USIMLINGANISHE MUNGU NA VITU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Nikiwa Zanzibar kati ya Mwaka 2010 na 2011 kuna tukio moja liliniacha nikishangaa sana. Kuna mama mmoja Mkristo ambaye alikuwa anateswa na majini na yalimsumbua sana hadi ikabidi atafute watumishi ili wamuombee. Mama huyo kanisani kwao alikuwa anaenda na kwenye dhehebu lake alikuwa ni muumini safi. Baada ya kuanza kuteswa na majini(Mshetani) aliombewa lakini hakufunguliwa. Ikabidi ashauriwe na watu wa karibu yake kwamba aende kwa watu wanaoitwa walokole ndipo ataombewa na kufunguliwa. Mama yule akatuma mtu kuja kumweleza Mchungaji ili akaombewe. Mchungaji wetu akanituma mimi na rafiki yangu mmoja ili twende tukamuombee. Tulienda na tukafika kwa yule mama, ajabu ni kwamba ndani kwake alikuwa ameweka sanamu kadhaa kubwa na ndogo. Sanamu zile kwa maelezo yake ni sanamu za Yesu na  Mariamu. Akasemwa kwamba tangu ujana wake amekuwa muumini mzuri na katika maombi yake yeye humwomba MUNGU huku akielekea sanamu mojawapo. Tukamwambia kwamba yuko tayari tuziharibu zile sanamu na kisha tumwombee ili afunguliwe?
Yule mama ghafla akawa mkali na akataka kukaa  kuombewa. Mtumishi mwenzangu ikabidi awe mpole na kuanza kumbeleza mama yule huku mimi nikitafakari sana tukio hilo la Yule mama kuhusiana na sanamu. Katika maelezo yake alisema pia kwamba wakati mwingine yeye hushika ka sanamu kadogo na kuomba huku akiwa amekashika mkononi. Nilishangaa lakini akakubali kuombewa na tukamuombea. Wakati tukimuombea alilipuka mapepo na mengine hadi yalisema kwamba yako ndani ya zile sanamu. Baada ya yule mama kufunguliwa alisema kwamba anajisikia vizuri na vitu vizito alivyokuwa anavihisi mwilini sasa vimeondoka. Baada ya hapo tulidhani basi ufahamu wa kukataa msaada wa sanamu umemrudia lakini alisema tu kwamba sanamu zile hawezi kuzitupa bali ataendeleanazo lakini hataziomba tena. Baada ya hapo tuliondoka na kumwacha yule mama akifurahia ushindi, lakini suala la sanamu hakulijua kwamba lina madhara na wakati mwingine mapepo hujificha ndani ya sanamu hizo ili yamtese. Ngoja tuendelee
Isaya 40:18-23 '' Basi, mtamlinganisha MUNGU na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani?  Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha.  Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika. Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia? Yeye(MUNGU) ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa; ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia.''

Katika jamii ya leo sio watu wote humwabudu MUNGU aliyeziumba mbingu na dunia.
Ukiwa nje ya Wokovu wa KRISTO wewe unaabudu sanamu.
Yohana 14: 6-10 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba(MUNGU0, ila kwa njia ya mimi.  Kama mngalinijua mimi(YESU), mngalimjua na Baba(MUNGU); tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba(MUNGU), yatutosha.
  YESUakamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi(YESU) amemwona Baba(MUNGU); basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
 Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba(MUNGU), na Baba(MUNGU) yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba(MUNGU) akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake.'
'


Ndio maana Biblia inasema kwamba kama huna YESU moja kwa moja huna MUNGU.
Kama YESU KRISTO hajakuokoa basi hakika MUNGU hajakuokoa.
1 Yohana 5:12 '' Yeye aliye naye Mwana(YESU), anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima.''

Katika jamii ya leo kuna kundi la pili wa wanaoabudu, hawa hudhani ni sawa kumwabudu MUNGU au kumuomba kupitia sanamu, ni dhambi kufanya hivyo. Kumbu 5:8-9 '' Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wako, ni MUNGU mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,''  

 Kuna ndugu wengine hutumia sanamu katika ibada zao na maombi lakini wao hudai kwamba sanamu hizo wanaziheshimu tu na sio kuziabudu. Ndugu yangu, hakuna andiko hata moja linalokuruhusu kuheshimu sanamu. Mweshimu MUNGU, Mweshimu Bwana YESU na Mweshimu ROHO MTAKATIFU na sio kuheshimu sanamu iliyochongwa na watu.
Heshimu Kanisa la MUNGU na usikubali kulidhalilisha kanisa kwa kutenda dhambi, usiheshimu sanamu, Heshimu Neno la MUNGU na sio kuhesimu sanamu.

Ndugu, kumbuka kwamba ukiabudu sanamu maana yake unamlinganisha MUNGU na sanamu, ni dhambi mbaya.
Ukiabudu wanadamu maana yake unamlinganisha MUNGU na wanadamu, ni dhambi mbaya na Biblia inasema
'' Watarudishwa nyuma, wataaibishwa sana, hao wanaotumainia sanamu za mawe, na kuziambia sanamu za madini, Ninyi ndinyi miungu yetu.-Isaya 42:17 '

 Ukiabudu majini maana yake unataka kumlinganisha MUNGU na hizo takataka za shetani.
Ukiabudu chochote au yeyote isipokuwa MUNGU wa mbinguni hakika umeabudu sanamu.
MUNGU wa kweli yuko katika Nafsi tatu na huyo ndiye MUNGU, Nje na yeye kuna saamu tu na vinyago.
1 Yohana 5:7 '' Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni, Baba(MUNGU), na Neno(YESU KRISTO), na ROHO MTAKATIFU, na watatu hawa ni umoja''
Anaabudiwa MUNGU katika Mwana(YESU) kwa njia ya ROHO MTAKATIFU.
Ukiabudu nje na hapa ujue unaabudu sanamu.
Ukimwabudu shetani ujue umeabudu sanamu.
Ukiabudu vitu au mizimu ya ukoo ujue umeabudu sanamu.
 MUNGU Baba anasema '' Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.-Isaya 42:8 ''

Ukiabudu malaika maana yake unataka kumlinganisha MUNGU na Malaika. MUNGU halingani na chochote kinachoonekana na kisichoonekana.
Yeremia 10:6 ''Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee BWANA; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.'' 
Wala hakuna aliye kama MUNGU.
Zaburi 83:18 ''Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote. ''

 MUNGU amekamilika na wala hahitaji msaa wote kutoka kokote au kutoka kwa yeyote.
1 Yohana 5:9-11 '' Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa MUNGU ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa MUNGU ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe(YESU). Yeye amwaminiye Mwana wa MUNGU anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini MUNGU amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao MUNGU amemshuhudia Mwanawe.  Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe ''
 Ndugu unahitaji nini zaidi?
Hakuna hakuna unachohitaji zaidi ila unahitaji tu YESU KRISTO akuokoe.
Huhitaji sanamu yeyote na wala huhitaji kufanya ibada yako kwa yeyote au kwa chochote bali unahitaji tu Kumwabudu MUNGU wa mbinguni huku ukiishi maisha ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.
Tunamkaribia Baba kwa njia ya Mwana katika ROHO MTAKATIFU.
Isaya 40:25-26 ''Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye(MUNGU) aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake. ''

MUNGU wetu ni mmoja tu katika nafsi tatu. Hafananishwi na chochote tukionacho na wala halingani na yeyote wala chochoye.
Zaburi 68:20 ''MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.''

Ndugu ambaye unamtegemea MUNGU wa mbinguni nakuomba songa mbele.
Hata wakati utachoka kuomba, hiyo haina maana kwamba MUNGU hawezi kukutendea muujiza wako. Tafuta kujua tatizo lako na sio kulalamika.
Hata kama umekata tamaa ya kupona au kupokea ushindi wako, bado MUNGU anabaki kuwa ni MUNGU tu hivyo usimwache na kuzifuata sanamu.
Tambua kwamba MUNGU anakuandalia kilicho bora zaidi hata ya unachoomba.
MUNGU anabaki kuwa ni MUNGU tu, hajawahi kuchoka na wala nguvu zake hazijawahi kupungua kwa vyovyote.
Ndugu mngoje BWANA huku ukifanya mambo matatu.
1. Mngoje MUNGU huku ukiomba.
2. Mngoje MUNGU huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu.
3. Mngoje MUNGU huku ukimtumikia KRISTO.
Isaya 40:28-31 ''Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye MUNGU wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.'
  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments