JINSI YA KUMILIKI NA KUTAWALA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tena katibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna aina tano(5) za baraka atoazo MUNGU kwa watu wake.
1. Baraka za afya.
2. Baraka za uchumi.
3. Baraka za ndoa.
4. Baraka za uzao.
5. Baraka za kutamalaki.
Baraka yake kutamalaki kwa jina lingine inaitwa Kumiliki na kutawala,  Sasa moja ya mamlaka ya Mteule wa MUNGU aliyeokolewa na Bwana YESU ni kumiliki na kutawala kwenye ulimwengu wa roho.
Tunamiliki na kutawala kwa sababu tuna mamlaka ya jina la YESU KRISTO.

Jukumu la kwanza tulilopewa wanadamu na MUNGU Muumba wetu ni kutawala.
Mwanzo 1:26-27 ''MUNGU akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; WAKATAWALE samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
MUNGU akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba''

Kwa jinsi hiyo mteule wa MUNGU hatakiwi kutawaliwa nguvu za kiumbe yeyote duniani anayetumika kishetani.
Mkristo hutakiwi kutawaliwa na chochote cha kipepo.
Sasa ili wewe Mteule usitawaliwe ni lazima ujue njia ya kushinda vita ya kiroho.
Safari ya wokovu ni ya kushindana.
Ni lazima tushinde falme zote za giza.

Baadhi ya Kanuni za kiroho ili tushinde falme za giza;

1. Ni lazima ujue ROHO MTAKATIFU yupo na ni lazima ujazwe nguvu za ROHO MTAKATIFU.
-Huwezi kupigana vita ambayo humuoni adui hivyo Watu wa MUNGU tunamhitaji ROHO MTAKATIFU ili atujulishe ndipo tutashinda kila vita ya kiroho katika ulimwengu wa roho.
ROHO MTAKATIFU hutupa pia kupambanua.
1 Kor 12:3 ''3 Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika ROHO wa MUNGU, kusema, YESU amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, YESU ni Bwana, isipokuwa katika ROHO MTAKATIFU ''


3. Ni lazima ulijue Neno la MUNGU na ujue kulitumia ili kuwashinda mawakala wa shetani.
 
Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. ''


 
 Mkristo ukitaka umiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho inakupasa kuhusika na yafuatayo:
1. Kuishi maisha matakatifu.
2. Kuomba katika ROHO MTAKATIFU.
3. Kuliishi kusudi la MUNGU na kumtumikia KRISTO.
4. Kufuata ufunuo wa maongozi ya ROHO MTAKATIFU.
5. Kumwamini MUNGU na kuziamini kazi zake kwa Kanisa.
6. Kujua kupigana vita ya kiroho.
7. Kujitenga na dhambi na machukizo yote ya dunia.

Kwa kufuata kanuni hizo zote saba hakika lazima umiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Waisraeli kama wateule wa MUNGU walipewa kumiliki.
Kumbu 9:1-4 " Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni, watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA. Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako."


Mataifa makubwa yenye nguvu ambayo hayatakiwi kuwa na nguvu mbele za Mkristo ni pamoja na wachawi wote, waganga, wakuu wa Giza wote, washirikina wote na kila mamlaka ya kipepo.
Hao unatakiwa uwatawale na sio wakutawale.
Unatakiwa wasiwe na nguvu juu yako, huko ndiko kuwamiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.

Inakupasa umiliki uzima na afya njema.
MUNGU anataka umiliki na kutawala.
Wachawi kama taifa kubwa lakini kwa Mteule wa KRISTO anayejitambua  hakika wachawi watapigwa na uchawi wao hautafanya kazi.
Teka waganga ili wakuondoe katika list ya watu wa kuonewa kipepo.
Mteule lazima umiliki na kuwatawala mataifa makubwa.
Inawezekana kuumwa kila mara ndio taifa kubwa linalokutesa.
Inawezekana kufungwa kipepo ili usipate kazi au usipate Mchumba ndio taifa kubwa linalokutesa, ndugu unatakiwa mataifa yako makubwa wasiwe na nguvu mbele zako.
Ni lazima upigane kiroho na kushinda.
Nenda na Bwana YESU na hakika utashinda.
Usikubali wachawi wakumiliki wewe.
Usikubali waganga wakumiliki wewe kwa madawa yao.
Usikubali ajali majanga na balaa vikumiliki wewe.
Usikubali washirikina na wasoma nyota wakumiliki wewe.
Usikubali wenye mapepo ya utambuzi ndio wakutabirie wewe na kukumiliki.
Usikubali mapepo/majini na wapunga pepo wakumiliki wewe.
Mteule wa KRISTO hatakiwi kumilikiwa na nguvu za giza.
Ndugu hakikisha umehamishwa kutoka utawala wa giza.
Wakolosai 1:12-17 ''mkimshukuru Baba(MUNGU), aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.  NAYE(MUNGU) ALITUOKOA KATIKA NGUVU ZA GIZA, AKATUHAMISHA NA KUTUINGIZA  KATIKA UFALME WA MWANA WA PENDO LAKE; ambaye katika yeye(YESU) tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa MUNGU asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.  Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.''
Mteule wa KRISTO hatakiwi kumilikiwa na nguvu za giza.
Ndugu kama una hirizi uliyopewa na mganga zamani na akakuambia ukiitupa unadhurika, hakika ichukue na kuipeleka kanisani ili ichomwe moto.
Kama una kitu chochote ulichopewa na mganga na bado umekitunza nakuomba kitupe au kipeleke kanisani kitachomwa moto na wala hutadhurika kwa lolote.
Futa connection yeyote kati yako wewe na ulimwengu wa roho wa giza.
Ni lazima sasa kila anayetumika kishetani ili kukudhuru atambue kwamba  wewe hudhuliki na uchawi na wala hudhuriki na hirizi au majini ya kurushwa, maana una miliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Kanisa la MUNGU haliwezi kutawaliwa wala kumilikiwa na nguvu za giza.
Ndugu yangu uliyeokolewa na Bwana YESU hakika majira yako ya kumiliki na kutawala ni sasa.
Majira yako ya kuwatawala wanaotumika kipepo wote ni sasa, kwa jina la YESU KRISTO.
BWANA MUNGU anataka sasa wewe uziharibu kazi zote za wanaotumika kipepo.
Bomoa madhabahu za kichawi zote katika familia yako, ukoo wako na katika eneo lako au kazi yako.
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''

Ndugu unahitaji tu kumpenda MUNGU.
Wampendao MUNGU ni wale tu wanaompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao na kisha kuanza kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na Biblia takatifu.
Ukifanya hivyo lazima umiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Kuna magonjwa ya kipepo hata hayana majina lakini magonjwa hayo yanawatesa watu wengi.
Kuna vifungo vingi vya kipepo wamefungwa watu.
Ndugu Mteule wa KRISTO uliye Muombaji nakuomba usikubali kumilikiwa na kutawaliwa na wanaotumika kipepo.
Muombe MUNGU akuondolee magonjwa na magonjwa hayo awapige nayo mawakala wa shetani walioyatuma kwako.
Kumb 7:15 '' Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao.''
Hakikisha unamiliki afya njema isiyoingiliwa na magonjwa ya kichawi.
Miliki afya njema kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Miliki na kutawala  kwa jina la YESU KRISTO.
huu ndio wakati wako wa kumiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho.
Jambo ligine hakikisha unamtumikia Bwana YESU, maana kumtumikia KRISTO kuna faida sana.
Kumtumikia KRISTO ndiko kumtumikia MUNGU na siku zote kumtumikia MUNGU kuna faida kubwa sana.
Kumbuka KRISTO YESU Mwokozi alikuja ili wewe umiliki na kutawala.
Ndugu ishi katika kusudi la MUNGU na hakika utamiliki na kutawala.
Kumb 5:32-33 '' Tunzeni basi, mtende kama mlivyoamriwa na BWANA, Mungu wenu; msikengeuke kwa mkono wa kuume wala wa kushoto. Endeni njia yote aliyowaagiza BWANA, Mungu wenu, mpate kuwa hai, na kufanikiwa, mkafanye siku zenu kuwa nyingi katika nchi mtakayoimiliki.''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu


Comments