INUKA UOMBE, MIMINA MOYO WAKO KWA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

INUKA UOMBE, MIMINA MOYO WAKO KWA MUNGU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Katika maisha wakati mwingine kuna kupitia katika magumu sana.
Wakati mwingine kuna kudharauliwa na kutukana na wakati mwingine kuna kuonewa na watu wabaya.
Wewe kama mteule wa MUNGU ni lazima ujue jambo la kwanza ni msaada wa MUNGU ndio unaouhitaji sana.

Maombolezo 2:19 " Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa BWANA; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu."
Katika andiko hili ni kipindi Waisraeli wamepelekwa uhamishoni Babeli.
Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwao lakini Yeremia Nabii alijua msaada ni kwa MUNGU ndio maana anawaambia watu "Inuka ulalamike mbele za MUNGU, Mimina moyo wako kama maji mbele zake ukiomba "
Inawezekana uko katika wakati ngumu sana.
Inawezekana kundi au Kanisa lenu liko katika wakati mgumu sana.
Ndugu muhimu kujua ni kuhitaji msaada wa MUNGU.
Inawezekana uko katika vita kubwa kiroho.
Inawezekana umeachwa bila hata kosa lolote.
Inawezekana umeondokewa na mtu muhimu sana kwako, oooh ni wakati mgumu sana.
Inawezekana unaonewa kazini.
Inawezekana unasimangwa kwa sababu hujapata mchumba au kwa sababu umekataliwa ghafla na mchumba wako.
Inawezekana unaumwa sana na watu hadi wameshaanza kutangaza kwamba umekufa, ooooh ni wakati mgumu sana sana.
Inawezekana wachawi wanakutisha.
Ndugu inuka uombe mbele za MUNGU aliye hai

Zaburi 62:8 '' Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.''
 
Kifunue mbele za MUNGU hicho kinachokusumbua .
Muombe MUNGU ili akulipizie kisasi kwa hao mawakala wa shetani wanaokuhangaisha.

Nakushauri ndugu kwamba wakati wa magumu yako epuka kuhesabu gharama bali mwite Bwana YESU akuokoe.
MUNGU kwetu ni MUNGU wa kuokoa 

Zaburi 68:20 '' MUNGU kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana. ''
 
UFANYE NINI WAKATI WA MAGUMU?

Jambo la kuzingatia ni kwamba yasiwe magumu uliyosababisha wewe kwa dhambi zako, kama ni hivyo unahitaji kutubu na kuacha dhambi.
Lakini kama ni magumu na hukusababisha wewe kwa kutenda dhambi basi fanya yafuatayo.
 
1. Omba mbele za MUNGU.
Danieli 6:10 ''
Hata Danielii, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za MUNGU wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.''
Viongozi wa serikali walipitisha sheria na Mfalme akaisaini, na sheria hiyo ya muda ilikuwa na lengo moja tu yaani kumfanya Danieli asimwabudu MUNGU Baba na akishindwa kuitii sheria hiyo auawe, ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Danieli lakini alijua nini cha kufanya wakati wa magumu, Biblia inasema '' akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za MUNGU ''
Wakati uko katika magumu sana ndugu inakupasa kumwomba MUNGU sana. Sina maana ya kwamba uwe kuomba MUNGU hadi uwe kwenye magumu, la hasha, bali omba siku zote na hata ikitokea uko katika magumu omba pia. Kwanini nimesema uombe wakati wa magumu? Ni kwa sababu wengi walio katika magumu hukosea sana wakati wa magumu yao. Wengi hulia tu bila kuomba, wengi huwaza vibaya, wengi hulalamika na kukufuru, wengi huhesabu gharama na kujuta kana kwamba hakuna msaada tena wakati msaada upo kwa MUNGU.
Unahitaji  ndugu kuomba wakati uko katika wakati mgumu.
Hata Bwana YESU wakati akiwa katika wakati mgumu aliomba ili kutufundisha sisi leo.
 Mathayo 26:36-39 ''Kisha YESU akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. ''
 
2. Mtegemee MUNGU kukuokoa huku ukikiri ushindi.
Danieli 3:17 ''
Kama ni hivyo, MUNGU wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.''
Vijana hawa watatu yaani Shadraka, na Meshaki, na Abednego  walikiri ushindi wa MUNGU kwao hata kipindi ambacho kuni zinachochewa ili watupiwe katika tanuru la moto. Ulikuwa ni wakati mgumu sana sana lakini hawakuacha kukiri ushindi wa MUNGU kwao wakisema mbele ya raisi wa nchi mwenye hasira kwamba '' MUNGU wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. ''
Ndugu, ukiwa katika wakati mgumu mtegemee Bwana YESU huku ukikiri ushindi wake kwako. Vijana hawa akina
Shadraka, na Meshaki, na Abednego kwa kumtegemea MUNGU wakati katika wakati mgumu, MUNGU aliwaokoa kiajabu sana sana.

3. Imba nyimbo za kumwabudu na kumsifu MUNGU.
Matendo 16:24-25 ''
Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba MUNGU na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.''
Paulo na Sila kipindi hiki walikuwa katika wakati mgumu sana, walikuwa wamefungwa gerezani bila kosa lolote na hakukuwa na dalili za kutoka. Walijua kanuni ya kiroho ya kufanya wakati wa magumu. Biblia inasema walikuwa wanaomba MUNGU, Lakini hawakuishia kuomba tu bali Biblia inasema  kwamba walikuwa wanafanya kitendo cha ''kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.''
MUNGU alituma Malaika ili kuwatoa katika magumu yao.
Hata wewe ukiwa katika magumu zingatia kanuni hii ya kumsifu MUNGU kwa nyimbo na pambio za kiutukufu na kukiri kwa kinywa chako kwamba yuko MUNGU Mbinguni anayeweza yote, na hata kwako ataweza kwa kukutoa katika magumu uliyopo.

4. Tafuta jambo jema la kufanya
Mwanzo 23:1-3 ''
Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba ndio umri wake Sara.  Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea. Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena, ''
Huu ni mfano hai wa mtu aliyekuwa katika wakati mgumu sana.

Ibrahimu alikuwa amefiwa na mke wake mpenzi Sarah, ni wakati mgumu sana. Ibrahimu alimlilia sana sana lakini baadae akaamua kutoka pale na kwenda kuongea na watoto wa Hethi, kitendo cha kutoka kina maana hata kwako unaweza ukatoka katika tukio lililoleta magumu kwako. Ukibaki umelishikilia jambo hilo utaendelea kulia na kuumia na haitakusaidia.
Mfano mumeo amesingiziwa kesi na kupelekwa selo. Umeumia sana na unaamua kujifungia chumbani asubuhi hadi jioni huku ukilia, ndugu hiyo haitaondoa tatizo na zaidi sana itaongeza  tatizo.
Kuna wakati ukiwa katika magumu unahitaji kitu chema cha kufanya, wakati huo nakuomba nenda ibadani.
Mtembelee Mchungaji wako au Mteule mwenzako wa KRISTO.
Soma Neno la MUNGU, Fanya maombi
Fanya kazi ndogo ndogo nyumbani kwako, kwa njia hiyo utakuwa vizuri rohoni na maumivu ya tatizo ulilopo yatapungua au kuondoka kabisa.

Ninaloweza kusema kwako ni hili wakati wa magumu ''Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa BWANA''

Katika maombi leo ombea haya pamoja na yale ambayo ROHO wa MUNGU ataweka ndani yako.
1. Haribu roho za kuwafanya watu wawe watumwa wa shetani.
2. Haribu roho za kukuondoa katika kusudi la MUNGU na mpango wa MUNGU.
3. Haribu roho za shetani za kutaka kuwatawala watu wa MUNGU.
4. Ikatae kwako roho ya mazoelea katika Neno la MUNGU.
5. ombea kibali chako cha kiutumishi katika kazi ya MUNGU.
6. Ombea utoaji wako wa matoleo.
7. Haribu roho za kuwatawanya watu wa MUNGU hata wasiwe wamoja na wasinie mamoja.
Kuna kupona kupitia maombi yako ya leo.
Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;''
  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments