na kumfanya hata afae katika jamii.
Lengo kuna changamoto nyingi zinawaathiri vijana, na changamoto kubwa ni uchumba kuvunjika na kuacha maumivu makubwa.
Vijana wengi leo wamejikuta katika mahusiano ya awali(Uchumba) lakini sio wote huishia kuingia katika ndoa, wengi sana uchumba huharibika kabla ya ndoa na kuwaachia maumivu, majeraha na mateso mengi. Kuna vyanzo vingi vinavyosababisha uchumba kuvunjika, kwa sehemu kidogo ngoja nizungumzie jambo hilo.


Vitu gani husababisha wachumba kuachana kabla ya kufunga Ndoa?

Kuna mambo mengi huchangia wachumba kuachana kabla ya kufunga ndoa mawili katika hayo ni haya;

1. Jambo la kwanza ambalo linaweza kusabanisha wachumba kuachana kabla ya kufunga ndoa ni shetani kupewa nafasi katika maisha yao ya uchumba.

Waefeso 4:27 "wala msimpe Ibilisi nafasi."

Wengi humpa shetani nafasi kwa kufanya uasherati.
Shetani akipewa nafasi hao wachumba huishia tu kutokuaminiana na kubaki kuchunguzana tu kwenye simu.
Kila mtu anakuwa mkali kupita kawaida kwenye suala la simu yake lakini ukweli ni kwamba simu kama haina ubia wa kipepo si hata ikichunguzwa haitakutwa na virus vya usaliti?

Kutokuaminiana kwingi huja baada shetani kupewa nafasi katika uchumba huo.
Kijana kabla hajamchumbia binti huwa amemwamini kwanza, hivyo kutokuaminiana kunakojitokeza baadae huja baada ya shetani kupewa nafasi.
Binti kabla hajamkubalia kijana ili wawe wachumba huwa anamwamini kwanza hivyo kutokuaminiana kunakojitokeza baadae huja baada ya shetani kupewa nafasi katika maisha yao.
Ukichunguza wachumba wengi ambao hawaaminiani ni kwa sababu ya kutokuishi maisha matakatifu.
Usaliti hutengeneza kutokuaminiana na usaliti huo huja kwa sababu ya kutokumcha MUNGU

2. Chanzo cha pili cha wachumba wengi kuachana ni kukosa tabia njema.

1 Wakorintho 15:33-34 " Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema . Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui MUNGU. Ninanena hayo niwafedheheshe."

Tabia njema Huharibiwa na mazungumzo mabaya, maana yake kile anachokisikia binti au kijana kinaweza kitu hicho kikamuondolea tabia njema.
Ukikosa Tabia njema maana yake una tabia mbaya.
Wachumba kuishi kama wameshafunga ndoa tayari hiyo ni Tabia mbaya sana tena ni dhambi.
Tabia hiyo inaweza kumfanya shetani apate nafasi katika uchumba huo na kupanda magugu ambayo yatawashinda wachumba kuyang'oa na kuishia kuachana na kuachiana majeraha ya moyo.
Maisha ya kuiga watu unaiwasikia kwenye TV au mitaani kunaweza kukakuondolea tabia njema na ukajikuta una tabia mbaya.

Hakuna haja ya kukosa Tabia njema kwa wachumba kipindi cha uchumba.
Ni muhimu kumcha MUNGU na kumtii daima.


Kitu cha tatu cha ziada juu ya vyanzo vya wachumba kuachana ni.
Wachumba huwa ni wasiri maisha yao lakini baadae huja kuonekana Kabisa kwamba hawafai.
Unakuta kijana aliwahi kuoa na akaacha mke na watoto lakini wakati huu anachumbia tena na kujidai kwamba hajawahi kuchumbia.
Unakuta binti akishazaa na anaendelea na uhusiano wa siri na mzazi mwenzake.
Kuzaa tu sio tatizo lakini ni lazima kuwa mkweli na unayeiishi kweli ya MUNGU

Kuoa au kuolewa ni malengo ya kila mwanadamu, ni ndoto ya kila mtu mwanaume kwa mwanamke.
Lakini wakati mwingine malengo hayo yanayeyuka kwa mtu kwa sababu ya;
1. Dharau.
2. Kutokujua majira na wakati wa MUNGU.
3. Kuishi maisha ya dhambi.
4. Tamaa.
5. Kukosa maombi.
6. Kujiona bora kuliko wengine.
7. Kuishi maisha ya dhambi.
8. Vifungo na laana zisizovunjwa.
9. Kuharibiwa ufahamu kipepo hata mtu anakuwa hajitambui.
10. Kutokumjua MUNGU na njia zake za Baraka.

 
Waebrania 13:4-5 ''Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.''



Changamoto nyingine kubwa sana ambayo inawapata vijana wacha MUNGU ni juu ya kupata mchumba mpagani.
Wengi huuliza kama ni dhambi kuoa au kuolewa na mpagani.
Inawezekana na wewe ni mmoja wa wanaojiuliza juu ya hilo.
 Je, ni dhambi ama ni kosa kuoa/kuolewa na mtu ambaye hajaokoka?

Ukwleli ni kwamba Sio dhambi ndugu yangu kuoa au kuolewa na mtu ambaye hajaokoka ila ni hatari kwako kwa maisha ya kiroho. Kumbuka katika Biblia kuna mifano hai ya kuonya juu ya hilo. 
Mfano mmojawapo ni huu.
1 Wafalme 21:25 '' (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. '' 
Ahabu alipomuoa Yezebeli mwabudu shetani alileta ibada ya shetani kwa waisraeli na akajenga hekalu la shetani ikulu, jambo hilo liliwatesa sana Israeli. 
Ahabu Mcha MUNGU alijikuta kwa ushawishi wa Yezebeli akiabudu shetani na kuwakosesha pia kundi la MUNGU.
Kumbuka pia Samson alipomuoa Delila ni mfano hai wa kuoa mtu asiye na YESU ndani yake, hana hofu ya MUNGU na hajui maisha ya Wokovu ni nini, ndio maana Samson akatobolewa macho na chanzo ni mkewe asiyeokoka.
Waamuzi 16:4-6 '' Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila.  Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe. '
Ukiendelea mbele kusoma maandiko hayo utagundua madhara ya wateule kuoa au kuolewa na wapinga Kristo.
Mfano mwingine ni Binti aliyeokoka anajichanganya na kuolewa na mpagani, hapo kama yule Binti alikuwa na huduma kanisani jua kwamba huduma imekufa, alikuwa anaabudu MUNGU sasa mmewe atamhamishisha kutoka kwa YESU na kuanza kuabudu mungu wa mumewe ambaye wala sio MUNGU aliye hai.
Japokuwa sio dhambi kuoa au kuolewa na mpagani lakini ni vyema wewe mteule wa KRISTO ulione hilo kama dhambi na usikubali hata siku moja kuoa au kuolewa na mtu asiyemcha MUNGU wako katika KRISTO YESU.

Kuolewa au Kuoa aliyeokoka inatakiwa iwe sheria kwa waenda mbinguni wote maana Biblia pia inasema msifungwe nira moja na wasioamini, ndoa ni nira mojawapo.
2 Kor 6:14 '' Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? ''
 Sasa ukifungwa nira moja ya ndoa na mtu asiyeokoka ni hatari sana kwako. unapoingia kwenye ndoa na mtu ambae hamjui YESU ni kazi kubwa sana na inabidi kujiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali, mfano unakuta mtu umeokoka unaingia familia/ukoo ambayo wanafanya matambiko, walevi, washirikina na tabia nyingine tofauti ambazo hazimpendezi MUNGU, ni hatari maana kama hujakomaa kiroho unaweza ukaingia makaribuni ukashangaa unaanza kunywa pombe kidogokidogo, wakifanya matambiko unashirikishwa na mwisho wa siku unakuwa kama wao, ni kwa neema ya MUNGU tu kuweza kusimama usitetereke, utapata changamoto pale utakapokataa kushiriki matendo wanayoyafanya utatukanwa utasemwa sana na kama hauko imara utashangaa unaiacha njia ya uzima.
Kijana unahitaji kuwa makini sana katika suala na kujiandaa kuingia katika ndoa.
 
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments