KATAA USHAWISHI WOWOTE WA KISHETANI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Maana ya neno ''Kushawishi'' ni kumpa mtu maelekezo ili kutaka kumfanya kufuata fikra zako au mawazo yako.
Neno ''Kushawishika''  maana yake ni kuvutiwa au kukubaliana  na kile kilichoonekana au kilichosikika.
Mithali 1:10 '' Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. '' 
 
Tuko katika wakati ambao upo ushawishi mwingi sana na wa vitu vingi sana, na vingine ni machukizo kwa MUNGU.
Waganga wa kienyeji wameweka mabango kila sehemu ili kuwashawishi watu wasio mjua MUNGU Muumbaji wao.
Kwenye Tv kuna matangazo mengi ya kuwataka watu kuhudhuria matamasha ya nyimbo za kidunia.
 Wakolosai 2:4 '' Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi.''
 
Wanaume na wanawake wengi leo huwashawishi watu wa jinsia tofauti na yao ili tu kufanya dhambi ya uzinzi na uasherati.
Matapeli wengi wanashawishi watu katika kuingia maagano ya giza.
Dini za kishetani zimejaa sana zama hizi, dini hizo zinampinga YESU KRISTO tu na Wokovu wake.
Madhehebu ya kishetani yapo na yanafanya kazi yake.
Kumb 13:6-8 ''Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako; katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia; usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche; '

Wengine wanadanganya kwamba MUNGU amesema na wao, ili tu kushawishi akili za watu wasio na ufahamu wa Kibiblia.
Watu wengi sana wanashawishika kipepo na kumwacha Bwana YESU Mwokozi. 
Wengine ni wahubiri, kwa tamaa za kupata mafanikio ya haraka yasiyo sahihi huigeuza injili ya KRISTO.
Wahubiri wengine kwa kutafuta heshima za duniani na kutafuta kuheshimiwa na watu hujiondoa katika kuhubiri kweli ya KRISTO na kuanza kuhubiri hadithi walizojitungia wenyewe, Biblia inaonya ikisema 
2 Timotheo 4:1-5 '' Nakuagiza mbele za MUNGU, na mbele za KRISTO YESU, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.''
 
Ndugu kumbuka kushawishika kipepo ni rahisi sana lakini kutoka kwenye dhambi iliyotokana na kishawishi cha kipepo ni vigumu.
Kushawishiwa kungia kwenye uzinzi ni rahisi sana lakini kuacha uzinzi imekuwa vigumu kwa watu wengi.
Kushawishiwa kwenda kwa mganga wa kuenyeji ni rahisi sana lakini kufunguliwa maagano ya kipepo aliyokuwekea mganga sio rahisi sana kama unavyodhani.
Kushawishika kujiunga dini ya kishetani inaweza kuwa rahisi tu lakini lakini kujitoa kwenye mikataba hiyo ya Giza inaweza kuwa ngumu.
Natambua Kabisa kwamba kwa Bwana YESU KRISTO ni rahisi sana kufunguliwa kifungo cha kishetani cha aina yeyote lakini hiyo haina maana kwamba mtu ajiunge tu kwenye mikataba ya kipepo akitegemea baadae atafunguliwa.
Ndugu tambua kwamba shetani anayajua hayo yote hivyo unapomruhusu akumiliki anakugeuza ufahamu hata hutaona umuhimu wa kukimbilia maombezi ili ufunguliwe.
Wengine waliingia mikataba hiyo ya kipepo wakitegemea siku moja watamrudia Bwana YESU na kufunguliwa lakini shetani aliwaua wakiwa bado kwenye utawala wake.
Nasema na mtu mmoja kupitia Ujumbe huu.
Ndugu usikubali Kushawishika kipepo ili uingie dhambini au uwe mbali na Wokovu wa MUNGU ulio wa thamani sana.
Kumbuka Kushawishika ni rahisi sana lakini kutoka katika vifungo inaweza ikakusumbua sana sana na usipopata Neema ya MUNGU,Kumbuka shetani atakuwekea roho ya kiburi ili uwe mbali zaidi na msaada wa pekee ambao ni YESU KRISTO tu.
Ndugu uwe makini sana na ushawishi mbalimbali maana shawishi ambazo zinakutoa katika Wokovu wa Bwana YESU ni hatari sana kwako.
Nakuomba uwe makini sana.
1 Yohana 4:1-3" Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani."

Leo wapo manabii wa uongo wengi sana sana na wengine wamejificha katika majina yasiyotokana na nabii.
Nabii wa uongo hatokani na jina ila anatokana na mafundisho yake ya uongo.
Mafundisho ya uongo ni mafundisho ya kuwatoa watu katika Wokovu wa Bwana YESU.
Uwe makini sana na shawishi mbalimbali maana kila ushawishi wa kukuweka kwenye dhambi hautokani na MUNGU huo ushawishi Bali ni roho ya mpinga Kristo na ambayo ni roho ya shetani mwenyewe.
MUNGU akusaidie kukataa ushawishi wa roho za mpinga Kristo.

Hata wahubiri Biblia haiwapi nafasi za kushawishi watu.
1 Kor 2:4-5 ''Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za ROHO na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za MUNGU.'' 
Watu wengi sana wametekwa na mafundisho yenye hekima ya kibinadamu na sio MUNGU.
Unaweza katika kushawishi watu basi ukaongeza na uongo wako, ndio maana MUNGU hataki wahubiri wawe washawishi bali wawe wahubiri, Neno la MUNGU limejitosheleza wala halihitaji mtu azidishe uongo wake ndipo watu washawishike.
Ufunuo fake siku hizi ni mwingi sana na huo wote ushawishi wa kipepo ili watu waiache kweli ya injili na kugeukia mafundisho ya uongo.
Ndugu yangu mpendwa, Jifunze kuisikia na kuielewa sauti ya MUNGU ili ujue kupambanua sauti isiyotokana na MUNGU.
Sauti ya MUNGU ni Neno la MUNGU katika muda sahihi na kwa kusudi sahihi.
Sauti ya MUNGU ni kile asemacho ROHO MTAKATIFU.
Ukifaulu kuisikia na kuielewa sauti ya MUNGU utakuwa mtu wa aina hii;-

1. Utajua sauti ya MUNGU kwa usahihi na utajua utende nini baada ya kuisikia sauti ya MUNGU.

2. Itakusaidia kuielewa sauti ya shetani na kuikemea na kutokuifanyia kazi.

3. Utazijua sauti za wanadamu zilizo kinyume na MUNGU na kwa njia hiyo hutazifanyia kazi.

Wapo watu wa kiroho waongo wengi sana leo hivyo ndugu uwe makini.
Wapo wahubiri waongo, wapo wachungaji wa uongo, wapo mitume wa uongo, wapo manabii wa uongo, wapo walimu wa uongo, wapo wainjilisti wa uongo na wapo maaskofu wa uongo.
Hao wote wameigeuza kweli ya KRISTO kwa tamaa zao na hila za shetani.
Wapo watumishi kwa sababu ya uovu wao na dhambi zao MUNGU alishawaacha ziku nyingi, wao hawajui kama MUNGU alishawaacha maana wao sasa ni watumishi wa shetani na sio watumishi wa KRISTO YESU.
Warumi 1:25-32 '' Kwa maana waliibadili kweli ya MUNGU kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. Hivyo MUNGU aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na MUNGU katika fahamu zao, MUNGU aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.
 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia MUNGU, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya MUNGU, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.''


Ndugu, katika maisha yako yote mche MUNGU Baba na mwabudu katika Roho na kweli ya KRISTO.
Katika ujana wako mpe YESU KRISTO nafasi ya kwanza.
Katika ndoa yako mpe MUNGU nafasi ya kwanza.
Katika kazi yako au katika masomo yako mpe MUNGU nafasi ya kwanza.
Katika maisha yako yote lipe Neno la KRISTO nafasi ya kwanza.
Omba pia MUNGU akupe nafasi katika kazi yake na katika huduma.
Katika huduma yako mpe ROHO MTAKATIFU nafasi ya kwanza.
Katika kuishi kwako kote hakikisha unampa MUNGU nafasi ya kwanza.

Marko 12:30 "nawe mpende BWANA Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote."

 Usiwafuate watumishi walevi na waongo.
Usiwafuate wanaofundisha kwamba hakuna mwisho wa dunia, usiwafuate wale wanaojiita MUNGU, usiwafuate wanaoabudu mawe au sanamu.
Usiwafuate wanaofundisha kunywa kidogo ila usilewe.
''Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe
utiaye sumu yako na kumlevya pia......Habaku
ki 2:15

Ndg, zangu nawasihini licha ya kuacha vileo unapaswa pia kutompa kileo yeyote awaye yule haijalishi ni baba, ni mama au ni nani?
Kwa kufanya hivyo unashiriki dhambi isiyo ya Kwako, kumbuka dhambi zote ni sawa na hukumu yake inajulikana.
MUNGU ampe kila mmoja macho ya ndani.

Hakikisha unajifunza Neno la kweli la MUNGU wa kweli.
Tii Neno la MUNGU la injili ya wokovu wa KRISTO YESU Mfalme wa uzima.
Kumbuka Mtu anaweza akafundishwa na kuelewa kwa njia zifuatazo;
1. Kwa kufundishwa na kuelekezwa Neno la MUNGU.
2. Kwa kujulishwa kitu cha ki MUNGU.
3. Kwa mifano.
4. Kwa shuhuda za wengine.
5. Kwa majaribu
6. Kwa mazingira aliyopo.
7. Kwa ndoto na maono n.k
MUNGU anataka ufundishwe na Neno lake ili ikusaidie kujua, kupata maarifa sahihi na kushinda.
Ni muhimu kujua pia kwamba wapo watu ambao hawakuruhusu Neno la MUNGU liwafundishe na kwa njia hiyo majaribu mabaya yaliwakuta na hayo ndio yakawafundisha kumcha MUNGU.
Binti mmoja alikuwa hataki Neno la MUNGU wala kumtii MUNGU, aliambiwa Neno la MUNGU akaishia kuwatukana waliompelekea neno la MUNGU, baadae alijikuta ana ukimwi na mimba ndipo jaribu hilo baya lilipomfunza jinsi ya kuwa mtii na jinsi ya kumcha MUNGU kwa unyenyekevu wote.
Usikupokubali kufunzwa na Neno la MUNGU ujue dunia itakufunza na mafunzo ya dunia huzaa maumivu kwako.
Majaribu yanaweza kukufundisha huku ukilia kwa uchungu mkubwa sana.
Ndugu nakuomba ling'ang'anie Neno la MUNGU kwa kulitii na kufanya litakavyo Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU lina ujumbe wa MUNGU, lina shuhuda, lina mifano hai na mambo mengi.
Usipokubali kufundishwa na Neno la MUNGU ujue majaribu yatachukua nafasi ya kukufundisha huku ukilia.
Ni kweli majaribu ya aina mbili.
Kuna majaribu yaliyokuja kwako kwa sababu umegoma kumtii MUNGU.
Ndugu uwe makini na kataa ushawishi wowote wa kipepo.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments